Friday, August 28, 2020

Wednesday, August 26, 2020

Thursday, August 20, 2020

MKUCHIKA AITAKA TAKUKURU KUHAKIKISHA WANANCHI WANAPATA HAKI PINDI WANAPOPOKEA HUDUMA

Na. James K. Mwanamyoto – Namtumbo

Tarehe 20 Agosti, 2020.

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imetakiwa kuhakikisha wananchi wanapata haki wanazostahili popote pale wanapoenda kupata huduma nchini, iwe ni kwenye taasisi za umma au binafsi.

Agizo hilo limetolewa wilayani Namtumbo jana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Kapt. (Mst) Mhe. George H. Mkuchika wakati akizindua jengo la Ofisi ya TAKUKURU Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma.

Mhe. Mkuchika amefafanua kuwa, TAKUKURU inatakiwa kuwajengea wananchi imani ya kiutendaji ili pale inapotokea wananyang’anywa haki zao na mtu au taasisi yoyote kwa njia za rushwa, TAKUKURU ndio iwe ni kimbilio lao huku wakiwa na imani kuwa watasaidiwa ipasavyo na taasisi hiyo.

“Nawasihi, endeleeni kuwang’ata wala rushwa na mafisadi wote ili mradi msimuonee au kumpendelea yeyote, na endeleeni kuifanya haki ndio nguzo ya utendaji kazi wenu wa kila siku,” Mhe. Mkuchika alihimiza.

Awali, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Bibi Sabina Seja akitoa maelezo kuhusu jengo hilo alisema, uzinduzi wa jengo la TAKUKURU Wilaya ya Namtumbo ni ushaidi tosha kuwa Serikali inayoongozwa na Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli imeonesha nia na dhamira ya dhati ya kukabiliana na vitendo vya rushwa, ubadhirifu wa mali za umma nchini.

Bibi Seja, amemtibitishia Mhe. Mkuchika kuwa, Watumishi wa TAKUKURU wilayani Namtumbo watatumia jengo la ofisi hiyo kuhakikisha wanapambana na vitendo vya rushwa, ufisadi na ubadhirifu kwa manufaa ya wananchi na maslahi ya taifa.

Mhe. Mkuchika amezindua jengo hilo la TAKUKURU Wilaya ya Namtumbo, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ambaye tangu aingie madarakani amefanya kazi kubwa ya kuimarisha na kuendeleza mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi nchini.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt. (Mst) Mhe. George H. Mkuchika akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Namtumbo (hawapo pichani) kabla ya kuzindua Jengo la ofisi ya TAKUKURU la wilaya hiyo Agosti 19, 2020.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt. (Mst) Mhe. George H. Mkuchika akikata utepe kuzindua jengo la Ofisi ya TAKUKURU Wilaya ya Namtumbo, Agosti 19, 2020. Wa kwanza kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Mhe. Christina Mndeme na kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa TAKUKURU, Bibi Sabina Seja.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt. (Mst) Mhe. George H. Mkuchika akizindua jengo la Ofisi ya TAKUKURU Wilaya ya Namtumbo. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Mhe. Christina Mndeme na Kaimu Mkurugenzi wa TAKUKURU, Bibi Sabina Seja.

Kaimu Mkurugenzi wa TAKUKURU, Bibi Sabina Seja akitoa maelezo    kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt. (Mst) Mhe. George H. Mkuchika kuhusu jengo la Ofisi ya TAKUKURU Wilaya ya Namtumbo kabla ya Waziri huyo kulizindua rasmi Agosti 19, 2020.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt. (Mst) Mhe. George H. Mkuchika akiwa katika picha ya pamoja na Watumishi wa TAKUKURU mara baada ya kuzindua jengo la Ofisi ya TAKUKURU Wilaya ya Namtumbo, Agosti 19, 2020. Kulia kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Mhe. Christina Mndeme na kushoto kwake ni Kaimu Mkurugenzi wa TAKUKURU, Bibi Sabina Seja.

