Friday, December 22, 2023

MHE. KIKWETE AWATAKA WATUMISHI WA UMMA KUTUMIA MIFUMO YA TEHAMA KUBORESHA UTENDAJI KAZI

 Na. Rainer Budodi - Dodoma

Tarehe 20 Desemba, 2023

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Kikwete amewataka watumishi wa Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Wizara ya Mambo ya Nje na Wakala wa Huduma ya Ununuzi Serikalini-GPSA kuzingatia mafunzo wanayopewa ili kuboresha utendaji kazi wa watumishi na taasisi kwa jumla.

Mhe. Kikwete amesema hayo jijini Dodoma wakati akifungua mafunzo ya matumizi ya mifumo ya kupima utendaji kazi wa watumishi na taasisi (PEPMIS, PIPMIS) na HR Assesment kwa nyakati tofauti.

Mhe. Kikwete ameongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan inalenga kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi, hivyo Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imebuni mifumo hiyo kwa lengo la kutatua changamoto za upimaji wa utendaji kazi wa watumishi na taasisi na zaidi kutambua hali halisi ya uwiano wa rasilimaliwatu katika utumishi wa umma.

Aidha, Mhe. Kikwete amesema kuwa mfumo wa zamani wa upimaji utendaji kazi wa watumishi kwa kujazaji fomu za OPRAS ulionekana kushindwa kupima uhalisia wa kiutendaji kwa watumishi wa umma. Hivyo mifumo hii ya PEPMIS na PIPMIS itatatua changamoto iliyokuwapo hapo awali na kuleta ufanisi zaidi.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Dkt. Tausi Kida ameishukuru na kuipongeza Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa kubuni na kusanifu mifumo hii muhimu itakayoleta ufanisi wa kiutendaji na kuzingatia haki na wajibu kwa watumishi wa umma na Serikali kwa jumla.

“Tumefurahia  ujio wa mifumo hii ambayo italeta chachu kwa watumishi wa umma katika kuwahudumia wananchi na kuifanya Serikali kuboresha maeneo yenye changamoto kwa watumishi na taasisi” Amesema Dkt. Kida.

Dkt. Kida ameongeza kuwa ofisi yake iko tayari kuunganisha mifumo hii ya PEPMIS, PIPMIS na HR Assessment kwenye Dira ya taifa ya mwaka 2050 ambayo itaenda kuonesha mwelekeo wa nchi kwa miaka 25 ijayo.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Kikwete akifungua mafunzo ya matumizi ya mfumo wa kupima utendaji kazi wa mtumishi na taasisi (PEPMIS na PIPMIS) kwa watumishi wa Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji katika ukumbi mdogo uliopo katika jengo Mkandarasi House Jijini Dodoma.


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Kikwete akiongea na watumishi wa Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji wakati akifungua mafunzo ya matumizi ya mfumo wa kupima utendaji kazi wa mtumishi na taasisi katika ukumbi uliopo Mkandarasi House Jijini Dodoma tarehe 19 Desemba, 2023. Kushoto ni Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Dkt. Tausi Kida na Kulia ni Mkurugenzi wa Idara ya Utawala wa Utumishi wa Umma, Ofisi ya Rais- UTUMISHI Bi. Felista Shuli.


Baadhi ya watumishi kutoka Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji wakifuatilia hotuba ya Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Kikwete wakati akifungua mafunzo ya matumizi ya mfumo wa kupima utendaji kazi wa mtumishi na taasisi katika ukumbi uliopo Mkandarasi House Jijini Dodoma. 


Baadhi ya watumishi kutoka Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji wakifuatilia hotuba ya Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Kikwete (Hayupo Pichani) wakati akifungua mafunzo ya matumizi ya mfumo wa kupima utendaji kazi wa mtumishi na taasisi katika ukumbi uliopo Mkandarasi House Jijini Dodoma. 



Thursday, December 21, 2023

WATUMISHI WA UMMA SASA KUJIPIMA UTENDAJI KAZI KWA KUTUMIA MIFUMO YA TEHAMA

 Na. Veronica Mwafisi- Dumila

Tarehe 20 Desemba, 2023

Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi amewaasa watumishi wa umma wa Halmashauri Wilaya ya Kilosa Kanda ya Dumila kujipima kupitia Mifumo Mipya ya PEPMIS, PIPMIS na HR Assessment kwa kujaza kazi wanazotekeleza kila siku ili mfumo uweze kutoa alama sahihi.

