Na. James K.
Mwanamyoto-Dodoma
Tarehe 11 Aprili, 2022
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama ameielekeza
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kushirikiana na Mamlaka ya
Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar (ZAECA) katika mapambano dhidi ya
rushwa ili kujenga taifa lenye maadili.
Mhe. Jenista ametoa maelekezo
hayo jijini Dodoma alipokuwa akizungumza na Watumishi wa TAKUKURU na ujumbe
kutoka Mamlaka ya ZAECA ulipomtembelea ofisini kwake kujitambulisha.
Mhe. Jenista amesema
ushirikiano anaoutaka uwe umejikita katika kujenga na kuimarisha utendaji kazi
wa TAKUKURU na ZAECA ili kuwa na mafanikio makubwa katika mapambano dhidi ya
rushwa.
“Ninaomba ushirikiano huo
ujikite zaidi katika kubadilishana uzoefu kwenye uchunguzi wa vitendo vya
rushwa, uendeshaji wa mashtaka na kuzuia vitendo vya rushwa,” Mhe. Jenista
amesisitiza.
Mhe. Jenista amesema
ushirikiano katika kupambana na rushwa hauepukiki kwani changamoto ya vitendo
vya rushwa ni suala mtambuka ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania licha ya
utofauti wa sheria zinazoongoza taasisi hizi mbili za TAKUKURU na ZAECA katika
mapambano dhidi ya rushwa, hivyo kuna ulazima wa kuwa na mbinu na mikakati ya
pamoja itakayoliwezesha taifa kupambana na vitendo vya rushwa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi
Mkuu wa ZAECA, Kamishna wa Polisi, Ahmed Makarani amesema amepokea ushauri wa Mhe.
Jenista wa kufanya kazi kwa ushirikiano na TAKUKURU na kuahidi kuuzingatia
katika utendaji kazi wao wa kila siku ili kufanikiwa katika mapambano dhidi ya
rushwa.
Ujumbe kutoka Mamlaka ya
Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar (ZAECA) uko jijini Dodoma kwa ziara ya
kikazi ya siku mbili yenye lengo la kubadilishana uzoefu wa utendaji kazi na
TAKUKURU ili kukabiliana na vitendo vya rushwa nchini.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala
Bora, Mhe. Jenista Mhagama akizungumza jijini Dodoma na Watendaji wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na
Rushwa (TAKUKURU) na ujumbe kutoka Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi
Zanzibar (ZAECA) uliomtembelea ofisini kwake kwa lengo la kujitambulisha.
Watendaji wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na Ujumbe
kutoka Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar (ZAECA) wakimsikiliza
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,
Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani) uliomtembelea jijini Dodoma kwa lengo la kujitambulisha.
Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma Bw.
Xavier Daudi akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista
Mhagama kuzungumza na Watendaji wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(TAKUKURU) na ujumbe kutoka Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar
(ZAECA) uliomtembelea ofisini kwake jijini Dodoma kwa lengo la kujitambulisha.
Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Bi. Neema Mwakalyelye akitambulisha
ujumbe kutoka Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar (ZAECA) kwa
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,
Mhe. Jenista Mhagama ulipomtembelea Waziri huyo ofisini kwake jijini Dodoma kwa
lengo la kujitambulisha.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na
Uhujumu Uchumi Zanzibar, Kamishna wa Polisi Ahmed Makarani akitoa neno la
shukrani kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama
wakati Watendaji wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na ujumbe
kutoka Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar (ZAECA) ulipomtembelea
ofisini kwake jijini Dodoma kwa lengo la kujitambulisha.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala
Bora, Mhe. Jenista Mhagama akiwa katika picha ya pamoja na Watendaji wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana
na Rushwa (TAKUKURU) na ujumbe wa Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi
Zanzibar (ZAECA) baada ya kuzungumza nao ulipomtembelea ofisini kwake jijini
Dodoma kwa lengo la kujitambulisha.
No comments:
Post a Comment