Na. Veronica Mwafisi-Arusha
Tarehe 06 Februari, 2024
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi
wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene amewataka watalaam wa
Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kutatua changamoto wanazokutana
nazo wananchi wanaotumia mifumo ya TEHAMA ili kurahisisha upatikanaji wa
huduma.
Mhe. Simbachawene ameyasema hayo leo wakati akifungua
kikao kazi cha nne (4) cha Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) katika Kituo cha
Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC).
“Nina furaha kubwa kwamba leo ninazungumza na watu
sahihi, hivyo ni imani yangu kuwa, kwa muda huu wa siku tatu mtakaokuwa hapa mtaweza
kuzungumza yale yaliyofanikiwa katika TEHAMA, mtakubaliana kwa uwazi lakini pia
mtazungumzia changamoto ambazo wateja wetu wanaotumia mifumo ya TEHAMA
wanakutana nazo,” Mhe. Simbachawene amesisitiza.
Ameongeza kuwa, kuimarika kwa Taasisi ya eGA kunatokana
na nia ya dhati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia
Suluhu Hassan ya kukuza matumizi ya TEHAMA katika utendaji kazi wa Serikali ili
kuwezesha utoaji wa huduma kwa umma kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanapata
huduma kwa urahisi popote walipo.
Amesema pamoja na yote yatakayozungumzwa katika kikao
kazi hicho, kikubwa ni suala la utoaji wa huduma kwa wananchi, kipimo chake ni
dhahiri kwani wananchi wakilalamika na kukaa kwenye foleni maana yake watumishi
hawajatimiza wajibu wao.
Hivyo kila mmoja awajibike katika eneo lake ili
kufikia azma ya dhati ya Rais. Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya utoaji wa
huduma bora kwa umma kwa ustawi wa taifa.
Akimkaribisha Waziri Simbachawene kufungua kikao kazi
hicho, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Juma
Mkomi amesema katika kuhakikisha TEHAMA inaimarika Serikalini kama ambavyo Rais
Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa akisisitiza mara kwa mara, Ofisi ya
Rais-UTUMISHI itaendelea kuboresha miundo ya kiutumishi pamoja na stahiki za
wataalam wa TEHAMA ili kuhakikisha wanatumia taaluma zao ipasavyo kuleta
matokeo chanya kwa maendeleo ya taifa letu.
Amesema mafanikio ya Serikali Mtandao ni jumuishi kwa
kada zote hivyo Ofisi ya Rais-UTUMISHI itaendelea kusimamia na kuboresha
mazingira ya utendaji kazi kwa kada zote ili kufanikisha ujenzi wa Serikali ya
Kidijitali.
Akielezea majukumu ya utekelezaji wa Mamlaka ya
Serikali Mtandao, Mkurugenzi Mkuu wa eGA Mhandisi Benedict Ndomba amesema Rais
Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kutokana na dhamira yake ya dhati ya kutaka kuwa
na Serikali Mtandao, kupitia Ofisi ya Rais-UTUMISHI amekuwa akitenga fedha za
kutosha kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya TEHAMA.
Amesema zaidi ya washiriki 1,000 kutoka taasisi za
umma wanashiriki kikao kazi hicho kinaongozwa na kaulimbiu isemayo ‘Uzingatiwaji
wa Sera, Sheria, Viwango na Miongozo ya Serikali Mtandao Kwa Ubadilishanaji
Salama wa Taarifa.’
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akifungua kikao kazi cha nne (4) cha Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC).
Sehemu ya washiriki wa kikao kazi cha nne (4) cha Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene (hayupo pichani) wakati akifungua kikao kazi hicho katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC).
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Juma Mkomi, akitoa maelezo ya awali kabla ya kumkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene kufungua kikao kazi cha nne (4) cha Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC).
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) Mhandisi Benedict Ndomba akielezea majukumu ya eGA kabla ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene kufungua kikao kazi cha nne (4) cha Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC).
Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene
akifuatilia kikao
kazi cha nne (4) cha Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) katika Kituo cha
Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC).
No comments:
Post a Comment