Amesema hayo wakati alipotembelea kanda ya kimafunzo ya Dumila kuona maendeleo ya Mafunzo ya Mifumo hiyo.

Bw. Daudi amesema kuwa, mafunzo hayo yanalenga kuwaongezea watumishi wa umma ujuzi na ari ya kutumia mifumo ya TEHAMA katika kupima utendaji kazi na utekelezaji wa shughuli mbalimbali Serikalini.

“Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan inafanya juhudi kubwa katika kusimamia na kutoa stahiki na maslahi mbalimbali kwa watumishi wa umma. Hivyo, ni jukumu la watumishi kumuunga mkono kwa kutoa huduma bora kwa umma” alisema Bw. Daudi.

Aidha, Bw. Daudi ameongeza kuwa, moja ya majukumu ya Ofisi ya Rais -UTUMISHI ni kusimamia utumishi wa umma, ndio maana Serikali imebuni mifumo hiyo ambayo itaboresha utendaji kazi Serikalini kwa kumpima mtumishi mmoja mmoja na taasisi.

Bw. Daudi amefafanua kuwa kupitia mfumo wa PEPMIS kila Mwajiri atakuwa na uwezo wa kuona namna watumishi wake wanavyofanya kazi kila siku.

Naibu Katibu Mkuu huyo, amesema amefurahishwa na namna watumishi wa umma katika mkoa wa Morogoro walivyoitikia wito wa kushiriki mafunzo hayo na wameonesha utayari wa kutumia mifumo hiyo ili kuunga mkono juhudi za Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan anayetaka kuona kunakuwa na utumishi wa umma bora na wenye kuhudumia wananchi kwa ufanisi mkubwa.

Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi akizungumza na baadhi ya Viongozi na Watumishi wa Halmashauri Wilaya ya Kilosa Kanda ya Dumila (hawapo pichani) alipowatembelea kuona maendeleo ya Mafunzo ya Mifumo ya PEPMIS, PIPMIS na HR Assesment kwa Mkoa wa Morogoro.


Baadhi ya Viongozi na Watumishi wa Halmashauri Wilaya ya Kilosa Kanda ya Dumila wakimsikiliza Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi alipowatembelea kuona maendeleo ya Mafunzo ya Mifumo ya PEPMIS, PIPMIS na HR Assesment kwa Mkoa wa Morogoro.


Mkurugenzi wa Idara ya TEHAMA Serikalini, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ambaye pia ni Msimamizi Mkuu wa Mafunzo ya Mifumo ya PEPMIS, PIPMIS na HR Assesment kwa Mkoa wa Morogoro, Bw. Priscus Kiwango akimueleza Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi maendeleo ya mafunzo ya mifumo hiyo.



Wednesday, December 20, 2023

WATUMISHI WA UMMA KILOSA, MIKUMI NA DUMILA WAPATA MAFUNZO YA MATUMIZI YA MIFUMO YA TEHAMA

 Na. Veronica Mwafisi- Kilosa, Mikumi na Dumila

Tarehe 19 Desemba, 2023

Mkurugenzi wa Idara ya TEHAMA Serikalini, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ambaye pia ni Msimamizi Mkuu wa Mafunzo ya PEPMIS, PIPMIS na HR Assesment kwa Mkoa wa Morogoro, Bw. Priscus Kiwango amewataka watumishi wa umma katika mkoa wa Morogoro kuzingatia mafunzo wanayopewa ili kuboresha utendaji kazi wao na taasisi kwa jumla.

Bw. Kiwango amesema mifumo hii itawawezesha viongozi kusimamia utendaji kazi wa watumishi wao bila upendeleo ikiwemo kupanda vyeo kwa haki, kupima utendaji kazi wa Taasisi za Umma na kufanya Tathmini ya hali ya Rasilimaliwatu Serikalini kwa lengo la kuimarisha utoaji wa huduma kwa umma.

Amesema hayo katika nyakati tofauti wakati wa mafunzo ya namna ya kutumia mifumo mipya ya PEPMIS, PIPMIS na HR Assesment kwa Watumishi wa Umma na taasisi zilizopo mkoani Morogoro katika Kanda tatu ikiwemo Mikumi, Kilosa Mjini na Dumila. 