Thursday, August 13, 2020

OFISI YA INTELIJENSIA YA TAKUKURU KUIMARISHA OPERESHENI ZA KIUCHUNGUZI DHIDI YA VITENDO VYA RUSHWA NCHINI

Na. James K. Mwanamyoto – Dodoma

Tarehe 13 Agosti, 2020.

Kurugenzi ya Intelijensia ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imedhamiria kuimarisha utekelezaji wa operesheni za kiuchunguzi za TAKUKURU dhidi ya vitendo vya rushwa vinavyojitokeza kwa maana ya ufuatiliaji na uchakataji wa taarifa za kiintelijensia zinazopatikana kutoka katika maeneo mbalimbali kwa lengo la kutokomeza vitendo vya rushwa nchini.

Hayo yamesemwa jana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Kapt. (Mst) Mhe. George H. Mkuchika wakati akitoa neno la utangulizi kumkaribisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa kuzindua jengo la Ofisi ya Intelijensia ya TAKUKURU lililojengwa Makao Makuu ya Nchi Dodoma.

Mhe. Mkuchika amefafanua kuwa, jengo hilo ni muhimu sana kwa Serikali ambayo imedhamiria kwa dhati kutokomeza vitendo vya rushwa nchini kwani litatumiwa ipasavyo na watumishi wa Kurugenzi ya Intelijensia ya TAKUKURU kufanya uchunguzi makini, ufuatiliaji wa kina na kuchakata taarifa za kiintelijensia kwa weledi.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Brig. Jenerali John Mbungo wakati akitoa maelezo kuhusu jengo hilo alisema, Kurugenzi ya Intelijensia ni sehemu ya ofisi za Makao Makuu ya TAKUKURU lakini kutokana na unyeti wa kazi zake imetengwa peke yake ili kuiongezea ufanisi kiutendaji.

“Kurugenzi hii ndio inayoshughulika na upatikanaji pamoja na uchakataji wa taarifa mbalimbali zinazosaidia kufanyika kwa operesheni za kiuchunguzi za kuzuia kutokea kwa vitendo vya rushwa nchini”, Brig. Mbungo amefafanua.

Kurugenzi ya Intelijensia ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ilianzishwa mwaka 2018 baada ya muundo mpya wa TAKUKURU kuidhinishwa Novemba 15, 2018 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa akikata utepe kuzindua jengo la Ofisi ya Intelijensia ya TAKUKURU Makao Makuu ya Nchi Dodoma, Agosti 12, 2020. Kushoto kwake ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Utumishi na Utawala Bora, Kapt. (Mst) Mhe. George H. Mkuchika, kulia kwake ni Naibu Waziri, Ofisi ya Rais-Utumishi na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa na Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Brig. Jenerali John Mbungo.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa akifungua jengo la Ofisi ya Intelijensia ya TAKUKURU Makao Makuu ya Nchi Dodoma, Agosti 12, 2020. Wengine ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Utumishi na Utawala Bora, Kapt. (Mst) Mhe. George H. Mkuchika, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais-Utumishi na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa na Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Brig. Jenerali John Mbungo.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa akimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Utumishi na Utawala Bora, Kapt. (Mst) Mhe. George H. Mkuchika alipowasili kwenye jengo la Ofisi ya Intelijensia ya TAKUKURU Makao Makuu ya Nchi Dodoma kwa ajili ya kulizindua. Anayeshuhudia ni Naibu Waziri, Ofisi ya Rais-Utumishi na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa akisalimiana na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais-Utumishi na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa alipowasili kwenye jengo la Ofisi ya Intelijensia ya TAKUKURU Makao Makuu ya Nchi Dodoma kwa ajili ya kulizindua. Anayeshuhudia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Utumishi na Utawala Bora, Kapt. (Mst) Mhe. George H. Mkuchika na Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Brig. Jenerali John Mbungo (mwenye sare za jeshi).


Sunday, August 9, 2020

TAKUKURU HAIKO TAYARI KUCHAFULIWA NA MTUMISHI WAKE ANAYEJIHUSISHA NA RUSHWA NA UBADHIRIFU

Na. James K. Mwanamyoto Mpwapwa

Tarehe 09 Agosti, 2020.

