Wednesday, July 28, 2021

TASAF YATOA MILIONI 193 KUBORESHA HUDUMA YA AFYA YA MAMA NA MTOTO KIJIJI CHA MKAMBARANI MKOANI MOROGORO

 Na. James K. Mwanamyoto-Morogoro

Tarehe 28 Julai, 2021

Serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) imetoa kiasi cha shilingi milioni 193 kwa ajili ya kujenga wodi ya mama na mtoto katika Kijiji cha Mkambarani Mkoani Morogoro ili kuboresha huduma ya afya ya uzazi.

Kiasi hicho cha fedha kimetolewa ikiwa ni utekelezaji wa ahadi aliyoitoa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi wakati wa ziara ya Kamati ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa tarehe 14 Machi, 2021 ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF mkoani Morogoro.

Akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Mkambarani, Mhe. Ndejembi amesema, wakati wa ziara ya Kamati hiyo ya Bunge, wananchi walieleza changamoto ya upatikanaji wa huduma ya afya ya uzazi inayowakabili akina mama pindi wanapohitaji huduma hiyo, hivyo Kamati iliishauri Serikali kuangalia uwezekano wa kutatua changamoto hiyo ili kuwaondolea adha akina mama wa Mkambarani kusafiri umbali mrefu kufuata huduma hiyo.

Aidha, Mhe. Ndejembi amewaasa watendaji wa Serikali wenye jukumu la kusimamia zahanati ya Mkambarani kuhakikisha fedha iliyotolewa inatumika kujenga wodi ya mama na mtoto kama ilivyokusudiwa, na kutoa wito kwa Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Albert Msando kufanya ufuatiliaji wa matumizi ya fedha hizo.

“Naelekeza kutumia utaratibu wa kufanya manunuzi pasipo kumtumia mkandarasi ili kupunguza gharama za ujenzi na kuziba mianya ya matumizi mabaya ya fedha.” Mhe. Ndejembi amesisitiza.

Mhe. Ndejembi ameongeza kuwa, Serikali sikivu ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan imetoa fedha hizo kwa ajili ya kuwezesha ujenzi wa wodi ya mama na mtoto ili wananchi wa Mkambarani wapate huduma bora, hivyo hatosita kumchukulia hatua yeyote atakayebainika kuzitumia vibaya fedha hizo za umma.

Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) licha ya kutoa ruzuku kwa walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini, umekuwa na mchango mkubwa wa kuboresha sekta ya afya kwa kutoa fedha za kujenga zahanati mbalimbali nchini ikiwepo ya Kijiji cha Mkambarani Mkoani Morogoro ili kutatua changamoto za upatikanaji wa huduma bora za afya zinazowakabili wananchi hususani wenye kipato cha chini.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Mkambarani ambacho TASAF imetoa shilingi milioni 193 kwa ajili ya ujenzi wa wodi ya mama na mtoto ili kuboresha huduma ya afya ya uzazi kijijini hapo.


Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Mkambarani wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (hayupo pichani) ambaye amewezesha kijiji chao kupata shilingi milioni 193 kutoka TASAF ili kujenga wodi ya mama na mtoto kijijini hapo.


Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Albert Msando akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi kuzungumza na wananchi wa Kijiji cha Mkambarani. 


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akiwaeleza wananchi wa Kijiji cha Mkambarani jitihada za Mbunge wao Mhe. Hamisi Taletale katika kufanikisha upatikanaji wa shilingi milioni 193 zilizotolewa na TASAF kwa ajili ya kujenga wodi ya Mama na Mtoto kijijini hapo. Aliyesimama nae ni Mbunge huyo Mhe. Hamisi Taletale. 


Diwani wa kata ya Mkambarani Mhe. Mboma Peter akimshukuru Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi kwa kuwezesha upatikanaji wa shilingi milioni 193 zilizotolewa na TASAF kwa ajili ya ujenzi wa wodi ya mama na mtoto katika kata yake.



