Thursday, March 26, 2015

KATIBU MKUU UTUMISHI ASTAAFU UTUMISHI WA UMMA

MAKABIDHIANO: Katibu Mkuu Utumishi Bw.George D. Yambesi (kushoto) akikabidhi ofisi baada ya kustaafu Utumishi wa Umma kwa Naibu Katibu Mkuu Utumishi Bw.HAB Mkwizu.   

HONGERA KWA KUWA MTUMISHI MIAKA 38: Katibu Mkuu -Utumishi Bw. George D. Yambesi (katikati) akipongezwa na Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Rasilimali Watu Bw. Aloyce Msigwa, (kushoto) ni Naibu Katibu Mkuu-Utumishi Bw. HAb Mkwizu. Bw. Yambesi amestaafu Utumishi wa Umma.

Wednesday, March 18, 2015

MHE.DKT.JAKAYA MRISHO KIKWETE AZINDUA KITUO CHA TAIFA CHA KUMBUKUMBU DODOMA

Rais wa Jamhuri ya Muuungano wa Tanzania Mh. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akihutubia wakati wa Uzinduzi wa Kituo cha Taifa cha Kumbukumbu Dodoma.

Rais wa Jamhuri ya Muuungano wa Tanzania Mh. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, viongozi wa Serikali na Washirika wa Maendeleo kwa pamoja wakikata utepe kuzindua Kituo cha Taifa cha Kumbukumbu Dodoma.
Rais wa Jamhuri ya Muuungano wa Tanzania Mh. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akiangalia moja ya faili lenye kumbukumbu za zamani katika Kituo cha Taifa cha Kumbukumbu Dodoma.
HOTUBA YA MHE. DKT. JAKAYA MRISHO KIKWETE,
RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
KATIKA SHEREHE YA UFUNGUZI RASMI WA KITUO
 CHA TAIFA CHA KUMBUKUMBU
DODOMA TAREHE 18 MACHI, 2015

·        Waheshimiwa Mawaziri,
·        Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma,
·        Waheshimiwa Wabunge,
·        Waheshimiwa Viongozi wa Vyama vya Siasa,
·        Ndugu Makatibu Wakuu,
·        Mheshimiwa Mwenyekiti wa Bodi ya Kumbukumbu
na Nyaraka za Taifa,
·        Mheshimiwa Mwenyekiti wa Bodi ya Udhamini ya
Mfuko wa Kuwaenzi Waasisi wa Taifa letu,
·        Ndugu Viongozi wa Taasisi Mbalimbali za Serikali,
·        Ndugu Wanahabari,
·        Wageni Waalikwa,
·        Mabibi na Mabwana.

Awali ya yote naomba nitoe shukrani zangu za dhati kwa kupata  nafasi ya kualikwa ili kuja kushirikiana nanyi katika tukio hili muhimu la ufunguzi rasmi wa   Kituo cha Taifa cha Kumbukumbu  (The National Record Centre) hapa Dodoma. Kipekee napenda kuipongeza Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma kwa kuandaa shughuli hii. Pia ninawashukuru wageni wote kwa kuja kushiriki katika tukio hili muhimu.

Wageni waalikwa, Mabibi na Mabwana, Ninaamini mtakubaliana nami kwamba, kumbukumbu ni nyenzo muhimu katika utendaji kazi Serikalini na Taasisi zake. Bila ya kuwa na kumbukumbu sahihi hatuwezi kujua tunakotoka na tunakokwenda na hivyo kushindwa kufikia maamuzi sahihi kwa wakati. Kumbukumbu hutumika kama kielelezo katika uwajibikaji na ni nguzo muhimu katika Utawala Bora. Ili Serikali iweze kufikia lengo hilo na kuwezesha umma kujua mwenendo wa Serikali yao, lazima kuwe na kumbukumbu zinazotunzwa vizuri na zinazopatikana kwa urahisi. Kukosekana kwa taarifa sahihi na kwa wakati unaofaa kunaweza kuwafanya Watendaji wa Serikali kushindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo na hivyo kusababisha ucheleweshwaji wa maamuzi au kutolewa kwa maamuzi yasiyo sahihi na yasiyokidhi matarajio ya wananchi. Aidha, ukosefu wa kumbukumbu hutoa mianya ya rushwa na ubadhirifu wa mali ya umma, matumizi mabaya ya madaraka na hata kuchelewesha au kuzuia haki kutendeka. Kasoro hizi huchangia sana katika kuzorotesha maendeleo ya uchumi wa Taifa na malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu Serikali yao na Taasisi zake.

