Na. Veronica Mwafisi-Arusha
Tarehe 8 Aprili, 2022
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amewataka
Waratibu wa TASAF kuwasilisha Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU)
idadi ya miradi ya TASAF iliyoibuliwa katika maeneo yao na thamani ya fedha inayotumika
katika kutekeleza miradi hiyo kwa ajili ya ufuatiliaji ili fedha zilizotolewa
zitumike kama ilivyokusudiwa kwa maendeleo ya taifa.
Mhe. Ndejembi ametoa maelekezo
hayo leo jijini Arusha wakati wa kikao kazi chake na Wakuu wa Wilaya za Mkoa wa
Arusha, Wakurugenzi, Waratibu wa TASAF, Wahasibu wa TASAF na Maafisi
Ufuatiliaji kilicholenga kuhimiza usimamizi mzuri wa fedha za miradi ya TASAF
mkoani Arusha.
Mhe. Ndejembi amesema TAKUKURU
ni lazima washirikishwe ili kujua namna fedha hizi zinavyotumika, hivyo ni
lazima kwa wanaohusika na fedha hizi wawe wazalendo kwa maslahi ya taifa lao na
thamani halisi ya fedha ionekene kwenye miradi iliyotekelezwa na kuongeza kuwa
kwa yeyote atakayeleta mzaha atachukuliwa hatua.
Mhe. Ndejembi amesema shilingi
bilioni 3 zimetolewa katika Mkoa wa Arusha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi
ya TASAF, hivyo amewataka Viongozi na Watendaji wa mkoa huo kuzisimamia
kikamilifu ili malengo yaliyowekwa ya wananchi kunufaika na miradi hii ifikiwe
na pia mikoa ambayo haikupata fedha hizo iweze kunufaika.
“Lengo lililonileta hapa leo
ni kuhusu usimamizi wa hizi shilingi bilioni 3 zilizoletwa na Serikali katika
mkoa huu, nimekuja kuona ni namna gani mtazitumia ili kutekeleza miradi ya
maendeleo nchini,” Mhe. Ndejembi amesisitiza.
Aidha, Mhe. Ndejembi amesema miradi ambayo wananchi wanachangia nguvu zao katika kuiendeleza iwekwe wazi ili kutofautisha gharama ambazo Serikali imetoa na mchango wa wananchi katika miradi hiyo.
Mhe. Ndejembi ameongeza kuwa,
katika kuibua miradi ni vizuri kuangalia mahitaji ya wananchi katika eneo
husika na endapo hitaji limeshatekelezwa basi ni vema kuangalia hitaji lingine kwa
kuzingatia taratibu zilizopo.
“Kama hitaji lilikuwa ni
kujenga madarasa, na tayari yameshajengwa, basi tuangalie mahitaji mengine ya
wananchi, unaweza kubadili mradi kwa kufuata taratibu, tuwasaidie wananchi kuibua
miradi ambayo ni endelevu,” Mhe. Ndejembi amesisitiza.
Sanjari na hayo, Mhe. Ndejembi
amewataka Waratibu hao wa TASAF kuhakikisha miradi yote iliyoibuliwa iwe
imekamilika ifikapo tarehe 30 Mei, 2022.
Mikoa mitano ambayo ni Geita,
Mwanza, Simiyu, Arusha na Njombe ndiyo iliyonufaika na fedha za miradi ya TASAF
Awamu ya Nne iliyotolewa kwa
ajili ya ukarabati wa vyumba na madarasa, mabweni, zahanati, vituo vya afya,
nyumba za watumishi wa vituo vya afya na walimu, ujenzi wa ukarabati wa vivuko,
barabara za vijijini na vyanzo vya maji.
Naibu
Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Deogratius Ndejembi akizungumza na Viongozi na Watendaji wa Mkoa wa Arusha
kuhusu usimamizi mzuri wa fedha za miradi ya TASAF inayotolewa na Serikali
wakati wa Kikao Kazi chake na Viongozi hao leo jijini Arusha.
Sehemu
ya Viongozi na Watendaji wa Mkoa wa Arusha wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya
Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi
leo jijini Arusha alipokuwa akizungumza nao
kuhusu usimamizi mzuri wa fedha za miradi ya TASAF mkoani humo.
Kaimu
Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha, Bw. Saidi Mabiye akitoa neno la utangulizi
kabla ya kumkaribisha Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa
Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi kuzungumza na Viongozi na
Watendaji wa Mkoa wa Arusha kuhusu usimamizi mzuri wa fedha za miradi ya TASAF
inayotolewa na Serikali.
Naibu
Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Deogratius Ndejembi akimsikiliza Mratibu wa TASAF (hayupo pichani) alipokuwa
akielezea miradi iliyokwisha kutekelezwa katika Mkoa wa Arusha wakati wa kikao
kazi cha Naibu Waziri huyo na Viongozi na Watendaji kuhusu usimamizi mzuri wa
fedha za miradi ya TASAF.
Mratibu
wa TASAF wa Halmashauri ya Wilaya ya Meru, Bi. Ritha Patrick akiainisha idadi
ya miradi ya TASAF iliyoibuliwa katika eneo lake analolisimamia kwa Naibu
Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Deogratius Ndejembi wakati wa kikao kazi chake na Viongozi na Watendaji wa Mkoa
wa Arusha juu ya usimamizi mzuri wa fedha za miradi ya TASAF.
No comments:
Post a Comment