Friday, March 31, 2023

MFUMO MPYA WA KUPIMA UTENDAJI KAZI KUBAINI MIKOA NA HALMASHAURI ZINAZOONGOZA KUKWEPA KUTOA UFAFANUZI WA MASUALA YA KIUTUMISHI

 

Na. James K. Mwanamyoto-Dodoma

Tarehe 31 Machi, 2023

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amesema mfumo mpya wa kupima utendaji kazi wa watumishi wa umma utatumika kubaini mikoa na halmashauri ambazo zinaongoza kukwepa jukumu la kutoa ufafanuzi wa masuala ya kiutumishi kwa kuwasilisha barua kwa Katibu Mkuu UTUMISHI kuomba ufafanuzi wa masuala ambayo mikoa na halmashauri hizo zina uwezo wa kutoa ufafanuzi kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo iliyopo.

Mhe. Jenista amesema hayo jijini Dodoma, wakati akizungumza na Wanasheria na Maafisa Utumishi kutoka katika Sekretarieti za Mikoa na Halmashauri za Wilaya, kabla ya kufungua kikao kazi cha maafisa hao kilicholenga kuzitafutia ufumbuzi changamoto wanazokabiliana nazo katika utekelezaji wa Sheria ya Utumishi wa Umma na kanuni zake.

Mhe. Jenista amesema, mfumo huo utawaweka kwenye kundi la kutowajibika watumishi wote watakaosababisha mikoa na halmashauri zao kukwepa jukumu la kutoa ufafanuzi wa masuala ya kiutumishi kwa kusingizia kuwa masuala hayo yanapaswa kutolewa ufanuzi na Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma.

Mhe. Jenista amehoji kwanini mwajiri amuandikie barua Katibu Mkuu-UTUMISHI kuomba ufafanuzi wa jambo wakati mwajiri huyo anaye Afisa Utumishi ambaye akishirikiana vizuri na Mwanasheria, kwa kutumia nyaraka zilizopo wana uwezo mkubwa wa kulitolea uamuzi jambo ambalo linaombwa kutolewa ufafanuzi na Katibu Mkuu-UTUMISHI.

“Maafisa Utumishi na Wanasheria mnapaswa kushirikiana katika kutoa ufafanuzi na kufanya maamuzi ya masuala ya kiutumishi kwa mujibu wa Kanuni, Sheria, Taratibu na Miongozo ya kiutumishi iliyopo badala ya kukwepa jukumu hilo,” Mhe. Jenista amesisitiza.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kitengo cha Huduma za Sheria, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bi. Hilda Kabissa amesema, kikao kazi hicho kimelenga kuibua na kuzitafutia ufumbuzi changamoto za utekelezaji wa Sheria ya Utumishi wa Umma na kanuni zake hususani wakati wa kushughulikia masuala ya kinidhamu ikiwa ni pamoja na kuzitafutia ufumbuzi changamoto za ucheleweshaji wa mafao ya wastaafu.

Mmoja wa washiriki wa kikao kazi hicho, ambaye ni Afisa Utumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero Bi. Alice Lunyata amesema amejipanga kutekeleza maelekezo ya Mhe. Jenista Mhagama ya kupunguza kuwasilisha maombi Ofisi ya Rais-UTUMISHI ya kupatiwa ufafanuzi wa masuala ya kiutumishi kwa kuwaelekeza, kuwapatia ufafanuzi na kuwaelimisha watumishi wa umma kuhusiana na masuala yao kwa mujibu wa Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo ya Utumishi wa Umma iliyopo.

Mshiriki mwingine ambaye ni Afisa Sheria wa Halmashauri ya Wilaya ya Tandahimba, Bw. Zuberi Sarahani amesema kuwa, yeye pamoja na Wanasheria wenzie watashirikiana na Maafisa Utumishi katika kutoa tafsiri sahihi ya Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo ili kupunguza idadi ya barua za kuomba ufafanuzi.

