Saturday, July 30, 2022

MHE. JENISTA AIASA TUME YA UTUMISHI WA UMMA KUSIMAMIA HAKI WAKATI WA KUTOA MAAMUZI YA MASHAURI YA KINIDHAMU

 Na. Veronica Mwafisi-Dodoma

Tarehe 30 Julai, 2022 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Jenista Mhagama ameiasa Tume ya Utumishi wa Umma kusimamia haki wakati wa kutoa maamuzi ya mashauri ya kinidhamu ya watumishi wa umma yaliyowasilishwa ili kutolewa maamuzi.

Mhe. Jenista ametoa nasaha hizo jijini Dodoma wakati wa kikao kazi chake na Makamishna wa Tume ya Utumishi wa Umma, kilichofanyika ofisini kwake kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji katika Tume ya Utumishi wa Umma.

Mhe. Jenista ameitaka Tume ya Utumishi wa Umma kutoa maamuzi ya mashauri yote ya kinidhamu kwa kuzingatia haki, kwa mujibu wa Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo ya Utumishi wa Umma iliyopo.

Waziri Jenista ameongeza kuwa, Tume isipo yashughulikia mashauri ya kinidhamu kwa haki na wakati, inakwamisha maendeleo ya nchi yasipatikane kwa wakati na ndio maana Serikali imekuwa ikiihimiza Tume ya Utumishi wa Umma kutekeleza wajibu wao kwa wakati na kwa kutenda haki.

 “Jambo la msingi hakikisheni haki inatendeka katika mashauri ya kinidhamu, mkifanya hivyo mtakuwa mnasimamia na kujenga nidhamu nzuri ya utendaji kazi katika Utumishi wa Umma,” Mhe. Jenista amesisitiza.

Aidha, Mhe. Jenista amezungumzia changamoto ukiukwaji wa Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo  ya utumishi wa umma unaofanywa na baadhi ya waajiri na watumishi, hivyo amewataka Makamishna wa Tume ya Utumishi wa Umma kufanyia kazi changamoto hiyo. 

Akizungumza kwa niaba ya Makamishna wa Tume ya Utumishi wa Umma, Mhe.  Balozi John Haule amemshukuru Mhe. Jenista Mhagama kwa kuwahimiza kutenda haki wakati wa kushughulikia mashauri ya kinidhamu na kumuahidi kuwa watatoa maamuzi ya mashauri ya kinidhamu kwa mujibu wa Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo iliyopo katika Utumishi wa Umma.

Tume ya Utumishi wa Umma imeundwa chini ya kifungu Na. 9 (1) cha Sheria ya Utumishi wa Umma, Sura ya 298. Tume hii ina jukumu la kufuatilia na kusimamia uendeshaji wa shughuli za rasilimaliwatu katika Taasisi za Umma ikiwa ni pamoja na kuhakikisha Utumishi wa umma unaendeshwa kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Taratibu.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Jenista Mhagama akizungumza na Makamishna wa Tume ya Utumishi wa Umma (hawapo pichani) wakati wa kikao kazi chake na Makamishna wa Tume hiyo chenye lengo la kuhimiza uwajibikaji.


Makamishna wa Tume ya Utumishi wa Umma wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Jenista Mhagama (meza kuu katikati) wakati akizungumza nao kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji.


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akitoa neno la utangulizi kabla ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Jenista Mhagama kuzungumza na Makamishna wa Tume ya Utumishi wa Umma jijini Dodoma.


Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Umma, Mhe. Jaji (Mst.) Hamisa Kalombola akitoa taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Tume ya Utumishi wa Umma kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Jenista Mhagama kabla ya Waziri huyo kuzungumza na Makamishna wa Tume hiyo kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji.


Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Umma, Mhe.  Balozi John Haule akitoa neno la shukrani kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Jenista Mhagama mara baada ya Waziri huyo kuzungumza nao kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji.


Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma, Bw. Mathew Kirama akiwatambulisha Makamishna wa Tume ya Utumishi wa Umma (hawapo pichani) kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Jenista Mhagama kabla ya Waziri huyo kuzungumza na Makamishna wa Tume hiyo kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akiwa katika picha ya pamoja na Makamishna wa Tume ya Utumishi wa Umma, mara baada ya kuzungumza na makamishna hao kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji.