Mkurugenzi Kiwango ameongeza kuwa mafunzo hayo yanaendelea kutolewa kwenye Halmashauri ya Wilaya Kilosa, Gairo, Morogoro mjini na kwa baadhi ya taasisi na kwa watendaji wa kata na vijiji, walimu wa sekondari na msingi, watumishi wa kilimo, mifugo na ustawi wa jamii.

“Mpaka sasa kwa mkoa wa Morogoro tumetoa mafunzo kwa taasisi 21 ikiwemo Ofisi ya RAS, Halmashauri ya Morogoro DC, Manispaa ya Morogoro, Mvomero, Malinyi, Mlimba, Ifakara Ulanga, Kilosa, Mikumi na Dumila na kwa mwenendo huu tutakamilisha mafunzo kwa wakati uliopangwa”. Alisema Bw. Kiwango.

Kwa upande wake, Mkufunzi wa mafunzo hayo ambaye ni Mkurugenzi Msaidizi anayesimamia huduma za Uuguzi na Ukunga nchini, Wizara ya Afya, Bw. Paul Mashauri amesema watumishi wa umma mkoa wa Morogoro wanaonesha utayari wa kutumia mifumo hii katika utendaji kazi wao kutokana na uwazi uliopo katika mifumo.

Naye, Mkurugenzi Msaidizi Mipango na Bajeti, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bi. Matilda Mtenga ambaye pia ni mkufunzi ameongeza kuwa, mwitikio wa watumishi wa umma katika mkoa wa Morogoro ni mkubwa na wanafurahi kuona ujio wa mifumo inayonesha uwezo wa  kila mtumishi wa umma.

Ofisi ya Rais-UTUMISHI inaendelea kutoa Mafunzo ya PEPMIS, PIPMIS na HR Assesment katika Mikoa yote Tanzania Bara na yanatarajiwa kuhitimishwa Desemba 31,2023.

Mkurugenzi wa Idara ya TEHAMA Serikalini, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ambaye pia ni Msimamizi Mkuu wa Mafunzo ya Mifumo ya PEPMIS, PIPMIS na HR Assesment kwa Mkoa wa Morogoro Bw. Priscus Kiwango akizungumza na baadhi ya Viongozi na Watumishi wa Halmashauri Wilaya ya Kilosa Kanda ya Mikumi wakati akifungua Mafunzo ya Mifumo hiyo katika Ukumbi wa Veta mkoani humo.


Baadhi ya Viongozi na Watumishi wa Halmashauri Wilaya ya Kilosa Kanda ya Mikumi wakimsikiliza Mkurugenzi wa Idara ya TEHAMA Serikalini, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ambaye pia ni Msimamizi Mkuu wa Mafunzo ya Mifumo ya PEPMIS, PIPMIS na HR Assesment kwa Mkoa wa Morogoro Bw. Priscus Kiwango (hayupo pichani) wakati akifungua Mafunzo ya Mifumo hiyo.


Baadhi ya Viongozi na Watumishi wa Halmashauri Wilaya ya Kilosa wakifuatilia Mafunzo ya Mifumo ya PEPMIS, PIPMIS na HR Assesment yanayotolewa na Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora mkoani Morogoro.


Mkurugenzi Msaidizi anayesimamia huduma za Uuguzi na Ukunga nchini, Wizara ya Afya, ambaye pia ni Mkufunzi wa mafunzo ya PEPMIS, PIPMIS na HR Assessment, Bw. Paul Mashauri akiwaelekeza watumishi wa Halmashauri Wilaya ya Kilosa, Kanda ya Mikumi mkoani Morogoro namna ya kuingia na kutumia Mifumo hiyo wakati wa mafunzo. 


Mkurugenzi Msaidizi Mipango na Bajeti, Wizara ya Mifugo na Uvuvi ambaye pia ni Mkufunzi wa mafunzo ya PEPMIS, PIPMIS na HR Assessment, Bi. Matilda Mtenga akiwaelekeza watumishi Halmashauri Wilaya ya Kilosa, Kanda ya Mikumi mkoani Morogoro namna ya kuingia na kutumia Mifumo hiyo wakati wa mafunzo. 



Thursday, December 14, 2023

WATUMISHI WA UMMA WAASWA KUTOKUWA NA HOFU NA MFUMO MPYA WA TATHIMINI YA WATUMISHI

 WATUMISHI WA UMMA WAASWA KUTOKUWA NA HOFU NA MFUMO MPYA WA TATHIMINI  YA WATUMISHI.


