Monday, December 8, 2025

WITO WATOLEWA KWA WATUMISHI WA OFISI YA RAIS-UTUMISHI KUIISHI MIONGOZO INAYOTOLEWA NA OFISI HIYO

 Antonia Mbwambo

Tarehe 8 Disemba, 2025.

Mkurugenzi wa Idara ya Uendelezaji Taasisi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Nolasco Kipanda ametoa rai kwa Watumishi wa Ofisi hiyo kuiishi Miongozo ya kiutendaji wanayoitoa kwa Watumishi wa Umma ili kuwa mfano bora wa kuigwa katika utekelezaji wa Miongozo hiyo hasa katika kuwahudumia wananchi.

Mkurugenzi Kipanda ameyasema hayo leo Desemba 8, 2025 alipokuwa akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu-UTUMISHI wakati akihitimisha Mafunzo ya Utoaji Huduma kwa Mteja yaliyotolewa na Chuo cha Serikali za Mitaa-Hombolo kwa watumishi wa Ofisi hiyo Mtumba Jijini Dodoma.

“Asili ya Ofisi yetu ni kutoa huduma, lakini pia sisi ndio tunaotoa miongozo inayoendesha Utumishi wa Umma nchini, hivyo tunapaswa kuiishi kikamilifu na kujenga taswira nzuri ya Ofisi na kuwa mfano kwa maslahi ya taifa,” Bw. Kipanda amesisitiza.

Aidha, amewapongeza watoa mada ya Huduma kwa Mteja kutoka Chuo cha Serikali za Mitaa-Hombolo kwa mawasilisho yao muhimu ya namna bora ya kuhudumia mteja kwa haraka na kwa wakati.

Kwa upande wake, Mhadhiri Msaidizi wa Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo Bi. Scholastica Tibitha alisema kuwa Watumishi wa Umma kwa dhamana waliyonayo wanatakiwa kutambua saikolojia ya mteja na kuzingatia mambo mbalimbali kabla ya kutoa majibu kwa mteja, mambo hayo ni pamoja na kusikiliza kuliko kuongea, kuheshimu mteja bila kujali hali au mahali alipotoka, kutoa majibu sahihi na yasiyo na ukakasi kwa mteja

Bi. Tibitha alitumia fursa hiyo kuwakumbusha watumishi hao kuwa kwa sasa wanahesabika katika kundi la watoa huduma lakini kesho watakuwa waomba huduma, hivyo wanatakiwa kutoa huduma wakiwa na dhana hiyo katika maisha yao ya utumishi wa umma.

Vile vile, Mhadhiri Msaidizi kutoka Chuo cha Serikali za Mitaa Bi. Esther Mdegipala alisisitiza kuwa wateja wa ndani na wa nje wanakuja kuomba huduma wakiwa na matarajio yao hivyo watumishi wa umma wanatakiwa kuwa watulivu, wasikivu na kuelewa hoja aliyonayo mteja kisha kukidhi matarajio yake kwa mujibu wa taratibu na kanuni.

Pia, aliwaomba watumishi kutumia mifumo ya TEHAMA katika utoaji wa huduma kwa kuwa mifumo hiyo inarahisisha kazi ya utoaji huduma kwa umma na inapunguza mianya ya rushwa.

Akihitimisha mafunzo hayo, Kaimu Mkurugenzi Utawala na Fedha Bw. Beyond Madege amesisitiza kuwa watumishi wa umma ni muhimu wakawa na taarifa sahihi za mteja ili kutoa huduma bora itakayomridhisha mteja huyo kwa Ustawi wa nchi.


Kaimu Mkurugenzi Utawala na Fedha kutoka Chuo cha Serikali za Mitaa Bw. Beyond Madege akitoa neno la hitimisho baada ya mada kutolewa na wawezeshaji kutoka chuo hicho katika eneo  maalum lililopo Ofisi ya Rais-UTUMISHI Mtumba jijini Dodoma leo tarehe 8 Disemba, 2025

Mkurugenzi wa Idara ya Uendelezaji Taasisi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Bw. Nolasco Kipanda akizungumza na Watumishi wa Ofisi hiyo kuiishi Miongozo ya kiutendaji wanayoitoa kwa Watumishi wa Umma baada ya wawezeshaji kutoka Chuo cha Serikali za Mitaa - Hombolo kuhitimisha mada iliyotolewa leo tarehe 8 Disemba, 2025 katika Ofisi hiyo iliyopo Mtumba jijini Dodoma.

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Bw. Xavier Daudi (wa kwanza kushoto) akifuatilia mada iliyokuwa ikitolewa na mwezeshaji kutoka Chuo cha Serikali za Mitaa -Hombolo wakati wa mafunzo leo tarehe 8       Disemba, 2025 ambayo hutolewa kila jumatatu ya wiki katika Ofisi hiyo iliyopo Mtumba Jijini Dodoma.Wengine ni Wakurugenzi, Wakurugenzi wasaidizi, Pamoja na watumishi wa Ofisi hiyo.