Tuesday, July 19, 2022

SUMA JKT YATAKIWA KUKABIDHI JENGO LA OFISI ZA KARAKANA YA NDEGE JULAI 31, 2022 ILI KUIWEZESHA TGFA KUTOA HUDUMA KWA UFANISI

 Na. Veronica Mwafisi – Dar es Salaam

Tarehe 19 Julai, 2022 

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amemtaka Mkandarasi SUMA JKT kuhakikisha anakabidhi jengo la ofisi za karakana ya ndege (HANGAR) kwa Wakala ya Ndege za Serikali (TGFA) tarehe 31 Julai, 2022, ili kuiwezesha TGFA kuongeza ufanisi katika kutoa huduma ya usafiri wa anga kwa viongozi wakuu wa nchi wakiwa katika utekelezaji wa majukumu ya kitaifa.

Mhe. Ndejembi ametoa maelekezo hayo jijini Dar es Salaam, mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa ofisi za karakana ya ndege na kuridhika na hatua iliyofikiwa.

Mhe. Ndejembi amesema ofisi yake inategemea tarehe 31 Julai, 2022 jengo la Ofisi ya Karakana ya Ndege litakabidhiwa kwa TFGA, kwani TGFA inategemewa sana na Serikali katika kutoa huduma bora za usafiri wa anga kwa viongozi wakuu wa kitaifa.

“Baada ya kufanya ukaguzi, nimeridhika na kiwango cha ubora na hatua ya ujenzi iliyofikiwa na mkandarasi katika ujenzi wa jengo hili la ofisi za karakana ya ndege,” Mhe. Ndejembi amefafanua.

Mhe. Ndejembi ameongeza kuwa, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama anawapongeza Mkandarasi SUMA JKT, Mshauri Mwelekezi DIT na Mzabuni TGFA kwa ujenzi uliozingatia ubora.

“Tumeona namna jengo lilivyo la kisasa, kwani limewekewa vifaa vya kupambana na moto ikiwa ni pamoja na kuwezesha matumizi mazuri ya umeme,” Mhe. Ndejembi amesisitiza.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Ndege za Serikali (TGFA), Mhandisi John Nzulule amemshukuru Waziri Jenista Mhagama na Naibu wake Mhe. Deogratius Ndejembi pamoja na wajumbe wa bodi, kwa kufanya ziara za kukagua maendeleo ya ujenzi katika nyakati tofauti, lengo likiwa ni kuhimiza ukamilishaji wa ujenzi wa ofisi za karakana ya ndege ambao hivi sasa upo katika hatua nzuri kutokana na ufuatiliaji wao.

Kukamilika kwa jengo la ofisi za karakana ya ndege (HANGAR) kutaiwezesha TGFA kutekeleza majukumu yake kikamilifu.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (wa kwanza kushoto) akisisitiza jambo kwa Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Ndege za Serikali, Mhandisi John Nzulule (wa pili kutoka kushoto) kuhusu ukamilishaji wa ujenzi wa jengo la ofisi ya Karakana ya Wakala ya Ndege za Serikali alipofanya ziara ya kikazi ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo hilo jijini Dar es Salaam.  


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akitoa maelekezo kwa wakandarasi wa SUMA JKT na wabunifu majengo wa DIT kuhusu ukamilishwaji wa ujenzi wa jengo la ofisi ya Karakana ya Wakala ya Ndege za Serikali alipofanya ziara ya kikazi ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo hilo jijini Dar es Salaam.  



Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Ndege za Serikali, Mhandisi John Nzulule akielezea maendeleo ya ujenzi wa ofisi ya Karakana ya Wakala ya Ndege za Serikali wakati Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (hayupo pichani) alipofanya ziara ya kikazi ya kukagua maendeleo ya ujenzi huo jijini Dar es Salaam.   


Mbunifu Majengo - DIT, Bw. Anderson Allan akifafanua jambo kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (wa kwanza kulia) wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo iliyolenga kukagua maendeleo ya ujenzi huo jijini Dar es Salaam.  


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (wa kwanza kushoto) akitoka kukagua jengo la ofisi ya Karakana ya Wakala ya Ndege za Serikali wakati alipofanya ziara ya kikazi ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo hilo jijini Dar es Salaam.  Wa pili kutoka kushoto ni Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Ndege za Serikali, Mhandisi John Nzulule


Mhandisi wa Umeme – DIT, Bw. Adam Liwondo (wa kwanza kushoto) akimuonesha Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (wa pili kutoka kushoto) maeneo ambayo umeme utapita wakati Naibu Waziri huyo alipofanya ziara ya kikazi iliyolenga kukagua maendeleo ya ujenzi huo jijini Dar es Salaam.  