Na Lusungu Helela-Dar es Salaam

Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya  Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Kikwete amesema Mfumo wa Mahitaji ya Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma (HRA) hauna lengo la kumuondoa kazini ama kuwaonea watumishi wa umma hivyo hawana sababu ya kuuhofia mfumo huo.

Mhe. Kikwete amebainisha hayo  wakati wa ufungaji wa mafunzo ya siku tatu kwa watumishi wa umma kutoka Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) Shirika la Masoko Kariakoo na Bodi ya Sukari Tanzania yaliyofanyika MOI.

Amesema lengo la mfumo huo ni kuiwezesha kupima utendaji wa watumishi wake kwa njia rahisi na kuongeza ufanisi wenye tija kazini.

“Mfumo huu  hauna lengo la kukomoa watu, tunatakuwa na utumishi wa umma unaotimiza majukumu, utawezesha kupamga utumishi wenye tija, huna sababu ya kuhofia” amesema Mhe: Kikwete

Amesema mifumo hiyo inakwenda kuonesha wapi kwenye mapungufu ili paweze kuboreshwa

Aidha aliipongeza MOI kwa kutoa huduma bora kwa Watanzania na kuitaka kuendelea na kasi hiyo kwa maslahi ya umma.

“MOI inaendelea kuwa bora hii yote ni juhudi zako Profesa Makubi na timu yako, hongera sana, tunahitaji utumishi wenye tija” amesema


Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Prof. Abel Makubi akimkaribisha Naibu Waziri huyo alimpongeza kwa kuitembelea MOI mara kwa mara na kwamba hatua hiyo inaongeza ari kwa watumishi kufanya kazi kwa umahiri.

Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya  Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Kikwete akizungumza  leo wakati wa ufungaji wa mafunzo ya siku tatu kwa watumishi wa umma kutoka Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) Shirika la Masoko Kariakoo na Bodi ya Sukari Tanzania yaliyofanyika MOI.


Mkurugenzi wa Uendelezaji Taasisi, Naolasci Kipanda ambaye pia ni Mwezeshaji wa Mafunzo ya Mfumo wa Mahitaji ya Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma (HRA) Nestory Kipanga akizungumza kabla ya kumkaribisha  Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya  Utumishi wa Umma na Utawala Bora,Mhe.Ridhiwani Kikwete leo wakati wa ufungaji wa mafunzo ya siku tatu kwa watumishi wa umma kutoka Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) Shirika la Masoko Kariakoo na Bodi ya Sukari Tanzania yaliyofanyika MOI.


Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya  Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Kikwete akiwa ameongozana na Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Prof. Abel Makubi wakati akitembelea Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) mara baada ya kufungua mafunzo kwa watumishi wa umma



Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Prof. Abel Makubi akizungumza  leo wakati wa ufungaji wa mafunzo ya siku tatu kwa watumishi wa umma kutoka Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) Shirika la Masoko Kariakoo na Bodi ya Sukari Tanzania yaliyofanyika MOI.
Sehemu ya watumishi wa MOI Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya  Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Kikwetewakati akizungumza nao katika ufungaji wa mafunzo ya Mfumo wa Mahitaji ya Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma (HRA)

Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya  Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Kikwete akiwa  na Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Prof. Abel Makubi wakati akitembelea Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) akiangalia baadhi ya mashine za kisasa za mionzi zilizopo katika Taasisi hiyo.



Tuesday, December 12, 2023

WATUMISHI WA UMMA KUJAZA KAZI WANAZOFANYA KATIKA MFUMO MAHALI POPOTE

 Na. Rainer Budodi na Veronica Mwafisi- Dodoma

Tarehe 12 Desemba, 2023

Mkurugenzi wa Idara ya Utawala wa Utumishi wa Umma, Ofisi ya Rais- UTUMISHI ambaye pia ni Msimamizi Mkuu wa Mafunzo ya PEPMIS, PIPMIS na HR Assesment kwa Mkoa wa Dodoma Bi. Felista Shuli amesema Serikali imedhamiria kuimarisha Utumishi wa Umma kwa kuhimiza uwajibikaji wa hiari wa mtumishi kwa kujaza kazi anazofanya kila siku katika mfumo mahali popote ili kuongeza tija katika utoaji wa huduma kwa umma.

