Friday, March 24, 2023

WATUMISHI WA SEKRETARIETI YA MAADILI YA VIONGOZI WATAKIWA KUYAFANYIA KAZI KWA UADILIFU NA WELEDI MALALAMIKO YA WANANCHI DHIDI YA VIONGOZI

 

Na. James K. Mwanamyoto-Dodoma

Tarehe 24 Machi, 2023

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama awewataka watumishi wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kuyafanyia kazi kwa uadilifu, weledi na busara malalamiko yanayowasilishwa na wananchi dhidi ya viongozi wa umma.

Mhe. Jenista ametoa maelekezo hayo wakati akifungua Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma katika Utumishi wa Umma, uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma.

Mhe. Jenista amewasisitiza watumishi hao kutenda haki katika kushughulikia malalamiko yanayowasilishwa na wananchi dhidi ya viongozi wa umma.

“Tendeni haki, kwani kutenda haki ni pamoja na kumuadhibu aliyebainika kufanya kosa na kutokumuadhibu ambaye hajafanya kosa na hizo zote ni haki kwa muktadha wa maadili na utawala bora,” Mhe. Jenista amesisitiza.

Mhe. Jenista amesema, ili taifa lisonge mbele linahitaji mchango wa kiutendaji wa watumishi wa Sekretarieti ya Maadili ya Maadili ya Viongozi wa Umma ambao wana jukumu kubwa la kuwaongoza Watanzania kuliletea taifa maendeleo kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo iliyopo.

Aidha, Mhe. Jenista amezitaka taasisi zote za umma kufanya mikutano ya mabaraza ya wafanyakazi kwa mujibu wa Waraka Na. 1 wa Rais wa Mwaka 1970 unaoendelea kutumika mpaka hivi sasa.

“Taasisi nyingine zimekuwa zikipanga bajeti bila kufanya mikutano ya mabaraza ya wafanyakazi, hiyo ni kuwanyima haki watumishi kutoa maoni na michango yao itakayowezesha utekelezaji mzuri wa bajeti,” Mhe. Jenista amefafanua na kuongeza kuwa, kitendo cha Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kufanya mkutano wa baraza la wafanyakazi ili kutathmini utekelezaji wa bajeti kinaashiria kuwa taasisi inaendeshwa kwa kuzingatia misingi ya maadili.

Kwa upande wake, Kamishna wa Maadili, Jaji (Mst) Mhe. Sivangilwa Mwangesi amesema kuwa mkutano huo wa Baraza la Wafanyakazi wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma ni wa pili kufanyika katika Mwaka wa Fedha 2022/23 ambao kwa mujibu wa utaratibu wa taasisi yake ni mkutano maalum kwa ajili ya kufanya mapitio ya utekelezaji wa bajeti ya Mwaka wa Fedha 2022/23 utakaofikia tamati Juni 31, 2023 pamoja na kujadili mpango mkakati wa kutekeleza bajeti ya mwaka wa fedha 2023/2024.

Mkutano huo wa Baraza la Wafanyakazi wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma umefanyika ikiwa ni utekelezaji wa  Waraka wa Mheshimiwa Rais Na. 1 wa Mwaka 1970 wenye maelekezo mahususi kwa taasisi zote za umma kuwa na mabaraza ya wafanyakazi kwa lengo la kuleta tija na ufanisi mahala pa kazi.

 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akiwaongoza wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi la Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kuimba wimbo wa mshikamano daima ikiwa ni sehemu ya kuhimiza uwajibikaji kwa wajumbe wa baraza hilo wakati wa Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma uliofanyika kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma.


 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akifungua Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma uliofanyika kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma.


Sehemu ya wajumbe wa Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani) wakati akifungua mkutano wa baraza hilo uliofanyika kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma.

 

 

Kamishna wa Maadili, Jaji Mstaafu Mhe. Sivangilwa Mwangesi akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama kufungua Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma uliofanyika kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma.

 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi la Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma mara baada ya kufungua mkutano wa baraza hilo kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma. Waliokaa kushoto ni Kamishna wa Maadili, Jaji Mstaafu, Mhe. Sivangilwa Mwangesi.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akiagana na Kamishna wa Maadili, Jaji Mstaafu Mhe. Sivangilwa Mwangesi mara baada ya Mhe. Jenista kufungua Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma.

 

 


No comments:

Post a Comment