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana, Programu ya Mabadiliko katika Utumishi wa Umma awamu ya pili (Public Service Reform Programme II – PSRP II) niliyoizindua mwezi Januari 2008, pamoja na mambo mengine ilijielekeza katika  kufanya mabadiliko kwenye mifumo ya utunzaji wa kumbukumbu na utoaji wa taarifa katika Utumishi wa Umma. Lengo kubwa la mabadiliko haya likiwa ni kuwa na Serikali yenye kuwajibika, uwazi na utawala bora. Chini ya Programu hii, Serikali iliona umuhimu wa kuangalia upya jinsi inavyozalisha taarifa zake, kuzitumia, kuzitunza na kuzihifadhi kwa ajili ya matumizi ya sasa na ya baadaye. Aidha, kabla ya uzinduzi wa Programu hii, Serikali ilibaini kuwepo kwa tatizo kubwa la utunzaji wa kumbukumbu hasa mlundikano mkubwa wa majalada katika Ofisi za Umma, ambayo yalihifadhiwa bila ya kufuata taratibu za utunzaji kumbukumbu. Hali hii kwa kiasi kikubwa pamoja na mambo mengine iliathiri utendaji wa Serikali katika kuwahudumia wananchi kama vile  ucheleweshaji wa kulipwa pensheni kwa watumishi wa umma, ugawaji holela wa viwanja na ucheleweshaji wa kusikilizwa kesi, rushwa na upotevu wa mali za umma. Kumbukumbu zinazotunzwa vizuri ni sawa na uti wa mgongo wa Serikali katika kufikia malengo yake kwa ukamilifu katika kutunga na kutekeleza Sera sahihi, kuweka mipango madhubuti, kuongeza ufanisi, tija, uwazi na uwajibikaji.


Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana, Ilani ya Uchaguzi ya Chama Tawala cha CCM ya mwaka 2010, inasisitiza upatikanaji wa taarifa sahihi kwa wananchi ambao ndiyo mamlaka iliyoiweka Serikali ya Awamu ya Nne madarakani. Aidha, Sera ya Taifa ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa ya Mwaka  2010 na Sheria ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa Na. 3 ya Mwaka 2002 zinaelekeza Serikali na Taasisi zake kuwa na majengo na vifaa vinayokidhi uhifadhi bora wa Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa. Kituo hiki ni moja ya vielelezo vya juhudi za Serikali katika kuhifadhi na kutunza kumbukumbu na nyaraka za Taifa ambazo ni dira ya kizazi kilichopo na kijacho kama sehemu ya urithi andishi na historia ya Taifa letu. Kuwepo kwa Kituo hiki, kutaongeza ufanisi katika utendaji na utoaji huduma bora kwa wananchi kwani kitakuwa ni chimbuko la taarifa mbalimbali zitakazoisaidia Serikali katika uendeshaji wa kazi zake za kila siku. 

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana, Miundombinu ya Kituo hiki ni ya Kisasa na itakuwa na uwezo wa kuhifadhi majalada zaidi 770,000. Kutokana na uwezo wa Kituo kuhifadhi majalada hayo, Taasisi za Umma zitaokoa zaidi ya mita za mraba 77,700 za ofisi zao ambazo zilikuwa zikitumika kuhifadhi majalada haya. Aidha, miundombinu hii imezingatia uzalishaji wa taarifa za Serikali katika Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), hivyo Kituo kimeunganishwa na mkongo wa Taifa ili kurahisisha mawasiliano Serikalini ikiwemo upatikanaji wa taarifa na nakala za kumbukumbu zitakazokuwa zinahitajika na watumiaji mbalimbali kwa haraka na uhakika zaidi kutoka katika Kituo hiki.

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana, Sera ya Taifa ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa ya mwaka 2010 na Sheria ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa Namba 3 ya mwaka 2002, zinaagiza Watendaji Wakuu wa Taasisi za Umma kusimamia taratibu na mifumo ya utunzaji kumbukumbu, usalama wa kumbukumbu na nyaraka na kuwajengea uwezo watumishi wa masjala katika kutunza na kuwezesha Serikali kutoa huduma bora kwa raia wake. Napenda nichukue nafasi hii kuwakumbusha Watendaji Wakuu wa Ofisi mbalimbali za umma kuhusu wajibu wao wa kutunza kumbukumbu zinazozalishwa katika Ofisi zao kwa mujibu wa Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo mbalimbali inayotolewa na mamlaka husika. Watendaji Wakuu wa Taasisi zote za Serikali wahakikishe wanahamishia katika Kituo hiki kumbukumbu zote zilizofungwa ili Kituo hiki kiweze kutunza kumbukumbu kwa kuzingatia viwango vya kitaifa na kimataifa.

