Na. James K. Mwanamyoto-Dodoma
Tarehe 30 Aprili, 2022
Naibu Waziri,Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Deogratius Ndejembi ameitaka
Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA)
kuzichukulia hatua stahiki taasisi zote za umma zinazokiuka matakwa ya Sheria
ya Serikali Mtandao Na. 10 ya mwaka 2019.
Mhe. Ndejembi ametoa maelekezo
hayo jijini Dodoma alipokuwa akifunga kikao kazi cha Wakuu wa Idara na Vitengo
vya TEHAMA Serikalini kilichohusu mafunzo ya uzingatiaji wa Sheria na Kanuni za
Serikali Mtandao.
Mhe. Ndejembi amesema e-GA ni mamlaka kamili hivyo, inapaswa
kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa sheria pale inapoona taasisi za umma zinajenga
mifumo ya TEHAMA bila kibali cha mamlaka hiyo au zinapokiuka Sheria, Kanuni, Taratibu
na Miongozo ya Serikali Mtandao.
“e-GA mna meno kisheria hivyo anzeni kuitekeleza Sheria ya Serikali
Mtandao kwa vitendo kwa kuzichukulia hatua mara moja taasisi zote zinakwenda
kinyume na sheria hiyo,” Mhe. Ndejembi amesisitiza.
Akizungumzia malalamiko ya
upatikanaji wa mtandao kwenye baadhi ya maeneo, Mhe. Ndejembi amewataka Wakuu
wa Idara na Vitengo vya TEHAMA kutafuta suluhisho la changamoto hiyo ambayo wananchi
wamekuwa wakiilalamikia pindi wanapohitaji huduma zinazotolewa na Taasisi za
Umma kupitia mifumo ya TEHAMA.
“Unakuta mwananchi anatembea
umbali mrefu kufuata huduma ya kulipa kodi kwa manufaa ya taifa, halafu
anaambiwa mtandao hakuna kwani mfumo haufanyi kazi, na wakati mwingine kwenye
halmashauri zetu kutengeneza namba ya malipo mwananchi anaambiwa mtandao uko
chini jambo ambalo linakwamisha utoaji wa huduma,” Mhe. Ndejembi amefafanua.
Ameongeza kuwa, Serikali ya
Awamu ya Sita kipaumbele chake kikubwa ni kuwa na Serikali ya Kidijitali itakayoondoa
changamoto ya wananchi kutopata huduma bora na kwa wakati, hivyo amewaasa wataalam
wa TEHAMA kutumia ujuzi wao katika kujenga mifumo imara itakayoboresha utoaji
wa huduma Serikalini.
Kwa upande wake, Kaimu Katibu
Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Hassan Kitenge
amesema, kikao kazi hicho cha wataalam wa TEHAMA kinadhihirisha dhamira ya
ofisi yake kupitia mamlaka ya Serikali Mtandao kuwa na jukwaa la kudumu la
kukumbushana mkakati wa kuhakikisha TEHAMA inatumika ipasavyo kurahisisha
utendaji kazi wa taasisi za Serikali kwa
lengo la kuboresha huduma zinazotolewa kwa wananchi.
Naye, Mkurugenzi Mkuu, Mamlaka
ya Serikali Mtandao (e-GA) Mhandisi
Benedict Ndomba amemhakikishia Mhe. Ndejembi kuwa, e-GA itaendelea kutekeleza
jukumu lake la msingi la kuratibu, kusimamia na kukuza jitihada za serikali
mtandao kwa taasisi za umma na kuhimiza uzingatiaji wa sera, sheria, kanuni na
miongozo ya Serikali Mtandao.
Kikao kazi hicho cha siku
mbili kimehudhuriwa na Wakurugenzi wa TEHAMA wa Wizara, Wakuu wa TEHAMA wa Idara
Zinazojitegemea, Mamlaka na Wakala za Serikali, Wakuu wa Vitengo vya TEHAMA wa
Mikoa, Majiji na Manispaa, Wakuu wa Vitengo vya TEHAMA wa Halmashauri za Wilaya
na Wakuu wa TEHAMA wa Taasisi za Umma.
Baadhi ya Wakuu wa Idara na Vitengo vya TEHAMA Serikalini wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (hayupo pichani) alipokuwa akifunga kikao kazi chao kilichofanyika jijini Dodoma.
Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa
Umma, Bw. Hassan Kitenge akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Naibu Waziri Mhe. Deogratius
Ndejembi kufunga kikao kazi cha Wakuu wa Idara na Vitengo vya TEHAMA Serikalini
kilichofanyika jijini Dodoma.
Mkurugenzi Mkuu, Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA)
Mhandisi Benedict Ndomba akielezea majukumu ya taasisi yake kwa Naibu Waziri
Mhe. Deogratius Ndejembi (hayupo pichani) kabla ya Naibu Waziri huyo kufunga
kikao kazi cha Wakuu wa Idara na Vitengo vya TEHAMA Serikalini kilichofanyika
jijini Dodoma.
No comments:
Post a Comment