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) haiko tayari kuchafuliwa na mtumishi wake yeyote anayejihusisha na vitendo vya rushwa na ubadhirifu ikizingatiwa kuwa, taasisi hiyo imejenga taswira nzuri kwa wananchi kwa kufanya kazi nzuri ya kupambana na vitendo vya rushwa na ubadhirifu wa rasilimali za umma katika kipindi cha miaka mitano ya utawala wa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ambaye amejipambanua kwa vitendo kuichukia rushwa.

Hayo yamesemwa jana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt. (Mst) Mhe. George H. Mkuchika, wakati akimkaribisha Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kuzindua Jengo la Ofisi ya TAKUKURU Wilaya ya Mpwapwa.

Mhe. Mkuchika amemhakikishia Makamu wa Rais kuwa, TAKUKURU haitamvumilia mtumishi yeyote atakayeshiriki vitendo vya rushwa na ubadhirifu ambavyo vinakwamisha huduma kwa wananchi na miradi mbalimbali ya maendeleo.

Sanjali na hilo, Mhe. Mkuchika amefarijika kuona TAKUKURU imeshawachukulia hatua watumishi wote wa taasisi hiyo waliohusika na ubadhirifu wa fedha za umma wakati wa ujenzi wa baadhi ya Ofisi za TAKUKURU Wilaya ikiwemo ya Chamwino iliyozinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli  tarehe 22 Julai, 2020 ambapo alibaini ubadhirifu huo baada kukagua jengo hilo na kutoridhishwa na thamani ya fedha iliyotumika.

Watumishi wote waliohusika na kubainika kujihusisha na ubadhirifu wamechukuliwa hatua stahiki za kinidhamu na kisheria na watafikishwa mahakamani hivi karibuni, Mhe. Mkuchika amemthibitishia Makamu wa Rais.

Awali, akitoa maelezo kuhusu jengo la Ofisi ya TAKUKURU Wilaya ya Mpwapwa, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Brig Jen. John Julius Mbungo, alisema aliunda tume huru ya uchunguzi iliyobaini ubadhirifu kwenye ujenzi wa Ofisi za TAKUKURU Wilaya ya Chamwino na Mpwapwa na kwenye Ofisi ya Intelijensia Dodoma ambapo tayari TAKUKURU imeshawachukulia hatua za kinidhamu na kisheria kwa waliobanika na watafikishwa mahakamani hivi karibuni.

Kufuatia hatua hiyo, Brig. Jen. Mbungo amemuomba Mhe. Samia Suluhu Hassan kumfikishia taarifa hiyo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ikiwa ni sehemu ya mrejesho wa utekelezaji wa maelekezo aliyoyatoa pindi alipobaini ubadhilifu huo wakati akizindua Jengo la Ofisi ya TAKUKURU Wilaya ya Chamwino.

 


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akikata Utepe  kuzindua rasmi Jengo la Ofisi ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Wilaya ya Mpwapwa Mkoani Dodoma Agosti 08, 2020.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Kapt. (Mst) Geoge Mkuchika akikamribisha  Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan (hayupo pichani) kuzungumza na Wananchi wa Wilaya ya Mpwapwa wakati wa hafla ya uzinduzi wa Jengo la Ofisi ya TAKUKURU ya wilaya hiyo uliofanyika Agosti 08, 2020.        

Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Brig Jen. John Julius Mbungo akitoa maelezo kuhusu ujenzi wa jengo la Ofisi ya TAKUKURU wilaya ya Mpwapwa kabla ya kumkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Kapt. (Mst) Mhe. Geoge Mkuchika wakati wa hafla ya uzinduzi wa Jengo la Ofisi ya TAKUKURU ya wilaya hiyo uliofanyika Agosti 08, 2020.    

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akizungumza na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Kapt. (Mst) Mhe. Geoge Mkuchika wakati wa hafla ya uzinduzi wa Jengo la Ofisi ya TAKUKURU Wilaya ya Mpwapwa Mkoani Dodoma uliofanyika Agosti 08, 2020.        

