Thursday, February 29, 2024

Monday, February 26, 2024

WAZIRI SIMBACHAWENE AITAKA TASAF ITOE KIPAUMBELE KWA KAYA MASKINI ZENYE WATU WENYE ULEMAVU


Na.Lusungu Helela

 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene ameutaka Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kuweka nguvu zaidi katika kuziingiza kaya maskini zenye watu wenye ulemavu kwenye Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini ili nao waweze kujiinua kiuchumi na kufikia malengo ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye anatamani kuona mpango huo unagusa makundi mengi zaidi yenye uhitaji.

 

Mhe. Simbachawene ameyasema hayo leo alipotembelea na kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF katika Kijiji cha Kinywang’anga Wilaya ya Iringa, ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya kikazi mkoani humo ya kukagua miradi mbalimbali inayotekelezwa na TASAF.

 

Amesema TASAF imekuwa mkombozi kwa wananchi wanaonufaika kupitia miradi mbalimbali inayotekelezwa na mpango huo huku akisisitiza kuwa katika awamu ijayo iwaangalie zaidi watu wenye ulemavu kwani wamekuwa wakikosa fursa nyingi kulingana na changamoto walizokuwa nazo. 

 

"Kaya zenye watu wenye ulemavu na hazijiwezi kimaisha zina mzigo mara mbili ukilinganisha na kaya zisizojiweza na hazina watu wenye ulemavu, hivyo ni lazima kaya zenye walemavu zipewe kipaumbele zaidi" amesisitiza Mhe.Simbachawene 

 

Amesema moja ya dhamira Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha kaya maskini zenye walemavu zinapata uhakika wa milo mitatu kama zilivyo kaya nyingine masikini.

 

Hata hivyo Mhe.Simbachawene amesema Serikali inafanya kazi kubwa ya kuhakikisha fedha zinazotoka zinafika kila mahali na kwa walengwa sahihi hasa waishio vijijini katika kuboresha maisha ya Watanzania kupitia miradi mbalimbali ikiwemo ya TASAF.

 

 

Amesema miradi inayotekelezwa na TASAF inagusa maisha ya wananchi moja kwa moja na kushirikisha jamii katika uhalisia wake akisema huo ndio msingi wa viongozi wa Tanzania.

 

 “Lengo la miradi la TASAF ni kuondoa umasikini wa kipato kwa mtu mmoja mmoja na kaya, ndio maana kuna wanufaika wanaopewa fedha za moja kwa moja ili kuwapa ahueni katika hali zao za maisha,” amesema Mhe. Simbachawene. 

 

Katika ziara hiyo, Mhe. Simbachawene alitembelea mradi wa ujenzi wa birika la kunyweshea mifugo katika Kijiji cha Kinywanga’nga akiguswa na utekelezaji wa mradi huo ambao unakwenda kuinua sekta ya uvuvi na kugusa moja kwa moja maisha ya wafugaji.

 

Awali Meneja wa Miradi ya Ajira za Muda Mfupi kutoka TASAF, Bw. Paul Kijazi amesema Halmashauri ya Wilaya ya Iringa ina afua tatu katika jamii ikiwemo ya kuhawilisha fedha inayotolewa kwa wananchi wa kaya zisizokuwa na uwezo wa kufanya kazi wakiwemo wazee.

 

“Katika Halmashauri ya Wilaya ya Iringa tuna vijiji 134 vyote vinahawilishiwa fedha, tumeshaleta shilingi bilioni 3.663 katika awamu ya pili ya TASAF kwa walengwa, lakini pia tulileta fedha shilingi bilioni 1.09 kwa ajili ya vifaa vilivyotumika katika ajira za muda mfupi.


 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akizungumza na walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini mara baada ya kukagua miradi mbalimbali inayotekelezwa na TASAF mkoani Iringa.


Sehemu ya walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao katika eneo la Migori mkoani Iringa.


Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Mhe. Veronica Kessy akizungumza na walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (hawapo pichani) kabla ya kumkaribisha Waziri Simbachawene kuzungumza nao mkoani humo.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akiwa na baadhi ya wananchi akikagua mradi wa birika la kunyweshea mifugo lililojengwa na walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika Kijiji cha Kinywang’anga kilichopo mkoani Iringa

 

Sehemu ya birika la kunyweshea mifugo lililojengwa na walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika Kijiji cha Kinywang’anga kilichopo   mkoani Iringa.

