Saturday, September 5, 2026

UTUMISHI SC YASHINDA 4-0 DHIDI YA MKONZE VETERANS

Na Eric Amani, Dodoma

Timu ya Utumishi Sports Club (UTUMISHI SC) imeendelea kuonyesha kiwango kizuri baada ya kupata ushindi mnono wa mabao 4-0 dhidi ya Mkonze Veterans katika mchezo wa kirafiki wa soka uliochezwa leo Septemba 05, 2026 katika uwanja wa John Merlin Jijini Dodoma.

UTUMISHI SC ilitawala mchezo kwa kiasi kikubwa, ikionyesha umakini, nidhamu na ushirikiano mzuri wa kikosi katika maeneo yote ya uwanja. Ushindi huo unaongeza morali kwa timu huku ukiendelea kujenga maandalizi na ushindani kuelekea mashindano ya SHIMIWI 2026 Mkoani Kilimanjaro.

Uongozi na wachezaji wa UTUMISHI SC wameendelea kuhimizana kuzingatia maadili ya Utumishi wa Umma ndani na nje ya Viwanja kuwa nidhamu, upendo, mshikamano na kujituma katika kila mchezo, kwa lengo la kuiweka timu katika kiwango bora zaidi ili kuelekea kutetea ubingwa walioutwaa katika mashindano ya SHIMIWI kwa mwaka 2025 ambayo yalifanyika Jijini Mwanza

 










Friday, September 4, 2026

MKURUGENZI FELISTER SHULI AONGOZA MAFUNZO YA MAADILI KWA WANAMICHEZO WA UTUMISHI

Na Eric Amani, Dodoma

Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Maadali, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Bi. Felister Shuli, Leo Septemba 4, 2026 katika Ukumbi wa Sekretariet ya Ajira ameongoza mafunzo ya maadili kwa wanamichezo wa Ofisi hiyo, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kuhakikisha wanamichezo wanaoshiriki mashindano kuzingatia misingi ya uadilifu, nidhamu, heshima na weledi.

Mafunzo hayo yamejikita katika kuwaelimisha wanamichezo kuhusu umuhimu wa kuzingatia maadili ya Utumishi wa Umma, sheria, taratibu na kanuni zinazoongoza utendaji wa mtumishi wa umma wakati wa mashindano ya SHIMIWI 2026 na Mengine.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Mkurugenzi Shuli amewataka wanamichezo hao kutambua kuwa wanaposhiriki katika mashindano, wanabeba taswira ya Ofisi ya Rais – Utumishi na hivyo wanapaswa kuwa mfano wa kuigwa katika nidhamu, mwenendo na matumizi sahihi ya lugha na vitendo.

Mnapokuwa uwanjani, siyo tu mnashindana kama wanamichezo, bali pia mnawakilisha taasisi yenu na Utumishi wa Umma kwa ujumla. Hivyo, kila mmoja anapaswa kuhakikisha mwenendo wake unaendelea kulinda heshima na taswira ya Ofisi,” amesisitiza.

Aidha, amewahimiza wanamichezo hao kutumia mafunzo hayo kama sehemu ya kujijenga katika maisha ya kila siku, kwa kuzingatia misingi ya uwajibikaji, kuheshimu viongozi, waamuzi, wapinzani na wenzao, pamoja na kuepuka vitendo vinavyoweza kuathiri taswira ya taasisi.

Kwa upande wao, wanamichezo walipata fursa ya kuuliza maswali na kupata ufafanuzi kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu maadili, nidhamu na wajibu wao kama watumishi wa umma wanaoshiriki michezo.

Mafunzo hayo ni sehemu ya jitihada za Ofisi ya Rais – Utumishi katika kuimarisha uelewa wa watumishi kuhusu maadili ya Utumishi wa Umma, huku michezo ikiendelea kutumika kama nyenzo ya kujenga afya, mshikamano, ushirikiano na kuongeza tija mahali pa kazi.