Muonekano wa jengo la ofisi ya Karakana ya Wakala ya Ndege za Serikali linaloendelea kujengwa jijini Dar es Salaam.  



Friday, July 15, 2022

MHE. NDEJEMBI AIELEKEZA TASAF KUJENGA UZIO SHULE YA SEKONDARI YA OLDONYOWAS ILI KULINDA MIUNDOMBINU YA SERIKALI

 Na. Veronica Mwafisi - Arusha

Tarehe 15 Julai, 2022

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi ameuelekeza uongozi wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kujenga uzio katika Shule ya Sekondari ya Oldonyowas iliyopo katika Kijiji cha Oldonyowas Halmashauri ya Wilaya ya Arusha, ili kulinda miundombinu ya Serikali iliyojengwa kwa jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ikiwa ni pamoja na kuimarisha usalama wa wanafunzi wa shule hiyo.

Mhe. Ndejembi ametoa maelekezo hayo, mara baada ya kukagua mabweni mawili ya wanafunzi wa kiume katika shule ya Sekondari Oldonyowas, wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika Halmashauri ya Wilaya ya Arusha.

“TASAF oneni ni kwa namna gani mtawezesha kwa haraka ujenzi wa uzio wa shule ya Sekondari ya Oldonyowas ili kuboresha usalama wa wanafunzi na kulinda miundombinu ambayo Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ametumia fedha nyingi za UVIKO katika kujenga mabweni ya wanafunzi wa kike na kiume pamoja na madarasa,” Mhe. Ndejembi amesisitiza.

Kwa upande wake, mmoja wa wananchi wa Kijiji cha Oldonyowas, Bi. Cecilia Sarakikya amesema ameupokea kwa mikono miwili mradi wa ujenzi wa mabweni kwasasabu utawasaidia watoto wao kupata sehemu ya kuishi katika mazingira ya shule, ikizingatiwa kuwa familia nyingi za wanafunzi wa shule hiyo ni za wafugaji ambao wanaishi pembezoni, hivyo kuwalazimu wanafunzi kutembea umbali mrefu ili kuhudhuria masomo.

Naye, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Bw. Oscar Maduhu ameitaka kamati ya ujenzi kuhakikisha ujenzi wa mabweni unakamilika kwa kiwango kinachostahili.

Sanjari na hilo, Bw. Maduhu amewataka wananchi wa Kijiji cha Oldonyowas kuyatunza mabweni hayo pindi yatakapokamilika, ili yawe na manufaa katika kuboresha mazingira ya utoaji wa elimu kwa watoto wa Kijiji hicho.

Mradi wa ujenzi wa mabweni mawili katika Kijiji cha Oldonyowas unaoendelea kukamilishwa, umefadhiliwa na OPEC kwa uratibu wa TASAF.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Oldonyowas katika shule ya Sekondari Oldonyowas mkoani Arusha wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Arusha.

 

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akisisitiza ujenzi wa uzio katika Shule ya Sekondari Oldonyowas wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Arusha.

 

Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Mhandisi Richard Ruyango akimshukuru Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi kwa kufanya ziara ya kikazi yenye lengo la kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini.

 

Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi wa shule ya Sekondari Oldonyowas Halmashauri ya Wilaya ya Arusha, Bw. Anael Salakiki akisoma taarifa ya utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi ya kukagua utekelezaji wa Mpango wa TASAF katika Halmashauri hiyo.

 

Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Bw. Oscar Maduhu akisisitiza kutunza miundombinu ya majengo yanayojengwa katika Kijiji cha Oldonyowas Halmashauri ya Wilaya ya Arusha wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi yenye lengo la kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini kwenye Halmashauri hiyo.

 

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akikagua nyaraka za ujenzi kwa ajili ya kujiridhisha na matumizi ya fedha zilizotolewa kwenye ujenzi wa bweni la wavulana shule ya Sekondari Oldonyowas wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Arusha.

 

Mmoja wa wananchi wa Kijiji cha Oldonyowas, Bi. Cecilia Sarakikya akitoa salamu za shukrani kwa TASAF kwa kuwezesha mradi wa ujenzi wa mabweni ya wanafunzi wa shule ya Sekondari Oldonyowas mkoani Arusha wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi ya kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Arusha.

 

Mwonekano wa bweni linalojengwa katika shule ya Sekondari Oldonyowas kwa ufadhili wa OPEC kupitia uratibu TASAF.