 

 


 Kibao kinachoonesha moja ya mradi uliotekelezwa na walengwa wa TASAF

Friday, February 23, 2024

WAZIRI SIMBACHAWENE ARIDHISHWA NA UTENDAJI KAZI WA MAMLAKA YA SERIKALI MTANDAO, AITAKA IONGEZE KASI KUSANIFU MIFUMO


 




Na Lusungu Helela- Iringa

 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora   Mhe. George Simbachawene aridhishwa na utendaji kazi wa  Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) huku akiitaka iongeze kasi zaidi katika  kusanifu na kutengeneza mifumo ya TEHAMA ili kuiwezesha Serikali  kutoa huduma kwa umma kwa haraka na ufanisi.

 

Mhe. Simbachawene ametoa kauli hiyo leo alipokuwa akizungumza na Watumishi  wa eGA-Kituo cha Iringa ambapo amewataka Watumishi hao kuhakikisha Serikali inaendeshwa kidigitali kwenye kila nyanja kupitia mifumo wanayoisanifu.

 

Amesema eGA ni taasisi muhimu katika dunia ya sasa ambapo Serikali inahitaji mapinduzi ya TEHAMA ili itoe huduma zake kwa wananchi kiurahisi na kwa haraka 

 

“Dunia inakwenda kasi na teknolojia ni kila kitu kwa sasa, hivyo ni muhimu kwa eGA kufanya utafiti, kubuni na  kutengeneza mifumo ya TEHAMA Serikalini kwa ajili ya kurahisisha utoaji wa huduma kwa umma” amesema Mhe. Simbachawene.

 

Mhe. Simbachawene ameongeza kuwa eGA imeweka juhudi kubwa katika kusimamia TEHAMA Serikalini na imetengeneza na inaendelea kutengeneza mifumo ya TEHAMA ambayo imewarahisishia wananchi kupata huduma kwa haraka, mahali popote na kwa gharama nafuu na kuchagiza utawala bora.

 

Aidha, Mhe. Simbachawene ameridhishwa na utendaji kazi wa Mamlaka ya Serikali Mtandao katika ofisi zake zilizopo Iringa na amewataka watumishi wa Mamlaka kwa jumla kuendelea kubuni Mifumo ya TEHAMA inayotatua changamoto zilizopo nchini pamoja na kuwa wazalendo kwa maslahi ya Taifa.

 

Vile vile, amewasisitiza watumishi wa eGA kuhakikisha mifumo inayotengenezwa na iliyopo inakuwa na uwezo wa kuwasiliana ili kuleta ufanisi katika kuwahudumia wananchi.

 

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao, Mhandisi Benedict Ndomba amemshukuru Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Simbachawene kwa kutenga muda wake kutembelea kituo hicho cha Iringa na kuahidi kutekeleza maagizo yote aliyotoa.

 

 



Sehemu ya Watumishi wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGa) Kituo cha Iringa wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao wakati wa ziara yake ya kikazi katika Kituo hicho.




Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete akizungumza na Watumishi wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGa) Kituo cha Iringa (hawapo pichani) kabla ya kumkaribisha Waziri Simbachawene kuzungumza nao.

 



Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao, Mhandisi Benedict Ndomba akitoa maelezo kuhusu  Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGa) Kituo cha Iringa kabla ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene kuzungumza na Watumishi hao.



Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akisaini kitabu mara baada ya kuwasili  Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGa) Kituo cha Iringa wakati wa ziara yake ya kikazi katika kituo hicho.


WAZIRI SIMBACHAWENE AITAKA TAKUKURU KUWADHIBITI WACHEZEAJI RASILIMALI ZA NCHI





Na.Lusungu Helela- Iringa 

 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene ameitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU kudhibiti mianya ya rushwa katika fedha za miradi ya maendeleo inayoendelea kutekelezwa na serikali nchini ili kuhakikisha thamani ya fedha inaonekana.

                    

Ametoa kauli hiyo  leo alipotembelea na kukagua ujenzi wa jengo la ofisi za TAKUKURU mkoani Iringa ambapo amemtaka Mkandarasi kukamilisha ujenzi wa jengo hilo  ifikapo mwezi Juni mwaka huu kama ilivyopangwa ili watumishi wa taasisi hiyo waweze kufanya kazi zao katika mazingira mazuri. 

 

“Tukawe watu wa kupekenyua pekenyua kwenye miradi hii inayotekelezwa na serikali kwani kuna watu wanatumia vibaya fedha za serikali, penyeni huko kuwadhibiti ili miradi ya maendeleo ikamilike kwa wakati na kwa viwango kama ilivyokusudiwa,” amesisitiza Mhe. Simbachwene

 

Amefafanua kuwa TAKUKURU inatakiwa kuhakikisha inasimamia na kudhibiti fedha zisipotee lakini bila kuathiri maendeleo ya miradi ya kimkakati inayotekelezwa nchini.

