Na. Veronica Mwafisi-Dodoma
Tarehe 13 Februari, 2023
Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe.
Jenista Mhagama, amesema watumishi wa ofisi yake wameunga mkono jitihada za
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan za
kulinda rasilimaliwatu nchini kwa kuchangia damu katika Hospitali ya Rufaa ya
Mkoa wa Dodoma itakayowasaidia wananchi, watumishi wa sekta ya umma na binafsi
wenye uhitaji.
Mhe. Jenista
amesema hayo wakati akihitimisha shughuli za kijamii zilizofanywa na ofisi yake
katika jiji la Dodoma kwa lengo la kujenga mahusiano mazuri na jamii.
Mhe. Jenista
amesema, watumishi wa ofisi yake wamechangia damu ili kuiwezesha benki ya damu
kuwa na akiba ya kutosha itakayokidhi mahitaji kwani anaamini damu hiyo licha
ya kuilenga jamii lakini pia itawasaidia watumishi wa umma na wa sekta binafsi watakaopata
changamoto ya uhitaji wa damu.
“Uchangiaji
huu wa damu uliofanywa na watumishi wa ofisi yangu utaimarisha afya ya
wananchi, watumishi wa umma na watumishi wa sekta binafsi ili wawe na tija
katika kuleta maendeleo na ustawi wa taifa,” Mhe. Jenista amefafanua.
Kwa upande
wake, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala
Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amesema damu iliyochangiwa na watumishi wa ofisi
yake itawasaidia watanzania wote wenye uhitaji wa damu.
Kutokana
uhitaji wa damu katika hospitali nyingi nchini, Mhe. Ndejembi ametoa wito kwa
watumishi wa taasisi nyingine za umma kujitokeza na kuchangia damu katika benki
ya damu ili damu hiyo itumike kuokoa maisha ya watanzania wenye uhitaji.
“Uchangiaji
huu wa damu ni mfano mzuri wa kuigwa na watumishi wa taasisi nyingine za umma
kwani Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anataka watumishi wa umma kuwa
karibu na jamii na kuendelea kujenga mahusiano mazuri na jamii inayowazunguka,”
Mhe. Ndejembi amesisitiza.
Mmoja wa
watumishi waliochangia damu, Bi. Mariam Mwanilwa ambaye ni Mkurugenzi wa Idara
ya Mishahara, Masilahi na Marupurupu amesema kuwa, anayo furaha baada ya kuchangia
damu ambayo anaamini itaokoa maisha ya watanzania wenye uhitaji.
Naye, Mkuu
wa Kitengo cha Damu Salama, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma Dkt. George
Mkira ameushukuru uongozi na watumishi wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI kwa uamuzi wa
kuchangia damu ili kuokoa maisha ya watanzania wenye uhitaji wa damu.
Dkt. Mkira
amesema, chupa 50 za damu zilizopatikana si haba kwani kwa makadirio damu hiyo
itawahudumia watoto wenye uhitaji wasiopungua mia na hamsini.
Ofisi ya
Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imetumia siku mbili
kushiriki huduma za kijamii kwa lengo la kujenga mahusiano mazuri na wananchi.
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Jenista Mhagama akizungumzia uchangiaji wa damu uliofanywa na watumishi wa
ofisi yake katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Dodoma wakati akihitimisha shughuli za kijamii zilizofanywa na ofisi yake jijini
Dodoma kwa lengo la kujenga mahusiano mazuri na jamii.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi
wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akiwaongoza watumishi wa
ofisi yake kupata vipimo vya awali kabla ya kuchangia damu katika Kituo Kidogo
cha Damu Salama, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius
Ndejembi akiwahamasisha watumishi wa ofisi yake kuchangia damu katika Kituo
Kidogo cha Damu Salama katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma. Katikati ni
Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Rasilimaliwatu Serikalini ACP. Ibrahim
Mahumi na wa kwanza kulia ni Mkurugenzi Idara ya Mikataba ya Utendaji kazi
Serikalini Bi. Zainabu Kutengezah.
Sehemu
ya Watumishi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
wakichangia damu katika Kitengo cha Damu Salama, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma
kwa lengo la kuokoa maisha ya watanzania wenye uhitaji wa damu.
Sehemu
ya Watumishi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
wakijiorodhesha kushiriki kuchangia damu katika Kituo Kidogo cha Damu Salama,
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, ikiwa ni sehemu ya kujenga mahusiano na
jamii.
Mkuu
wa Kitengo cha Damu Salama, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Dkt. George Mkira akitoa shukrani kwa Uongozi
na watumishi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa kuchangia damu ili kuokoa maisha ya watanzania wenye uhitaji.
No comments:
Post a Comment