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana, Kazi iliyofanyika ya kusanifu, kujenga na kuweka vifaa vya kisasa vya kuhifadhia kumbukumbu ni nzuri na ya gharama kubwa. Nachukua nafasi hii, kuwaelekeza wote mnaosimamia uendeshaji wa Kituo hiki kuhakikisha kwamba kinatunzwa na kufanya kazi ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.  Serikali kwa upande wake itaendelea kutenga bajeti ya kutosha kwa ajili ya kutunza na kukiendeleza Kituo hiki ambacho ni cha pekee katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana, Kabla sijamaliza hotuba yangu, naomba niwashukuru Washirika wetu  wa Maendeleo  kwenye Programu ya Mabadiliko katika Utumishi wa Umma, ambao kwa kushirikiana na Serikali yetu wamechangia katika kufanikisha ujenzi na uwekaji wa vifaa vya kisasa katika Kituo hiki.  Kwa kutambua umuhimu wa kumbukumbu na nyaraka walikubali kuchangia ujenzi wa Kituo hiki muhimu kwa nchi yetu. Hivyo, kwa namna ya pekee ninawashukuru sana Benki ya Dunia, Serikali ya Uingereza kupitia DfID na Serikali ya Canada kupitia CIDA kwa kuwezesha ujenzi wa Kituo hiki.

Mwisho ninapenda niwashukuru wote mliohudhuria sherehe hii ya ufunguzi wa Kituo cha Taifa cha Kumbukumbu - Dodoma.  Ni matarajio yangu kuwa Kituo hiki kitakuwa chachu ya kuleta uwajibikaji, uwazi na utawala bora kwa Taasisi zote za Serikali.


Asanteni kwa kunisikiliza!!

Friday, March 13, 2015

KATIBU MKUU UTUMISHI ATEULIWA KUWA KAMISHNA TUME YA UTUMISHI WA UMMA

Rais Jakaya Kikwete (kushoto), akimwapisha Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, George Yambesi, kuwa Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Umma, wakati alipokuwa akiwaapisha makamishna wa tume hiyo, Ikulu, Dar es Salaam.

Wednesday, March 4, 2015

VACANCY ANNOUNCEMENT




THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
PRESIDENT’S OFFICE
PUBLIC SERVICE MANAGEMENT

 Applications are hereby invited from qualified and experienced Tanzanians for the following Vacant post advertised by the Commonwealth Secretariat:

(i)           Director, Political Division
(i)   Duty Station: London, United Kingdom
(ii)  Deadline for Applications:  16th March, 2015
                                                    
SUBMISSION OF APPLICATIONS:

  •   For more information regarding Terms of Reference of the advertised post; qualifications, tenure of appointment, and remuneration please visit the Commonwealth Secretariat’s website, (www.thecommonwealth.org/jobs).
  • Applications must be submitted online to the address provided in the above mentioned website.
  • NB: appropriately qualified Women are highly encouraged to apply for this post.
  • A copy of the application should be sent to:-  
Permanent Secretary,
President’s Office - Public Service Management,
Human Resources Development Division,
                                    8 Kivukoni Road,
                                    P.O. BOX 2483,
                                    11404 DAR ES SALAAM.
                                    Fax No: + 255-22-2125299 or + 255-22-2127806


UTUMISHI YAENDELEA NA VIKAO KAZI KWA NJIA YA MTANDAO (VIDEO CONFERENCE)

Baadhi ya maofisa wa TAMISEMI,TaGLA na mikoa ya Ruvuma, Mara na Mbeya wakishiriki kikao kazi kwa njia ya video (Video Conference) .

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais – Utumishi Bw. HAB Mkwizu (katikati) akiongoza kikao kazi kwa njia ya video (Video Conference) kilichofanyika kati ya Utumishi,TAMISEMI,TaGLA na mikoa ya Ruvuma ,Mara,Mbeya, Singida na Pwani.

Baadhi ya Maofisa wa Ofisi ya Rais – Utumishi wakiwa katika kikao kazi kwa njia ya video (Video Conference) kati ya Utumishi,TAMISEMI,TaGLA na mikoa ya Ruvuma ,Mara,Mbeya, Singida na Pwani.