 

"Palipo na shilingi ya Mama Samia waambieni TAKUKURU tupo ila katika kufanya haya tusikwamishe maendeleo" amesisitiza Mhe. Simbachawene.

 

Kufuatia hatua hiyo, Mhe. Simbachawene ameitaka Taasisi hiyo kuwachukulia hatua wale wote wanaokwamisha shughuli za maendeleo na hivyo kukwamisha utendaji wa Rais Mhe. Dkt.  Samia suluhu Hassan.

 

"Dhibitini mianya ya kuchezea rasilimali za nchi ikiwemo fedha zinazotengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo, sehemu ambako fedha imesimamiwa vizuri matokeo mazuri yameonekana, naomba niwasihi kuendelea kuwadhibiti ipasavyo wachezea fedha za maendeleo" amesema Mhe. Simbachawene.

 

Ameongeza kuwa anataka kuona TAKUKURU ikichukua hatua kwa wale wote wanaokwamisha nia nzuri ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na kama hatua hizo hazichukuliwi basi miradi mizuri iliyotekelezwa ionekane ili wananchi wazidi kuwa na imani na serikali yao.

 

Akitoa taarifa ya ujenzi wa jengo hilo, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, CP. Salum Hamduni amesema ujenzi wa jengo hilo la ghorofa moja hadi kukamilika kwake mwezi Juni mwaka huu utagharimu zaidi ya shilingi billioni 1.4.

 

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Halima Dendego ameishukuru serikali kwa kutoa fedha za ujenzi wa jengo hilo huku akiipongeza TAKUKURU kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kusimamia fedha za serikali zisipotee kwa maslahi binafsi ya baadhi ya watu.



Sehemu ya muonekano wa Jengo la ghorofa moja la Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU mkoani Iringa linaloendelea kujengwa mkoani humo ambapo linatarajiwa kukamalika mwezi Juni mwaka huu. 



Sehemu ya Watumishi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU mkoani Iringa wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene (Hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao mara baada ya kukagua ujenzi wa jengo la ghorofa moja linaloendelea kujengwa  mkoani humo

 



Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete akizungumza na Watumishi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU Mkoani Iringa (hawapo pichani) kabla ya Waziri Simbachawene mara baada ya kukagua ujenzi wa jengo la ghorofa moja linaloendelea kujengwa  mkoani humu


 



Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akipata maelezo kutoka kwa Mkandarasi wakati akikagua ujenzi wa jengo la TAKUKURU Mkoani Iringa linaloendelea kujengwa Mkoani humo.

                                   


             

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akiwa na baadhi ya Watumishi wa TAKUKURU Mkoani Iringa wakati akikagua ujenzi wa jengo la TAKUKURU Mkoani Iringa linaloendelea kujengwa Mkoani humo.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Wednesday, February 21, 2024

MHE. SIMBACHAWENE AELEKEZA KUSIMAMISHA MISHAHARA YA VIONGOZI WALIOSHINDWA KUSIMAMIA WATUMISHI KUTEKELEZA ZOEZI LA PEPMIS

 


Na. Lusungu Helela-Iringa

Tarehe 21 Februari, 2024

 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene amemuelekeza Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bw. Juma Mkomi kusimamisha mishahara ya Viongozi walioshindwa kuwasimamia watumishi wao kujisajili na kujaza mipango kazi yao katika Mfumo wa Usimamizi wa Utendaji Kazi kwa Watumishi wa Umma na Taasisi za Umma (PEPMIS/PIPMIS) na kukwamisha utekelezaji wa zoezi hilo lenye masilahi mapana katika utumishi wa umma na taifa kwa ujumla.

 

Mhe. Simbachawene ametoa maelekezo hayo leo mkoani Iringa alipokuwa akizungumza na Wajumbe wa Baraza Kuu la Wafanyakazi katika Utumishi wa Umma Tanzania Bara wakati akifungua Baraza hilo.

 

Amesema ujenzi wa mfumo wa PEPMIS/PIPMIS pamoja na mifumo mingine ya TEHAMA ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye amedhamiria kwa dhati kuwa na Serikali ya kidijitali itakayorahisisha utendaji kazi wa watumishi wa umma kwa lengo la kutoa huduma bora kwa wananchi.