Tuesday, July 27, 2021

“WATUMISHI WA UMMA MNA DENI LA KULIPA KWA WANANCHI NA MHESHIMIWA RAIS”- Mhe. Ndejembi

Na. James K. Mwanamyoto-Pwani

Tarehe 27 Julai, 2021 

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amewataka Watumishi wa Umma nchini kulipa deni kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzani, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa huduma bora kwa wananchi na kutumia weledi wao kujenga uchumi wa taifa.

Akizungumza kwa nyakati tofauti na watumishi wa Halmashauri ya Mji Kibaha, Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha na Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze mkoani Pwani, Mhe. Ndejembi amesema kuwa Mhe. Rais alipoingia madarakani, alitoa maelekezo kwa Waajiri wote kuzingatia maslahi ya watumishi wa umma hususani suala la upandishwaji wa madaraja jambo ambalo hivi sasa limetekelezwa na linaendelea kutekelezwa na waajiri wote kikamilifu ikiwa ni pamoja na kulipa stahili za watumishi kwa wakati.

Amesema waajiri wote nchini wametekeleza maelekezo ya Mhe. Rais, hivyo Watumishi wa Umma hawana budi kufanya kazi kwa bidii na uadilifu kwani hakuna haki isiyokuwa na wajibu.

“Ni muda mrefu tumekuwa tukililia haki ya kupandishwa madaraja na kupewa stahili nyingine, Rais wetu ametusikia kwani wote waliostahili kupanda madaraja, wamepanda na wenye madai ya stahili zao mbalimbali wamepatiwa, hivyo hili ni deni na ili kulilipa deni hili tunapaswa kujituma kwa kufanya kazi kwa bidii na uadilifu,” Mhe. Ndejembi amesisitiza.

Ameongeza kuwa, Serikali itaendelea kujali maslahi ya Watumishi wa Umma kwasababu watumishi ndio injini ya Serikali, hivyo wanalazimika kuendelea kutekeleza wajibu wao ipasavyo.

Aidha, Mhe. Ndejembi amezungumzia changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika zoezi la upandishwaji wa madaraja kwa Watumishi wa Umma kutokana na baadhi yao kukosa sifa kwa kutojaza Fomu ya Mfumo wa Wazi wa Mapitio na Tathmini ya Utendaji Kazi (OPRAS).

“Changamoto ya upandishwaji madaraja kwa baadhi ya Watumishi ni kupuuza ujazaji wa OPRAS, hawajazi kwa wakati na wanajaza kwasababu wanaona ni kigezo tu cha upandaji wa madaraja.” Mhe. Ndejembi amefanua.

Ili kuongeza ufanisi kiutendaji, Mhe. Ndejembi amewahimiza Watumishi wa umma nchini kufanya kazi kwa ushirikiano ili kufanikisha lengo la Serikali la kutoa huduma bora kwa wananchi.

Katika hatua nyingine Mhe. Ndejembi amewataka Watumishi wa Umma kushiriki katika kutoa elimu kwa walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wanaonufaika na Mradi wa kutoa ajira za muda.

Amesema suala la usimamizi wa walengwa wa TASAF ni la watumishi wote, hivyo ni vema watumishi wenye utalaam katika fani mbalimbali wakatoa elimu ya kuwawezesha walengwa kutimiza malengo yao badala ya kuwaachia Waratibu wa TASAF pekee.

Aidha, amewataka walengwa wa TASAF kutumia vizuri ruzuku wanayoipata kujikwamua katika lindi la umaskini ili hapo baadae waache kutegemea ruzuku ya TASAF.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Chalinze, Mhe. Ridhiwan Kikwete amesema kilio kikubwa cha Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze kilikuwa ni suala la upandishwaji wa madaraja jambo ambalo limetekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita. 

