Wednesday, July 6, 2022

MHE. JENISTA AWATAKA MAAFISA UTUMISHI KUWA WALEZI WA WATUMISHI WA UMMA

Na. James K. Mwanamyoto-Tunduru

Tarehe 06 Julai, 2022 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amewataka Maafisa Utumishi katika taasisi za umma kuwa walezi wa watumishi wa umma walio katika maeneo wanayoyasimamia kwa lengo la kutatua kero na changamoto zinazowakabili watumishi wa umma ili waweze kutoa mchango kwa ustawi taifa. 

Mhe. Jenista amesema hayo alipokuwa akizungumza na Watumishi wa Serikali wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma wakati wa ziara yake ya kikazi katika halmashauri hiyo iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua kero na changamoto zinazowakabili watumishi wa umma wilayani Tunduru. 

Mhe. Jenista amesema, Maafisa Utumishi wote katika taasisi za umma wanatakiwa kuwa kama wazazi wa watumishi walio katika maeneo yao ya kazi, hivyo hawana budi kuwalea katika misingi bora ya kiutumishi na kuzingatia ustawi wao ili waweze kutekeleza jukumu la kuuhudumia umma kikamilifu. 

“Afisa Utumishi wa Halmashauri hii ya Tunduru naomba nikukabidhi rasmi watumishi hawa wa halmashauri yako ukiwa ndiye baba na mama kwenye malezi ya kiutumishi na uhakikishe unakuwa ni sehemu ya utatuzi wa changamoto zinazowakabili na furaha yao,” Mhe. Jenista amesisitiza 

Mhe. Jenista amesema, kumekuwa na changamoto kwa baadhi ya Maafisa Utumishi kuwa kikwazo kwa ustawi wa watumishi na kuwataka kubadilika ili kubeba jukumu la malezi ya watumishi wa umma. 

Ameongeza kuwa Maafisa Utumishi wanao uwezo wa kutatua shida na changamoto zinazowakabili watumishi wa umma katika maeneo yao ya kazi hivyo kuwapunguzia kadhia ya watumishi hao kusafiri umbali mrefu kutoka katika vituo vyao vya kazi hadi Dodoma kwa ajili ya utatuzi wa masuala yao ya kiutumishi. 

Aidha, Mhe. Jenista amesema, kuanzia sasa hategemei kupokea simu ya malalamiko ya watumishi wa umma kuhusu masuala ya kiutumishi kwani anaamini Maafisa Utumishi watatekeleza jukumu lao la malezi kikamilifu. 

Mhe. Jenista anaendelea na ziara yake ya kikazi mkoani Ruvuma ya kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma na kutatua changamoto zinazowakabili ili kuboresha utendaji kwa lengo la kutoa huduma bora kwa wananchi.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akizungumza na Watumishi wa Serikali wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani humo iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi hao.


Watumishi wa Serikali wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao wakati wa ziara ya kikazi ya Waziri huyo mkoani Ruvuma iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi hao.


Afisa Utumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru, Bw. Masanja Kengese akisikiliza maelekezo ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani) ya kumtaka kuwa mlezi wa watumishi walio katika eneo lake la kazi.


 

No comments:

Post a Comment