Na. James K.
Mwanamyoto-Dodoma
Tarehe 11 Machi, 2023
Naibu Waziri,
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani
Kikwete amesema utaratibu wa kufanya mazoezi unaoendelezwa na watumishi wa ofisi
yake ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuimarisha afya ili kuweza kutoa huduma bora
kwa wananchi.
Mhe. Kikwete amesema hayo jijini
Dodoma, mara baada ya kumaliza kuwaongoza watumishi wa ofisi yake kufanya
mazoezi ya kuimarisha afya zao yaliyofanyika katika eneo la Ofisi ya
Rais-UTUMISHI lililopo Mji wa Serikali, Mtumba jijini Dodoma.
Mhe. Kikwete amesema, ofisi
yake inatekeleza kwa vitendo maelekezo ya Rais wa Awamu ya Sita Mhe. Dkt. Samia
Suluhu Hassan ya kuwataka watumishi wa umma wanapomaliza kutekeleza majukumu
yao ya kila siku kutenga muda wa kufanya mazoezi ili kuimarisha afya ya akili
na mwili kwa lengo la kuendelea kutekeleza majukumu yao kikamilifu pamoja na
kutoa mchango katika ujenzi wa taifa.
Aidha, kupitia mazoezi hayo,
Mhe. Kikwete ametoa wito kwa watumishi wote wa umma nchini kupitia taasisi zao
kushiriki katika mazoezi ya kuimarisha afya zao ili waweze kutekeleza majukumu
yao kikamilifu kwa maendeleo ya taifa.
“Watumishi wa umma wenzangu kuimarisha
afya ni jambo la msingi, hivyo, tushiriki katika mazoezi ili afya zetu
ziimarike na kuweza kufikia malengo yetu kiutendaji,” Mhe. Kikwete amesisitiza.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu,
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Juma Mkomi amesema afya ni
mtaji kwa mtumishi yeyote kwani bila kuwa na afya nzuri hakuna atakayeweza
kutekeleza majukumu yake kikamilifu, hivyo ushiriki wa watumishi katika mazoezi
ni jambo linalopaswa kupewa kipaumbele na waajiri pamoja na watumishi wa umma.
Bw. Mkomi amesema anaungana na
Mhe. Ridhiwani Kikwete kuwasisitiza watumishi wote wa umma nchini kufanya
mazoezi yatakayoimarisha afya zao ili kutoa huduma bora wananchi.
Uongozi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora umeweka utaratibu wa watumishi wake kushiriki mazoezi ya pamoja kila ijumaa ya wiki kwa kutambua umuhimu wa kuwa na rasilimaliwatu yenye tija katika utoaji wa huduma bora kwa wananchi na wadau wa masuala ya utumishi wa umma na utawala bora.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani akifurahia jambo na Katibu Mkuu wa ofisi
yake Bw. Juma Mkomi, mara baada ya Naibu Waziri huyo kuongoza mazoezi ya
kuimarisha afya za watumishi wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI yaliyofanyika katika
ofisi iliyopo Mji wa Serikali, Mtumba jijini Dodoma.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani (mwenye nguo nyeusi ya mazoezi) akiongoza mazoezi
ya kuimarisha afya za watumishi wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI yaliyofanyika katika
ofisi iliyopo Mji wa Serikali, Mtumba jijini Dodoma.
Katibu
Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Juma Mkomi (wa pili
kutoka kulia) akishiriki mazoezi ya viungo wakati Naibu
Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Ridhiwani (hayupo pichani) akiongoza mazoezi ya kuimarisha afya za
watumishi wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI yaliyofanyika katika ofisi iliyopo Mji wa
Serikali, Mtumba jijini Dodoma.
Sehemu
ya watumishi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora, wakishiriki mazoezi ya kuimarisha afya
yaliyoongozwa na Naibu Waziri wa ofisi hiyo Mhe.
Ridhiwani (hayupo pichani) katika eneo la Ofisi ya Rais-UTUMISHI lililopo
Mji wa Serikali, Mtumba jijini Dodoma.
No comments:
Post a Comment