Na Mwandishi Wetu- DODOMA
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa ameziagiza Taasisi za Serikali ambazo
hazijajiunga na mfumo wa kielektroni utakaowezesha mifumo ya Serikali
kuwasiliana (GovESB) kujiunga na mfumo huo
ifikapo Julai 30 mwaka huu ili kuendana na mabadiliko ya teknolojia
katika kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi.
Mhe. Majaliwa ametoa maagizo hayo
wakati akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.
Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya
Utumishi wa Umma yaliyofanyika katika viwanja vya Chinangali Park Jijini
Dodoma.
“Taasisi zote za umma ambazo hazijajiunga na
mfumo huu mwisho ni Julai 30 mwaka huu, wote mhakikishe mmejiunga GovESB, huu
ni msisitizo ambao ulitolewa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa
kila taasisi ipeleke mfumo wake eGA, idadi ya taasisi zilizounganishwa ni
chache, hakuna gharama na hutakiwi kupanga bajeti”
Mhe. Majaliwa ameongeza kuwa mfumo huo
unafaida kubwa katika utumishi wa umma kwani utasaidia kurahisisha utendaji,
kutoa taarifa kwa wakati, kuondoa makosa ya kibinadamu katika kuwahudumia
wananchi pamoja na kuwabana wala rushwa. “Nimefurahi kujulishwa kwamba jumla
ya mifumo 223 kutoka kwenye taasisi 185 imeunganishwa na kusomana”.
Aidha, Mhe. Majaliwa ametoa wito kwa taasisi
zote za umma zenye mifumo na zinazoendelea kubuni mifumo zihakikishe mifumo
hiyo inasomana na inaweza kubadilishana taarifa kupitia mfumo huo wa GovESB
ikiwa ni njia mojawapo ya kuendelea kuboresha huduma za Serikali.
Kadhalika, Mhe. Majaliwa ameitaka Mamlaka ya
Serikali Mtandao (eGA) kuhakikisha mifumo iliyounganishwa inaendelea
kubadilishana taarifa pamoja na kujiridhisha kwa kila anayeingia awe na uwezo
wa kuwasiliana na wengine wote waliomo ndani.
Katika hatua nyingine, Mhe. Majaliwa ametoa
wito kwa watumishi wa umma kuzingatia miiko na maadili ya utumishi katika
utekelezaji wa majukumu yao kwa kuzingitia Sera na Sheria kwa manufaa na
maendeleo ya Taifa letu.
“Nitumie nafasi hii kuwapongeza sana
watumishi wote wa umma nchini, niwahikishie kuwa serikali ya awamu ya sita iko
pamoja nanyi, fanyeni hivyo kwa ajili ya manufaa na maendeleo ya Taifa letu”,
amesema Mhe. Majaliwa.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe.George Simbachawene
amesema Tanzania imetambulika kimataifa ambapo mwaka 2022 Benki ya Dunia
ilifanya utafiti kuhusu ukomavu wa matumizi ya teknolojia duniani katika utoaji
wa huduma za Serikali na ushirikishwaji wa wananchi.
Amefafanua kuwa ripoti ya utafiti huo
iliyotolewa Machi, 2023 ilibanisha kuwa Tanzania imefanikiwa kupanda daraja
kutoka kundi B hadi kundi A na kushika nafasi ya 26 duniani, nafasi ya 2 Afrika
na nafasi ya kwanza katika nchi za Afrika Mashariki.
Katika tukio hilo, Mhe. Majaliwa amezindua
mifumo miwili ambayo ni Mfumo wa kielektroni unaowezesha mifumo ya Serikali
kuwasiliana na kubadilishana taarifa ujulikanao kama Government
Enterprises Service Bus (GovESB) pamoja na Mfumo wa e-Wekeza unaomuwezesha
Mtumishi wa Umma kuwekeza katika Mfuko wa Faida (Faida Fund).
Siku ya Utumishi wa Umma husherehekewa Juni
23 kila mwaka na nchi wanachama wa Umoja wa Afrika kwa lengo la kutambua
mchango wa Watumishi wa Umma katika maendeleo ya nchi zao na Bara la Afrika kwa
ujumla.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa akizungumza alipomwakilisha Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu
Hassan katika kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yaliyofanyika kwenye
Viwanja vya Chinangali jijini Dodoma.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene
akitoa maneno ya utangulizi kabla ya kumkaribisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa kuzungumza na Watumishi wa Umma
na Wananchi wakati alipomwakilisha Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan
katika kilele cha Wiki ya Utumishi wa Umma kwenye Viwanja vya Chanangali
jijini Dodoma.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa (kulia) akiteta jambo na Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bw. Juma Mkomi
(kushoto) wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yaliyofanyika kwenye
Viwanja vya Chinangali jijini Dodoma.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa akisalimiana na viongozi mbalimbali alipowasili
kwenye viwanja vya Chinangali jijini Dodoma kumwakilisha Rais Mhe. Dkt.
Samia Suluhu Hassan katika kilele cha Wiki ya Utumishi wa Umma, Juni 23,
2025.
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-UTUMISHI
(wa pili kutoka kulia) akimsikiliza Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa (hayupo pichani) wakati alipokuwa akitembelea
mabada katika kilele cha Wiki ya
Utumishi wa Umma kwenye viwanja vya Chinangali jijini Dodoma.Wa kwanza kulia ni Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasilioano Serikalini Bi. Mary Mwakapenda.
Wakurugenzi na Wakurugenzi
Wasaidizi kutoka Ofisi ya Rais- UTUMISHI wakifuatilia hotuba ya Waziri
Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa wakati
akimwakilisha Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kilele cha Maadhimisho
ya Wiki ya Utumishi wa Umma yaliyofanyika kwenye Viwanja vya Chinangali
jijini Dodoma.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa akimkabidhi tuzo maalum ya pongezi Afisa
TEHAMA wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA), Bw. Salum Mohamed kwa kushiriki katika
usanifu na ujenzi wa Mfumo wa Ubadilishanaji Taarifa Serikalini ((Government
Enterprise Service Bus-GovESB) katika kilele cha Wiki ya Utumishi wa Umma kwenye viwanja vya Chinangali jijini Dodoma.
Watumishi wa Umma na Wananchi
wakiwa katika Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma 2025 yaliyofanyika katika
Viwanja vya Chinangali jijini Dodoma.
Baadhi ya Watumishi wa Ofisi ya
Rais-UTUMISHI wakifuatilia hotuba ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa wakati akimwakilisha Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu
Hassan katika kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yaliyofanyika kwenye
Viwanja vya Chinangali jijini Dodoma. Wengine ni Watumishi wa Umma kutoka Wizara
na Taasisi mbalimbali na Wananchi waliohudhuria hafla hiyo.
Baadhi ya Watumishi wa Ofisi ya
Rais-UTUMISHI wakifuatilia hotuba ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa wakati akimwakilisha Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu
Hassan katika kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yaliyofanyika kwenye
Viwanja vya Chinangali jijini Dodoma. Wengine ni Watumishi wa Umma kutoka Wizara
na Taasisi mbalimbali na Wananchi waliohudhuria hafla hiyo.