Na. Mary Mwakapenda-Dar
es Salaam
Tarehe 29 Machi, 2023
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete ameielekeza Menejimenti ya Watumishi Housing Investments (WHI) kujenga nyumba za watumishi kwenye maeneo yenye fursa na mazingira mazuri ya kuishi ili kuwawezesha watumishi wote hata walio kwenye maeneo ya pembezoni kupata makazi bora ya kuishi yatakayowawezesha kutekeleza majukumu yao kikamilifu.
Mhe. Kikwete ametoa maelekezo
hayo leo wakati wa ziara yake ya kikazi ya kujitambulisha na kuhimiza
uwajibikaji kwa watumishi wa Watumishi Housing Investments jijini Dar es
Salaam.
Mhe. Kikwete amesema pamoja na
kazi nzuri iliyofanywa na inayoendelea kufanywa na Watumishi Housing
Investments, ni vizuri zaidi wakafikiria kujenga nyumba nyingi zaidi maeneo
yenye uhitaji mkubwa wa nyumba hizo, akitolea mfano wa maeneo ya pembezoni mwa
nchi ambayo ndio yenye uhitaji mkubwa wa nyumba.
“Mnafanya kazi nzuri sana ya
ujenzi wa nyumba hizi, lakini mnatakiwa kuangalia fursa, maeneo gani yana
uhitaji mkubwa wa nyumba, hasa maeneo ya pembezoni ili hata wanaohamishiwa huko
wafurahie maisha na kutekeleza kikamilifu jukumu la kutoa huduma bora kwa wananchi,”
Mhe. Kikwete amesisitiza.
Mhe. Kikwete ameongeza kuwa, pamoja
na haki na stahiki nyingine wanazopata watumishi, mazingira mazuri ya kuishi ni
jambo lingine la msingi ambalo linapaswa kupewa kipaumbele na WHI wakati wa
utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa nyumba za kuishi watumishi wa umma.
Mhe. Kikwete amesema ni
matarajio ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu
Hassan kuona watumishi wa umma wanafanya kazi kwa bidii na maarifa, hivyo
katika kufikia malengo ya Mhe. Rais, Watumishi Housing Investments wana nafasi
kubwa ya kuunga mkono lengo hilo la Mheshimiwa Rais kwa kujenga nyumba bora kwa
ajili ya kuziuza na kuwapangisha watumishi wa umma nchini.
“Taasisi zinazojenga nyumba
ziko nyingi, wengine wanajikita kwenye ujenzi wa nyumba kwa ajili ya mwananchi
yeyote lakini sisi Watumishi Housing Investments tuna malengo yetu ambayo
yamejikita kwa watumishi wa umma na wanachama wa mifuko ya hifadhi ya jamii,
hivyo tunapaswa kuhakikisha malengo ya taasisi yanatimia.
Mhe. Kikwete ameisisitiza
Menejimenti ya taasisi hiyo kutosita kuwashirikisha Viongozi na Menejimenti ya
Ofisi ya Rais, menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora pale
wanapokutana na changamoto au kama kuna mwongozo wowote wanaouhitaji katika utekelezaji
wa majukumu yao.
Aidha, Mhe. Kikwete ameitaka
taasisi hiyo kutangaza utekelezaji wa majukumu ya taasisi yao ili yafahamike
kwa wahusika.
“Watumishi wanahitaji kuyajua
majukumu yenu, mjitahidi kujitangaza ili kuwafikia kiurahisi tunaowalenga na
kuifanya taasisi yetu kuwa kimbilio la watumishi pale wanapohitaji kuwa na
nyumba iwe ya kununua au kupangisha,” Mhe. Kikwete amefafanua.
Mhe. Kikwete amehitimisha ziara yake ya kikazi ya
kuhimizia uwajibikaji kwa watumishi wa taasisi za umma zilizo chini ya Ofisi ya
Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri,
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani
Kikwete akizungumza na Menejimenti ya Watumishi Housing Investments (WHI) wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga
kujitambulisha na kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa WHI jijini Dar es
Salaam.
Sehemu ya
Menejimenti ya Watumishi Housing Investments (WHI) wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala
Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao
wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kujitambulisha na kuhimiza
uwajibikaji kwa watumishi wa WHI jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa
Watumishi Housing Investments (WHI), Dkt. Fred Msemwa akiwasilisha taarifa ya utekelezaji kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala
Bora, Ridhiwani Kikwete wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu
Waziri huyo iliyolenga kujitambulisha na kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa
taasisi hiyo jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri,
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani
Kikwete akimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji wa Watumishi Housing Investments (WHI),
Dkt. Fred Msemwa alipokuwa akiwasilisha
taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya taasisi yake wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu
Waziri huyo iliyolenga kujitambulisha na kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa
WHI Dar es Salaam.
Naibu Waziri,
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani
Kikwete akifurahia jambo wakati wa kikao kazi chake na Menejimenti ya Watumishi
Housing Investments (WHI) akiwa kwenye ziara ya kikazi iliyolenga kuhimiza
uwajibikaji kwa watumishi wa taasisi hiyo jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri,
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani
Kikwete akiagana na Mkurugenzi Mtendaji wa Watumishi Housing Investments (WHI), Dkt. Fred
Msemwa baada ya kuhitimisha ziara yake ya kikazi iliyolenga kuhimiza
uwajibikaji kwa watumishi wa taasisi hiyo jijini Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment