Wednesday, October 27, 2021

SERIKALI YAPONGEZWA KWA KUBUNI MIFUMO YA TEHAMA YA KUTATUA KERO ZA WANANCHI


Na. James K. Mwanamyoto-Dodoma

Tarehe 27 Oktoba, 2021

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Abdallah Chaurembo ameipongeza Serikali kupitia Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) kwa kubuni mifumo ya utoaji huduma kwa wananchi na kutatua kero zinazowakabili pindi wanapohitaji huduma katika taasisi za umma.

Mhe. Chaurembo ametoa pongezi hizo leo wakati wa kikao kazi cha kamati yake na Uongozi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kilichofanyika katika Kituo cha Utafiti na Ubunifu cha Mamlaka ya Serikali Mtandao jijini Dodoma.

Mhe. Chaurembo amesema, kamati yake inaridhika na utendaji kazi wa Ofisi hiyo hasa katika kubuni mifumo ya TEHAMA inayosaidia kuondoa malalamiko ya wananchi.

Mhe. Chaurembo amesema kamati yake itaendelea kutoa ushirikiano kwa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na kuwasisitiza wajumbe wa kamati yake kutoa elimu ya matumizi ya mifumo hiyo kwa wananchi wanapokuwa kwenye maeneo yao ya utawala.

“Mambo mazuri sana yamefanywa na Ofisi hii pamoja na taasisi zake, hasa hili la kubuni mifumo ya TEHAMA inayoondoa malalamiko, hivyo wajumbe wa kamati hii tuwasaidie kutoa elimu ya umuhimu wa mifumo hii kwa wananchi, tuwasisitize wananchi watumie mifumo hii kuondoa malalamiko,” Mhe. Chaurembo amesisitiza.

Akitoa neno la utangulizi, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema, Serikali kupitia wataalam wa ndani wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) imekuwa ikibuni mifumo mbalimbali kwa lengo la kusogeza huduma za Serikali karibu na wananchi na kuwaweka wananchi karibu na Serikali yao.

Mhe. Mchengerwa amesema kuwa Ofisi yake iliona ni vema kufanya ubunifu wa kutengeneza mifumo ya TEHAMA ya utoaji huduma kutokana na changamoto mbalimbali ambazo zimekuwa zikiwakabili Watumishi wa Umma na wananchi kwa kipindi cha muda mrefu.

Akifafanua jinsi mfumo mmojawapo uliobuniwa na wataalam hao ujulikanao kwa jina la Sema na Waziri wa UTUMISHI unavyofanya kazi, Mhe. Mchengerwa amesema, mfumo huu unamuwezesha mwananchi kuwasilisha kero au lalamiko lake moja kwa moja kwake na kulifanyia kazi.

Mhe. Mchengerwa amewaomba Wajumbe wa Kamati ya USEMI kutoa elimu ya faida za mfumo huu kwa watumishi na wananchi katika maeneo yao ili utumike kutatua changamoto zinazowakabili.

“Mkiwa kama wawakilishi wa wananchi, tunaomba mtusaidie kupeleka ujumbe kwa wananchi kuhusu faida za mfumo huu kwani tunataka kupunguza kabisa malalamiko na kutatua changamoto za kiutumishi zinazowakabili Watumishi wa Umma kwa muda mrefu.” Mhe. Mchengerwa ameongeza.

Sanjari na hilo, Mhe. Mchengerwa ameishukuru kamati kwa kuiongoza na kuishauri vema ofisi yake na kuahidi kuendelea kutekeleza maelekezo yote yanayotolewa na kamati hiyo kwa maslahi ya taifa.

Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA), Mkurugenzi Mkuu wa eGA, Mhandisi Benedict Ndomba amesema Kituo cha Utafiti na Ubunifu cha Mamlaka ya Serikali Mtandao kimelenga kwenye ubunifu na utafiti  katika TEHAMA ili kuwa na mifumo itakayoboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Mhandisi Ndomba amesema falsafa ya Kituo hicho ni kutumia wataalam wa ndani katika kujenga mifumo hiyo ya TEHAMA ili kuweza kutatuta matatizo yetu wenyewe. 


Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Mhe. Abdallah Chaurembo akiongoza kikao kazi cha kamati yake na Uongozi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wakati wa ziara ya kamati hiyo kwenye Kituo cha Utafiti na Ubunifu cha Mamlaka ya Serikali Mtandao jijini Dodoma.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akijibu hoja za Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa wakati wa kikao kazi cha kamati hiyo na Uongozi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kilichofanyika kwenye Kituo cha Utafiti na Ubunifu cha Mamlaka ya Serikali Mtandao jijini Dodoma.


Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao, Mhandisi Benedict Ndomba akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya taasisi yake kwa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa wakati wa kikao kazi cha kamati hiyo na Uongozi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kilichofanyika kwenye Kituo cha Utafiti na Ubunifu cha Mamlaka ya Serikali Mtandao jijini Dodoma.


Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa wakifuatilia taarifa ya utekelezaji wa Mamlaka ya Serikali Mtandao iliyokuwa ikiwasilishwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Mhandisi Benedict Ndomba wakati wa kikao kazi cha kamati hiyo na Uongozi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kilichofanyika kwenye Kituo cha Utafiti na Ubunifu cha Mamlaka ya Serikali Mtandao jijini Dodoma.


Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa Mhe. Saasisha Mafuwe akiwasilisha hoja wakati wa kikao kazi cha kamati hiyo na Uongozi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kilichofanyika kwenye Kituo cha Utafiti na Ubunifu cha Mamlaka ya Serikali Mtandao jijini Dodoma.



Naibu Mkatibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Francis Michael akitoa ufafanuzi wa hoja za kiutumishi zilizowasilishwa na Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa wakati wa kikao kazi cha kamati hiyo na Uongozi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kilichofanyika kwenye Kituo cha Utafiti na Ubunifu cha Mamlaka ya Serikali Mtandao jijini Dodoma.

 

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Mhe. Abdallah Chaurembo akiwa katika picha ya pamoja na Wajumbe wa Kamati yake na Watendaji wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora mara baada ya kuhitimisha ziara ya kamati hiyo kwenye Kituo cha Utafiti na Ubunifu cha Mamlaka ya Serikali Mtandao jijini Dodoma.


 

Tuesday, October 26, 2021

SITARAJII KUSIKIA MTUNZA KUMBUKUMBU NA NYARAKA ANAVUJISHA SIRI ZA SERIKALI-Mhe Mchengerwa


Na. Nasra H. Mondwe-Arusha

Tarehe 26 Oktoba, 2021

 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa amewataka Watunza Kumbukumbu na Nyaraka katika taasisi za umma kutekeleza majukumu yao kwa weledi ili kujiepusha na uvujishaji wa siri za serikali.

Mhe. Mchengerwa ametoa wito huo wakati akifungua Mkutano wa 9 wa Chama cha Taaluma ya Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania katika ukumbi wa ACC jijini Arusha.

Mhe. Mchengerwa amesema, dhamana waliyonayo Watunza Kumbukumbu ni kubwa, hivyo ni vema wakazingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za utunzaji wa kumbukumbu pamoja na viapo vyao kwasababu utoaji wa siri za Serikali ni kosa kubwa kisheria na kwa mujibu wa taratibu za Utumishi wa Umma.

Waziri Mchengerwa amewaasa washiriki wa Mkutano huo kuhakikisha wanajiepusha na siasa na mambo mengine yanayosababisha kutoa siri za Serikali.

Mhe. Mchengerwa amesisitiza kuwa, Serikali ya Awamu Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan inathamini mchango wa Watumishi wa Umma na itaendelea kulinda maslahi yao ikiwa ni pamoja na kutatua changamoto zinazowakabili Watunza Kumbukumbu, hivyo hakuna sababu ya watumishi kutoa siri za Serikali na badala yake wanapaswa kuwa waadilifu kiutendaji na kuwa watiifu kwa Serikali yao.

Akizungumzia juu ya stahiki mbalimbali za Watumishi wa Umma, Mhe Mchengerwa amewaagiza waajiri wote kuhakikisha wanalipa stahili zote za watumishi ikiwepo madai ya malimbikizo ya mishahara na kuongeza kuwa wanapaswa kutenga muda wa kusikiliza kero za watumishi na kuzitafutia uvumbuzi.

Mhe. Mchengerwa amewasisitiza waajiri kuheshimu kada zote kwani kila kada ina umuhimu wake katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku ya Serikali.

 “Waajiri ziheshimuni kada zote, msidharau kada za watu wa chini kwani hawa ni watu muhimu katika utekelezaji wa majukumu yetu na sisi kama Serikali tutaendelea kuzipigania kada hizi,” Mhe. Mchengerwa amesisitiza.

Akimkaribisha Mhe. Mchengerwa kufungua mkutano huo, Mwenyekiti wa Chama cha Taaluma ya Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania (TRAMPA), Bi. Josephine Manase amesema lengo la chama chao ni kujengeana uwezo na kupeana hamasa ya utekelezaji wa majukumu kwa ufanisi ili kutoa mchango katika utekelezaji wa majukumu ya Serikali ya kila siku.

Aidha, Bi. Manase amemuomba Mhe. Mchengerwa kwa nafasi ya uongozi aliyonayo kukisaidia chama chake kumuomba Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kuwa Mgeni Rasmi katika Mkutano ujao wa 10 wa Chama cha Taaluma ya Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania utakaofanyika Zanzibar, ikizingatiwa kuwa kazi ya kwanza ya Mhe. Rais ilikuwa ni ya utunzaji wa kumbukumbu Serikalini.

Mkutano huo wa siku tatu unaongozwa na kauli mbiu isemayo “Imarisha Utunzaji wa Kumbukumbu na Nyaraka ili kuwezesha Uwazi, Uwajibikaji na Utawala Bora katika Kutoa Huduma kwa Umma.”

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akizungumza na washiriki wa mkutano mkuu wa 9 wa Chama cha Taaluma ya Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania alipokuwa akifungua mkutano huo jijini Arusha. 


