Na. James K. Mwanamyoto-Dodoma
Tarehe 10 Machi, 2023
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete amewataka watumishi wa Idara ya Utawala wa
Utumishi wa Umma kujibu kwa wakati barua za masuala ya kiutumishi ili kuepuka
malalamiko yasiyo ya lazima ambayo yamekuwa yakielekezwa katika Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
Mhe.
Kikwete ametoa maelekezo hayo jijini Dodoma wakati wa kikao kazi chake na
watumishi wa idara hiyo kilicholenga kufahamu majukumu yanayotekelezwa na kuhimiza
uwajibikaji.
Mhe.
Kikwete amewasisitiza watumishi wa idara hiyo ya Utawala wa Utumishi wa Umma
kutosita kujibu barua za wadau kwa wakati hata kama zina mapungufu, ili
wahusika wafahamu mapungufu yaliyopo kwenye masuala yao ya kiutumishi ambayo
yamewasilishwa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi
wa Umma na Utawala Bora kwa ajili ya kupata kibali au kutolewa maamuzi.
“Natambua kuna mapungufu ya masuala ya kiutumishi katika barua
mnazolalamikiwa kutozijibu kwa wakati, lakini mnapaswa kuzijibu kwani
msipofanya hivyo, mnatoa mwanya kwa wahusika kuilalamikia ofisi na hatimaye kuichafua
taswira nzuri ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala
Bora,” Mhe. Kiwete amefafanua.
Aidha, amewataka watumishi wa idara hiyo kuchakata utoaji wa vibali vya uhamisho wa watumishi wa
umma kwa kuzingatia takwimu zinazoainishwa na Mfumo wa Tathmini ya Hali na
Mgawanyo wa Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma ili vibali vya uhamisho
vinavyotolewa visiathiri utendaji kazi wa baadhi ya taasisi katika eneo la
utoaji huduma bora kwa wananchi.
Kuhusiana na utendaji kazi wa Idara ya Utawala wa Utumishi wa Umma kwa ujumla, Mhe. Kikwete amewapongeza watumishi wa idara hiyo kwa kutekeleza majukumu yao kikamilifu licha ya kuwa ni mengi na yenye changamoto nyingi.
Mhe. Kikwete ameongeza kuwa, watumishi wa idara hiyo wanatakiwa
kuendelea kufanya kazi kwa bidii na weledi ili kutimiza azma ya Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kutoa huduma bora kwa
wananchi.
Sanjari na hilo, Mhe. Kikwete amesema utendaji kazi wa watumishi
wa idara hiyo ukiendelea kuwa mzuri utasaidia kulifikia lengo la Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan la kuuboresha
utumishi wa umma utakaowavutia walio katika sekta binafsi kuomba kuajiriwa
Serikalini ili kuwahudumia wananchi.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anaendelea
kutekeleza kwa vitendo azma yake ya kuujenga utumishi wa umma pamoja na
kuboresha mazingira ya utendaji kazi ya watumishi wa umma ili wawe na tija katika
utoaji wa huduma na maendeleo ya taifa.
Naibu
Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Ridhiwani Kikwete akizungumza na watumishi wa Idara ya Utawala wa Utumishi wa
Umma (hawapo pichani) wakati wa kikao kazi chake na watumishi wa idara hiyo
kilichofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI Mtumba jijini Dodoma kwa
lengo la kufahamu majukumu ya Idara hiyo na kuhimiza uwajibikaji.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma
na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Kikwete akimsikiliza Mkurugenzi Msaidizi
anayesimamia sehemu ya Maafisa Waandamizi, Bw. Mohamed Gombati wakati wa kikao
kazi cha Naibu Waziri huyo na watumishi wa Idara ya Utawala wa Utumishi wa Umma
kilichofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI Mtumba jijini Dodoma.
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma,
Bw. Juma Mkomi akisisitiza jambo wakati wa kikao kazi cha Naibu Waziri, Ofisi
ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani
Kikwete (hayupo pichani) na watumishi wa Idara ya Utawala wa Utumishi wa Umma kilichofanyika
katika Ukumbi wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI Mtumba jijini Dodoma.
Mkurugenzi wa Idara ya Utawala wa Utumishi wa Umma Bi.
Felista Shuli akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Idara yake kwa
Naibu waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,
Mhe. Ridhiwani Kikwete wakati wa kikao kazi cha Naibu Waziri huyo na watumishi
wa Idara hiyo, kilichofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI Mtumba
jijini Dodoma.
Mkurugenzi Msaidizi anayesimamia sehemu ya Maafisa
Waandamizi, Bw. Mohamed Gombati akitoa ufafanuzi wa majukumu ya sehemu anayoisimamia
kwa Naibu waziri, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala
Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete (hayupo pichani) wakati wa kikao kazi cha Naibu
Waziri huyo na watumishi wa Idara ya Utawala wa Utumishi wa Umma kilichofanyika
katika Ukumbi wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI Mtumba jijini Dodoma.
No comments:
Post a Comment