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akiondoa Kitambaa kuzindua rasmi Jengo la Ofisi ya Taasisi ya Kuzuwia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU Wilaya ya Mpwapwa Mkoani Dodoma Agosti 08, 2020.

Friday, August 7, 2020

DKT. MWANJELWA AITAKA TPSC KUFANYA TAFITI ZITAKAZOTUMIKA KUBORESHA UTUMISHI WA UMMA NCHINI


Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) kimetakiwa kuhakikisha kinafanya tafiti zenye tija zitakazoiwezesha Serikali kufanya maboresho ya utendaji kazi katika taasisi za umma nchini, ili taasisi hizo ziweze kutoa mchango katika maendeleo ya taifa.

Wito huo umetolewa jana na Naibu Waziri,  Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa  wakati wa Mahafali ya 32 ya Chuo cha Utumishi wa Umma yaliyofanyika katika Kampasi ya Tabora.

Dkt. Mwanjelwa amesisitiza kuwa, taasisi zinazofanywa ni lazima ziendane na kasi ya mabadiliko ya kiuchumi hususani wakati huu ambao nchi imeingia katika uchumi wa kati.

“Ni muhimu kufanya tafiti zenye tija katika kuboresha Utumishi wa Umma ili uwe na manufaa katika maendeleo ya kichumi na taifa kwa ujumla,” Dkt. Mwanjelwa alisisitiza.

Aidha, Dkt. Mwanjelwa amewataka waajiri katika taasisi za umma kuwawezesha Watumishi wa Umma kupata mafuzo yanayotolewa na TPSC  ili kuwaongezea ujuzi na weledi utakaowawezesha kutoa huduma bora kwa wananchi,  ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono jitihada za Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli za kuboresha huduma kwa umma.

Sanjali na hilo, Dkt. Mwanjelwa amewahimiza waajiri kuwawezesha watumishi  kupata mafunzo maalum ya kuwaandaa kufanya mitihani ya Utumishi wa Umma kulingana na kada zao ambayo ipo kwa mujibu wa taratibu za kiutumishi.

Katika hatua nyingine Dkt. Mwanjelwa amewakumbusha wahitimu kujilinda dhidi ya magonjwa hatarishi yatakayoathiri afya zao na kushindwa kutumia elimu na ujuzi walioupata katika ujenzi wa taifa.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu na Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania, Dkt. Emmanuel Shindika amesema, chuo kimeendelea kuwajengea uwezo watumishi wake kitaaluma ili kuhakikisha Watumishi wa Umma na wananchi wanaopata fursa ya mafunzo katika chuo chake wanapata elimu bora na ujuzi utakaowawezesha kutoa mchango katika maendeleo ya taifa.

Kuhusu idadi ya wahitimu, Dkt. Shindika amesema, jumla ya wanachuo 1,917 kutoka katika kampasi sita za Dar es Salaam, Tabora, Mtwara, Mbeya, Singida na Tanga wamehitimu katika Mahafali ya 32 ya Chuo cha Utumishi wa Umma  kwa mwaka 2020 yaliyofanyika katika Kampasi ya Tabora.

 

Naibu Waziri,  Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa, akiongoza maandamano ya Wahitimu wa kozi mbalimbali katika mahafali ya 32  ya Chuo cha Utumishi wa Umma yaliyofanyika katika Kampasi ya Tabora. Kushoto kwake ni Mtendaji Mkuu na Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania, Dkt. Emmanuel Shindika na kulia kwake ni Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania, Dkt. Charles Msonde.

Naibu Waziri , Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa akimtunuku cheti mmoja wa wahitimu wa Chuo cha Utumishi wa Umma wakati wa Mahafali ya 32 ya Chuo hicho yaliyofanyika jana katika Kampasi ya Tabora.

Naibu Waziri,  Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa akiimba wimbo pamoja na wanakwaya wa Chuo cha Utumishi wa Umma  wakati wa Mahafali ya 32 ya Chuo hicho mjini Tabora yaliyofanyika jana katika Kampasi ya Tabora.