Baadhi ya washiriki wa mkutano mkuu wa 9 wa Chama cha Taaluma ya Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania wakimsikiliza   Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa (hayupo pichani) alipokuwa akifungua mkutano huo jijini Arusha.


Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Francis Michael akitoa ufafanuzi wa masuala ya kiutumishi wakati wa mkutano mkuu wa 9 wa Chama cha Taaluma ya Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania jijini Arusha. 


Mwenyekiti wa Chama cha Taaluma ya Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania, Bi. Josephine Manase akielezea lengo la mkutano wa chama chao kabla ya kumkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa kufungua mkutano mkuu wa 9 wa Chama cha Taaluma ya Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania jijini Arusha. 


Katibu wa Chama cha Taaluma ya Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania, Bw. Francis Mathias akitambulisha makundi ya washiriki wa mkutano wa mkuu wa 9 wa Chama cha Taaluma ya Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania jijini Arusha. 


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akipokea tuzo kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ya kutambua mchango mahili wa Mhe. Rais katika kuendeleza taaluma ya menejimennti ya utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka na kwa uongozi wa uwazi na uwajibikaji, wakati wa mkutano mkuu wa 9 wa Chama cha Taaluma ya Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania jijini Arusha.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akipokea tuzo kutambua mchango wake wa kuunga mkono juhudi za utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka katika Utumishi wa Umma wakati wa mkutano mkuu wa 9 wa Chama cha Taaluma ya Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania jijini Arusha.


Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Francis Michael akipokea cheti kwa niaba ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora cha kutambua mchango wa Ofisi hiyo kwa Watunza Kumbukumbu na Nyaraka wakati wa mkutano mkuu wa 9 wa Chama cha Taaluma ya Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania jijini Arusha. 


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Watendaji kutoka taasisi za umma walioshiriki mkutano mkuu wa 9 wa Chama cha Taaluma ya Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania mara baada ya kufungua mkutano huo jijini Arusha. 


 

Monday, October 25, 2021

MHE. MCHENGERWA AELEKEZA MIRADI YA TASAF ITEKELEZWE BILA ITIKADI ZA KIDINI NA KISIASA


Na. Nasra H. Mondwe-Arusha

Tarehe 25 Oktoba, 2021

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa amewataka Viongozi na Watendaji wanaosimamia utekelezaji wa Awamu ya Nne ya Mradi wa Kupunguza Umaskini Tanzania kutekeleza mradi huo bila kujali itikadi za dini wala siasa kwani suala la maendeleo kwa wananchi halina ubaguzi.

Mhe. Mchengerwa ametoa maelekezo hayo wakati akizindua kikao kazi cha utekelezaji wa Awamu ya Nne ya Mradi wa Kupunguza Umaskini Tanzania kilichofanyika leo jijini Arusha.

Mhe. Mchengerwa amesema, utekelezaji wa mradi huo utaendeleza na kuimarisha dhana ya uwazi, ukweli, ushirikishwaji na uwajibikaji kwani Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ina imani kuwa miradi ya kupunguza umaskini katika halmashauri zetu itaboresha maisha ya wananchi wengi na kuimarisha ustawi wao.

Amewakumbusha washiriki wa kikao kazi hicho kuwa, utekelezaji wa mradi huu unahitaji umakini mkubwa ili kuhakikisha miradi ya kijamii inayotekelezwa inaonyesha thamani ya fedha, hivyo amewataka wajumbe wazingatie maelekezo ili kuweza kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Mhe. Mchengerwa amewasisitiza Viongozi na Watendaji kufanya kazi kwa weledi na kuzingatia miongozo iliyowekwa ili kumuunga mkono Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ambaye amesimama kidete kuhakikisha wananchi hususani wanyonge wanapata huduma bora za kijamii ili kupunguza umaskini.

Akizungumzia juu ya matumizi sahihi ya fedha zilizotolewa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo, Mhe. Mchengerwa amemtaka Mkurugenzi Mtandaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kuishirikisha Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) katika kila mkoa ili kujiridhisha na uwepo wa tija ya miradi hiyo kwa wananchi na ni kwa namna gani miradi hiyo itaweza kuwakomboa.

“Mimi kama Waziri wa Utawala Bora, sitarajii kusikia ubadhirifu wa aina yoyote katika mikoa yote hiyo mitano ambayo miradi hii imeilenga, na pia sitegemei kusikia TAKUKURU inakwenda kupambana badala ya kwenda kuzuia ili tuweze kupata tija tuliyokusudia,” Mhe. Mchengerwa amesisitiza.

Mhe. Mchengerwa amesema, ni jukumu la kila mmoja katika mkoa na wilaya kufanya ufuatiliaji wa karibu na kwa umakini mkubwa wa matumizi ya fedha ya kila mradi kwani utekelezaji wa miradi hiyo ndio kipimo cha kila kiongozi na mtendaji kwenye ngazi ya mikoa na wilaya.

