Wednesday, July 29, 2020

HAYATI MKAPA ALIKUWA MTUMISHI WA UMMA KWA NYADHIFA MBALIMBALI


Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro akisoma wasifu wa Hayati Benjamin William Mkapa wakati wa Ibada ya mazishi ya Rais Mstaafu huyo wa Awamu ya Tatu yaliyofanyika kijiji cha Lupaso mkoani Mtwara, amesema hayati Benjamin William Mkapa aliutumikia umma katika nyadhifa mbalimbali hivyo atakumbukwa na Watanzania wote kwa utumishi wake uliotukuka.

Dkt. Ndumbaro alifafanua kuwa, Hayati Benjamin William Mkapa alianza kazi rasmi Serikalini kama Afisa Tawala katika Wilaya ya Dodoma, Mkoani Dodoma mnamo Mwezi Aprili, 1962 kabla ya kujiunga na masomo ya Shahada ya Uzamili ya Diplomasia katika Chuo Kikuu cha Columbia nchini Marekani.

Alisema, mara baada ya kuhitimu shahada hiyo ya Uzamili nchini Marekani, Hayati Mkapa alirejea nchini na kufanya kazi katika Wizara ya Mambo ya Nje kwenye Dawati la Afrika akiwa na cheo cha Afisa wa Mambo ya Nje.

Aliainisha kuwa, akiwa Afisa wa Mambo ya Nje, miongoni mwa kazi alizokuwa akizifanya ni pamoja na kuchukua muhtasari wa mazungumzo ya Waziri wa Mambo ya Nje au Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anapokuwa na wageni.

Dkt. Ndumbaro aliongeza kuwa, sehemu kubwa ya utumishi wa Hayati Benjamin William Mkapa Serikalini, alihudumu kama kiongozi katika nyadhifa mbalimbali ambapo mnamo Aprili, 1972 aliteuliwa kuwa Mhariri Mtendaji wa kwanza wa Magazeti ya Serikali ya Kiingereza ya Daily News na Sunday News.

Dkt. Ndumbaro alisema, mwaka 1974 hadi 1976  Hayati Benjamin William Mkapa aliteuliwa kuwa Mwandishi wa Habari wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kazi ambayo aliifanya kwa ufanisi mkubwa na mnamo mwaka 1976 aliteuliwa kuanzisha Shirika la Habari Tanzania (SHIHATA) na kuhudumu katika shirika hilo kama Mkurugenzi  Mkuu wa Shirika.

Sanjali na nafasi hizo, mwaka 1977 Hayati Benjamin William Mkapa aliteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na kufanikiwa kuiongoza Wizara hiyo kwa miaka mitatu, na mwaka 1982 alihudumu kama Balozi wa Tanzania nchini Canada na ilipofika mwaka  1983 alihamishiwa nchini Marekani kuwa Balozi wa Tanzania nchini humo ambako alifanya kazi hiyo hadi mwaka 1984.

Kutokana na utendaji kazi mzuri wa Hayati Benjamin William Mkapa, mnamo mwaka 1984 aliteuliwa tena kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na kufanikiwa kufanya kazi hiyo kwa miaka sita hadi mwaka 1990 alipoteuliwa tena kuwa Waziri wa Habari na Utangazaji na kuifanya kazi hiyo hadi mwaka 1992.

Aidha, Dkt. Ndumbaro alisema, Mwaka 1992 Hayati Benjamin William Mkapa alihudumu kama Waziri wa Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Juu wadhifa alioutumikia hadi mwaka 1995 alipoamua kugombea na akashinda Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro akisoma wasifu wa Rais Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Hayati Benjamin William Mkapa  wakati wa mazishi ya Hayati Mkapa Kijijini Lupaso mkoani Mtwara.


HAYATI MKAPA ALICHUKIA SANA RUSHWA NA UMASKINI NA KUAMUA KUANZISHA TAKUKURU, TASAF NA MKURABITA 

Na Mary Mwakapenda- Masasi

Tarehe 29 Julai, 2020

Hayati Benjamin William Mkapa wakati wa utawala wake pamoja na mambo mengine aliyoyafanya kwa manufaa ya Taifa, atakumbumbukwa na watanzania kwa kuchukia rushwa na umaskini na  hatimaye kuanzisha Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) na Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA) ambapo kwa kiwango kikubwa TAKUKURU imesaidia kupambana na Rushwa wakati  TASAF na MKURABITA zimeboresha maisha ya wananchi wenye kipato cha chini.

Hayo yamesemwa jana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt. (Mst) Mhe. George Huruma Mkuchika (Mb) kijijini Lupaso-Masasi alipokuwa akikagua maandalizi ya sehemu ambayo mwili wa Hayati Mkapa utapumzishwa.

Akifafanua kwa undani sababu za Hayati Mkapa kuanzisha Taasisi hizo, Mhe. Mkuchika amesema kuwa, alichukia sana rushwa, hivyo alimteua Mhe. Jaji Joseph Sinde Warioba kufanya utafiti ili kujua sababu za rushwa, mianya ya rushwa na nini kifanyike kuzuia rushwa nchini na matokeo ya utafiti huo yakawa ni chachu ya kuanzisha na kuimarishwa kwa TAKUKURU.

Mhe. Mkuchika ameongeza kuwa, Hayati Mkapa alichukia sana umasikini na aligundua kwamba Watanzania wengi waliishi maisha duni ya mlo mmoja kwa siku, hivyo aliwasisitiza wananchi kupambana na umaskini na kwa huruma yake alianzisha Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) ili kuzisaidia kaya maskini, Mfuko ambao uliendelezwa na Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete na sasa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ambaye hivi karibuni alizindua Sehemu ya Pili ya Awamu ya Tatu ya Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini.

Aidha, amesema, Hayati Mkapa alianzisha MKURABITA ili wananchi wapate Hati za Hatimiliki za Kimila zinazotolewa kwa Mujibu wa Sheria Na. 5 ya Ardhi ya Vijiji ya Mwaka 1999 ambazo zinawawezesha kujipatia mikopo kwenye taasisi za kifedha na kujikwamua kiuchumi.

Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Hayati Benjamin William Mkapa alifariki dunia tarehe 23/07/2020 na anazikwa leo Kijijini kwake Lupaso-Masasi, Mkoani Mtwara.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt. (Mst) Mhe. George Huruma Mkuchika (Mb) akisaini Kitabu cha Maombolezo Kijijini Lupaso - Masasi nyumbani kwa Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Hayati Benjamini William Mkapa aliyefariki dunia tarehe 23/7/2020.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt. (Mst) Mhe. George Huruma Mkuchika (Mb) akiwaeleza Waandishi wa Habari Kijijini Lupaso - Masasi kuhusu jitihada alizozifanya    Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Hayati Benjamin William Mkapa katika kupambana na rushwa na umaskini nchini. 


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt. (Mst) Mhe. George Huruma Mkuchika akimsikiliza Bw. Dunstan Mkapa ambaye ni Mdogo wa Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Hayati Benjamini William Mkapa, wakati akizungumza nae Kijijini Lupaso – Masasi. Kushoto kwake ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Mtwara, Bw. Alphayo Kidata.




Sunday, July 12, 2020