Ameyasema hayo leo tarehe 12 Desemba, 2023 wakati wa kufungua mafunzo ya matumizi ya Mfumo wa Kupima Utendaji Kazi wa Watumishi wa Umma na Taasisi (PEPMIS na PIPMIS) na Mfumo Maalum wa Tathmini ya hali ya Rasilimaliwatu Serikalini (HR Assesment) kwa viongozi na watumishi wa Wizara ya Fedha katika ukumbi wa Hazina Jijini Dodoma.

Bi. Felista amefafanua kuwa mfumo wa PEPMIS utawezesha viongozi kusimamia utendaji kazi wa watumishi bila upendeleo na utaongeza ufanisi, PIPMIS itawezesha kupima utendaji kazi wa Taasisi za Umma  na HR Assesment itawezesha kufanya Tathmini ya hali ya Rasilimaliwatu Serikalini na kuitumia ipasavyo.

Aidha, Bi. Shuli ameongeza kuwa hali ya mafunzo kwa Mkoa wa Dodoma inaendelea vizuri na anaamini yatakamilika kama ilivyopangwa kwa kuwa pande zote zinazohusika na mafunzo zinatoa ushirikiano mkubwa kwa wakati.

“Wawezeshaji wote wako vizuri na watumishi kutoka katika Wizara na Taasisi zote wanaitikia wito na wanakuja na kompyuta ambazo ni kitendea kazi muhimu sana katika mafunzo haya” amesema Bi.Felista.

Vilevile, amesema mfumo wa PEPMIS umekuja kuwa mbadala wa OPRAS ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anayelenga kuimarisha mifumo ya uwajibikaji inayowezesha viongozi na watumishi wa umma kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi wakati na mahali popote.

Awali, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu wa Wizara ya Fedha Bw. Renatus Msagira amesema watumishi wako tayari kujifunza na kutumia mifumo hiyo kwa ufanisi kwa maendeleo ya taifa.

“Tuko tayari na hatutakuwa kikwazo katika utekelezaji wa jitihada hizi muhimu za Serikali ambazo lengo lake ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora kwa wakati” amesisitiza Bw. Msagira.

Mafunzo ya PEPMIS, PIPMIS na HR Assesment yanaendeshwa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora katika Mikoa yote Tanzania Bara na yatahitimishwa Desemba 31,2023.

Mkurugenzi wa Idara ya Utawala wa Utumishi wa Umma, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ambaye pia ni Msimamizi Mkuu wa Mafunzo ya PEPMIS, PIPMIS na HR Assesment kwa Mkoa wa Dodoma Bi. Felista Shuli akizungumza na Viongozi na Watumishi wa Wizara ya Fedha wakati akifungua Mafunzo ya Mifumo hiyo katika Ukumbi wa Hazina jijini Dodoma.

Baadhi ya Viongozi na Watumishi wa Wizara ya Fedha wakimsikiliza Mkurugenzi wa Idara ya Utawala wa Utumishi wa Umma, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ambaye pia ni Msimamizi Mkuu wa Mafunzo ya PEPMIS, PIPMIS na HR Assesment kwa Mkoa wa Dodoma Bi. Felista Shuli (hayupo pichani) wakati akifungua Mafunzo ya Mifumo hiyo jijini Dodoma.


Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Utawala, Ofisi ya Rais UTUMISHI Bi. Nyasinde Mukono (Aliyesimama) akifafanua jambo kwa Mkurugenzi Mkuu wa LATRA, CPA. Habibu Suluo (Wa kwanza kulia) wakati wa Mafunzo ya Mfumo wa Upimaji wa Utendajikazi wa Watumishi Serikalini (PEPMIS) kwa Menejimenti ya LATRA yaliyofanyika katika ukumbi mdogo wa Bunge jijini Dodoma.


Menejimenti ya LATRA ikiendelea na mafuzo ya Mfumo wa Upimaji wa Utendaji kazi wa Watumishi Serikalini (PEPMIS) yanayoendeshwa na Ofisi ya Rais-UTUMISHI jijini Dodoma.


Baadhi ya Viongozi wa LATRA wakifanya mafunzo kwa vitendo ya Mfumo wa Upimaji na Utendajikazi wa Watumishi Serikalini (PEPMIS) yanayotolewa na Ofisi ya Rais-UTUMISHI jijini Dodoma.