“Ni jukumu la kila Kiongozi, Watendaji, Maafisa wote wa Halmashauri zote, Waratibu wa TASAF na Maafisa wa TAKUKURU katika kila mkoa na wilaya kusimamia fedha za miradi zinazotolewa na Mhe. Rais kwa lengo la kuzinyanyua kaya zilizo na hali ngumu na kuondosha mazingira duni katika maeneo yao kwani hicho ndio kipimo chenu cha utendaji,” Mhe. Mchengerwa amesisitiza.

Akimkaribisha Mhe. Mchengerwa kuzindua Mradi huo, Mkuu wa Mkoa wa Arusha. Mhe. John Mongella amemshukuru Mhe. Mchengerwa kwa kufanya uzinduzi katika Mkoa wa Arusha na kuahidi kufanyia kazi maelekezo ambayo Mhe. Mchengerwa amekuwa akiyatoa sehemu mbalimbali juu ya usimamizi mzuri wa miradi inayotekelezwa na Serikali.

Amesema Mhe. Samia amekuwa akifanya mambo makubwa kwani amekuwa akitoa fedha nyingi hivyo, hawana budi kumuunga mkono na kuahidi kuwa hakuna ubadhirifu wowote utakaotokea katika utekelezaji wa miradi hiyo.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa TASAF, Bw. Ladislaus Mwamanga ameleezea lengo la kikao kazi hicho kuwa ni kuelekezana juu ya majukumu ya kila mmoja atakayeshiriki katika utekelezaji wa miradi hiyo ili kufanikisha malengo yaliyokusudiwa.

Lengo la utekelezaji wa Awamu ya Nne ya Mradi wa Kupunguza Umaskini Tanzania ni kuwakomboa wananchi dhidi ya mazingira ya umaskini, maradhi na ujinga kwa kuboresha upatikanaji wa huduma za kiuchumi, kijamii katika ngazi zote za jamii zilizo katika halmashauri.

Miradi itakayotekelezwa katika awamu hiyo ni ujenzi na ukarabati wa vyumba vya madarasa, mabweni, zahanati, vituo vya afya nyumba za watumishi wa vituo vya afya na walimu, ujenzi na ukarabati wa vivuko, barabara za vijijini na vyanzo vya maji. Jumla ya miradi 1,500 itakatekelezwa katika wilaya 33 za Mikoa ya Arusha, Njombe, Simiyu, Geita na Mwanza.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akizungumza na Viongozi na Watendaji watakaosimamia utekelezaji wa Awamu ya Nne ya Mradi wa Kupunguza Umaskini Tanzania wakati wa uzinduzi wa mradi huo uliofanyika leo jijini Arusha.

Baadhi ya Viongozi na Watendaji wa Mkoa wa Arusha watakaotekeleza Awamu ya Nne ya Mradi wa Kupunguza Umaskini Tanzania wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao wakati akizindua Awamu ya Nne ya Mradi wa Kupunguza Umaskini Tanzania leo jijini Arusha.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akiteta na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. John Mongella wakati wa uzinduzi wa Awamu ya Nne ya Mradi wa Kupunguza Umaskini Tanzania uliofanyika leo jijini Arusha.


Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. John Mongella akitoa maelezo ya awali kabla ya kumkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa kuzindua Awamu ya Nne ya Mradi wa Kupunguza Umaskini Tanzania leo jijini Arusha.

Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Bw. Ladislaus Mwamanga akielezea lengo la Mradi wa Kupunguza Umaskini Tanzania uliozinduliwa leo jijini Arusha na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi na Watendaji watakaosimamia utekelezaji wa Awamu ya Nne ya Mradi wa Kupunguza Umaskini Tanzania mara baada ya kunduzia mradi huo leo jijini Arusha.

 


 

Wednesday, October 20, 2021

HALMASHAURI ZATAKIWA KUANDAA MPANGO WA RASILIMALIWATU NA URITHISHANAJI MADARAKA UTAKAOBORESHA UTENDAJI KAZI KATIKA UTUMISHI WA UMMA

 Na. Veronica E. Mwafisi-Dodoma

Tarehe  20 Oktoba, 2021

Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Hassan Kitenge amezitaka Halmashauri kuandaa Mpango wa Rasilimaliwatu na Urithishanaji Madaraka ili kuwezesha taasisi za umma kutoa huduma bora na endelevu.

Bw. Kitenge amesema hayo leo Jijini Dodoma, wakati akifungua mafunzo ya kuandaa Mpango wa Rasilimaliwatu na Urithishanaji Madaraka kwa Maafisa Utumishi Waandamizi wa Halmashauri za Mikoa ya Mara, Kigoma, Singida na Dodoma. 

Amesema, kutokana na Sheria ya Utumishi wa Umma ya Mwaka 2002 na Sera ya Menejimenti ya Ajira ya Mwaka 2008, waajiri katika Wizara na Taasisi za umma  wamepewa sehemu kubwa ya majukumu  ya kusimamia masuala muhimu yanayohusu watumishi wao, hivyo Mpango wa Rasilimaliwatu na Urithishanaji Madaraka ni nyenzo muhimu katika usimamizi wa watumishi.