Thursday, September 3, 2026

TIMU YA MPIRA WA PETE UTUMISHI YAENDELEA KUIMARIKA, YAICHAPA DOM KINGS 68–42

 Na Eric Amani, Dodoma

Timu ya Mpira wa Pete ya Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imeendelea kuonyesha kiwango kizuri na kuimarika kuelekea mashindano ya SHIMIWI 2026, baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 68–42 dhidi ya timu ya Dom Kings katika mchezo wa mazoezi uliofanyika Agosti 2, 2026 jijini Dodoma.

Katika mchezo huo, Utumishi ilionesha uwezo mzuri wa kiufundi, kasi, umakini na ushirikiano wa wachezaji, hali iliyoiwezesha kutawala mchezo na kupata ushindi wa mabao 68, huku Dom Kings ikiambulia mabao 42.

Mchezo huo ni sehemu ya maandalizi ya timu hiyo kuelekea Mashindano ya Michezo ya Wizara, Idara za Serikali na Mikoa (SHIMIWI) 2026, yanayotarajiwa kufanyika mkoani Kilimanjaro. Maandalizi ya mashindano hayo yameendelea kushika kasi, huku taasisi mbalimbali za Serikali zikiendelea kuimarisha timu zao kupitia mazoezi na michezo ya kirafiki.

Ushindi dhidi ya Dom Kings unaongeza morali kwa kikosi cha Utumishi na kutoa fursa kwa benchi la ufundi kuendelea kutathmini uwezo wa wachezaji, kubaini maeneo yanayohitaji maboresho na kujenga muunganiko bora wa timu kabla ya kuingia kwenye ushindani wa SHIMIWI 2026.

Kwa upande wa wachezaji, ushindi huo umeonesha dhamira yao ya kufanya vizuri katika mashindano hayo, huku wakisisitiza umuhimu wa kuendelea na mazoezi, nidhamu na mshikamano ili kuhakikisha timu inakuwa tayari kwa ushindani mkubwa.









Wednesday, September 2, 2026

SERIKALI KUWEKA MUUNDO MAALUM WA UTUMISHI KWA WATAALAMU WA AFYA WENYE UBOBEZI

Naibu Waziri Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Regina Qwaray amesema Miundo ya Maendeleo ya Utumishi huandaliwa kwa kuzingatia mahitaji ya kiutumishi, majukumu ya kada, pamoja na viwango vya elimu na sifa za kitaaluma vinavyotolewa na taasisi za elimu zilizoidhinishwa.

Mhe. Qwaray amebainisha hayo leo Septemba Mosi 2026 Bungeni Jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Mbulu Vijijini Mhe. Dkt. Emmanuel Qambaji Nuwas, lililouliza Serikali ina mpango gani wa kutambua kwenye Muundo wa Utumishi wa Umma Wataalam wa Kada ya Afya wenye Elimu ngazi ya ubobezi.

Akijibu swali hilo, amesema Ofisi ya Rais Utumishi, ilipokea mapendekezo ya Muundo wa Utumishi kwa Wataalamu wa Kada ya Afya wenye Elimu ngazi ya ubobezi na taratibu kwa ajili ya uchambuzi wa kina na hatua za kupata idhini zinaendelea.



TAALUMA YA UDEREVA KUWA NA STAHA, HADHI NA HESHIMA

Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuboresha taaluma na kazi ya Udereva nchini kwa lengo la kuhakikisha inakuwa na staha, hadhi na heshima sawa na kada nyingine katika Utumishi wa Umma.

Akijibu Swali Na. 59 lililoulizwa Bungeni jijini Dodoma na Mbunge wa Mlalo, Mhe. Rashid Abdallah Shangazi, kuhusu mkakati wa Serikali wa kuhakikisha taaluma na kazi ya udereva inakuwa na staha, hadhi na heshima, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Regina Qwaray amesema Serikali inaendelea kuchukua hatua za kimkakati katika eneo hilo.