Afisa Utumishi Mwandamizi, Idara ya Uendelezaji Sera, Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bi. Judith Abdallah akiwaelekeza washiriki wa Mafunzo ya Mfumo wa Upimaji wa Utendajikazi wa Watumishi Serikalini (PEPMIS) kutoka TANESCO, REA na EWURA jijini Dodoma.


Washiriki kutoka TANESCO, REA na EWURA wakiwa kwenye mafunzo ya Mfumo wa Upimaji wa Utendajikazi wa Watumishi Serikalini (PEPMIS) yanayotolewa na Ofisi ya Rais-UTUMISHI katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention jijini Dodoma.

 





 



MHE. KIKWETE ASEMA USHIRIKIANO UTABORESHA OFISI YA NYARAKA ZANZIBAR

 MHE. KIKWETE ASEMA USHIRIKIANO UTABORESHA OFISI YA NYARAKA ZANZIBAR


Na. Lusungu Helela- Dar es Salaam 


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Kikwete amewahakikishia Wajumbe wa Kamati ya Kusimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa ya Baraza la Wawakilishi  Zanzibar  kuwa    Idara ya  Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa   ipo tayari kushirikiana na Ofisi ya Nyaraka Zanzibar inaboreshwa kwa maslahi mapana ya pande zote mbili  za Muungano.


Mhe. Kikwete ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Desemba 12, 2023 wakati akizungumza na Wajumbe wa Kamati hiyo walipotembelea ofisi za Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa Kanda ya Mashariki zilizopo Jijini Dar es Salaam.

Mhe. Kikwete ameeleza lengo la ziara ya Kamati ya Kusimamia Ofisi za Viongozi  Wakuu wa Kitaifa ya Baraza la Wawakilishi  Zanzibar kwenye ofisi za Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa jijini Dar es Salaam ni kujifunza na kubadilishana uzoefu wa namna ya kutunza na kuhifadhi nyaraka na kumbukumbu za Taifa kwa maslahi ya vizazi vijavyo.


 “Tupo tayari kushirikiana nanyi ili kuhakikisha kumbukumbu na nyaraka za Waasisi wa Taifa letu zinalindwa na kuhifadhiwa kwa ajili ya kutusaidia kufanya uamuzi wenye mwelekeo sahihi na kulinda maslahi ya  kizazi cha sasa na cha baadaye’’ amesisitiza Mhe. Kikwete


Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Ikulu, Jamal Kassim Ali ameiomba Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa kuunga mkono jitihada mbalimbali zitakazofanywa na Ofisi ya Nyaraka Zanzibar kwa lengo la kuiboresha na kuhakikisha kumbukumbu na Nyaraka za Viongozi Wakuu wa Zanzibar zinatunzwa na kuhifadhiwa kwa maslahi mapana ya Taifa.

“Ofisi yetu ni changa na hivi karibuni tutasherehekea miaka 60 ya mapinduzi, hivyo tuomba ushirikiano wenu wa namna bora ya kutunza kumbukumbu za viongozi mbalimbali hususani kumbukumbu za Hayati Abeid Aman Karume” alisema Mhe. Jamal Kassim Ali.


Naye, Mwenyekiti wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mhe. Machano Othman Said amesema kuwa utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka za taifa ni shughuli muhimu sana katika maendeleo ya nchi. Hivyo,
Mhe. Machano ameisihi Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa kuwa tayari kutoa elimu, vifaa na uzoefu wa namna bora ya kutumia teknolojia katika uendeshaji wa  Ofisi ya Nyaraka Zanzibar.


Naibu Waziri  Ofisi ya Rais,  Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Kikwete akizungumza   Wajumbe wa Kamati ya Kusimamia Ofisi za Viongozi  Wakuu wa Kitaifa ya Baraza la Wawakilishi  Zanzibar  waliofanya zaira leo katika   Ofisi ya Rais, Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Kanda ya Mashariki Jijini Dar es Salaam kwa lengo la kujifunza na kubadilishana uzoefu wa namna ya kutunza na kuhifadhi nyaraka na kumbukumbu