Amefafanua kuwa, bila kuwa na jitihada na mipango mahususi, Halmashauri zinaweza kuwa na watumishi wachache  wenye sifa na uwezo wa kujaza nafasi za madaraka pindi zitakapokuwa wazi, hivyo kuwepo kwa mipango hiyo kutawezesha  kusimamia rasilimaliwatu kwa utaratibu mzuri pamoja na kubaini mahitaji na upatikanaji  wa rasilimaliwatu kwa wakati.

“Halmashauri zinatakiwa kuwa na watumishi wa kutosha wenye sifa na uwezo unaotakiwa mahali pa kazi ili kuleta tija na kuboresha utendaji kazi kwa lengo la kutoa huduma bora kwa umma,” Bw. Kitenge amesisitiza.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Mkurugenzi Msaidizi Rasilimaliwatu – TAMISEMI, Bw. Marko Masaya, ameishukuru Ofisi ya Rais-UTUMISHI kwa kuandaa mafunzo hayo ambayo yatawasaidia kuandaa Mipango ya Rasilimaliwatu na Urithishanaji Madaraka kwa usahihi.

Bw. Masaya amemhakikishia Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais UTUMISHI kuwa Ofisi ya Rais – TAMISEMI kama wasimamizi wa Mamlaka ya Serikali za Mitaa watahakikisha maelekezo ya Ofisi ya Rais – UTUMISHI yanatekelezwa kikamilifu.

Akimkaribisha Kaimu Katibu Mkuu-UTUMISHI kufungua mafunzo hayo, Kaimu Mkurugenzi Idara ya Uendelezaji Rasilimaliwatu, Ofisi ya Rais – UTUMISHI, Dkt. Edith Lwiza amesema mafunzo hayo yanafanyika kwa muda wa wiki moja na yanashirikisha washiriki kutoka Halmashauri za Sekretarieti za Mikoa ya Mara, Kigoma, Singida na Dodoma.

Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Hassan Kitenge akifungua Mafunzo ya Kuandaa Mpango wa Rasilimaliwatu na Urithishanaji Madaraka kwa Maafisa Utumishi Waandamizi wa Halmashauri  za Mikoa ya Mara, Kigoma, Singida na Dodoma yanayofanyika katika Ukumbi wa VETA jijini Dodoma.


Kaimu Mkurugenzi Idara ya Uendelezaji Rasilimaliwatu Ofisi ya Rais – UTUMISHI, Dkt. Edith Lwiza, akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Hassan Kitenge kufungua Mafunzo ya Kuandaa Mpango wa Rasilimaliwatu na Urithishanaji Madaraka kwa Maafisa Utumishi Waandamizi wa Halmashauri za Mikoa ya Mara, Kigoma, Singida na Dodoma yanayofanyika katika Ukumbi wa VETA jijini Dodoma.


Baadhi ya washiriki wa Mafunzo ya Kuandaa Mpango wa Rasilimaliwatu na Urithishanaji Madaraka wakimsikiliza Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Hassan Kitenge (hayupo pichani) wakati akifungua mafunzo hayo yanayofanyika katika Ukumbi wa VETA jijini Dodoma.


Mwakilishi wa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Mkurugezi Msaidizi Rasilimaliwatu – TAMISEMI, Bw. Marko Masaya, akiishukuru Ofisi ya Rais-UTUMISHI kwa kuandaa Mafunzo ya Kuandaa Mpango wa Rasilimaliwatu na Urithishanaji Madaraka kwa Maafisa Utumishi Waandamizi wa Halmashauri za Mikoa ya Mara, Kigoma, Singida na Dodoma yanayofanyika katika Ukumbi wa VETA jijini Dodoma.


Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Hassan Kitenge akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa Mafunzo ya Kuandaa Mpango wa Rasilimaliwatu na Urithishanaji Madaraka kwa Maafisa Utumishi Waandamizi wa Halmashauri za Mikoa ya Mara, Kigoma, Singida na Dodoma yanayofanyika katika Ukumbi wa VETA jijini Dodoma.



SERIKALI YA AWAMU YA SITA IMEJIKITA KATIKA MISINGI YA HAKI ILI KILA MTANZANIA APATE HUDUMA STAHIKI KATIKA TAASISI ZA UMMA


Na. James K. Mwanamyoto-Dar es Salaam

Tarehe 20 Oktoba, 2021 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais, Samia Suluhu Hassan imejikita katika misingi ya utoaji haki ili kumuwezesha kila Mtanzania kupata huduma bora zinazotolewa na Taasisi za Umma nchini.

Mhe. Mchengerwa amesema hayo jana usiku jijini Dar es Salaam, wakati akimuwakilisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa kwenye Sherehe ya Kuadhimisha Siku ya Kuzaliwa Mtume Muhammad S. A. W iliyofanyika nje ya Msikiti wa Ibadhi jijini Dar es Salaam.

Mhe. Mchengerwa amesema, Rais wa Awamu ya Sita Mhe. Samia Suluhu Hassan anasisitiza sana viongozi na watendaji katika taasisi zote za umma kutenda haki ili wananchi wapate huduma stahiki.

