Na. Nasra H. Mondwe-Arusha
Tarehe 26 Oktoba, 2021
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed
Mchengerwa amewataka Watunza Kumbukumbu na Nyaraka katika taasisi za umma
kutekeleza majukumu yao kwa weledi ili kujiepusha na uvujishaji wa siri za
serikali.
Mhe.
Mchengerwa ametoa wito huo
wakati akifungua Mkutano wa 9 wa Chama cha Taaluma ya Menejimenti ya Kumbukumbu
na Nyaraka Tanzania katika ukumbi wa ACC jijini Arusha.
Mhe.
Mchengerwa amesema, dhamana waliyonayo Watunza Kumbukumbu ni kubwa, hivyo ni
vema wakazingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za utunzaji wa kumbukumbu pamoja
na viapo vyao kwasababu utoaji wa siri za Serikali ni kosa kubwa kisheria na
kwa mujibu wa taratibu za Utumishi wa Umma.
Waziri
Mchengerwa amewaasa washiriki wa Mkutano huo kuhakikisha wanajiepusha na siasa na
mambo mengine yanayosababisha kutoa siri za Serikali.
Mhe.
Mchengerwa amesisitiza kuwa, Serikali ya Awamu Sita inayoongozwa na Mhe. Rais
Samia Suluhu Hassan inathamini mchango wa Watumishi wa Umma na itaendelea
kulinda maslahi yao ikiwa ni pamoja na kutatua changamoto zinazowakabili
Watunza Kumbukumbu, hivyo hakuna sababu ya watumishi kutoa siri za Serikali na
badala yake wanapaswa kuwa waadilifu kiutendaji na kuwa watiifu kwa Serikali
yao.
Akizungumzia
juu ya stahiki mbalimbali za Watumishi wa Umma, Mhe Mchengerwa amewaagiza
waajiri wote kuhakikisha wanalipa stahili zote za watumishi ikiwepo madai ya
malimbikizo ya mishahara na kuongeza kuwa wanapaswa kutenga muda wa kusikiliza
kero za watumishi na kuzitafutia uvumbuzi.
Mhe.
Mchengerwa amewasisitiza waajiri kuheshimu kada zote kwani kila kada ina
umuhimu wake katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku ya Serikali.
“Waajiri ziheshimuni kada zote, msidharau kada
za watu wa chini kwani hawa ni watu muhimu katika utekelezaji wa majukumu yetu
na sisi kama Serikali tutaendelea kuzipigania kada hizi,” Mhe. Mchengerwa
amesisitiza.
Akimkaribisha
Mhe. Mchengerwa kufungua mkutano huo, Mwenyekiti wa Chama cha Taaluma ya Menejimenti
ya Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania (TRAMPA), Bi. Josephine Manase amesema lengo
la chama chao ni kujengeana uwezo na kupeana hamasa ya utekelezaji wa majukumu
kwa ufanisi ili kutoa mchango katika utekelezaji wa majukumu ya Serikali ya kila
siku.
Aidha,
Bi. Manase amemuomba Mhe. Mchengerwa kwa nafasi ya uongozi aliyonayo kukisaidia
chama chake kumuomba Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kuwa Mgeni Rasmi katika
Mkutano ujao wa 10 wa Chama cha Taaluma ya Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka
Tanzania utakaofanyika Zanzibar, ikizingatiwa kuwa kazi ya kwanza ya Mhe. Rais
ilikuwa ni ya utunzaji wa kumbukumbu Serikalini.
Mkutano
huo wa siku tatu unaongozwa na kauli mbiu isemayo “Imarisha Utunzaji wa
Kumbukumbu na Nyaraka ili kuwezesha Uwazi, Uwajibikaji na Utawala Bora katika
Kutoa Huduma kwa Umma.”
Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akizungumza na washiriki
wa mkutano mkuu wa 9 wa Chama cha Taaluma ya Menejimenti ya Kumbukumbu na
Nyaraka Tanzania alipokuwa akifungua mkutano huo jijini Arusha.
Baadhi ya washiriki
wa mkutano mkuu wa 9 wa Chama cha Taaluma ya Menejimenti ya Kumbukumbu na
Nyaraka Tanzania wakimsikiliza Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Mohamed Mchengerwa (hayupo pichani) alipokuwa akifungua mkutano huo jijini
Arusha.
Mwenyekiti
wa Chama cha Taaluma ya Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania, Bi.
Josephine Manase akielezea lengo la mkutano wa chama chao kabla ya kumkaribisha
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,
Mhe. Mohamed Mchengerwa kufungua mkutano mkuu wa 9 wa
Chama cha Taaluma ya Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania jijini
Arusha.
Katibu wa Chama
cha Taaluma ya Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania, Bw. Francis
Mathias akitambulisha makundi ya washiriki wa mkutano wa mkuu wa 9 wa Chama cha
Taaluma ya Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania jijini Arusha.
Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Mohamed Mchengerwa akipokea tuzo kutambua mchango wake wa kuunga mkono juhudi
za utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka katika Utumishi wa Umma wakati wa mkutano
mkuu wa 9 wa Chama cha Taaluma ya Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania
jijini Arusha.
Naibu Katibu
Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt.
Francis Michael akipokea cheti kwa niaba ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora cha kutambua mchango wa Ofisi hiyo kwa Watunza
Kumbukumbu na Nyaraka wakati wa mkutano mkuu wa 9 wa Chama cha Taaluma ya
Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania jijini Arusha.
Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Mohamed Mchengerwa akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Watendaji kutoka
taasisi za umma walioshiriki mkutano mkuu wa 9 wa Chama cha Taaluma ya
Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania mara baada ya kufungua mkutano
huo jijini Arusha.
No comments:
Post a Comment