Saturday, April 30, 2022

OFISI YA RAIS - UTUMISHI INAWATAKIA WATUMISHI WA UMMA SHEREHE NJEMA YA SIKU YA WAFANYAKAZI DUNIANI (MEI MOSI) 2022

 


MHE. NDEJEMBI AIELEKEZA e-GA KUZICHUKULIA HATUA TAASISI ZINAZOKIUKA SHERIA YA SERIKALI MTANDAO


Na. James K. Mwanamyoto-Dodoma

Tarehe 30 Aprili, 2022

Naibu Waziri,Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Deogratius Ndejembi ameitaka Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) kuzichukulia hatua stahiki taasisi zote za umma zinazokiuka matakwa ya Sheria ya Serikali Mtandao Na. 10 ya mwaka 2019.

Mhe. Ndejembi ametoa maelekezo hayo jijini Dodoma alipokuwa akifunga kikao kazi cha Wakuu wa Idara na Vitengo vya TEHAMA Serikalini kilichohusu mafunzo ya uzingatiaji wa Sheria na Kanuni za Serikali Mtandao.

Mhe. Ndejembi amesema e-GA ni mamlaka kamili hivyo, inapaswa kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa sheria pale inapoona taasisi za umma zinajenga mifumo ya TEHAMA bila kibali cha mamlaka hiyo au zinapokiuka Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo ya Serikali Mtandao.

e-GA mna meno kisheria hivyo anzeni kuitekeleza Sheria ya Serikali Mtandao kwa vitendo kwa kuzichukulia hatua mara moja taasisi zote zinakwenda kinyume na sheria hiyo,” Mhe. Ndejembi amesisitiza.

Akizungumzia malalamiko ya upatikanaji wa mtandao kwenye baadhi ya maeneo, Mhe. Ndejembi amewataka Wakuu wa Idara na Vitengo vya TEHAMA kutafuta suluhisho la changamoto hiyo ambayo wananchi wamekuwa wakiilalamikia pindi wanapohitaji huduma zinazotolewa na Taasisi za Umma kupitia mifumo ya TEHAMA.

“Unakuta mwananchi anatembea umbali mrefu kufuata huduma ya kulipa kodi kwa manufaa ya taifa, halafu anaambiwa mtandao hakuna kwani mfumo haufanyi kazi, na wakati mwingine kwenye halmashauri zetu kutengeneza namba ya malipo mwananchi anaambiwa mtandao uko chini jambo ambalo linakwamisha utoaji wa huduma,” Mhe. Ndejembi amefafanua.

Ameongeza kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita kipaumbele chake kikubwa ni kuwa na Serikali ya Kidijitali itakayoondoa changamoto ya wananchi kutopata huduma bora na kwa wakati, hivyo amewaasa wataalam wa TEHAMA kutumia ujuzi wao katika kujenga mifumo imara itakayoboresha utoaji wa huduma Serikalini.

Kwa upande wake, Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Hassan Kitenge amesema, kikao kazi hicho cha wataalam wa TEHAMA kinadhihirisha dhamira ya ofisi yake kupitia mamlaka ya Serikali Mtandao kuwa na jukwaa la kudumu la kukumbushana mkakati wa kuhakikisha TEHAMA inatumika ipasavyo kurahisisha utendaji kazi wa  taasisi za Serikali kwa lengo la kuboresha huduma zinazotolewa kwa wananchi.

Naye, Mkurugenzi Mkuu, Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) Mhandisi Benedict Ndomba amemhakikishia Mhe. Ndejembi kuwa, e-GA itaendelea kutekeleza jukumu lake la msingi la kuratibu, kusimamia na kukuza jitihada za serikali mtandao kwa taasisi za umma na kuhimiza uzingatiaji wa sera, sheria, kanuni na miongozo ya Serikali Mtandao.

Kikao kazi hicho cha siku mbili kimehudhuriwa na Wakurugenzi wa TEHAMA wa Wizara, Wakuu wa TEHAMA wa Idara Zinazojitegemea, Mamlaka na Wakala za Serikali, Wakuu wa Vitengo vya TEHAMA wa Mikoa, Majiji na Manispaa, Wakuu wa Vitengo vya TEHAMA wa Halmashauri za Wilaya na Wakuu wa TEHAMA wa Taasisi za Umma.


 Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akifunga kikao kazi cha Wakuu wa Idara na Vitengo vya TEHAMA Serikalini kilichofanyika jijini Dodoma.