“Mimi kama Waziri mwenye dhamana ya kumsaidia Mhe. Rais kusimamia Utumishi wa Umma na Utawala Bora ninawahakikishia kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita itajikita katika misingi ya haki ili kila mmoja wetu apate haki,” Mhe. Mchengerwa amesisitiza.

Ameongeza kuwa, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ambayo anaiongoza imeendelea na itaendelea kuwasisitiza viongozi na watumishi wote wa umma katika Taasisi za Umma kuhakikisha wanatenda haki ili wananchi wafurahie huduma zitolewazo na Serikali kupitia taasisi zake.

Mhe. Mchengerwa amewaomba Watanzania wote kila mmoja kwa imani yake kumuombea Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ili aweze kuwa na afya njema itakayomuwezesha kutimiza ndoto yake ya kuwaletea maendeleo Watanzania wote.

Aidha, Mhe. Mchengerwa amewata Watanzania wote kuilinda amani kwani Mtume Muhammad S. A. W aliwaasa binadamu wote bila kujali itikadi zao kiimani, kulinda amani na ndio maana Mhe. Rais Samia Suluhu mara kwa mara amekuwa mstari wa mbele kuwahimiza Watanzania wote kuilinda amani iliyopo.

“Amani ni lazima ianzie miongoni mwetu, ni lazima ianzie kwenye familia zetu, tulizungumze neno amani kwenye familia zetu na kwenye jamii yetu, na tukumbushane kuwa Tanzania ni yetu sote hivyo, tunao wajibu wa kuilinda amani tuliyonayo,” Mhe. Mchengerwa amefafanua.

Sanjari na hilo, Mhe. Mchengerwa amewahimiza Watanzania kuwa na mshikamano na kuthaminiana ili taifa liweze kupiga hatua haraka katika maendeleo.

Waziri Mchengerwa amesema, kumthamini mwanadamu mwenzio ni agizo la Mwenyezi Mungu na Mtume wake Muhammad S. A. W, hivyo Watanzania hatuna budi kuthaminiana kwani ni agizo la Mwenyezi Mungu Muumba wa Mbingu na Nchi.

Kuhusiana na janga la COVID 19, Mhe. Mchengerwa amesema kuwa, Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akiwasisitiza watanzania kupata chanjo ili kujikinga na janga hilo, hivyo amewaomba waumini wa dini zote kumuunga mkono Mhe. Rais kwa kupata chajo ya UVIKO 19 ili taifa liendelee kuwa na wananchi wenye afya bora ambao watashiriki vema katika shughuli mbalimbali za maendeleo.

Akitoa neno la shukrani kwa mgeni rasmi kwa niaba ya waandaaji wa Sherehe ya Kuadhimisha Siku ya Kuzaliwa Mtume Muhammad S. A. W, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda na Biashara Mhe. Suleiman A. Saddiq amesema, Rais wa Awamu ya Sita Mhe. Samia Suluhu Hassan ana nia njema na taifa lake.

Ameongeza kuwa, Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ana mipango madhubuti ya kuinua uchumi wa taifa letu ili wananchi wapate ajira, huduma nzuri za matibabu, shule na kujenga miundombinu itakayoliwezesha taifa kupiga hatua katika maendeleo na ndio maana anajenga mahusiano na wadau wa maendeleo duniani.

Sherehe hiyo ya Kuadhimisha Siku ya Kuzaliwa Mtume Muhammad S.A.W iliyofanyika tarehe 19 Oktoba, 2021 iliandaliwa na Mkurugenzi Mtendaji wa NIDA TEXTILE MILLS TANZANIA LIMITED Bw. Hamza Rafiq Pardesi.

 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akizungumza na waumini wa dini ya kiislam wakati wa Sherehe ya Kuadhimisha Siku ya Kuzaliwa Mtume Muhammad S.A.W iliyofanyika nje ya Msikiti wa Ibadhi jijini Dar es Salaam.

Waumini wa dini ya kiislam wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa (hayupo pichani) wakati wa Sherehe ya Kuadhimisha Siku ya Kuzaliwa Mtume Muhammad S.A.W iliyofanyika nje ya Msikiti wa Ibadhi jijini Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda na Biashara Mhe. Suleiman A. Saddiq akitoa neno la shukrani kwa Mhe. Mchengerwa kwa niaba ya waandaaji wa Sherehe ya Kuadhimisha Siku ya Kuzaliwa Mtume Muhammad S.A.W iliyofanyika nje ya Msikiti wa Ibadhi jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akishiriki dua ya kumuombea Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan wakati wa Sherehe ya Kuadhimisha Siku ya Kuzaliwa Mtume Muhammad S.A.W iliyofanyika nje ya Msikiti wa Ibadhi jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akiongoza zoezi la kukata keki katika Msikiti wa Ibadhi jijini Dar es Salaam iliyoandaliwa kwa ajili ya Kuadhimisha Siku ya Kuzaliwa Mtume Muhammad S.A.W.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akilishwa keki na Mkurugenzi Mtendaji wa NIDA TEXTILE MILLS TANZANIA LIMITED Bw. Hamza Rafiq Pardesi, iliyoandaliwa kwa ajili ya Kuadhimisha Siku ya Kuzaliwa Mtume Muhammad S.A.W.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akimlisha keki Mkurugenzi Mtendaji wa NIDA TEXTILE MILLS TANZANIA LIMITED Bw. Hamza Rafiq Pardesi, iliyoandaliwa kwa ajili ya Kuadhimisha Siku ya Kuzaliwa Mtume Muhammad S.A.W.