Amesema miongoni mwa hatua hizo ni kuboresha Muundo wa Maendeleo ya Utumishi wa Kada ya Udereva, hatua inayolenga kuimarisha nafasi na maendeleo ya watumishi katika kada hiyo pamoja na kuweka mazingira yanayowezesha utekelezaji wa majukumu yao kwa ufanisi.

“Serikali imeendelea kuboresha mafunzo ya kitaaluma na viwango vya elimu kwa kada ya udereva ili kuwawezesha watumishi kuwa na ujuzi na weledi unaoendana na mahitaji ya sasa ya utendaji kazi” amesema Qwaray.

Aidha, amesema Serikali pia inaendelea kuimarisha motisha na maslahi ya kada ya udereva, hatua ambayo inalenga kuongeza morali, ufanisi na tija katika utekelezaji wa majukumu yao.

Amesisitiza kuwa hatua hizo zinaendelea kuzingatia umuhimu wa kuhakikisha kada ya udereva inakuwa na mazingira bora ya utendaji kazi yanayomwezesha mtumishi kukidhi na kumudu mazingira ya utendaji kazi na hivyo kuchangia katika utoaji wa huduma bora kwa wananchi.




TRAMPA YAWASILISHA RIPOTI YA MAANDALIZI YA MKUTANO MKUU WA 14 WA CHAMA HICHO KWA WAZIRI MHE. RIDHIWANI KIKWETI


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Kikwete akizungumza na Viongozi wa TRAMPA waliofika ofisini kwake kwa ajili ya kuwasilisha ripoti ya maandalizi ya Mkutano Mkuu wa 14 wa chama hicho utakaofanyika Jijini Dodoma tarehe 21-25 Septemba, 2026. Aliyesimama ni Mwenyekiti wa TRAMPA Bi. Devota Mrope.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Kikwete akipokea ripoti ya maandalizi ya Mkutano Mkuu wa 14 wa TRAMPA utakaofanyika Jijini Dodoma kutoka kwa Mwenyekiti wa TRAMPA Bi. Devota Mrope. Zoezi hilo limefanyika ofisini kwake Mtumba Jijini Dodoma Septemba 1, 2026.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Kikwete akizungumza na Viongozi wa TRAMPA mara baada ya kupoke ripoti ya maandalizi ya Mkutano Mkuu wa 14 wa TRAMPA utakaofanyika Jijini Dodoma tarehe 21-25 Septemba, 2026.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Kikwete akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Wakurugenzi wa Ofisi yake na Viongozi wa TRAMPA mara baada ya kupoke ripoti ya maandalizi ya Mkutano Mkuu wa 14 wa TRAMPA utakaofanyika Jijini Dodoma tarehe 21-25 Septemba, 2026.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Kikwete akizungumza na Viongozi wa TRAMPA (hawapo pichani) mara baada ya kupoke ripoti ya maandalizi ya Mkutano Mkuu wa 14 wa TRAMPA utakaofanyika Jijini Dodoma tarehe 21-25 Septemba, 2026.

Tuesday, September 1, 2026

KATIBU MKUU MKOMI AONGOZA KIKAO CHA KAMATI KUU YA UFUATILIAJI NA TATHIMINI

 Na Eric Amani, Dodoma

Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Juma Mkomi ameongoza Kikao cha Kamati Kuu ya Ufuatiliaji na Tathmini kilichojadili Taaifa ya Ufuatiliaji wa Utekelezaji wa Majukumu ya Ofisi ya Rais – Utumishi kwa Robo ya Nne ya Mwaka wa Fedha 2025/2026.

Kikao hicho kimefanyika leo Septemba 01, 2026 katika ukumbi wa Nyaraka Jijini Dodoma kwa lengo la kupitia na kutathmini kiwango cha utekelezaji wa majukumu, mipango, shughuli na malengo yaliyowekwa na Ofisi katika kipindi cha robo ya nne ya mwaka wa fedha 2025/2026.

