Na. James K. Mwanamyoto-Tanga
Tarehe 29 Machi, 2023
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amewapongeza
wakazi wa Majani ya Chai Kata ya Maweni jijini Tanga kwa kukipambania Chuo cha
Utumishi wa Umma (TPSC) kupata eneo la kujenga kampasi itakayokuwa na manufaa
ya vizazi vyao, kwa wakazi wa mkoa huo na Watanzania wote watakaopata fursa ya
kupata elimu katika kampasi hiyo pindi ujenzi wake utakapokamilika.
Mhe. Jenista ametoa pongezi hizo
wakati akizungumza na wananchi wa Majani ya Chai Kata ya Maweni jijini Tanga
alipoenda kuwatembelea kwa lengo la kuwashukuru kwa kukiunga mkono Chuo cha
Utumishi wa Umma kupata umiliki wa kiwanja ili kujenga kampasi jijini humo.
Mhe. Jenista amesema kuwa, wakazi wa
Majani ya Chai jijini Tanga wametoa somo kwa Watanzania kwani maeneo mengine,
Serikali ikitaka kujenga miundombinu endelevu kwenye eneo lenye mgogoro wa ardhi
mara nyingi wananchi wanakuwa upande wa wanaodai kumiliki viwanja licha ya kushindwa
kuviendeleza, hivyo wananchi wa Majani ya Chai wanapaswa kuwa mfano wa kuigwa
kwa kupambania ujenzi wa chuo kwa manufaa ya taifa.
“Nimefurahishwa sana na uamuzi wenu wa kulilinda na kulipambania eneo hili na hatimaye Chuo cha Utumishi wa Umma kimepata kiwanja cha kujenga kampasi na kuongeza kuwa, limekuwa ni somo tosha ya namna ya kuisaidia Serikali kupata eneo la kujenga miundombinu yenye tija kwa Serikali na wananchi pia,” Mhe. Jenista amesisitiza.
Mhe. Jenista amesema, changamoto
iliyokuwepo ilikuwa ni upatikanaji wa eneo la kujenga kampasi ya chuo jijini
Tanga, hivyo amemshukuru Kamishna wa Ardhi jijini Tanga kwa kutoa taarifa rasmi
kuwa kiwanja hicho ni mali ya Chuo cha Utumishi wa Umma mara baada ya kufanyika
kwa mchakato wote wa kisheria wa umilikishaji ardhi kwenye eneo lililokuwa na
mgogoro.
“Tumejipanga kujenga kampasi yetu
wenyewe kwani tunapanga jengo la kuendesha shughuli za chuo ambalo
linatugharimu shilingi milioni 84 kwa mwaka, hivyo leo wananchi wa Majani ya
Chai mmeokoa fedha hiyo ya Serikali na kuiwezesha Serikali kutekeleza mpango wa
kujenga uwezo wa rasilimali watu iliyonayo kupitia mafunzo yatakayotolewa na
kampasi hiyo kwa watumishi wa umma,” Mhe. Jenista amefafanua.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya
Tanga, Mhe. Hashim Mgandilwa amesema wananchi wa eneo hilo wametekeleza wajibu
wao kwa kukipambania Chuo cha Utumishi wa umma kupata eneo la kujenga kampasi
jijini Tanga, hivyo amewataka kuendelea kulilinda eneo hilo mpaka ujenzi
utakapokamilika.
Naye, Diwani wa Kata ya Maweni, Mhe. Joseph Kolivasi amemshukuru Mhe. Jenista kwa kuwatembelea wananchi wa kata yake na kuongeza kuwa, anaamimi kuwa Kampasi ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanga itaanza kujengwa mapema iwezekenavyo na si kujengwa katika eneo lingine kama ambavyo wananchi wa eneo analolitawala wanavyotarajia.
Mmoja wa wakazi wa Kata ya Maweni, Mzee Abdallah Kilo amesema amefurahia kitendo cha Chuo cha Utumishi wa Umma kupewa umiliki wa eneo hilo ili kujenga kampasi kwa manufaa ya kizazi kijacho, kwani ndio jambo ambalo yeye na wenzie wamekuwa wakilipambania kwa nguvu zao zote.
Kaimu Mkuu wa Chuo na Mtendaji Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) Dkt. Ernest Mabonesho amewashukuru wananchi wa eneo hilo kwa kuunga mkono jitihada za chuo chake kupata kiwanja kwa ajili ya kujenga kampasi jijini Tanga na kuongeza kuwa eneo hilo limepatikana kwa jitihada za wananchi hao.
Dkt. Mabonesho amemshukuru Kamishna
wa Ardhi kwa kukamilisha taratibu za kisheria zilizokiwezesha chuo chake kumiliki
kiwanja hicho kwa ajili ya ujenzi wa Kampasi ya Tanga.
Sanjari na hilo, amemshukuru Mhe. Jenista Mhagama kwa uamuzi wake wa kuwatembelea wananchi wa eneo hilo ili kuwashukuru kwa mchango wao katika upatikanaji wa kiwanja hicho.
Chuo cha Utumishi wa Umma kimemilikishwa eneo la ekari 12 kwa ajili ya ujenzi wa kampasi yake jijini Tanga, kampasi inayotarajiwa kutoa mchango wa kujenga uwezo wa kiutendaji wa rasilimaliwatu ya taifa.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akizungumza na wananchi wa Majani ya Chai kata ya Maweni jijini Tanga alipoenda kuwatembelea kwa lengo la kuwashukuru kwa jitihada zao za kukiunga mkono Chuo cha Utumishi wa Umma kupata hati ya kumiliki kiwanja kwa ajili ya kujenga kampasi ya chuo hicho jijini humo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akiwa na viongozi pamoja na wananchi wa Majani ya Chai Kata ya Maweni jijini Tanga wakati akiwasili eneo ambao Chuo cha Utumishi wa Umma kimepata kiwanja kwa ajili ya kujenga kampasi yake jijini Tanga.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akioneshwa ramani ya kiwanja cha Chuo cha Utumishi wa Umma na Kamishna wa Ardhi jijini Tanga alipowasili eneo ambalo chuo hicho kitajenga kampasi yake jijini humo.
Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Mhe. Hashim Mgandilwa akizungumza na wananchi wa Majani ya Chai kata ya Maweni jijini Tanga kabla ya kumkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama kuzungumza na wananchi hao.
Diwani wa Kata ya Maweni, Mhe. Joseph Kolivasi akimshukuru Mhe. Jenista Mhagama kwa kuwatembelea wananchi wa kata yake wakati alipoenda kulitazama eneo ambalo Chuo cha Utumishi wa Umma kitajenga kampasi yake jijini Tanga.
Kaimu Mkuu wa Chuo na Mtendaji Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) Dkt. Ernest Mabonesho akiwashukuru wananchi wa Majani ya Chai Kata ya Maweni jijini Tanga kwa kuunga mkono jitihada za chuo chake kupata kiwanja kwa ajili ya kujenga kampasi jijini humo.
Mmoja wa wakazi wa Kata ya Maweni jijini Tanga, Mzee Abdallah Kilo akieleza furaha yake kwa Mhe. Jenista Mhagama mara baada ya Chuo cha Utumishi wa Umma kupata haki ya umiliki wa kiwanja itakayowawezesha kujenga kampasi katika kata yake.
Mwonekano wa sehemu ya kiwanja ambacho Chuo cha Utumishi wa Umma kimemilikishwa kwa ajili ya ujenzi wa Kampasi yake jijini Tanga.
No comments:
Post a Comment