Friday, December 22, 2023

MHE. KIKWETE AWATAKA WATUMISHI WA UMMA KUTUMIA MIFUMO YA TEHAMA KUBORESHA UTENDAJI KAZI

 Na. Rainer Budodi - Dodoma

Tarehe 20 Desemba, 2023

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Kikwete amewataka watumishi wa Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Wizara ya Mambo ya Nje na Wakala wa Huduma ya Ununuzi Serikalini-GPSA kuzingatia mafunzo wanayopewa ili kuboresha utendaji kazi wa watumishi na taasisi kwa jumla.

Mhe. Kikwete amesema hayo jijini Dodoma wakati akifungua mafunzo ya matumizi ya mifumo ya kupima utendaji kazi wa watumishi na taasisi (PEPMIS, PIPMIS) na HR Assesment kwa nyakati tofauti.

Mhe. Kikwete ameongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan inalenga kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi, hivyo Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imebuni mifumo hiyo kwa lengo la kutatua changamoto za upimaji wa utendaji kazi wa watumishi na taasisi na zaidi kutambua hali halisi ya uwiano wa rasilimaliwatu katika utumishi wa umma.

Aidha, Mhe. Kikwete amesema kuwa mfumo wa zamani wa upimaji utendaji kazi wa watumishi kwa kujazaji fomu za OPRAS ulionekana kushindwa kupima uhalisia wa kiutendaji kwa watumishi wa umma. Hivyo mifumo hii ya PEPMIS na PIPMIS itatatua changamoto iliyokuwapo hapo awali na kuleta ufanisi zaidi.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Dkt. Tausi Kida ameishukuru na kuipongeza Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa kubuni na kusanifu mifumo hii muhimu itakayoleta ufanisi wa kiutendaji na kuzingatia haki na wajibu kwa watumishi wa umma na Serikali kwa jumla.

“Tumefurahia  ujio wa mifumo hii ambayo italeta chachu kwa watumishi wa umma katika kuwahudumia wananchi na kuifanya Serikali kuboresha maeneo yenye changamoto kwa watumishi na taasisi” Amesema Dkt. Kida.

Dkt. Kida ameongeza kuwa ofisi yake iko tayari kuunganisha mifumo hii ya PEPMIS, PIPMIS na HR Assessment kwenye Dira ya taifa ya mwaka 2050 ambayo itaenda kuonesha mwelekeo wa nchi kwa miaka 25 ijayo.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Kikwete akifungua mafunzo ya matumizi ya mfumo wa kupima utendaji kazi wa mtumishi na taasisi (PEPMIS na PIPMIS) kwa watumishi wa Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji katika ukumbi mdogo uliopo katika jengo Mkandarasi House Jijini Dodoma.


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Kikwete akiongea na watumishi wa Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji wakati akifungua mafunzo ya matumizi ya mfumo wa kupima utendaji kazi wa mtumishi na taasisi katika ukumbi uliopo Mkandarasi House Jijini Dodoma tarehe 19 Desemba, 2023. Kushoto ni Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Dkt. Tausi Kida na Kulia ni Mkurugenzi wa Idara ya Utawala wa Utumishi wa Umma, Ofisi ya Rais- UTUMISHI Bi. Felista Shuli.


Baadhi ya watumishi kutoka Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji wakifuatilia hotuba ya Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Kikwete wakati akifungua mafunzo ya matumizi ya mfumo wa kupima utendaji kazi wa mtumishi na taasisi katika ukumbi uliopo Mkandarasi House Jijini Dodoma. 


Baadhi ya watumishi kutoka Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji wakifuatilia hotuba ya Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Kikwete (Hayupo Pichani) wakati akifungua mafunzo ya matumizi ya mfumo wa kupima utendaji kazi wa mtumishi na taasisi katika ukumbi uliopo Mkandarasi House Jijini Dodoma. 



No comments:

Post a Comment