“Mhe. Naibu Waziri tunashukuru sana kwa kututembelea, changamoto kubwa iliyokuwa ikitusumbua ni upandishwaji wa madaraja, suala ambalo limeshafanyiwa kazi, tunamshukuru Mhe. Rais kwa kuliona hili na kulitekeleza.” Mhe. Ridhiwan ameongeza. 

Mhe. Ndejembi amefanya ziara ya kikazi katika halmashauri hizo kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma, kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF, ikiwa ni pamoja na kujiridhisha na utekelezaji wa maelekezo ya Mhe. Rais ya upandishwaji wa madaraja kwa Watumishi wa Umma nchini. 


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza na Watumishi wa Halmashauri ya Mji Kibaha mkoani Pwani (hawapo pichani) wakati wa ziara yake ya kikazi yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma mkoani humo.


Baadhi ya Watumishi wa Umma wa Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze mkoani Pwani wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao kwenye ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo wakati wa ziara yake ya kikazi yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi hao.


Afisa Misitu wa Halmashauri ya Mji Kibaha mkoani Pwani, Bw. William Msemo akiwasilisha hoja ya kiutumishi kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao kwenye ukumbi wa Halmashauri ya Mji huo wakati wa ziara yake ya kikazi yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi hao.


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza na Walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wa Kitongoji cha Mwanabwito wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha (hawapo pichani) wakati wa ziara yake ya kikazi yenye lengo la kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF mkoani Pwani.


Walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini wa Kitongoji cha Mwanabwito, Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa Miradi ya TASAF mkoani Pwani.


Mbunge wa Jimbo la Chalinze, Mhe. Ridhiwani Kikwete akitoa neno la shukrani kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi alipofanya ziara ya kikazi yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma Wilayani Chalinze.


Mbunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini, Mhe. Michael Mwakamo akitoa neno la shukrani kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi alipofanya ziara ya kikazi yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma na kukagua miradi ya TASAF wilayani Kibaha.


Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa TASAF, Bw. Paul Kijazi akitoa maelezo kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi kuhusu mradi wa jengo la kitega uchumi la kikundi cha Wazee wa Mlandizi lililojengwa na TASAF.


Kikundi cha Wazee wa Mlandizi kilichonufaika na mradi wa jengo la kitega uchumi lililojengwa na TASAF wakiwa mbele ya jengo hilo.

 


 

Monday, July 12, 2021

NDEJEMBI AIELEKEZA TPSC KUWAANDAA WATUMISHI KIDIJITALI

 


NDEJEMBI AIELEKEZA TPSC KUWAANDAA WATUMISHI KIDIJITALI


Na. James K. Mwanamyoto-Dar es Salaam

Tarehe 12 Julai, 2021

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi ameuelekeza uongozi wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) kutoa mafunzo yatakayowezesha kuwa na kizazi cha Watumishi wa Umma wanaoendana na mabadiliko ya teknolojia katika utoaji wa huduma.

Mhe. Ndejembi ametoa maelekezo hayo leo jijini Dar es Salaam wakati akihitimisha ziara yake ya kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa TPSC Makao Makuu na Kampasi ya Dar es Salaam.

Mhe. Ndejembi amesema, TPSC haina budi kutoa mafunzo ya kidijitali ili kutekeleza azma ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe, Samia Suluhu Hassan ya kuifanya Tanzania kuwa ya kidijitali ikiwa ni pamoja na kuuboresha Utumishi wa Umma kuwa wa kidijitali.

Mhe. Ndejembi amefafanua kuwa, ili kutoa huduma bora kwa wananchi na kwa wakati, Watumishi wa Umma nchini wanapaswa kujengewa uwezo wa kutekeleza majukumu yao kwa njia ya kidijitali.