Naye, Mkuu wa Idara ya Utawala na Utumishi wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Bi. Tamko Ally amesema baada ya kupokea maelekezo ya Mhe. Jenista Mhagama watahakikisha wanashirikiana na Wanasheria kusoma nyaraka na kuchambua hoja zilizowasilishwa katika taaasi zao.

Kikao kazi hicho kilichoandaliwa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kimehudhuriwa na Maafisa Utumishi na Wanasheria kutoa Sekretarieti za Mikoa 16 na Halmashauri za Wilaya 84.

 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akizungumza na Wanasheria na Maafisa Utumishi wa Sekretarieti za Mikoa na Halmashauri za Wilaya, kabla ya kufungua kikao kazi cha maafisa hao jijini Dodoma kilicholenga kuzitafutia ufumbuzi changamoto za utekelezaji wa Sheria ya Utumishi wa Umma na kanuni zake.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akiwa na Wanasheria na Maafisa Utumishi wa Sekretarieti za Mikoa na Halmashauri za Wilaya, kabla ya kufungua kikao kazi cha maafisa hao kilicholenga kuzitafutia ufumbuzi changamoto za utekelezaji wa Sheria ya Utumishi wa Umma na kanuni zake.

 

 

Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama kuzungumza na Wanasheria na Maafisa Utumishi wa Sekretarieti za Mikoa na Halmashauri za Wilaya, wakati wa kikao kazi cha maafisa hao kilicholenga kuzitafutia ufumbuzi changamoto za utekelezaji wa Sheria ya Utumishi wa Umma na kanuni zake.


 

Mkurugenzi wa Kitengo cha Huduma za Sheria, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bi. Hilda Kabissa akieleza lengo la kikao kazi cha Wanasheria na Maafisa Utumishi wa Sekretarieti za Mikoa na Halmashauri za Wilaya, kilichofunguliwa jijini Dodoma na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama.

 

 

Afisa Utumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero, Bi. Alice Lunyata akieleza namna alivyojipanga kutekeleza maelekezo ya Mhe. Jenista Mhagama aliyoyatoa jijini Dodoma wakati akifungua kikao kazi chao kilicholenga kuzitafutia ufumbuzi changamoto za utekelezaji wa Sheria ya Utumishi wa Umma na kanuni zake.

   

Afisa Sheria wa Halmashauri ya Wilaya ya Tandahimba, Bw. Zuberi Sarahani akieleza namna alivyojipanga kutekeleza maelekezo ya Mhe. Jenista Mhagama aliyoyatoa jijini Dodoma wakati akifungua kikao kazi chao kilicholenga kuzitafutia ufumbuzi changamoto za utekelezaji wa Sheria ya Utumishi wa Umma na kanuni zake.


Mkuu wa Idara ya Utawala na Utumishi wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Bi. Tamko Ally akieleza namna alivyojipanga kutekeleza maelekezo ya Mhe. Jenista Mhagama aliyoyatoa jijini Dodoma wakati akifungua kikao kazi chao kilicholenga kuzitafutia ufumbuzi changamoto za utekelezaji wa Sheria ya Utumishi wa Umma na kanuni zake.

 

 

 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akiwa katika picha ya pamoja na watendaji wa ofisi yake,  Wanasheria na Maafisa Utumishi wa Sekretarieti za Mikoa na Halmashauri za Wilaya, mara baada ya kufungua kikao kazi cha maafisa hao kilicholenga kuzitafutia ufumbuzi changamoto za utekelezaji wa Sheria ya Utumishi wa Umma na kanuni zake.


 

 

Sehemu ya Wanasheria na Maafisa Utumishi wa Sekretarieti za Mikoa na Halmashauri za Wilaya wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani) wakati Waziri huyo akifungua kikao kazi cha maafisa hao jijini Dodoma kilicholenga kuzitafutia ufumbuzi changamoto za utekelezaji wa Sheria ya Utumishi wa Umma na kanuni zake.