 

Tuesday, October 19, 2021

Sunday, October 17, 2021

DKT. NDUMBARO AWATAKA WAAJIRI KUWAPATIA HAKI KWA WAKATI WATUMISHI WANAOTEKELEZA WAJIBU WAO IPASAVYO

 Na. Veronica Mwafisi­­-ARUSHA

Tarehe 17 Oktoba, 2021

Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro amewataka Waajiri katika Taasisi za Umma kutekeleza azma ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuwapatia haki kwa wakati Watumishi wa Umma wanaotekeleza majukumu yao kikamilifu ili kuwajengea morali ya utendaji kazi.

Dkt. Ndumbaro ametoa wito huo jijini Arusha kwa nyakati tofauti wakati akizungumza na watumishi wa Chuo cha Ufundi Arusha (ATC) na Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) akiwa kwenye ziara yake ya kikazi, yenye lengo la kusikiliza na kutatua kero na changamoto zinazowakabili Watumishi hao wa umma.

Dkt. Ndumbaro amesema, suala la uzingatiaji wa haki za Watumishi wa Umma limepewa kipaumbele na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, hivyo viongozi katika Taasisi za Umma wanapaswa kutenda haki kwa watumishi walio chini yao ili watumishi hao waweze kufanya kazi kwa moyo na uzalendo.

Sanjari na hilo, Dkt. Ndumbaro amehimiza suala la uadilifu katika Utumishi wa Umma ambalo limepewa msisitizo na Serikali ya Awamu ya Sita hivyo amewataka viongozi katika taasisi zote za umma kuwa mfano wa kuigwa kwa uadilifu.

“Watumishi wa Umma tunapaswa kuwa waadilifu kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo iliyopo katika Utumishi wa Umma,” Dkt. Ndumbaro amesisitiza.

Aidha, Dkt. Ndumbaro amehimiza uwajibikaji katika Utumishi wa Umma kwa kuwataka viongozi na Watumishi wa Umma kuwajibika ipasavyo kwa Serikali iliyopo madarakani kwa wananchi wanaofuata huduma katika Taasisi za Umma.

“Serikali inawahimiza waajiri kuhakikisha Watumishi wa Umma wanafanya kazi kwa bidii, juhudi, maarifa na watambue mchango wa watumishi wanaofanya kazi kwa bidii,” Dkt. Ndumbaro amefafanua.

Kuhusiana na watumishi wanaoshindwa kutekeleza wajibu wao, Dkt. Ndumbaro amewataka waajiri kuwachukulia hatua stahiki ili wabadilike na kuendana na Kaulimbiu ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ya KAZI IENDELEE.

“Tuwachukulie hatua watumishi wote wanaobainika kutofanya kazi kwa bidii, tuwarekebishe kwa maneno au kuwaandikia barua, hivyo wasionewe haya kwani wataharibu taswira nzuri ya Utumishi wa Umma,” Dkt. Ndumbaro amesisitiza.

Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro amehitimisha ziara yake ya kikazi ya siku moja jijini Arusha, iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua kero na changamoto zinazowakabili Watumishi wa Umma wa Chuo cha Ufundi Arusha (ATC) na Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA).

Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro (katikati) akizungumza na watumishi wa Chuo cha Ufundi Arusha na Chuo cha Uhasibu Arusha kuhusu masuala ya kiutumishi wakati wa ziara yake ya kikazi jijini Arusha yenye lengo la kusikiliza na kutatua kero na changamoto zinazowakabili Watumishi hao.   


Baadhi ya Watumishi wa Chuo cha Ufundi Arusha wakimsikiliza Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro (aliyekaa katikati meza kuu) wakati wa ziara ya kikazi ya Katibu Mkuu huyo, iliyolenga kusikiliza na kutatua kero zinazowakabili watumishi wa chuo hicho.


Mtumishi wa Chuo cha Uhasibu Arusha, Bi. Anna Nyambo akiwasilisha changamoto yake ya kiutumishi kwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro (hayupo pichani) wakati wa ziara ya kikazi ya Katibu Mkuu huyo yenye lengo la kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa Chuo cha Uhasibu Arusha.


Mkuu wa Chuo cha Ufundi Arusha, Dkt. Musa Chacha (aliyenyoosha kidole) akimuonyesha Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro (aliyevaa kofia nyekundu) mchoro wa jengo la kituo cha afya katika Chuo cha Ufundi Arusha wakati wa ziara ya  kikazi ya Katibu Mkuu huyo iliyokuwa na lengo la kusikiliza na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa chuo hicho.