Akihimiza utekelezaji wa maelekezo ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa ya kuwataka waajiri kuwapeleka watumishi wao TPSC ili kupata mafunzo ya kuwajengea uwezo kiutendaji, Mhe. Ndejembi amesema maelekezo hayo sio ombi bali ni lazima, hivyo akiwa ni msaidizi wa Waziri Mchengerwa atahakikisha anafanya ufuatiliaji wa utekelezaji wa agizo hilo. 

“Haiwezekani, Waziri mwenye dhamana ya Utumishi na Utawala Bora atoe maelekezo halafu yasitekelezwe na viongozi wanaosimamia taasisi za umma, hivyo nitahakikisha ninafanya ufuatiliaji,” Mhe. Ndejembi amesisitiza.

Mhe. Ndejembi ameongeza kuwa, kwa bahati nzuri Chuo cha Utumishi wa Umma kina kampasi sita zilizoko Mbeya, Mtwara, Tabora, Tanga, Singida na Dar es Salaam, hivyo waajiri hawana kisingizio cha kutowapeleka watumishi wao kupata mafunzo kwani TPSC inatoa huduma hiyo kila kanda kupitia kampasi zake na kuongeza kuwa watumishi hao wanaweza kuhudhuria mafunzo hayo kwa awamu.

Mhe. Ndejembi amesema Waajiri watakaoshindwa kuwapeleka Watumishi wao TPSC kupata mafunzo watalazimika kutoa maelezo ya kimaandishi juu ya sababu za kutotekeleza maelekezo hayo. 

Aidha, amewaasa Watumishi wa Umma kuhakikisha wanatekeleza maelekezo ya Mhe. Mchengerwa kwa kuwakumbusha waajiri kuwapatia fursa hiyo ya mafunzo TPSC. 

Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo na Mtendaji Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC), Dkt. Selemani Shindika amemshukuru Mhe. Ndejembi kwa kuweka msisitizo wa maelekezo ya Mhe. Mchengerwa ya kuwataka waajiri kuwapekeleka watumishi wao TPSC kupata mafunzo.

Dkt. Shindika amesema, chuo chake ni jiko halisia la kuwapika Watumishi wa Umma kwani kinafundisha maadili na miiko ya Utumishi wa Umma ili Watumishi wa Umma watekeleze wajibu wao kikamilifu.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amehitimisha ziara ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji katika Kampasi ya Dar es Salaam ikiwa ni baada ya kuzitembelea Kampasi za Mbeya, Tabora, Mtwara, Singida na Tanga.

                                                                                                                                  

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza na Watumishi wa TPSC Makao Makuu na Kampasi ya Dar es Salaam leo jijini Dar es Salaam wakati akihitimisha ziara yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa TPSC.


Baadhi ya Watumishi wa Umma wa TPSC Makao Makuu na Kampasi ya Dar es Salaam wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius (hayupo pichani) Ndejembi alipokuwa akizungumza nao leo jijini Dar es Salaam wakati akihitimisha ziara yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa TPSC.


Mkuu wa Chuo na Mtendaji Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC), Dkt. Selemani Shindika akiwasilisha taarifa fupi ya utekelezaji ya Chuo cha Utumishi wa Umma, Kampasi ya Dar es Salaam kabla ya kumkaribisha Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi kuzungumza na Watumishi wa TPSC Makao Makuu na Kampasi ya Dar es Salaam leo jijini Dar es Salaam wakati akihitimisha ziara yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa TPSC.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akipata maelezo ya utunzaji wa kumbukumbu kutoka kwa Msajili Msaidizi, Bw. Faraja Mbwilo wa TPSC Kampasi ya Dar es Salaam leo jijini Dar es Salaam wakati akihitimisha ziara yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa TPSC.


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza na wanafunzi kwenye moja ya madarasa ya TPSC Kampasi ya Dar es Salaam leo jijini Dar es Salaam wakati akihitimisha ziara yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa TPSC.