Akizungumza wakati wa kikao hicho, Bw. Mkomi amesisitiza umuhimu wa ufuatiliaji na tathmini katika kuhakikisha kuwa mipango na shughuli za Ofisi zinatekelezwa kwa ufanisi, kwa wakati na kwa kuzingatia viashiria vya utendaji vilivyowekwa.

Amesema ufuatiliaji na tathmini ni nyenzo muhimu katika kupima matokeo ya utekelezaji wa mipango ya Serikali, kutambua maeneo yanayohitaji maboresho na kuwezesha uongozi kufanya maamuzi yanayozingatia ushahidi.

“Ni muhimu taarifa za ufuatiliaji na tathmini zisitumike tu kwa ajili ya kuonesha kiwango cha utekelezaji, bali pia ziwe msingi wa kufanya maboresho na kuchukua hatua stahiki pale ambapo utekelezaji haujafikia malengo yaliyokusudiwa,” amesema Bw. Mkomi.

Katika hatua nyingine, amewataka viongozi na watendaji wa Ofisi kuhakikisha utekelezaji wa majukumu yao unaendana na mipango na vipaumbele vilivyowekwa, huku wakizingatia matumizi bora ya rasilimali, uwajibikaji na utoaji wa huduma zenye tija kwa wananchi.

Pamoja na mambo mengine, kamati pia imejadili maeneo yanayohitaji kuimarishwa katika kipindi kijacho, ikiwemo kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa mipango, kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji wa utekelezaji wa shughuli na kuhakikisha taarifa za utendaji zinawasilishwa kwa wakati na kwa kuzingatia viashiria vilivyowekwa.

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais – UTUMISHI Bw. Juma Mkomi akizungumza na viongozi mbalimbali wa Ofisi ya Rais – UTUMISHI wakati wa Kikao cha Kamati Kuu ya Ufuatiliaji na Tathmini katika Ukumbi wa Nyaraka Jijini Dodoma Agosti 1, 2026


Baadhi ya Wakurugenzi kutokea Ofisi ya Rais – UTUMISHI wakifatilia Kikao cha Kamati Kuu ya Ufuatiliaji na Tathmini katika Ukumbi wa Nyaraka Jijini Dodoma Agosti 1, 2026


Viongozi Mbalimbali kutokea Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wakimsikiliza Katibu Mkuu Ofisi ya Rais – UTUMISHI Bw. Juma Mkomi (Aliyeshikilia Mic) wakati wa Kikao cha Kamati Kuu ya Ufuatiliaji na Tathmini Septemba 1, 2026 Jijini Dodoma



Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma Bw. Nolasco J. Kipanda akifatilia Kikao cha Kamati Kuu ya Ufuatiliaji na Tathmini kinacho ratibiwa na Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Septemba 1, 2026 katika Ukumbi wa Nyaraka uliyopo Jijini Dodoma


Meneja Mipango na Maendeleo Bi. Mwanaidi Mdee kutokea Chuo Cha Utumishi wa Umma (TPSC) akiwasilisha mada katika Kikao cha Kamati Kuu ya Ufuatiliaji na Tathmini Septemba 1, 2026 


Monday, August 31, 2026

NAIBU KATIBU MKUU LWANGILI AWATAKIA KHERI NA BARAKA WATUMISHI WALIOZALIWA MWEZI AGOSTI HUKU AKIWASISITIZA KUWATUMIKIA WANANCHI KWA UFASAHA

Na Antonia Mbwambo-Dodoma

Tarehe 31 Agosti, 2026

Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bi. Prisca Lwangili, ameungana na Menejimenti na Watumishi wa Ofisi hiyo kuwatakia kheri na baraka Watumishi waliozaliwa mwezi Agosti, katika kumbukizi ya siku zao za kuzaliwa huku akiwasisitiza kuwatumikia wananchi kwa ufasaha.

