Thursday, March 12, 2026

KATIBU MKUU-UTUMISHI AWASISITIZA WATUMISHI WA UMMA KUFANYA KAZI KWA BIDII ILI KULETA TIJA KATIKA JAMII


Na. Antonia Mbwambo na Eric Amani-Dodoma.

Tarehe 12 machi, 2026

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bw. Juma Mkomi, amewasisitiza Wajumbe wa Baraza la wafanyakazi la Ofisi yake kufanya kazi kwa bidii na weledi kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za utendaji ili kuleta mabadiliko yenye tija kwa maendeleo ya taifa.

Bw. Mkomi ameyasema hayo leo tarehe 12 Machi, 2026 wakati wa Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi la Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora uliolenga kupitisha Mpango na Bajeti ya Ofisi hiyo ya Mwaka wa Fedha 2026/27 uliofanyika katika ukumbi wa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa jijini Dodoma.

“Katika kufikia Utumishi wa Umma uliotukuka, nitoe wito kwa wajumbe wote wa baraza, kutekeleza majukumu yenu ipasavyo ili kutoa huduma bora itakayotatua changamoto za wananchi.” Bw. Mkomi alisema.

Aidha Katibu Mkuu Mkomi amewataka wajumbe wa mkutano huo kuhakikisha kunakuwa na ushirikishwaji wa Watumishi katika mikakati inayopangwa na  kamati hiyo ili kuongeza uelewa wa masuala ya kiutumishi na kuwa na mtazamo chanya utakaoleta ufanisi katika utendaji wao .

Ameongeza kuwa ni muhimu kukawa na mafunzo kwa wajumbe wa Baraza hilo ili kuwajengea uwezo kwa matokeo chanya katika maeneo yao ya kazi.

Bw. Mkomi alimshukuru mwakilishi wa Katibu Mkuu TUGHE Taifa, ambaye ni Mwenyekiti wa TUGHE Mkoa wa Dodoma Bw. Maulidi Kipeneku kwa ushiriki wake katika mkutano huo na kuahidi kuwa Ofisi ya Rais-UTUMISHI itashirikiana na TUGHE wakati wote katika kuhakikisha Baraza linatekeleza majukumu yake kikamilifu.

Awali Bw. Kipenuke aliipongeza Ofisi hiyo kwa kuzingatia sheria ya kufanya baraza ya wafanyakazi kwa wakati. “Mmekuwa kioo, mabaraza yanafanyika kwa wakati na ni shirikishi, huku akiwatasisitiza wajumbe kutoa michango yao ili kuwawakilisha kwa ufasaha watumishi katika Idara na Vitengo vyao.” Alisisitiza Bw. Kipenuke.   


Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma Bw. Juma Mkomi akizingumza na Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi kutoka Ofisi hiyo wakati wa Mkutano wa baraza hilo katika Ukumbi wa Ofisi ya Kumbukumbu na Nyaraka  leo  machi  12, 2026 Jijini Dodoma.



Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa TUGHE Taifa ambaye pia ni Mwenyekiti wa TUGHE Mkoa wa Dodoma Bw. Maulid Kipeneku (Aliyesimama) akitoa neno la salamu kwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma Bw. Juma Mkomi (Aliyekaa) na washiriki wote wa mkutano wa baraza la wafanyakazi kutoka Ofisi hiyo (Hawapo Pichani) jijini Dodoma Machi 12, 2026.



Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma Bw. Juma Mkomi (Aliyekaa Katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi hiyo mara baada ya Kuhitimisha Mkutano wa Baraza hilo leo machi 12, 2026 Jijini Dodoma.




Sehemu ya Wakurugenzi kutoka Idara na Vitengo mbalimbali Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wakipitia agenda za mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa ofisi hiyo leo Machi 12, 2026 jijini Dodoma. 



Afisa Mchumi kutoka Idara ya Mipango, Ofisi ya Rais - UTUMISHI Bw. Rifati H. Almasi akiwasilisha mada kwa Katibu Mkuu ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi Bw. Juma Mkomi (hayupo Pichani) wakati wa Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi ya hiyo Machi 12, 2026 Jijini Dodoma.

Wajumbe wa Mkutano wa Baraza la wafanyakazi kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wakiwa katika picha ya pamoja wakati wa  Mkutano wa baraza hilo uliyofanyika Leo Machi 12, 2026 jijini Dodoma, Mkutano huo uliongozwa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais - UTUMISHI  ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza hilo Bw. Juma Mkomi.



                                                                                                                                                                                             

No comments:

Post a Comment