Na. Veronica Mwafisi- Dumila
Tarehe 20 Desemba, 2023
Naibu Katibu
Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi amewaasa watumishi wa umma wa
Halmashauri Wilaya ya
Kilosa Kanda ya Dumila kujipima kupitia Mifumo Mipya ya PEPMIS, PIPMIS na HR
Assessment kwa kujaza kazi wanazotekeleza kila siku ili mfumo uweze kutoa alama
sahihi.
Amesema hayo wakati alipotembelea kanda ya
kimafunzo ya Dumila kuona maendeleo ya Mafunzo ya Mifumo hiyo.
Bw. Daudi amesema kuwa, mafunzo hayo
yanalenga kuwaongezea watumishi wa umma ujuzi na ari ya kutumia mifumo ya
TEHAMA katika kupima utendaji kazi na utekelezaji wa shughuli mbalimbali Serikalini.
“Serikali ya Awamu ya Sita
inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu
Hassan inafanya juhudi kubwa katika kusimamia na kutoa stahiki na maslahi mbalimbali
kwa watumishi wa umma. Hivyo, ni jukumu la watumishi kumuunga mkono kwa kutoa
huduma bora kwa umma” alisema Bw. Daudi.
Aidha, Bw. Daudi ameongeza kuwa, moja
ya majukumu ya Ofisi ya Rais -UTUMISHI ni kusimamia utumishi wa umma, ndio
maana Serikali imebuni mifumo hiyo ambayo itaboresha utendaji kazi Serikalini
kwa kumpima mtumishi mmoja mmoja na taasisi.
Bw. Daudi amefafanua kuwa kupitia
mfumo wa PEPMIS kila Mwajiri atakuwa na uwezo wa kuona namna watumishi wake
wanavyofanya kazi kila siku.
Naibu
Katibu Mkuu huyo, amesema amefurahishwa na namna watumishi wa umma katika mkoa
wa Morogoro walivyoitikia wito wa kushiriki mafunzo hayo na wameonesha utayari
wa kutumia mifumo hiyo ili kuunga mkono juhudi za Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan
anayetaka kuona kunakuwa na utumishi wa umma bora na wenye kuhudumia wananchi kwa
ufanisi mkubwa.
Naibu
Katibu
Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi akizungumza na baadhi ya Viongozi na Watumishi wa Halmashauri Wilaya
ya Kilosa Kanda ya Dumila (hawapo pichani) alipowatembelea
kuona maendeleo ya Mafunzo ya Mifumo ya PEPMIS, PIPMIS na HR Assesment kwa Mkoa
wa Morogoro.
Baadhi ya Viongozi na Watumishi wa Halmashauri
Wilaya ya Kilosa Kanda ya Dumila wakimsikiliza Naibu
Katibu Mkuu, Ofisi
ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi alipowatembelea kuona
maendeleo ya Mafunzo ya Mifumo ya PEPMIS, PIPMIS na HR Assesment kwa Mkoa wa Morogoro.
Mkurugenzi wa Idara ya TEHAMA
Serikalini, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
ambaye pia ni Msimamizi Mkuu wa Mafunzo ya Mifumo ya PEPMIS, PIPMIS na HR
Assesment kwa Mkoa wa Morogoro, Bw. Priscus
Kiwango akimueleza Naibu Katibu Mkuu, Ofisi
ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi maendeleo ya mafunzo ya
mifumo hiyo.
No comments:
Post a Comment