Makamu Mkuu wa Chuo, Utawala, Fedha na Mipango, Bibi. Asantina Sebastian akitoa neno la shukrani kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi leo jijini Dar es Salaam wakati Naibu Waziri huyo akipokuwa akihitimisha ziara yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa TPSC.

 

Wednesday, July 7, 2021

ZIARA YA MARAIS NA MAWAZIRI WAKUU WASTAAFU KUTEMBELEA MIRADI YA KIMKAKATI ILIANDALIWA NA MHE. RAIS ILI KUWAWEZESHA WASTAAFU HAO KUJIONEA MCHANGO WALIOUTOA WAKATI WA UONGOZI WAO - Mchengerwa


Na. James K. Mwanamyoto-Dar es Salaam

Tarehe 07 Julai, 2021

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema ziara ya siku mbili ya Marais na Mawaziri Wakuu Wastaafu ya kutembelea Mradi wa Kufua Umeme kwa Nguvu za Maji wa Julius Nyerere na wa Ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), iliandaliwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ili kutoa fursa kwa viongozi hao wastaafu wa kitaifa kuona maendeleo ya mchango walioutoa wakati wa uongozi wao ikiwa ni pamoja kuwapa fursa ya kushuhudia hatua ambayo Serikali imefikia katika ujenzi wa miradi hiyo mikubwa ya kimkakati.

Mhe. Mchengerwa amesema hayo jijini Dar es Salaam mara baada ya viongozi hao wastaafu wa kitaifa kuhitimisha ziara yao ya kujionea maendeleo ya ujenzi wa miradi hiyo mikubwa ya kimkakati inayotekelezwa na Serikali.

Mhe. Mchengerwa amempongeza Rais wa Awamu ya Sita, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuwaandalia ziara hiyo mahususi Waheshimiwa Marais na Mawaziri Wakuu wastaafu ambao wakati wa uongozi wao walitoa mchango mkubwa katika kujenga misingi imara ya utekelezaji wa miradi hiyo ya kimkakati yenye tija katika uchumi wa taifa.

Mhe. Mchengerwa amesema, Marais na Mawaziri Wakuu wastaafu wamefurahi kuona mawazo na mapendekezo waliyoyatoa kuhusu utekelezaji wa miradi hiyo yamefanyiwa kazi kikamilifu na Serikali ya Awamu ya Tano na kuendelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozo makini wa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan.

Waziri Mchengerwa amefafanua kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita inaendeleza miradi ya kimkakati iliyokusudiwa kutekelezwa na Marais Wastaafu na kuongeza kuwa, mipango ya utekelezaji wa miradi hiyo ya kimkakati ilianza muda mrefu wakati wa utawala wa Waheshimiwa Marais hao wastaafu.

“Mipango yote ya kuwa na miradi ya kimkakati ilianza wakati wa uongozi wa Baba wa Taifa Mwalimu Julius K. Nyerere na kuendelezwa na Marais wote wastaafu na hivi sasa inaendelea kutekelezwa na Rais Samia Suluhu Hassani,” Mhe. Mchengerwa amesisitiza. 

Akijibu swali la Mwandishi wa Habari kuhusu mchango wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora katika usimamizi wa utekelezaji wa miradi ya kimkakati, Mhe. Mchengerwa amesema kuwa ofisi yake inahusika katika usimamizi wa miradi hiyo kwani wanaosimamia miradi hiyo ni Watumishi wa Umma ambao wameajiriwa na Serikali ili kuwatumikia watanzania.

Sanjari na hilo, Mhe. Mchengerwa amesema kuwa, Mhe. Rais ameelekeza miradi yote ya kimkakati ikamilike kwa wakati hivyo akiwa ni msaidizi wa Mhe. Rais katika kutekeleza jukumu la usimamizi wa masuala ya kiutumishi na utawala bora, ofisi yake inawajibika kusimamia utekelezaji wa miradi hiyo ya kimkakati  ili wananchi ambao ndio walengwa wakuu wanufaike na miradi hiyo kiuchumi.