Afisa Utumishi wa Ofisi ya Rais - UTUMISHI, Bi. Salama Mohamed (aliyenyoosha mkono) akifafanua jambo kwa baadhi ya Watumishi wa Chuo cha Uhasibu Arusha waliowasilisha changamoto za masuala ya kiutumishi wakati wa ziara ya kikazi ya Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro (hayupo pichani) iliyolenga kutatua changamoto za watumishi wa Chuo cha Ufundi Arusha na Chuo cha Uhasibu Arusha. Kushoto kwake ni Afisa Utumishi, wa Ofisi ya Rais – UTUMISHI, Bw. Ally Ngowo.


Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro (katikati mstali wa mbele) akiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Chuo cha Ufundi Arusha mara baada ya kuzungumza nao wakati wa ziara yake ya kikazi jijini Arusha iliyokuwa na lengo la kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa chuo hicho. Kulia kwake ni Mkuu wa Chuo hicho cha Ufundi Arusha, Dkt. Musa Chacha.



Tuesday, October 12, 2021

MHESHIMIWA RAIS ANATAKA WATUMISHI WA UMMA KUFANYA KAZI KWA UADILIFU BILA KUSHINIKIZWA-Mhe. Mchengerwa

Na. James K. Mwanamyoto-Dodoma

Tarehe 12 Oktoba, 2021

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa amewataka Watumishi wa Umma kuwa na utamaduni wa kufanya kazi kwa uadilifu bila kushinikizwa wakati wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo, kama ambavyo Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akisisitiza.

Mhe. Mchengerwa ametoa wito huo leo ofisini kwake, wakati wa mkutano wake na Waandishi wa Habari uliolenga kutoa mrejesho wa masuala ya kiutumishi yaliyojitokeza wakati wa ziara yake ya kikazi aliyoifanya hivi karibuni katika Mikoa ya Mwanza, Mara na Simiyu.

Mhe. Mchengerwa amesema, Mhe. Rais amedhamiria kuwa na watendaji waadilifu, hivyo ofisi yake imejipajipanga kuhakikisha watumishi wote wa umma wanasimamia vema fedha zinazotolewa kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo.

Ameongeza kuwa, Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan atajisikia fahari kuona  Watumishi wa Umma wanatekeleza majukumu yao kikamilifu bila kushinikizwa na viongozi wao.

“Inawezekana wapo baadhi ya watumishi wanataka kutekeleza wajibu wao kwa kushinikizwa jambo ambalo Mhe. Rais halitaki kwani anataka kila mtumishi awajibike bila kusimamiwa,” Mhe. Mchengerwa amesisitiza.

Aidha, Mhe. Mchengerwa amewataka Watumishi wa Umma nchini kuzingatia maelekezo ya Mhe. Rais kuhusu utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO 19 aliyoyatoa tarehe 10 Oktoba, 2021.

Amewaasa Watumishi wa Umma kutekeleza mpango huo kwa weledi, uadilifu na uzalendo ili ukamilike kwa wakati na kuwa na manufaa kwa wananchi na maendeleo ya taifa kwa ujumla.

“Kama ambavyo Mhe. Rais amesisitiza, muda wa utekelezaji wa mpango huo ni miezi 9 tu, hivyo hakutakuwa na muda wa nyongeza,” Mhe. Mchengerwa amefafanua.

Mhe. Mchengerwa amesema, Watumishi wa Umma waliopewa dhamana ya kusimamia mradi huo wanapaswa kutekeleza mradi kwa weledi na uzalendo ili kumuenzi Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Mchango wa Watumishi wa Umma katika Utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO ni muhimu kwa maendeleo na ustawi wa taifa. 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa (wapili kutoka kulia) akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo pichani) leo jijini Dodoma kuhusu mrejesho wa masuala ya kiutumishi yaliyojitokeza wakati wa ziara yake ya kikazi aliyoifanya katika Mikoa ya Mwanza, Mara na Simiyu.


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.Deogratius Ndejembi (aliyesimama) akimkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa wakati wa kikao cha Mhe. Mchengerwa na Waandishi wa Habari kilichofanyika leo jijini Dodoma kuhusu mrejesho wa masuala ya kiutumishi yaliyojitokeza wakati wa ziara yake ya kikazi aliyoifanya katika Mikoa ya Mwanza, Mara na Simiyu. 


Baadhi ya Watendaji wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa alipokuwa akizungumza na Waandishi wa Habari leo jijini Dodoma kuhusu mrejesho wa masuala ya kiutumishi yaliyojitokeza wakati wa ziara yake ya kikazi aliyoifanya katika Mikoa ya Mwanza, Mara na Simiyu.


Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro (aliyesimama) akitoa neno la utangulizi kabla ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa kuzungumnza na Waandishi wa Habari leo jijini Dodoma kuhusu mrejesho wa masuala ya kiutumishi yaliyojitokeza wakati wa ziara yake ya kikazi aliyoifanya katika Mikoa ya Mwanza, Mara na Simiyu.