Tarehe 09 Machi, 2023
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete ameitaka Idara ya Mishahara, Motisha na Marupurupu kubuni njia mbalimbali za kutoa motisha kwa watumishi wa umma ambazo zitatumiwa na waajiri Serikalini ili kuwajengea ari na morali ya kutoa huduma bora kwa wananchi ikiwa ni pamoja na kutoa mchango katika maendeleo ya taifa.
Mhe. Kikwete ametoa maelekezo
hayo jijini Dodoma wakati wa kikao kazi chake na watumishi wa idara hiyo kilicholenga
kufahamu majukumu yanayotekelezwa na kuhimiza uwajibikaji.
Mhe. Kikwete amesema,
zitafutwe njia nzuri na sahihi za kuwapa motisha watumishi wa umma ambazo
hazitaathiri bajeti ya utekelezaji wa vipaumbele vya Serikali pamoja na miradi
ya maendeleo inayotekelezwa kwa lengo la kuboresha miundombinu ya utoaji huduma
muhimu kwa wananchi.
Mhe. Kikwete amefafanua kuwa,
motisha kwa watumishi wa umma si lazima iwe fedha bali inaweza kufanyika kwa
kuboresha mazingira ya kazi kwa kuwapatia watumishi wa umma vitu mbalimbali kwa
mfano bima ya afya ya uhakika itakayowawezesha kupata huduma bora ya matibabu
na kuimarisha afya ili waendelee kuwahudumia wananchi ipasavyo.
“Motisha isijikite sana kwenye
fedha, izingatie pia kuboresha mazingira ambayo yatamuwezesha mtumishi wa umma
kutekeleza majukumu yake kikamilifu,” Mhe. Kikwete amesisitiza.
Mhe. Kikwete ameongeza kuwa, yeye
binafsi anaamini kwamba licha ya mtumishi wa umma kupata stahiki ya mshahara
wake lakini motisha kwa mtumishi wa umma ni jambo muhimu sana katika
kumuongezea ari, morali na ufanisi wa utendaji kazi.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amedhamiria kuujenga utumishi wa umma unaowajibika kwa wananchi kwa kutoa huduma bora, hivyo motisha kwa watumishi wa umma ni sehemu ya kulifikia lengo la kuujenga utumishi wa umma unaowajibika kwa umma.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete akizungumza na watumishi wa Idara ya Mishahara, Motisha na Marupurupu (hawapo pichani) wakati wa kikao kazi chake na watumishi wa Idara hiyo kilichofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI Mtumba jijini Dodoma kwa lengo la kufahamu majukumu ya Idara hiyo na kuhimiza uwajibikaji.
Sehemu ya watumishi wa Idara
ya Mishahara, Motisha na Marupurupu wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete (hayupo
pichani) wakati wa kikao kazi cha Naibu Waziri huyo na watumishi hao kilichofanyika
katika Ukumbi wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI Mtumba jijini Dodoma.
Mkurugenzi wa Idara ya Mishahara, Motisha na Marupurupu, Bi. Mariam Mwanilwa akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Idara yake kwa Naibu waziri, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete (hayupo pichani) wakati wa kikao kazi cha Naibu Waziri huyo na watumishi wa Idara hiyo, kilichofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI Mtumba jijini Dodoma.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete akifuatilia taarifa ya utekelezaji wa Idara ya Mishahara, Motisha na Marupurupu iliyokuwa ikiwasilishwa na Mkurugenzi wa Idara hiyo, Bi. Mariam Mwanilwa (hayupo pichani) wakati wa kikao kazi cha Naibu Waziri huyo na watumishi wa Idara hiyo kilichofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI Mtumba jijini Dodoma kwa lengo la kufahamu majukumu ya Idara hiyo na kuhimiza uwajibikaji.
Mkurugenzi
Msaidizi sehemu ya Mishahara na Motisha, Bwana Ghubas Vyagusa akiwasilisha
taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya sehemu yake kwa Naibu waziri, Ofisi ya
Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete
(hayupo pichani) wakati wa kikao kazi cha Naibu Waziri huyo na watumishi wa
Idara ya Mishahara, Motisha na Marupurupu kilichofanyika katika Ukumbi wa Ofisi
ya Rais-UTUMISHI Mtumba jijini Dodoma.
No comments:
Post a Comment