Kutokana na maelekezo hayo ya Mhe. Rais, Mhe. Mchengerwa amesema hakutakuwa na nyongeza ya muda ili kukamilisha miradi hiyo ya kimkakati, hivyo amewataka watendaji katika wizara zinazosimamia ujenzi wa Mradi wa Kufua Umeme kwa Nguvu za Maji wa Julius Nyerere na wa Ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kuhakikisha wanatekeleza wajibu wao kikamilifu ili kuwezesha miradi hiyo ikamilike kwa wakati.

Ziara hiyo ya Viongozi wastaafu wa Kitaifa iliyolenga kuwawezesha kuona maendeleo ya ujenzi wa miradi ya kitaifa ya kimkakati ilihudhuriwa na Rais Mstaafu Mhe. Ali Hassan Mwinyi, Rais Mstaafu Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete na Mawaziri wakuu wastaafu ambao ni Mhe. Cleopa Msuya, Mhe. John Malecela na Mhe. Mizengo Pinda.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam, mara baada ya Waheshimiwa Marais na Mawaziri Wakuu wastaafu kuhitimisha ziara yao ya siku mbili kujionea maendeleo ya ujenzi wa miradi mikubwa ya kimkakati inayotekelezwa na Serikali.


Marais wastaafu Mhe. Ali Hassan Mwinyi na Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete wakiwa na Mawaziri Wakuu wastaafu Mhe. John Malecela na Mhe. Peter Pinda wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi wengine mbele ya andaki ambalo reli ya kisasa (SGR) imepita eneo la Kilosa mkoani Morogoro.

 

Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete akizungumza na Waandishi wa Habari eneo la Kilosa Morogoro wakati wa ziara ya viongozi wakuu wastaafu wa kitaifa ya kujionea maendeleo ya Reli ya Kisasa (SGR) inayojengwa na Serikali.



Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete akisaini kitabu cha wageni akiwa safarini kurejea jijini Dar es Salaam ndani ya treni inayotoa huduma ya usafiri kwa kutumia Reli ya Kisasa (SGR) inayojengwa na Serikali.

Watendaji wa Serikali waliombatana na Marais wastaafu Mhe. Ali Hassan Mwinyi na Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete na Mawaziri Wakuu wastaafu Mhe. John Malecela na Mhe. Peter Pinda wakiingia na viongozi hao kwenye moja ya andaki ambalo reli ya kisasa (SGR) imepita eneo la Kilosa mkoani Morogoro.



Watendaji wa Serikali waliombatana na Marais wastaafu Mhe. Ali Hassan Mwinyi na Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete na Mawaziri Wakuu wastaafu Mhe. John Malecela na Mhe. Peter Pinda wakiwa ndani ya andaki ambalo reli ya kisasa (SGR) imepita eneo la Kilosa mkoani Morogoro.


 

Monday, July 5, 2021

WATAALAMU WA NDANI WAPONGEZWA NA VIONGOZI WASTAAFU WA KITAIFA KWA KUSIMAMIA UJENZI WA MRADI WA KUFUA UMEME WA JULIUS NYERERE

 Na. James K. Mwanamyoto-Rufiji

Tarehe 06 Julai, 2021

Viongozi Wakuu wa Kitaifa Wastaafu Waheshimiwa Marais na Mawaziri Wakuu wamewapongeza wataalamu wa ndani kwa kusimamia vizuri ujenzi wa Mradi wa Kufua Umeme kwa Nguvu za Maji wa Julius Nyerere (Julius Nyerere Haydropower Project) ambao ujenzi wake umefikia asilimia hamsini na nne (54%).

Pongezi hizo wamezitoa walipoutembelea mradi huo kwa lengo la kujionea maendeleo ya mradi na kutoa ushauri utakaoboresha ukamilishaji wa ujenzi wa mradi huo mkubwa wa kitaifa unaojengwa na Serikali kwa kutumia fedha za ndani. 

Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, Mhe. Ali Hassan Mwinyi amesema amefurahishwa na namna wataalamu wa kitanzania walivyoweza kusimamia mradi huo kwa ustadi mkubwa hivyo amewapongeza kwa kutumia vema taaluma yao kusimamia ujenzi wa Mradi huo wa Kufua Umeme kwa Nguvu za Maji wa Julius Nyerere. 

Naye, Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete amewapongeza waliohusika kuchora mchoro wa mradi, wakandarasi na wasimamizi wa ujenzi wa mradi huo na kwa kipekee amemshukuru Rais wa Awamu ya Sita Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuupokea mradi na kuuendeleza. 

Aidha, Mhe. Kikwete amempongeza Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Mhe. John Pombe Joseph Magufuli kwa uamuzi wake wa kutafuta fedha na kuanza ujenzi wa mradi huo ili kutimiza ndoto ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. 

Mhe. Kikwete amesema, ndoto ya Baba wa Taifa ilikuwa ni kujenga bwawa kubwa la kuzalisha umeme, lenye shughuli ya utalii, litakalopunguza mafuriko sehemu ya chini ya mto Rufiji na kuwezesha kilimo cha umwagiliaji kitakacholisha takribani watu milioni ishirini, hivyo ametoa wito kwa wadau wa kilimo waanze kujipanga kutumia fursa ya kilimo cha umwagiliaji.

Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. John Malecela amesema, watanzania wanapaswa kujivuna kwa kutekeleza mradi huo kwa fedha zao wenyewe na kuongeza kuwa, watanzania wajisikie fahari kwani mradi huo unasimamiwa na wazawa ambao wameonesha uzalendo kwa taifa kwa kusimamia vema ujenzi wake.

Mhe. Malecela amefafanua kuwa, tangu taifa lipate uhuru halijawahi kutekeleza mradi mkubwa kama huo wa Kufua Umeme kwa Nguvu za Maji wa Julius Nyerere hivyo watanzania hawanabudi kujivunia mradi huo.

Akizungumzia ujenzi wa mradi huo, Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. Cleopa Msuya amempongeza Waziri wa Nishati Mhe. Medard Karemani na wataalamu wake wa kitanzania kwa kujitoa na kuwajibika kikamilifu katika usimamizi wa ujenzi wa mradi huo. 

Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. Mizengo Pinda ameipongeza Wizara ya Nishati kwa usimamizi mzuri wa mradi huo mkubwa ambao ujenzi wake umefikia asilimia 54% na kutoa wito kwa watanzania kuhakikisha mradi huo unatumika vizuri ili kukamilisha ndoto ya Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Waziri wa Nishati, Mhe. Medard Karemani amesema mradi ukikamilika nchi itakuwa na umeme wa kutosha, wa uhakika na wenye gharama nafuu hivyo ametoa wito kwa wenye nia ya kuwekeza kujitokeza na kuwekeza kwenye shughuli za kilimo, umwagiliaji na utalii.

Mhe. Karemani amesisitiza kuwa, kupitia uzoefu wa usimamizi wa mradi huo watanzania tumejifunza kwamba hata miradi mingine itakayoanza kutekelezwa itasimamiwa na watanzania wenyewe kwani wataalamu wazawa wanao uwezo huo.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa amewataka viongozi wote wanaosimamia miradi ya mikubwa ya kimkakati na mingine kuhakikisha ina kamilika kwa wakati kama ilivyopangwa.

Mhe. Mchengerwa amefafanua kuwa, Rais wa Awamu ya Sita Mhe. Samia Suluhu Hassan amedhamiria kukamilisha mradi huo ifikapo mwakani ikiwa ni pamoja na kukamilisha miradi mingine ya kimkakati na kutoa wito kwa wasimamizi wa miradi kusimamia vizuri kwa kuzingatia thamani ya fedha iliyotumika na kuwaonya watakaokwamisha miradi kuwa watachukuliwa hatua stahiki.