Baadhi ya Wakuu wa Idara na Vitengo vya TEHAMA Serikalini wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (hayupo pichani) alipokuwa akifunga kikao kazi chao kilichofanyika jijini Dodoma.


Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Hassan Kitenge akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Naibu Waziri Mhe. Deogratius Ndejembi kufunga kikao kazi cha Wakuu wa Idara na Vitengo vya TEHAMA Serikalini kilichofanyika jijini Dodoma.

   

Mkurugenzi Mkuu, Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) Mhandisi Benedict Ndomba akielezea majukumu ya taasisi yake kwa Naibu Waziri Mhe. Deogratius Ndejembi (hayupo pichani) kabla ya Naibu Waziri huyo kufunga kikao kazi cha Wakuu wa Idara na Vitengo vya TEHAMA Serikalini kilichofanyika jijini Dodoma.


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Deogratius Ndejembi (wa kwanza kulia) akiteta na watendaji wa ofisi yake kabla ya kufunga kikao kazi cha Wakuu wa Idara na Vitengo vya TEHAMA Serikalini kilichofanyika jijini Dodoma.

Friday, April 29, 2022

BW. HASSAN SHAIBU MFANYAKAZI HODARI WA OFISI YA RAIS - UTUMISHI KWA MWAKA 2021/2022

 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akiwasalimia watumishi wa Ofisi yake jijini Dodoma kabla ya kuanza kwa kikao cha kumchagua mfanyakazi hodari wa Ofisi hiyo kwa mwaka 2021/2022.  

Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa umma, Dkt. Laurean Ndumbaro akizungumza na watumishi wa ofisi yake kwenye kikao cha kumchagua mfanyakazi hodari wa Ofisi hiyo kwa mwaka 2021/2022. 

Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa umma na Utawala Bora, Bw. Mussa Magufuli akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Katibu Mkuu, ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa umma, Dkt. Laurean Ndumbaro kuzungumza na watumishi wa ofisi hiyo wakati wa kikao cha kumchagua mfanyakazi hodari wa Ofisi hiyo kwa mwaka 2021/2022. 


Sehemu ya Wakurugenzi wa Idara na Vitengo wa Ofisi ya Rais Memeijimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, wakimsikiliza Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa umma, Dkt. Laurean Ndumbaro (hayupo pichani) kwenye kikao cha kumchagua mfanyakazi hodari wa Ofisi hiyo kwa mwaka 2021/2022.

Sehemu ya Watumishi wa Ofisi ya Rais Memeijimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wakimsikiliza Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa umma, Dkt. Laurean Ndumbaro (hayupo pichani) alipokuwa akimtangaza mfanyakazi hodari wa Ofisi yake kwa mwaka 2021/2022.

 

Mfanyakazi hodari wa Ofisi ya Rais Memeijimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Bw. Hassan Shaibu akiwa amesimama mbele ya Watumishi wenzake kuwashukuru mara baada ya kuchaguliwa kuwa mfanyakazi hodari wa Ofisi hiyo kwa mwaka 2021/2022.  

Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt.Laurean Ndumbaro (wapili kutoka kushoto) akiwaongoza wasimamizi waliokuwa wakizihesabu kura baada ya kumchagua mfanyakazi hodari wa ofisi yake.  Kulia kwake ni Mkurugenzi wa Utawala Rasilimaliwatu Bw. Mussa Magufuli na kushoto kwake ni Mwakilishi wa TUGHE Tawi la Utumishi Bi. Mwadawa Nchemwa.

Baadhi ya watumishi wa Ofisi ya Rais - Memeijimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wakimpongeza mtumishi mwenzao Bw. Hassan Shaibu (watatu kutoka kushoto) baada ya kutangazwa kuwa mfanyakazi hodari wa ofisi hiyo kwa mwaka 2021/2022. 


Mwakilishi wa TUGHE Tawi la Ofisi ya Rais - UTUMISHI Bi. Mwadawa Nchemwa akiwafahamisha watumishi wa Ofisi hiyo vigezo vya kumpata mfanyakazi hodari wakati wa kikao cha kuchagua mfanyakazi hodari wa Ofisi hiyo kwa mwaka 2021/2022.  Wakwanza kulia kwake ni Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt.Laurean Ndumbaro na wapili kulia ni Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu Bw. Mussa Magufuli.

Mmoja kati wa wasimamizi wa uchaguzi wa kumpata mfanyakazi hodari wa   Ofisi ya Rais Memeijimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Elibariki Kahungya akigawa karatasi za kupigia kura kwa ajili ya kumpata mtumishi mfanyakazi hodari wa Ofisi hiyo kwa mwaka 2021/2022.