Na. James K. Mwanamyoto – Dodoma
Tarehe 13 Agosti, 2020.
Kurugenzi ya Intelijensia ya Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imedhamiria kuimarisha utekelezaji wa operesheni
za kiuchunguzi za TAKUKURU dhidi ya vitendo vya rushwa vinavyojitokeza kwa
maana ya ufuatiliaji na uchakataji wa taarifa za kiintelijensia zinazopatikana
kutoka katika maeneo mbalimbali kwa lengo la kutokomeza vitendo vya rushwa
nchini.
Hayo yamesemwa jana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Kapt. (Mst) Mhe. George H.
Mkuchika wakati akitoa neno la utangulizi kumkaribisha Waziri Mkuu wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa kuzindua jengo la Ofisi
ya Intelijensia ya TAKUKURU lililojengwa Makao Makuu ya Nchi Dodoma.
Mhe. Mkuchika amefafanua kuwa, jengo hilo ni muhimu sana
kwa Serikali ambayo imedhamiria kwa dhati kutokomeza vitendo vya rushwa nchini
kwani litatumiwa ipasavyo na watumishi wa Kurugenzi ya Intelijensia ya TAKUKURU
kufanya uchunguzi makini, ufuatiliaji wa kina na kuchakata taarifa za
kiintelijensia kwa weledi.
Awali, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Brig. Jenerali John
Mbungo wakati akitoa maelezo kuhusu jengo hilo alisema, Kurugenzi ya
Intelijensia ni sehemu ya ofisi za Makao Makuu ya TAKUKURU lakini kutokana na
unyeti wa kazi zake imetengwa peke yake ili kuiongezea ufanisi kiutendaji.
“Kurugenzi hii ndio inayoshughulika na upatikanaji pamoja
na uchakataji wa taarifa mbalimbali zinazosaidia kufanyika kwa operesheni za
kiuchunguzi za kuzuia kutokea kwa vitendo vya rushwa nchini”, Brig. Mbungo
amefafanua.
Kurugenzi ya Intelijensia ya Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ilianzishwa mwaka 2018 baada ya muundo mpya wa
TAKUKURU kuidhinishwa Novemba 15, 2018 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa akikata utepe kuzindua jengo la Ofisi ya
Intelijensia ya TAKUKURU Makao Makuu ya Nchi Dodoma, Agosti 12, 2020. Kushoto
kwake ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Utumishi na Utawala Bora, Kapt. (Mst)
Mhe. George H. Mkuchika, kulia kwake ni Naibu Waziri, Ofisi ya Rais-Utumishi na
Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa na Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Brig.
Jenerali John Mbungo.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa akifungua jengo la Ofisi ya Intelijensia ya
TAKUKURU Makao Makuu ya Nchi Dodoma, Agosti 12, 2020. Wengine ni Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Rais-Utumishi na Utawala Bora, Kapt. (Mst) Mhe. George H.
Mkuchika, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais-Utumishi na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary
Mwanjelwa na Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Brig. Jenerali John Mbungo.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa akimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais-Utumishi na Utawala Bora, Kapt. (Mst) Mhe. George H. Mkuchika alipowasili
kwenye jengo la Ofisi ya Intelijensia ya TAKUKURU Makao Makuu ya Nchi Dodoma
kwa ajili ya kulizindua. Anayeshuhudia ni Naibu Waziri, Ofisi ya Rais-Utumishi
na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa akisalimiana na Naibu Waziri, Ofisi ya
Rais-Utumishi na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa alipowasili kwenye jengo
la Ofisi ya Intelijensia ya TAKUKURU Makao Makuu ya Nchi Dodoma kwa ajili ya
kulizindua. Anayeshuhudia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Utumishi na Utawala
Bora, Kapt. (Mst) Mhe. George H. Mkuchika na Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Brig.
Jenerali John Mbungo (mwenye sare za jeshi).
No comments:
Post a Comment