Naye, Mkurugenzi wa Idara ya Habari MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali Bw. Greyson Msigwa amewahakikishia watanzania kuwa, miradi yote mikubwa ya kimkakati itakamilika kwa wakati kama ambavyo Rais wa Awamu ya Sita Mhe. Samia Suluhu Hassan amedhamiria. 

Ujenzi wa Mradi huo wa Kufua Umeme kwa Nguvu za Maji wa Julius Nyerere (Julius Nyerere Haydropower Project) unatarajia kukamilika tarehe 14 Juni, 2022 na utakuwa na uwezo wa kufua umeme wa Megawati 2115.

Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, Mhe. Ali Hassan Mwinyi akizungumza na Waandishi wa Habari wakati wa ziara ya viongozi wakuu wa wastaafu wa kitaifa ya kujionea maendeleo ya ujenzi wa Mradi wa Kufua Umeme kwa Nguvu za Maji wa Julius Nyerere unaojengwa na Serikali kwa kutumia fedha za ndani.


Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete akizungumza na Waandishi wa Habari wakati wa ziara ya viongozi wakuu wastaafu wa kitaifa ya kujionea maendeleo ya ujenzi wa Mradi wa Kufua Umeme kwa Nguvu za Maji wa Julius Nyerere unaojengwa na Serikali kwa kutumia fedha za ndani.


Mwonekano wa mendeleo ya ujenzi wa eneo mojawapo la Mradi wa Kufua Umeme kwa Nguvu za Maji wa Julius Nyerere unaojengwa na Serikali kwa kutumia fedha za ndani.


Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. John Malecela akizungumza na Waandishi wa Habari wakati wa ziara ya viongozi wakuu wastaafu wa kitaifa ya kujionea maendeleo ya ujenzi wa Mradi wa Kufua Umeme kwa Nguvu za Maji wa Julius Nyerere unaojengwa na Serikali kwa kutumia fedha za ndani.


Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. Mizengo Pinda akizungumza na Waandishi wa Habari wakati wa ziara ya viongozi wakuu wastaafu wa kitaifa ya kujionea maendeleo ya ujenzi wa Mradi wa Kufua Umeme kwa Nguvu za Maji wa Julius Nyerere unaojengwa na Serikali kwa kutumia fedha za ndani.


Waziri wa Nishati, Mhe. Medard Karemani akizungumza na Waandishi wa Habari wakati wa ziara ya viongozi wakuu wastaafu wa kitaifa ya kujionea maendeleo ya ujenzi wa Mradi wa Kufua Umeme kwa Nguvu za Maji wa Julius Nyerere unaojengwa na Serikali kwa kutumia fedha za ndani.

 


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akizungumza na Waandishi wa Habari wakati wa ziara ya viongozi wakuu wastaafu wa kitaifa ya kujionea maendeleo ya ujenzi wa Mradi wa Kufua Umeme kwa Nguvu za Maji wa Julius Nyerere unaojengwa na Serikali kwa kutumia fedha za ndani.


Viongozi wakuu wastaafu wa kitaifa wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Taasisi za Umma mara baada ya kumaliza ziara yao ya kujionea maendeleo ya ujenzi wa Mradi wa Kufua Umeme kwa Nguvu za Maji wa Julius Nyerere unaojengwa na Serikali kwa kutumia fedha za ndani.


Mkurugenzi wa Idara ya Habari MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali Bw. Greyson Msigwa akizungumza na Waandishi wa Habari wakati wa ziara ya viongozi wakuu wastaafu wa kitaifa ya kujionea maendeleo ya ujenzi wa Mradi wa Kufua Umeme kwa Nguvu za Maji wa Julius Nyerere unaojengwa na Serikali kwa kutumia fedha za ndani.