Tarehe 01
Februari, 2023
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi amewataka waajiri katika taasisi za umma kutokwepa jukumu la kuwachukulia hatua za kinidhamu watumishi watakaobanika kukiuka maadili ya utendaji kazi katika taasisi zao.
Bw.
Daudi ametoa wito huo jijini Dodoma wakati akifunga kikao kazi cha siku
mbili cha wadau wa usimamizi wa maadili katika utumishi wa umma kilicholenga
kujadili matokeo ya utafiti ya hali ya uzingatiaji maadili katika utumishi wa
umma ya mwaka 2022.
Bw. Daudi amesema pamoja na
uwepo wa Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo inayosimamia maadili katika
Utumishi wa Umma, bado baadhi ya Watendaji wanashindwa kusimamia maadili na
kuchukua hatua stahiki kwa watumishi wanaobainika kukiuka maadili.
“Waajiri wengi mkiwemo baadhi
yenu ndani ya kikao hiki ambao mnasimamia masula ya utawala na rasilimawatu, mna
kawaida ya kukwepa jukumu la kuchukua hatua za kinidhamu kwa watumishi wasio
waadilifu na badala yake mnaelekeza masuala hayo Ofisi ya Rais Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala ili yafanyiwe kazi jambo ambalo sio sahihi.” Bw.
Daudi amefafanua.
Bw. Daudi ameongeza kuwa,
Waajiri watakaowasilisha Ofisi ya Rais-UTUMISHI masuala ya kinidhamu ya
watumishi wanaowasimamia, hayatafanyiwa kazi badala yake yatarejeshwa ili
waajiri hao watekeleze jukumu lao.
Bw. Daudi amesisitiza kuwa,
jukumu la kumchukulia hatua mtumishi ambaye si mwadilifu ni la Mwajiri, hivyo
hakuna sababu ya kusita kufanya maamuzi kwa masilahi mapana ya Utumishi wa Umma
na kuongeza kuwa, Ofisi ya Rais-UTUMISHI haitashughulikia shauri la kinidhamu la
mtumishi lililowasilishwa kwa matarajio ya mtumishi husika kuhamishiwa kituo kingine
cha kazi kwani kwa kufanya hivyo ni kuhamisha tatizo.
Akielezea
majukumu yaliyotekelezwa na kikao kazi hicho, Mkurugenzi wa Usimamizi wa
Maadili, Bi. Leila Mavika amesema kikao kazi kimebainisha maeneo yenye
changamoto za uadilifu katika Utumishi wa Umma na kuainisha mikakati madhubuti
ya kuimarisha uadilifu katika Utumishi wa Umma.
Kwa
upande wake Mwenyekiti wa kikao kazi hicho ambaye pia ni Mkurugenzi wa Mipango Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Cosmas Ngangaji amesema,
washiriki wa kikao kazi hicho wametekeleza ipasavyo jukumu lao kwa kutoa
mapendekezo yatakayoimarisha maadili katika Utumishi wa Umma kutokana na
mapungufu yaliyoainishwa katika taarifa ya utafiti ya hali ya uzingatiaji
maadili katika utumishi wa umma ya mwaka 2022
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi
wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi akifunga kikao
kazi cha siku mbili cha wadau wa usimamizi wa maadili katika
utumishi wa umma kilicholenga kujadili matokeo ya tafiti ya hali ya uzingatiaji
maadili katika utumishi wa umma ya mwaka 2022, jijini Dodoma.
Sehemu ya wadau wa usimamizi wa maadili katika
utumishi wa umma wakimsikiliza Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi (hayupo pichani) wakati akifunga kikao kazi cha siku mbili cha wadau hao
kilicholenga kujadili matokeo ya tafiti ya hali ya uzingatiaji maadili katika
utumishi wa umma ya mwaka 2022, jijini Dodoma.
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi
wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi akisikiliza
maazimio ya kikao kazi cha siku mbili cha wadau wa usimamizi wa
maadili katika utumishi wa umma kilicholenga kujadili matokeo ya tafiti ya hali
ya uzingatiaji maadili katika utumishi wa umma ya mwaka 2022 jijini Dodoma.
Kulia kwake ni Mwenyekiti
wa kikao kazi hicho, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Mipango Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Cosmas Ngangaji na
kushoto kwake ni Mkurugenzi wa Usimamizi wa Maadili, Bi. Leila Mavika.
Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Ufuatiliaji wa Uzingatiaji
wa Maadili, Bi. Janeth Mishinga akiwasilisha maazimio yaliyopendekezwa na wadau
wa usimamizi wa maadili katika utumishi wa umma kabla ya Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi kufunga kikao
kazi cha wadau hao cha siku mbili kilicholenga kujadili matokeo ya tafiti ya hali
ya uzingatiaji maadili katika utumishi wa umma ya mwaka 2022, jijini Dodoma.
No comments:
Post a Comment