Wednesday, March 15, 2023

KAMATI YA BUNGE YA UTAWALA YARIDHISHWA NA JITIHADA ZA MLENGWA WA TASAF WILAYANI UYUI NA KUMCHANGIA 530,000/= KUMUWEZESHA KUKAMILISHA UJENZI WA NYUMBA YA KUISHI

Na. James K. Mwanamyoto-Uyui

Tarehe 15 Machi, 2023

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Mhe. Florent Kyombo amesema kamati yake imeridhishwa na jitihada za mlengwa wa TASAF Kata ya Magiri Wilayani Uyui, Bi. Amina Abdallah kwa kutumia vizuri ruzuku anayoipokea kuanza ujenzi wa nyumba bora ya kuishi, kitendo ambacho kimewashawishi wajumbe wa kamati hiyo kumchangia fedha kiasi cha shilingi 530,000/= ili kuuunga mkono jitihada za mlengwa huyo.

Mhe. Kyombo amesema hayo akiwa katika Kata ya Migiri Wilayani Uyui mkoani Tabora wakati wa ziara ya kikazi ya kamati hiyo iliyolenga kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika wilaya hiyo.

Mhe. Kyombo amesema kitendo cha Mlengwa huyo wa TASAF Bi. Amina Abdallah kujenga nyumba na kufungua mgabiashara ya kilinge cha kuuza kahawa kimetoa somo la nidhamu ya matumizi ya fedha kwa walengwa wengine licha ya kupata kiasi kidogo cha ruzuku.

Mhe. Kyombo amesema kuwa, kazi inayofanywa na TASAF kwa usimamizi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora katika kuzikwamua kaya maskini inaonekana kwa macho kupitia namna walengwa walivyoboresha maisha yao.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amesema kitendo cha wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria kuguswa na kumchangia mlengwa wa TASAF, Bi. Amina Abdallah kimezingatia utu na nia ya dhati ya wajumbe wa kamati hiyo kuunga mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita za kuboresha maisha ya kaya maskini nchini kupitia TASAF.

Aidha, Mhe. Mhagama amuelekeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Uyui na Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo kuhakikisha wanasimamia ujenzi wa nyumba ya mlengwa huyo wa TASAF inakamilika kwa wakati na kuahidi kuwa atarejea tena katika makazi ya mlengwa huyo ili kujiridhisha na utekelezaji wa maelekezo yake.

Naye, Mlengwa huyo wa TASAF Bi. Amina Abdallah amesema, ruzuku ya TASAF imemuwezesha kujenga nyumba bora ya kuishi ambayo inakaribia kukamilika na kuongeza kuwa, kabla ya kuanza kupokea ruzuku ya TASAF kiwanja alichojenga nyumba hiyo kilikaa kwa miaka 10 bila kuendelezwa.

“Nilipoanza kupata ruzuku nilijiwekea utaratibu wa kutumia nusu ya ruzuku kununua matofali, baadae kuanza ujenzi na kununua bati na kiasi kilichokuwa kinasalia nilianza kuendesha biashara ya kigenge cha kuuza kahawa ambayo naendelea nayo mpaka hivi sasa,” Bi. Abdallah amefanua.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, imehitimisha ziara ya kikazi ya siku moja katika Halmashauri ya Wilaya ya Uyui iliyolenga kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika halmashauri hiyo ambao unaratibiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).




Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Mhe. Florent Kyombo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama na Naibu Waziri wake Mhe. Ridhiwani Kikwete wakimkabidhi fedha mlengwa wa TASAF Wilayani Uyui Bi. Amina Abdallah zilizochangwa na Wajumbe wa Kamati hiyo kumuwezesha mlengwa huyo kukamilisha ujenzi wa nyumba aliyoanza kuijenga kutokana na ruzuku ya TASAF anayoipata. 


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akiwashukuru wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Utawala, Katiba na Sheria kwa upendo waliouonyesha kwa mlengwa wa TASAF, katika Kata ya Migiri Wilayani Uyui Bi. Amina Abdallah kwa mchango wa kumuwezesha mlengwa huyo kukamilisha ujenzi wa nyumba aliyoanza kuijenga kutokana na ruzuku ya TASAF anayoipata.


Mlengwa wa TASAF wa Kata ya Magiri wilayani Uyui, mkoani Tabora Bi. Amina Abdallah akitoa neno la shukurani kwa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Utawala, Katiba na Sheria, vingozi na watendaji wa Serikali baada ya kumpatia fedha kiasi cha shilingi 530,000 kumuwezesha kukamilisha ujenzi wa nyumba aliyoianza kuijenga kutokana na ruzuku ya TASAF anayoipata.


Mlengwa wa TASAF wa Kata ya Magiri wilayani Uyui, mkoani Tabora, Bi. Amina Abdallah akipokea michango ya fedha kutoka kwa Mhe. Jenista Mhagama na Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Utawala, Katiba na Sheria, vingozi na watendaji wa Serikali waliyomchangia kumuwezesha kukamilisha ujenzi wa nyumba aliyoianza kuijenga kutokana na ruzuku ya TASAF anayoipata.


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete akitoa mchango kwa Mlengwa wa TASAF wa Kata ya Magiri wilayani Uyui, mkoani Tabora, Bi. Amina Abdallah ikiwa ni sehemu ya kuwaunga mkono Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Utawala, Katiba na Sheria, vingozi na watendaji wa Serikali waliomchangia mlengwa huyo ili kumuwezesha kukamilisha ujenzi wa nyumba aliyoianza kuijenga kutokana na ruzuku ya TASAF anayoipata.


Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Mhe. Florent Kyombo (wa tatu kutoka kulia) Viongozi na Watendaji wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora pamoja na viongozi wa CCM Wilaya ya Uyui wakiwa katika picha ya pamoja na mlengwa wa TASAF Wilayani Uyui Bi. Amina Abdallah mbele ya nyumba iliyojengwa na mlengwa huyo kutokana na ruzuku ya TASAF anayoipata. 


 

No comments:

Post a Comment