Na. Nasra H. Mondwe-Arusha
Tarehe 25 Oktoba, 2021
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa amewataka Viongozi na Watendaji wanaosimamia utekelezaji wa Awamu ya Nne ya Mradi wa Kupunguza Umaskini Tanzania kutekeleza mradi huo bila kujali itikadi za dini wala siasa kwani suala la maendeleo kwa wananchi halina ubaguzi.
Mhe. Mchengerwa ametoa
maelekezo hayo wakati akizindua kikao kazi cha utekelezaji wa Awamu ya Nne ya Mradi
wa Kupunguza Umaskini Tanzania kilichofanyika leo jijini Arusha.
Mhe. Mchengerwa amesema, utekelezaji
wa mradi huo utaendeleza na kuimarisha dhana ya uwazi, ukweli, ushirikishwaji
na uwajibikaji kwani Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Samia
Suluhu Hassan ina imani kuwa miradi ya kupunguza umaskini katika halmashauri
zetu itaboresha maisha ya wananchi wengi na kuimarisha ustawi wao.
Amewakumbusha washiriki wa
kikao kazi hicho kuwa, utekelezaji wa mradi huu unahitaji umakini mkubwa ili
kuhakikisha miradi ya kijamii inayotekelezwa inaonyesha thamani ya fedha, hivyo
amewataka wajumbe wazingatie maelekezo ili kuweza kufikia malengo
yaliyokusudiwa.
Mhe. Mchengerwa amewasisitiza
Viongozi na Watendaji kufanya kazi kwa weledi na kuzingatia miongozo iliyowekwa
ili kumuunga mkono Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ambaye amesimama kidete
kuhakikisha wananchi hususani wanyonge wanapata huduma bora za kijamii ili
kupunguza umaskini.
Akizungumzia juu ya matumizi
sahihi ya fedha zilizotolewa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo, Mhe.
Mchengerwa amemtaka Mkurugenzi Mtandaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF)
kuishirikisha Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) katika kila mkoa
ili kujiridhisha na uwepo wa tija ya miradi hiyo kwa wananchi na ni kwa namna
gani miradi hiyo itaweza kuwakomboa.
“Mimi kama Waziri wa Utawala
Bora, sitarajii kusikia ubadhirifu wa aina yoyote katika mikoa yote hiyo mitano
ambayo miradi hii imeilenga, na pia sitegemei kusikia TAKUKURU inakwenda kupambana
badala ya kwenda kuzuia ili tuweze kupata tija tuliyokusudia,” Mhe. Mchengerwa
amesisitiza.
Mhe. Mchengerwa amesema, ni
jukumu la kila mmoja katika mkoa na wilaya kufanya ufuatiliaji wa karibu na kwa
umakini mkubwa wa matumizi ya fedha ya kila mradi kwani utekelezaji wa miradi
hiyo ndio kipimo cha kila kiongozi na mtendaji kwenye ngazi ya mikoa na wilaya.
“Ni jukumu la kila Kiongozi,
Watendaji, Maafisa wote wa Halmashauri zote, Waratibu wa TASAF na Maafisa wa
TAKUKURU katika kila mkoa na wilaya kusimamia fedha za miradi zinazotolewa na Mhe.
Rais kwa lengo la kuzinyanyua kaya zilizo na hali ngumu na kuondosha mazingira
duni katika maeneo yao kwani hicho ndio kipimo chenu cha utendaji,” Mhe.
Mchengerwa amesisitiza.
Akimkaribisha Mhe. Mchengerwa
kuzindua Mradi huo, Mkuu wa Mkoa wa Arusha. Mhe. John Mongella amemshukuru Mhe.
Mchengerwa kwa kufanya uzinduzi katika Mkoa wa Arusha na kuahidi kufanyia kazi
maelekezo ambayo Mhe. Mchengerwa amekuwa akiyatoa sehemu mbalimbali juu ya
usimamizi mzuri wa miradi inayotekelezwa na Serikali.
Amesema Mhe. Samia amekuwa akifanya
mambo makubwa kwani amekuwa akitoa fedha nyingi hivyo, hawana budi kumuunga
mkono na kuahidi kuwa hakuna ubadhirifu wowote utakaotokea katika utekelezaji
wa miradi hiyo.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu
wa TASAF, Bw. Ladislaus Mwamanga ameleezea lengo la kikao kazi hicho kuwa ni kuelekezana
juu ya majukumu ya kila mmoja atakayeshiriki katika utekelezaji wa miradi hiyo
ili kufanikisha malengo yaliyokusudiwa.
Lengo la utekelezaji wa Awamu
ya Nne ya Mradi wa Kupunguza Umaskini Tanzania ni kuwakomboa wananchi dhidi ya
mazingira ya umaskini, maradhi na ujinga kwa kuboresha upatikanaji wa huduma za
kiuchumi, kijamii katika ngazi zote za jamii zilizo katika halmashauri.
Miradi itakayotekelezwa katika
awamu hiyo ni ujenzi na ukarabati wa vyumba vya madarasa, mabweni, zahanati,
vituo vya afya nyumba za watumishi wa vituo vya afya na walimu, ujenzi na
ukarabati wa vivuko, barabara za vijijini na vyanzo vya maji. Jumla ya miradi 1,500
itakatekelezwa katika wilaya 33 za Mikoa ya Arusha, Njombe, Simiyu, Geita na
Mwanza.
Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Mohamed Mchengerwa akizungumza na Viongozi na Watendaji watakaosimamia utekelezaji
wa Awamu ya Nne ya Mradi wa Kupunguza Umaskini Tanzania wakati wa uzinduzi wa
mradi huo uliofanyika leo jijini Arusha.
Baadhi ya
Viongozi na Watendaji wa Mkoa wa Arusha watakaotekeleza Awamu ya Nne ya Mradi
wa Kupunguza Umaskini Tanzania wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa
(hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao wakati akizindua Awamu ya Nne ya
Mradi wa Kupunguza Umaskini Tanzania leo jijini Arusha.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akiteta na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. John Mongella wakati wa uzinduzi wa Awamu ya Nne ya Mradi wa Kupunguza Umaskini Tanzania uliofanyika leo jijini Arusha.
Mkuu wa Mkoa
wa Arusha, Mhe. John Mongella akitoa maelezo ya awali kabla ya kumkaribisha Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Mohamed Mchengerwa kuzindua Awamu ya Nne ya Mradi wa Kupunguza Umaskini
Tanzania leo jijini Arusha.
Mkurugenzi
Mtendaji wa TASAF, Bw. Ladislaus Mwamanga akielezea lengo la Mradi wa Kupunguza
Umaskini Tanzania uliozinduliwa leo jijini Arusha na Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa.
Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Mohamed Mchengerwa akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi na Watendaji
watakaosimamia utekelezaji wa Awamu ya Nne ya Mradi wa Kupunguza Umaskini
Tanzania mara baada ya kunduzia mradi huo leo jijini Arusha.
No comments:
Post a Comment