Na. Lusungu Helela-Iringa
Tarehe 21 Februari, 2024
Waziri wa Nchi, Ofisi
ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George
Simbachawene amemuelekeza Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bw. Juma Mkomi
kusimamisha mishahara ya Viongozi walioshindwa kuwasimamia watumishi wao
kujisajili na kujaza mipango kazi yao katika Mfumo wa Usimamizi wa Utendaji
Kazi kwa Watumishi wa Umma na Taasisi za Umma (PEPMIS/PIPMIS) na kukwamisha
utekelezaji wa zoezi hilo lenye masilahi mapana katika utumishi wa umma na
taifa kwa ujumla.
Mhe. Simbachawene
ametoa maelekezo hayo leo mkoani Iringa alipokuwa akizungumza na Wajumbe wa
Baraza Kuu la Wafanyakazi katika Utumishi wa Umma Tanzania Bara wakati akifungua
Baraza hilo.
Amesema ujenzi wa
mfumo wa PEPMIS/PIPMIS pamoja na mifumo mingine ya TEHAMA ni utekelezaji wa maelekezo
ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan
ambaye amedhamiria kwa dhati kuwa na Serikali ya kidijitali itakayorahisisha
utendaji kazi wa watumishi wa umma kwa lengo la kutoa huduma bora kwa wananchi.
“Mfumo
huu wa PEPMIS na PIPMIS ni mbadala wa Mfumo wa Wazi wa Upimaji wa Utendaji kazi
(OPRAS) na Mfumo wa Mikataba wa Utendaji Kazi wa Taasisi (IPCS) ulioonekana
kuwa na changamoto za usimamizi wa utendaji kazi
zilizojitokeza katika utekelezaji wa mfumo wa awali wa OPRAS hivyo mfumo huu
umeboreshwa ili kuondokana na changamoto hizo, hivyo ni wajibu wa kila mtumishi
kushiriki kikamilifu katika kutekeleza mfumo huu muhimu,” Mhe. Simbachawene
amesisitiza.
Amesema mifumo hii ya TEHAMA ni nyenzo muhimu
katika kutekeleza majukumu na inalenga kuleta tija, ufanisi na kuchangia kwa
kiwango kikubwa katika maendeleo ya watumishi wa Umma na nchi kwa ujumla.
Amesema wanaotakiwa kuwajibishwa kwanza kwa
kushindwa kutekeleza zoezi hili la PEPMIS/PIPMIS ni viongozi ambao wameshindwa
kuwasimamia watumishi wao, hivyo hatua za kusimamisha mshahara zianze kwa viongozi
huku watumishi ambao hawajatekeleza wapewe muda wa kutekeleza na wakishindwa,
hatua zichukuliwe kwa watumishi hao.
Vilevile, amekemea tabia ya baadhi ya Waajiri
kukataa kuwapokea watumishi wanaohamishiwa kwenye taasisi wanazoziongoza na
baadhi kutoruhusu watumishi kuhama hata pale inapoelekezwa na Mamlaka kwani kwa
kufanya hivyo ni ukosefu wa maadili na ni jambo ambalo halikubaliki.
‘’Hili jambo sio sahihi kwenye Utumishi wa Umma
kwani kuna baadhi ya Waajiri wanaendesha ofisi za Umma kwa utashi na matakwa
binafsi’’ amesisitiza Mhe. Simbachawene
Akitoa maelezo ya awali kuhusu baraza hilo, Katibu
Mkuu-UTUMISHI, Bw. Juma Mkomi ambaye ndiye Mwenyekiti wa Baraza hilo amesema
elimu ya utekelezaji wa Mifumo ya TEHAMA ikiwemo Mfumo wa PEPMIS/PIPMIS na
Mfumo wa Kubaini Mahitaji ya Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma (HR
Assessment) imetolewa nchi nzima lakini kumekuwa na kutowajibika kwa baadhi ya
viongozi katika kuwasimamia watumishi wao kutekeleza zoezi hilo.
Katibu Mkuu Mkomi amesema hatua zimeshaanza
kuchukuliwa na zinaendelea kuchukuliwa kwa wote ambao wameshindwa kutekeleza
zoezi hilo.
Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya wajumbe wa
Baraza, Makamu Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Wafanyakazi katika Utumishi wa Umma
Tanzania Bara, Bw. Joel Kaminyoge amemshukuru Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu
Hassan kwa kuboresha masilahi na stahiki za watumishi wa umma nchini kwani
malalamiko mengi ya watumishi ikiwemo kudai stahiki zao yamepungua kwa kiasi
kikubwa.
Amesema kufuatia maboresho makubwa aliyoyafanya
Mhe. Rais, jukumu walilo nalo sasa ni kuwahimiza watumishi wa umma kufanya kazi
kwa bidii na uadilifu ili kutoa huduma bora kwa umma kama ambavyo serikali
imekusudia.
Baraza Kuu la Wafanyakazi katika Utumishi wa Umma
Tanzania Bara lilianzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Majadiliano ya pamoja katika
Utumishi wa Umma Sura 105.
Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
George Simbachawene akizungumza na Wajumbe wa Baraza Kuu la Wafanyakazi katika
Utumishi wa Umma Tanzania Bara (hawapo pichani) alipokuwa akifungua Baraza hilo
leo mkoani Iringa.
Naibu Waziri,
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani
Kikwete akizungumza na Wajumbe wa Baraza Kuu la Wafanyakazi katika Utumishi wa
Umma Tanzania Bara (hawapo pichani) kabla ya Waziri Simbachawene kufungua Baraza
hilo leo mkoani Iringa.
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Juma Mkomi akitoa maelezo kuhusu Baraza Kuu la Wafanyakazi katika Utumishi wa Umma Tanzania Bara kabla ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene kufungua Baraza hilo leo mkoani Iringa
Makamu
Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Wafanyakazi katika Utumishi wa Umma Tanzania Bara,
Bw. Joel Kaminyoge akitoa neno la shukrani kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene baada
ya Waziri huyo kufungua Baraza Kuu la Tano la Wafanyakazi katika Utumishi wa
Umma Tanzania Bara leo mkoani Iringa
Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
George Simbachawene akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Wajumbe wa Baraza
Kuu la Wafanyakazi katika Utumishi wa Umma Tanzania Bara mara baada ya kufungua
Baraza hilo mkoani Iringa.
No comments:
Post a Comment