Friday, June 19, 2020

SERIKALI MTANDAO IMEPUNGUZA GHARAMA ZA HUDUMA KWA WANANCHI NA MIANYA YA RUSHWA SERIKALINI.








Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Dkt. Mary Mwanjelwa akizisisitiza Taasisi za Umma kushirikiana na Mamlaka ya Serikali Mtandao katika kutekeleza sheria mtandao jiji Dodoma.


 

SERIKALI MTANDAO IMEPUNGUZA GHARAMA ZA HUDUMA KWA WANANCHI NA MIANYA YA RUSHWA SERIKALINI-Dkt. Mwanjelwa

Na. Aaron Mrikaria-Dodoma

18 Juni, 2020

Utoaji huduma kupitia Serikali Mtandao katika Taasisi za Umma nchini umekuwa na tija kwa wananchi kwa kuwapunguzia gharama za kusafiri umbali mrefu kufuata huduma katika Taasisi za Umma, ikiwa ni pamoja na kupunguza mianya ya rushwa kwa watumishi wanaowahudumia wananchi  katika taasisi za umma.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Mary Mwanjelwa jijini DODOMA wakati akizungumzia maboresho ya huduma kwa njia ya TEHAMA yaliyofanywa na Serikali katika Taasisi za Umma kwa lengo la kuwarahisishia wananchi kupata huduma bora na kwa wakati.

Dkt. Mwanjelwa amesema, hivisasa wananchi wanaohudumiwa na ofisi yake na katika baadhi ya Taasisi za umma nchini wanapata mrejesho wa masuala yao kupitia simu za viganjani au barua pepe zao mara baada ya masuala hayo kupokelewa ili kushughulikiwa, pasipo kuwalazimu kufika katika ofisi yake na taasisi hizo ambapo wangelazimika kuingia gharama na hata kuombwa rushwa na baadhi ya watumishi wasio waadilifu. 

“Malipo ya bili za maji, umeme na mengineyo katika taasisi za umma nchini hufanywa popote kwa njia ya mtandao, hakika Serikali mtandao imesaidia kuokoa pesa na muda ambao ungetumiwa na wananchi kwa kupanga foleni ili kulipia bili hizo”, Dkt. Mwanjelwa amefafanua.

Kuhusu mapambano dhidi ya Rushwa, Dkt, Mwanjelwa amesema, ukusanyaji wa mapato ya Serikali umeboreshwa kwa malipo kufanywa kielektroniki hivyo kupunguza mianya, rushwa na upotevu wa fedha za umma.

Kutokana na umuhimu wa Serikali Mtandao, naziagiza taasisi zote za umma nchini kutekeleza matakwa ya Sheria ya Serikali Mtandao namba 10 ya mwaka 2019 ili kutoa huduma bora kwa wananchi.

 “Taasisi za Umma zinapaswa kuzingatia kikamilifu matakwa yote ya sheria ya Serikali Mtandao pamoja na kanuni zake katika matumizi yoyote yale ya TEHAMA yanayofanywa na kuongeza kuwa, taasisi zitakazo kaidi agizo hili zitakuchukuliwa hatua kwa mujibu wa Kanuni, Sheria, Taratibu na miongozo iliyopo” Dkt. Mwanjelwa amesisitiza.

Aidha Dkt. Mwanjelwa amezitaka Taasisi za Umma kuwa na utaratibu wa kuwasilisha mapendekezo ya miradi ya TEHAMA kwenye Mamlaka ya Serikali Mtandao kwa ajili ya ushauri na maboresho kabla ya kuanza utekelezaji wake.

Sanjali na hilo, Dkt. Mwanjelwa amezielekeza Taasisi za Umma kuzingatia viwango na miongozo iliyoidhinishwa wakati wa usanifu, ujenzi,  uendeshaji wa mifumo na miundombinu ya TEHAMA ili kuhakikisha mifumo hiyo inakuwa na ubora unaotakiwa na usalama wa taarifa.

Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania liliipitisha rasmi Sheria ya Serikali Mtandao Namba 10 ya mwaka 2019 na tangazo lake kutolewa na Serikali kupitia tangazo namba 75 katika Gazeti la Serikali ili kuifanya Serikali Mtandao kuwa mamlaka kamili na hatimaye kutekeleza azma ya Serikali ya kutoa huduma bora kwa wananchi na wadau wake kwa njia ya TEHAMA.

 




Sunday, June 14, 2020

UJUMBE WA MHE. DKT. MWANJELWA KWA WATUMISHI WA UMMA


SERIKALI YAZIELEKEZA TAASISI ZA UMMA KUADHIMISHA WIKI YA UTUMISHI WA UMMA MWAKA 2020 KWA KUDUMISHA USHIRIKIANO NA WADAU


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora (Mb), Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) akitoa maelekezo ya namna ya kuadhimisha Wiki ya Utumishi wa Umma mwaka 2020 mapema leo, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt (Mst) Mhe. George Mkuchika (Mb).