 

“Mfumo huu wa PEPMIS na PIPMIS ni mbadala wa Mfumo wa Wazi wa Upimaji wa Utendaji kazi (OPRAS) na Mfumo wa Mikataba wa Utendaji Kazi wa Taasisi (IPCS) ulioonekana kuwa na changamoto za usimamizi wa utendaji kazi zilizojitokeza katika utekelezaji wa mfumo wa awali wa OPRAS hivyo mfumo huu umeboreshwa ili kuondokana na changamoto hizo, hivyo ni wajibu wa kila mtumishi kushiriki kikamilifu katika kutekeleza mfumo huu muhimu,” Mhe. Simbachawene amesisitiza.

 

Amesema mifumo hii ya TEHAMA ni nyenzo muhimu katika kutekeleza majukumu na inalenga kuleta tija, ufanisi na kuchangia kwa kiwango kikubwa katika maendeleo ya watumishi wa Umma na nchi kwa ujumla.

Amesema wanaotakiwa kuwajibishwa kwanza kwa kushindwa kutekeleza zoezi hili la PEPMIS/PIPMIS ni viongozi ambao wameshindwa kuwasimamia watumishi wao, hivyo hatua za kusimamisha mshahara zianze kwa viongozi huku watumishi ambao hawajatekeleza wapewe muda wa kutekeleza na wakishindwa, hatua zichukuliwe kwa watumishi hao.

 

Vilevile, amekemea tabia ya baadhi ya Waajiri kukataa kuwapokea watumishi wanaohamishiwa kwenye taasisi wanazoziongoza na baadhi kutoruhusu watumishi kuhama hata pale inapoelekezwa na Mamlaka kwani kwa kufanya hivyo ni ukosefu wa maadili na ni jambo ambalo halikubaliki.

 

‘’Hili jambo sio sahihi kwenye Utumishi wa Umma kwani kuna baadhi ya Waajiri wanaendesha ofisi za Umma kwa utashi na matakwa binafsi’’ amesisitiza Mhe. Simbachawene

 

Akitoa maelezo ya awali kuhusu baraza hilo, Katibu Mkuu-UTUMISHI, Bw. Juma Mkomi ambaye ndiye Mwenyekiti wa Baraza hilo amesema elimu ya utekelezaji wa Mifumo ya TEHAMA ikiwemo Mfumo wa PEPMIS/PIPMIS na Mfumo wa Kubaini Mahitaji ya Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma (HR Assessment) imetolewa nchi nzima lakini kumekuwa na kutowajibika kwa baadhi ya viongozi katika kuwasimamia watumishi wao kutekeleza zoezi hilo.

 

Katibu Mkuu Mkomi amesema hatua zimeshaanza kuchukuliwa na zinaendelea kuchukuliwa kwa wote ambao wameshindwa kutekeleza zoezi hilo.

 

Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya wajumbe wa Baraza, Makamu Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Wafanyakazi katika Utumishi wa Umma Tanzania Bara, Bw. Joel Kaminyoge amemshukuru Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha masilahi na stahiki za watumishi wa umma nchini kwani malalamiko mengi ya watumishi ikiwemo kudai stahiki zao yamepungua kwa kiasi kikubwa.

 

Amesema kufuatia maboresho makubwa aliyoyafanya Mhe. Rais, jukumu walilo nalo sasa ni kuwahimiza watumishi wa umma kufanya kazi kwa bidii na uadilifu ili kutoa huduma bora kwa umma kama ambavyo serikali imekusudia.

 

Baraza Kuu la Wafanyakazi katika Utumishi wa Umma Tanzania Bara lilianzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Majadiliano ya pamoja katika Utumishi wa Umma Sura 105.

 

 


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akizungumza na Wajumbe wa Baraza Kuu la Wafanyakazi katika Utumishi wa Umma Tanzania Bara (hawapo pichani) alipokuwa akifungua Baraza hilo leo mkoani Iringa.



Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete akizungumza na Wajumbe wa Baraza Kuu la Wafanyakazi katika Utumishi wa Umma Tanzania Bara (hawapo pichani) kabla ya Waziri Simbachawene kufungua Baraza hilo leo mkoani Iringa.



Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Juma Mkomi akitoa maelezo kuhusu Baraza Kuu la Wafanyakazi katika Utumishi wa Umma Tanzania Bara kabla ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene kufungua Baraza hilo leo mkoani Iringa

Makamu Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Wafanyakazi katika Utumishi wa Umma Tanzania Bara, Bw. Joel Kaminyoge akitoa neno la shukrani kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene baada ya Waziri huyo kufungua Baraza Kuu la Tano la Wafanyakazi katika Utumishi wa Umma Tanzania Bara leo mkoani Iringa


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Wajumbe wa Baraza Kuu la Wafanyakazi katika Utumishi wa Umma Tanzania Bara mara baada ya kufungua Baraza hilo mkoani Iringa.