Bi. Lwangili ametoa pongezi hizo leo tarehe 31 Agosti, 2026 mara baada ya kuhitimisha mafunzo yaliyohusu Taratibu za Ushughulikiaji wa Mashauri ya Nidhamu yaliyotolewa katika eneo maalumu la Ofisi ya Rais-UTUMISHI Mtumba Jijini Dodoma

Ametumia fursa hiyo kuwashukuru Watumishi hao kwa kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa kujituma, uadilifu na kuzingatia uwajibikaji katika utumishi.

Amewatakia Watumishi hao afya njema, furaha na mafanikio katika maisha yao, huku akiwahimiza kuendelea kumshukuru Mungu kwa zawadi ya uhai na nafasi ya kuwatumikia wananchi.

Aidha, amewaombea Mungu awabariki, awaongoze na awatimizie kila jambo jema alilolipanga kuwapa Mwenyezi Mungu katika maisha yao, huku akiwatakia maisha yenye amani, furaha, upendo na mafanikio.









NAIBU KATIBU MKUU LWANGILI ASISITIZA UZINGATIAJI WA SHERIA KATIKA USHUGHULIKIAJI WA MASHAURI YA NIDHAMU KATIKA UTUMISHI WA UMMA

Na Antonia Mbwambo – Dodoma

Tarehe 31 Agosti, 2026

Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bi. Prisca Lwangili, amesisitiza umuhimu wa kuzingatia Sheria, Taratibu na Kanuni katika kushughulikia mashauri ya nidhamu katika Utumishi wa Umma, akieleza kuwa uzingatiaji wa misingi hiyo ni muhimu katika kuhakikisha haki inatendeka.

Bi. Lwangili ameyasema hayo leo, tarehe 31 Agosti, 2026, wakati akihitimisha mafunzo ya uelewa kwa Watumishi wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI yaliyofanyika katika eneo maalumu la Ofisi hiyo Mtumba Jijini Dodoma.

Bi. Lwangili amesema katika kushughulikia masuala ya nidhamu ni muhimu kuhakikisha kuwa thamani na utu wa mtu vinalindwa, huku hatua zote zikichukuliwa kwa kuzingatia Sheria, Taratibu na Kanuni zilizowekwa.

“Ni muhimu kuhakikisha kuwa katika kushughulikia mashauri ya nidhamu, Sheria, Taratibu na Kanuni zinafuatwa ili haki itendeke, huku tukilinda thamani na utu wa mtu, amesema Bi. Lwangili.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuwakumbusha Watumishi wa Umma kuhusu madhara ya kutokuzingatia Sheria, Taratibu na Kanuni katika utekelezaji wa majukumu yao, akieleza kuwa uelewa huo utasaidia kupunguza makosa na kuwaepusha watumishi na changamoto ya kufikishwa katika mashauri ya kinidhamu.

Kwa upande wake mwezeshaji wa mafunzo hayo ambaye ni  Afisa Sheria Mwandamizi, kutoka Ofisi ya Rais-UTUMISHI Bw. Edwin Bilikundi, amesema usimamizi wa nidhamu katika Utumishi wa Umma umejengwa katika dhana mbili kuu ambazo ni kurekebisha mwenendo wa Mtumishi (corrective measures) na utoaji wa adhabu (sanction approach). Amesema njia ya kurekebisha inalenga kumsaidia Mtumishi kutambua kosa na kujirekebisha, wakati utoaji wa adhabu hutumika pale kosa linapothibitika, hususan kwa makosa yanayojirudia au yenye uzito.

Bw. Bilikundi ameongeza kuwa mchakato wa kinidhamu unapaswa kuanza kwa uchunguzi wa awali unaolenga kubaini ukweli na uzito wa tuhuma, pamoja na kuamua hatua stahiki za kuchukua.

