Tarehe 09 Agosti, 2020.
Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) haiko tayari kuchafuliwa na mtumishi wake yeyote
anayejihusisha na vitendo vya rushwa na ubadhirifu ikizingatiwa kuwa, taasisi
hiyo imejenga taswira nzuri kwa wananchi kwa kufanya kazi nzuri ya kupambana na
vitendo vya rushwa na ubadhirifu wa rasilimali za umma katika kipindi cha miaka
mitano ya utawala wa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mhe. Dkt. John
Pombe Joseph Magufuli ambaye amejipambanua kwa vitendo kuichukia rushwa.
Hayo yamesemwa jana na Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt.
(Mst) Mhe. George H. Mkuchika, wakati
akimkaribisha Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia
Suluhu Hassan kuzindua Jengo la Ofisi ya TAKUKURU Wilaya ya Mpwapwa.
Mhe. Mkuchika amemhakikishia
Makamu wa Rais kuwa, TAKUKURU haitamvumilia mtumishi yeyote atakayeshiriki
vitendo vya rushwa na ubadhirifu ambavyo vinakwamisha huduma kwa wananchi na miradi
mbalimbali ya maendeleo.
Sanjali na hilo, Mhe.
Mkuchika amefarijika kuona TAKUKURU imeshawachukulia hatua watumishi wote wa
taasisi hiyo waliohusika na ubadhirifu wa fedha za umma wakati wa ujenzi wa
baadhi ya Ofisi za TAKUKURU Wilaya ikiwemo ya Chamwino iliyozinduliwa na Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli tarehe 22 Julai, 2020 ambapo alibaini ubadhirifu
huo baada kukagua jengo hilo na kutoridhishwa na thamani ya fedha iliyotumika.
Watumishi wote waliohusika
na kubainika kujihusisha na ubadhirifu wamechukuliwa hatua stahiki za kinidhamu
na kisheria na watafikishwa mahakamani hivi karibuni, Mhe. Mkuchika
amemthibitishia Makamu wa Rais.
Awali, akitoa maelezo kuhusu
jengo la Ofisi ya TAKUKURU Wilaya ya Mpwapwa, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Brig
Jen. John Julius Mbungo, alisema aliunda tume huru ya uchunguzi iliyobaini
ubadhirifu kwenye ujenzi wa Ofisi za TAKUKURU Wilaya ya Chamwino na Mpwapwa na kwenye
Ofisi ya Intelijensia Dodoma ambapo tayari TAKUKURU imeshawachukulia hatua za
kinidhamu na kisheria kwa waliobanika na watafikishwa mahakamani hivi karibuni.
Kufuatia hatua hiyo, Brig.
Jen. Mbungo amemuomba Mhe. Samia Suluhu Hassan kumfikishia taarifa hiyo Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ikiwa ni sehemu
ya mrejesho wa utekelezaji wa maelekezo aliyoyatoa pindi alipobaini ubadhilifu
huo wakati akizindua Jengo la Ofisi ya TAKUKURU Wilaya ya Chamwino.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mhe. Samia Suluhu Hassan, akikata Utepe kuzindua rasmi Jengo la Ofisi ya
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Wilaya ya Mpwapwa Mkoani
Dodoma Agosti 08, 2020.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Kapt. (Mst) Geoge Mkuchika
akikamribisha Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan (hayupo pichani) kuzungumza na Wananchi wa
Wilaya ya Mpwapwa wakati wa
hafla ya uzinduzi wa Jengo la Ofisi ya TAKUKURU ya wilaya hiyo uliofanyika
Agosti 08, 2020.
Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU,
Brig Jen. John Julius Mbungo akitoa maelezo kuhusu ujenzi wa jengo la Ofisi ya
TAKUKURU wilaya ya Mpwapwa kabla ya kumkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora Kapt. (Mst) Mhe. Geoge Mkuchika wakati
wa hafla ya uzinduzi wa Jengo la Ofisi ya TAKUKURU ya wilaya hiyo uliofanyika
Agosti 08, 2020.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mhe. Samia Suluhu Hassan, akizungumza na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Kapt. (Mst) Mhe. Geoge
Mkuchika wakati wa hafla ya uzinduzi wa Jengo la Ofisi ya TAKUKURU Wilaya
ya Mpwapwa Mkoani Dodoma uliofanyika Agosti 08, 2020.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mhe. Samia Suluhu Hassan, akiondoa Kitambaa kuzindua rasmi Jengo la Ofisi ya
Taasisi ya Kuzuwia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU Wilaya ya Mpwapwa Mkoani
Dodoma Agosti 08, 2020.
No comments:
Post a Comment