Na. Lusungu
Helela-Dodoma
Tarehe 20 Februari,
2024
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bw. Juma Mkomi amewataka
Maafisa Rasilimaliwatu wote serikalini kuhakikisha wanaweka kumbukumbu sahihi
za watumishi wa umma wanaotarajia kustaafu kabla ya miezi sita ili kuwaondolea
usumbufu wa kufuatilia mafao yao pindi wanapostaafu.
Ametoa kauli hiyo leo jijini Dodoma wakati akizungumza
kwenye kikao kazi na watumishi wa Ofisi yake, ikiwa ni mwendelezo
wa kuhimiza utendaji na uwajibikaji kwa
watumishi wa umma nchini.
Katibu Mkuu Mkomi amesema haikubaliki mtumishi anapewa barua ya
kustaafu huku baadhi ya taarifa za michango ya mafao yake haiko sawa.
‘’Mtumishi anapewa barua ya kumtaarifu kustaafu kabla ya miezi
sita halafu baadaye anaanza kusumbuliwa eti michango ya mafao haionekani, sasa
hiyo barua aliyopewa kabla ya miezi sita ilikuwa na maana gani" amehoji Bw.
Mkomi.
Amesisitiza kuwa suala hili lazima lifanyiwe kazi kwa kuwa
watumishi hao wanaostaafu wamelitumikia taifa kwa moyo hivyo kuhangaishwa sio
haki.
Katika hatua nyingine, Bw. Mkomi ametoa onyo kwa watumishi
wanaovujisha siri za serikali ambapo ameahidi wale wote watakaobainika watachukuliwa
hatua kali za kisheria ili iwe fundisho kwa wengine.
Amesema kitendo hicho ni kinyume cha maadili ya utumishi wa
umma ambapo ametumia fursa hiyo kuwaasa watumishi hao kujiepusha na tabia hiyo.
Pia, Katibu Mkuu Mkomi amewataka watumishi wa umma kuzingatia
maadili ya utendaji wanapotoa huduma kwa wananchi kwani maadili ndio msingi wa
utumishi wa umma.
Kwa kusisitiza hilo amewataka watumishi wa Ofisi yake kuwa mfano
wa uzingatiaji wa maadili kwa vile Ofisi hiyo ni kioo cha Utumishi wa umma
nchini.
Naye Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu, Bw. Musa
Magufuli amemshukuru Katibu Mkuu Mkomi kwa kutenga muda kuzungumza na watumishi
wa Ofisi yake licha ya majukumu mazito yanayomkabili huku akiahidi maagizo yote
aliyoyatoa yatatekelezwa.
Awali katika kikao kazi hicho, mada mbalimbali zilitolewa kwa
watumishi hao ikiwemo Maadili kwa Watumishi wa Umma, Kukabiliana
na Msongo wa Mawazo, PSSSF Kiganjani na faida ya kujiunga na SACCOS ya Ofisi ya
Rais-UTUMISHI.
Katibu Mkuu
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Juma Mkomi akizungumza na
watumishi wa ofisi yake (hawapo pichani) wakati wa kikao kazi chake na
watumishi hao kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi
jijini Dodoma.
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Juma Mkomi, akiteta na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi wakati wa kikao kazi cha Katibu Mkuu huyo na watumishi wa Ofisi yake kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi jijini Dodoma
No comments:
Post a Comment