Amesisitiza kuwa uzingatiaji wa hatua na muda uliowekwa katika Sheria, Kanuni na Taratibu ni muhimu katika kuhakikisha mchakato wa nidhamu unakuwa wa haki na wenye msingi sahihi wa kisheria.

Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bi. Prisca Lwangili akizungumza na Watumishi wa Ofisi hiyo (hawapo pichani) wakati Naibu Katibu Mkuu huyo akihitimisha mafunzo yaliyolenga kuwajengea Watumishi hao uelewa kuhusu Ushughulikiaji wa Mashauri ya Nidhamu katika Utumishi wa Umma, yaliyofanyika tarehe 31 Agosti, 2026 katika eneo maalumu la Ofisi hiyo, Mtumba, jijini Dodoma.

Baadhi ya Wakurugenzi na Watumishi kutoka Ofisi ya Rais-UTUMISHI, wakifurahia jambo wakati walipokuwa wakifuatilia mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kiutendaji leo tarehe 31 Agosti, 2026 katika eneo maalumu la Ofisi hiyo Mtumba jijini Dodoma

Afisa Sheria Mwandamizi, kutoka Ofisi ya Rais-UTUMISHI Bw. Edwin Bilikundi akiendesha mafunzo ya uelewa kuhusu Ushughulikiaji wa Mashauri ya Nidhamu katika Utumishi wa Umma kwa Watumishi wa Ofisi hiyo leo tarehe 31 Agosti 2026 katika eneo maalumu la Ofisi hiyo, Mtumba, jijini Dodoma.

Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Musa Magufuli akisisitiza jambo wakati wa mafunzo ya uelewa kuhusu Ushughulikiaji wa Mashauri ya Nidhamu katika Utumishi wa Umma Mtumba Jijini Dodoma


Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bi. Prisca Lwangili  akisisitiza jambo wakati akihitimisha mafunzo ya kuwajengea Watumishi hao uelewa kuhusu Ushughulikiaji wa Mashauri ya Nidhamu katika Utumishi wa Umma, yaliyofanyika tarehe 31 Agosti, 2026 katika eneo maalumu la Ofisi hiyo, Mtumba, jijini Dodoma

Baadhi ya Watumishi kutoka Ofisi ya Rais-UTUMISHI, wakifurahia jambo wakati walipokuwa wakifuatilia mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kiutendaji leo tarehe 31 Agosti, 2026 katika eneo maalumu la Ofisi hiyo Mtumba jijini Dodoma

Baadhi ya Wakurugenzi na Watumishi kutoka Ofisi ya Rais-UTUMISHI, wakifurahia jambo wakati walipokuwa wakifuatilia mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kiutendaji leo tarehe 31 Agosti, 2026 katika eneo maalumu la Ofisi hiyo Mtumba jijini Dodoma

Baadhi ya Wakurugenzi na Watumishi kutoka Ofisi ya Rais-UTUMISHI, wakifurahia jambo wakati walipokuwa wakifuatilia mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kiutendaji leo tarehe 31 Agosti, 2026 katika eneo maalumu la Ofisi hiyo Mtumba jijini Dodoma

Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bi. Prisca Lwangili (wa pili kutoka kushoto) akifurahia jambo wakati alipokuwa akifuatilia mafunzo kuhusu Ushughulikiaji wa Mashauri ya Nidhamu katika Utumishi wa Umma leo Agosti 31, 2026 Mtumba Jijini Dodoma

Mkurugenzi wa Idara ya Utawala wa Utumishi wa Umma, SACP. Ibrahim Mahumi kutoka Ofisi ya Rais-UTUMISHI akisisitiza jambo wakati wa mafunzo ya uelewa kuhusu Ushughulikiaji wa Mashauri ya Nidhamu katika Utumishi wa Umma Mtumba Jijini Dodoma