 

 

 


Tuesday, February 20, 2024

KATIBU MKUU-UTUMISHI AWATAKA MAAFISA RASILIMALIWATU KUWEKA KUMBUKUMBU SAHIHI ZA WATUMISHI KABLA YA KUSTAAFU I

 


Na. Lusungu Helela-Dodoma

Tarehe 20 Februari, 2024

 

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bw. Juma Mkomi amewataka Maafisa Rasilimaliwatu wote serikalini kuhakikisha wanaweka kumbukumbu sahihi za watumishi wa umma wanaotarajia kustaafu kabla ya miezi sita ili kuwaondolea usumbufu wa kufuatilia mafao yao pindi wanapostaafu.

 

Ametoa kauli hiyo leo jijini Dodoma  wakati akizungumza  kwenye kikao kazi na  watumishi  wa Ofisi yake,   ikiwa ni mwendelezo wa kuhimiza utendaji na  uwajibikaji kwa watumishi wa umma nchini.

 

Katibu Mkuu Mkomi amesema haikubaliki mtumishi anapewa barua ya kustaafu huku baadhi ya taarifa za michango ya mafao yake haiko sawa.

 

‘’Mtumishi anapewa barua ya kumtaarifu kustaafu kabla ya miezi sita halafu baadaye anaanza kusumbuliwa eti michango ya mafao haionekani, sasa hiyo barua aliyopewa kabla ya miezi sita ilikuwa na maana gani" amehoji Bw. Mkomi.

 

Amesisitiza kuwa suala hili lazima lifanyiwe kazi kwa kuwa watumishi hao wanaostaafu wamelitumikia taifa kwa moyo hivyo kuhangaishwa sio haki.

 

Katika hatua nyingine, Bw. Mkomi ametoa onyo kwa watumishi wanaovujisha siri za serikali ambapo ameahidi wale wote watakaobainika watachukuliwa hatua kali za kisheria ili iwe fundisho kwa wengine.

 

Amesema kitendo hicho ni kinyume cha maadili ya utumishi wa umma ambapo ametumia fursa hiyo kuwaasa watumishi hao kujiepusha na tabia hiyo.

 

Pia, Katibu Mkuu Mkomi amewataka watumishi wa umma kuzingatia maadili ya utendaji wanapotoa huduma kwa wananchi kwani maadili ndio msingi wa utumishi wa umma.

 

Kwa kusisitiza hilo amewataka watumishi wa Ofisi yake kuwa mfano wa uzingatiaji wa maadili kwa vile Ofisi hiyo ni kioo cha Utumishi wa umma nchini.

 

Naye Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu, Bw. Musa Magufuli amemshukuru Katibu Mkuu Mkomi kwa kutenga muda kuzungumza na watumishi wa Ofisi yake licha ya majukumu mazito yanayomkabili huku akiahidi maagizo yote aliyoyatoa yatatekelezwa.

 

Awali katika kikao kazi hicho, mada mbalimbali zilitolewa kwa watumishi hao ikiwemo Maadili kwa Watumishi wa Umma, Kukabiliana na Msongo wa Mawazo, PSSSF Kiganjani na faida ya kujiunga na SACCOS ya Ofisi ya Rais-UTUMISHI.

 

 

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Juma Mkomi akizungumza na watumishi wa ofisi yake (hawapo pichani) wakati wa kikao kazi chake na watumishi hao kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi jijini Dodoma. 

Sehemu ya watumishi wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI wakimsikiliza Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Juma Mkomi, alipokuwa akizungumza nao wakati wa kikao kazi chake na watumishi hao kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi jijini Dodoma.



 Sehemu ya watumishi wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI wakimsikiliza Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Juma Mkomi, alipokuwa akizungumza nao wakati wa kikao kazi chake na watumishi hao kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi jijini Dodoma.


Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Juma Mkomi, akiteta na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi wakati wa kikao kazi cha Katibu Mkuu huyo na watumishi wa Ofisi yake kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi jijini Dodoma


 

 Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu, Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bw. Musa Magufuli akitoa maneno ya utangulizi wakati wa kikao kazi cha Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Juma Mkomi na watumishi wa Ofisi hiyo kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi jijini Dodoma.

 

 


 Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Juma Mkomi (katikati) akifafanua hoja za watumishi wa Ofisi yake wakati wa kikao kazi cha Katibu Mkuu huyo na watumishi hao kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi jijini Dodoma

 

 


 Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Usimamizi wa Maadili, Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bi. Janeth Mishinga akiwasilisha mada kuhusu maadili katika utumishi wa umma kwa watumishi wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI wakati wa kikao kazi cha Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bw. Juma Mkomi na watumishi wa Ofisi yake kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi jijini Dodoma.