Na. Mary Mwakapenda-Dar es Salaam
Tarehe 28 Machi, 2023
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete ameitaka Menejimenti ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kuwapatia elimu ya kutosha Waratibu wa TASAF katika halmashauri ili waweze kuwahudumia walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini kwa upendo ili kufikia malengo ya Serikali ya kuwakwamua walengwa hao katika lindi la umaskini na kuwainua kiuchumi.
Mhe. Kikwete ametoa maelekezo
hayo jijini Dar es Salaam, wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kuhimiza
uwajibikaji kwa watumishi wa TASAF.
Mhe. Kikwete amesema, lengo la kuanzishwa kwa TASAF ni kuwawezesha watu wasiojiweza kabisa kiuchumi kuondokana na hali hiyo duni kwa kuwapatia ruzuku itakayowasaidia kupiga hatua ya maendeleo kiuchumi hivyo ni vema waratibu wakapewa ujuzi wa namna ya kuwahudumia walengwa hao ili kufikia lengo la Serikali la kuanzisha mpango wa TASAF.
“Kuna changamoto kubwa kwa baadhi ya waratibu wa TASAF katika halmashauri kutowahudumia vizuri walengwa wa TASAF, ni vema wakapewa elimu ya kuweza kuzungumza na walengwa kwani fedha zimetengwa kwa ajili yao, wasipohudumiwa kwa upendo itakuwa haina maana ya uanzishwaji wa Mfuko huo,” Mhe. Kikwete amesisitiza.
Mhe. Kikwete amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anatamani kuona wananchi wote wanainuka kiuchumi, hivyo walengwa wakihudumiwa kwa upendo na kuelekezwa namna ya kutumia ruzuku wanayoipata basi malengo ya Mhe. Rais yatakuwa yamefikiwa na hata walengwa hao wataona umuhimu wa uwepo wa Serikali yao na pia Serikali itaungwa mkono na walengwa hao katika kuinua uchumi wa taifa.
Aidha, Mhe. Kikwete ameitaka Menejimenti hiyo kupitia Kitengo cha Habari kuuhabarisha umma juu ya utekelezaji wa majukumu ya taasisi yao ili kuepusha watu wasio na nia njema kuzungumza mabaya juu ya utekelezwaji wa majukumu ya TASAF.
Mhe. Kikwete amesema TASAF inafanya kazi nzuri ya kuwainua walengwa kiuchumi, lakini mazuri hayo hayasemwi mara kwa mara, hivyo ni vizuri yakasemwa ili kuepukana na watu wanaoharibu taswira nzuri ya taasisi na Serikali kwa ujumla.
“Tuisemee taasisi yetu kwa yale yote ambayo tunapaswa kuyasemea ili wananchi na walengwa watambue umuhimu wa TASAF kwani yakisemwa na wengine ambao sio wahusika watapotosha umma na kutulazimu kuanza kukanusha jambo ambalo halileti picha nzuri kwa taasisi na Serikali kwa ujumla.
Mhe. Kikwete ameongeza kuwa iwapo kuna taarifa za upotoshwaji zimetolewa kwenye vyombo vya habari au mitandao ya kijamii, ni vema kuzitolea ufafanuzi wa haraka ili umma upate kuelewa ukweli halisi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), Bw. Ladislaus Mwamanga amemshukuru Naibu Waziri kwa kufanya ziara katika taasisi yake na kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi hao.
Bw. Mwamanga amemuahidi Mhe. Kikwete kuwa yeye pamoja na menejimenti ya taasisi yake watayafanyia kazi maelekezo yote aliyoyatoa kwa ajili ya ustawi wa taifa.
Mhe. Kikwete anaendelea na ziara yake ya kikazi ya kuhimizia uwajibikaji kwa watumishi wa taasisi za umma zilizo chini ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
Naibu Waziri,
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani
Kikwete akimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii
(TASAF), Bw. Ladislaus Mwamanga alipokuwa akiwasilisha
taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya taasisi yake wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu
Waziri huyo iliyolenga kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa taasisi hiyo
jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri,
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani
Kikwete akimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii
(TASAF), Bw. Ladislaus Mwamanga alipokuwa akitoa
ufafanuzi wa masuala mbalimbali ya utekelezaji wa majukumu ya taasisi yake wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu
Waziri huyo iliyolenga kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa taasisi hiyo
jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa
Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), Bw. Ladislaus Mwamanga akiitambulisha menejimenti ya taasisi yake kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala
Bora, Ridhiwani Kikwete wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu
Waziri huyo iliyolenga kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa taasisi hiyo
jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri,
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani
Kikwete akifurahia jambo na Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii
(TASAF), Bw. Ladislaus Mwamanga wakati wa kikao kazi cha Naibu Waziri, huyo na Menejimenti ya TASAF jijini Dar
es Salaam.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete (waliokaa katikati) akiwa katika picha ya
pamoja na Menejimenti ya Mfuko wa
Maendeleo ya Jamii (TASAF) jijini Dar es Salaam wakati wa ziara yake ya
kikazi iliyolenga kuhimiza uwajibikaji wa watumishi wa
taasisi hiyo.
No comments:
Post a Comment