Na. James K. Mwanamyoto-Siha
Tarehe 2 Machi, 2023
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amesema Serikali haitamvumilia mwajiri yeyote katika taasisi za umma atakayeshindwa kusimamia haki za watumishi kama ilivyoelekezwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mhe. Jenista ametoa kauli hiyo katika Halmashauri ya Wilaya ya Siha wakati wa kikao kazi chake na watumishi wa halmashauri hiyo kilicholenga kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma na kusikiliza changamoto za watumishi hao kwa lengo la kuzitatua.
Mhe. Jenista amesema, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alipoingia tu madarakani kwa mara ya kwanza, aliainisha vipaumbele vyake, ikiwamo kusimamia haki na stahiki za watumishi wa umma, wajibu na kufanya kazi kwa hiari bila kushurutishwa na kuongeza kuwa aliainisha vipaumbele hivyo kwani anaamini rasilimaliwatu ndio rasilimali inayowezesha shughuli zote za serikali kufanyika kwa ufasaha ili kutoa huduma zenye viwango kama ilivyokusudiwa.
Mhe. Jenista amemshukuru Mhe. Rais kwa kuwaamini na kuwateua katika nyadhifa walizonazo yeye pamoja na wasaidizi wake, hivyo anamuahidi kusimamia utekelezaji wa vipaumbele alivyovianisha ili maono yake ya kuwa na utumishi uliotukuka yanafikiwa.
Mhe. Jenista ameongeza kuwa, haki na stahiki zinaendana na wajibu, hivyo kama ambavyo Mhe. Rais ameonyesha kuwajali watumishi wa umma katika kusimamia haki na stahili zao, basi nao hawana budi kuwajibika kikamilifu ili kuhakikisha huduma bora kwa umma zinatolewa.
“Mhe. Rais anatamani kuona kila mtumishi anapenda kufanya kazi kila wakati na bila kushurutishwa ili kutoa huduma bora kwa umma na ndio maana ameweka masilahi yenu mbele, hivyo na mimi na wasaidizi wangu tutahakikisha azma hiyo ya Mhe. Rais inafikiwa,” Mhe. Jenista amesisitiza.
Aidha, Mhe. Jenista amewasisitiza Watendaji kupitia Maafisa Utumishi wao kubeba jukumu la utumishi wao katika kusikiliza na kutatua kwa wakati changamoto zinazowakabili watumishi ili kuwawezesha watumishi kufanya kazi kwa bidii na kutoa huduma bora.
Amesema Afisa Utumishi anapaswa kuwa ni sehemu ya maisha ya watumishi kwani kwa kufanya hivyo, kero za watumishi zitatatuliwa kwa wakati wakiwa katika vituo vyao vya kazi badala ya kupelekwa Ofisi ya Rais-UTUMISHI jambo ambalo linaweza kusababisha changamoto hizo kuchelewa kufanyiwa kazi na kusababisha kukwamisha utekelezaji wa majukumu ya watumishi husika.
Akimkaribisha Mhe. Jenista kuzungumza na watumishi, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kumuamini na kumteua kushika wadhifa huo na kuahidi kufanya kazi kwa bidii na ushirikiano ili kuweza kutimiza malengo ya serikali ya kuwa na utumishi imara.
Mhe. Kikwete amewahakikishia watumishi hao nia njema aliyo nayo Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa watumishi na kuwataka watumishi hao kufanya kazi kwa bidii na kutoa huduma bora kwa wananchi.
“Watendaji msiogope, Rais wetu, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa maelekezo mazuri juu ya masilahi yenu, hivyo kwa mtu mwenye akili timamu ni lazima ajitafakari kwa kufanya kazi kwa bidii kwani ndio malengo makuu ya Serikali ya Awamu ya Sita.” Mhe. Kikwete amesisitiza.
Serikali ya Awamu ya Sita
inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kusimamia
upatikanaji wa haki na stahiki za watumishi wa umma ili kujenga ari na morali
ya utendaji kazi itakayowawezesha wananchi kupata huduma bora kutoka katika
taasisi za umma.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma
na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akizungumza na watumishi wa Halmashauri
ya Wilaya ya Siha wakati wa kikao kazi chake na watumishi hao katika
halmashauri hiyo mkoani Kilimanjaro.
Sehemu ya watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Siha, mkoani
Kilimanjaro wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani)
alipokuwa akizungumza nao wakati wa kikao kazi cha Waziri huyo na watumishi hao
kwenye ukumbi wa halmashauri ya wilaya hiyo.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete akitoa neno la utangulizi kabla ya
kumkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama kuzungumza na watumishi wa Halmashauri ya
Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma
na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akisikiliza hoja za watumishi wakati wa
kikao kazi chake na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Siha mkoani
Kilimanjaro kilicholenga kuhimiza uwajibikaji. Walioketi wa kwanza kulia ni
Naibu Waziri wake Mhe. Ridhiwani Kikwete, wa pili ni Naibu Waziri wa Afya,
ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Siha, Mhe. Godwin Mollel na wa kwanza kushoto
ni Mkuu wa Wilaya ya Siha, Mhe. Dkt. Christopher Timbuka.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma
na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama, Naibu Waziri wake Mhe. Ridhiwani Kikwete
pamoja na viongozi wengine wa Serikali wakiimba wimbo wa mshikamano daima kuhimiza
utendaji kazi wa ushirikiano kwa watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Siha,
mkoani Kilimanjaro wakati wa ziara yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji kwa
watumishi wa halmashauri hiyo.
Naibu Waziri wa Afya ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Siha, Mhe.
Godwin Mollel, akitoa shukurani kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti
ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama kwa kutembelea jimbo
lake na kuzungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Siha mkoani
Kilimanjaro pamoja na kusikiliza changamoto zinazowakabili kwa lengo la
kuzitatua.
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Siha, Bi. Pendo
Mangali akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya halmashauri kwa
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,
Mhe. Jenista Mhagama wakati wa kikao kazi cha Waziri huyo na watumishi wa
Halmashauri ya Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro.
No comments:
Post a Comment