Wajumbe wa Kamati ya Kusimamia Ofisi za Viongozi  Wakuu wa Kitaifa ya Baraza la Wawakilishi  Zanzibar wakimsikiliza Mkurugenzi wa Vituo vya Kumbukumbu, Gasper Kileo wakati akiwaonesha baadhi ya Nyaraka na Kumbukuku muhimu zinazopatikana katika Ofisi hiyo  leo wakati walipotembelea  Ofisi ya Rais, Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Kanda ya Mashariki Jijini Dar es Salaam kwa lengo la kujifunza na kubadilishana uzoefu wa namna ya kutunza na kuhifadhi nyaraka na kumbukumbu


 Mwenyekiti  wa Kamati ya Kusimamia Ofisi za Viongozi  Wakuu wa Kitaifa ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Mhe. Machano Said   akizungumza na    Wajumbe wa Kamati  hiyo ya  Baraza la Wawakilishi  Zanzibar  waliofanya ziara  mara baada ya Naibu Waziri  Ofisi ya Rais,  Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Kikwete kuwakaribisha  katika   Ofisi ya Rais, Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Kanda ya Mashariki Jijini Dar es Salaam kwa lengo la kujifunza na kubadilishana uzoefu wa namna ya kutunza na kuhifadhi nyaraka na kumbukumbu

Mwenyekiti  wa Kamati ya Kusimamia Ofisi za Viongozi  Wakuu wa Kitaifa ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Mhe. Machano Said   akiwa kwenye picha na  baadhi ya wajumbe wa  timu ya menejimenti ya Ofisi ya Rais, Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa pamoja na   Wajumbe wa Kamati  hiyo ya  Baraza la Wawakilishi  Zanzibar  mara baada ya kufanya ziara  katika   Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Kanda ya Mashariki Jijini Dar es Salaam kwa lengo la kujifunza na kubadilishana uzoefu wa namna ya kutunza na kuhifadhi nyaraka na kumbukumbu,  wa pili kulia ni Naibu Waziri  Ofisi ya Rais,  Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Kikwete

 


Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Kikwete akiwaonesha baadhi ya  Wajumbe wa Kamati ya Kusimamia Ofisi za Viongozi  Wakuu wa Kitaifa ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar baadhi ya hotuba ya  Baba wa Taifa  Mwl. Julius Kambarage Nyerere aliyoitoa wakati wa harakati za kudai uhuru wa Tanganyika  wakati Wajumbe  walipofanya ziara  leo ya kutembelea Ofisi ya Rais,  Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Kanda ya Mashariki Jijini Dar es Salaam kwa lengo la kujifunza na kubadilishana uzoefu wa namna ya kutunza na kuhifadhi nyaraka na kumbukumbu,   

Mkurugenzi Mkuu  Ofisi ya Rais, Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Firmin Msiangi    akiwaonesha Wajumbe wa Kamati ya Kusimamia Ofisi za Viongozi  Wakuu wa Kitaifa ya Baraza la Wawakilishi  Zanzibar baadhi ya Nyaraka muhimu zinazopatikana  katika   Ofisi ya Rais, Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Kanda ya Mashariki Jijini Dar es Salaam wakati  Wajumbe wa Kamati hiyo wakati  wakifanya  ziara kwa lengo la kujifunza na kubadilishana uzoefu wa namna ya kutunza na kuhifadhi nyaraka na kumbukumbu.


Naibu Waziri  Ofisi ya Rais,  Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Kikwete akizungumza na  Mkurugenzi Mkuu  Ofisi ya Rais, Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Firmin Msiangi mara baada ya kuwasili      katika   Ofisi ya Rais, Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Kanda ya Mashariki Jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kukutana na   Wajumbe wa Kamati ya Kusimamia Ofisi za Viongozi  Wakuu wa Kitaifa ya Baraza la Wawakilishi  Zanzibar  waliofanya ziara  leo Jijini Dar es Salaam


Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Kikwete akiangalia baadhi ya  Wajumbe wa Kamati ya Kusimamia Ofisi za Viongozi  Wakuu wa Kitaifa ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar baadhi ya hotuba ya  Baba wa Taifa  Mwl. Julius Kambarage Nyerere aliyoitoa wakati wa harakati za kudai uhuru wa Tanganyika  wakati Wajumbe  walipofanya ziara  leo ya kutembelea Ofisi ya Rais,  Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Kanda ya Mashariki Jijini Dar es Salaam kwa lengo la kujifunza na kubadilishana uzoefu wa namna ya kutunza na kuhifadhi nyaraka na kumbukumbu,