Mhadhiri Msaidizi kutoka Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo Bi. Scholastica Tibitha akisisitiza jambo juu ya umuhimu wa kutoa Huduma Bora kwa Mteja wakati akiendesha mafunzo kwa Watumishi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ikiwa ni sehemu ya kuwajengea uwezo wa kiutendaji yaliyofanyika leo tarehe 8 Disemba, 2025 katika Ofisi hiyo iliyopo mtumba jijini Dodoma  


Mhadhiri Msaidizi kutoka Chuo cha Serikali za Mitaa Bi. Esther Mdegipala akitoa Mafunzo kwa Watumishi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ikiwa ni sehemu ya kuwajengea uwezo wa kiutendaji yaliyofanyika katika eneo maalumu la Ofisi hiyo Mtumba jijini Dodoma leo tarehe 8 Disemba, 2025.

Mhadhiri Msaidizi kutoka Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo Bi. Scholastica Tibitha akitoa mada iliyohusu Umuhimu wa kutoa Huduma Bora kwa Mteja alipokuwa akiendesha mafunzo kwa Watumishi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ikiwa ni sehemu ya kuwajengea uwezo wa kiutendaji yaliyofanyika leo tarehe 8 Disemba, 2025 katika Ofisi hiyo iliyopo mtumba jijini Dodoma  







 

Friday, December 5, 2025

MHE. KIKWETE AIELEKEZA TASAF KUFANYA TATHMINI NA UFUATILIAJI WA SHUGHULI ZA MPANGO ILI KUONA NI KWA KIWANGO GANI MALENGO YA MPANGO YANAFIKIWA

Na Veonica Mwafisi-Dar es Salaam

Tarehe 05 Disemba, 2025

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete ameielekeza Menejimenti ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kufanya tathmini na ufuatiliaji wa shughuli za Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini ili kuona ni kwa kiwango gani malengo ya Mpango huo yanafikiwa, kubainisha changamoto na kuzishughulikia ili kuboresha utendaji kazi na matokeo yanayotarajiwa.

Mhe. Kikwete ameyasema hayo leo tarehe 05 Disemba, 2025 alipokuwa akizungumza na Menejimenti ya TASAF wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa TASAF jijini Dar es Salaam.

Amesema kufanya tathmini kutafichua mambo mengi ambayo yalikuwa hayajulikani katika utekelezaji ambapo itasaidia kuboresha awamu nyingine ya Mpango. “Tufanye tathmini tuangalie kwanini kunakuwa na utofauti katika mafanikio ili tuone tunasaidiaje, je wasimamizi wa eneo fulani wana ubunifu zaidi kuliko wa eneo lingine? Amejiuliza, na kuongeza kuwa haya mambo ni vizuri yakawa shirikishi ili kuboresha zaidi tutakapoingia kwenye awamu nyingine ya Mpango,” Mhe. Kikwete ameongeza

Aidha, ameitaka TASAF kuzungumza mafanikio na changamoto za utekelezaji wa mradi huo kwa walengwa na wananchi. “Tutoke, tuseme mafanikio na changamoto kwanini wamekosa, watu waambiwe ukweli, TASAF imefanya mambo makubwa, tuwaonyeshe waliohitimu, wamefanya nini mpaka kufanikiwa na walioshindwa kufanikiwa wanatakiwa kufanya nini.” Mhe. Kikwete amesisitiza.

Mhe. Kikwete ameipongeza taasisi hiyo kwa kazi nzuri waliyoifanya kwa uendelea kuhawilisha ruzuku kwa kaya maskini zinazokidhi vigezo vya Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini pamoja na kutekeleza miradi ya maendeleo kwenye Sekta za Afya, Elimu, Maji, Mazingira na ujasiriamali.

Pamoja na pongezi hizo ameitaka TASAF kuendelea kuboresha shughuli za kuwezesha utekelezaji wa Miradi ya Jamii ya kutoa Ajira ya muda ili kupunguza changamoto ya ukosefu wa Ajira, kuwezesha jamii kutekeleza miradi ya kuendeleza miundombinu ya huduma za jamii katika Sekta za Afya, Elimu, Maji, Mazingira na ujasiriamali na uendelea kufungamanisha mikakati mbalimbali ya kuwezesha wananchi kiuchumi ili kuhakikisha matokeo yanayopatika kwenye kila mkakati yanaharakisha kasi ya kuondoa umaskini wa wananchi.

Vile vile ameitaka Taasisi hiyo kuimarisha miundombinu ya mifumo ili kulinda usalama wa taarifa za walengwa na kuungamanisha mifumo wa walengwa na mifumo mingine ya Serikali pamoja na kuongeza idadi ya walengwa wanaolipwa kwa njia za kielektroniki ili kupunguza dosari za malipo ya ruzuku.

Mhe. Kikwete amesema malengo makubwa ya yeye na Naibu Waziri Mhe. Mhe. Regina Qwaray kutembelea TASAF leo ni kujitambulisha na kuendelea kufanya kazi kwa ushirikiano ili kufikia malengo ya TASAF yaliyokusudiwa.

“Mimi sio mgeni katika Ofisi hii, hivyo ninawaahidi tutaendelea kushirikiana kama ambavyo tulikuwa tukifanya siku zote nilipokuwa hapa kwa nafasi ya Naibu Waziri. Kuletwa kwangu katika Ofisi hii ni kuja kuongeza nguvu ili kupata matokeo chanya ikiwemo ubunifu katika maeneo mbalimbali. Tufanye kazi tuliyopangwa kufanya tukiongozwa na misingi yetu ya utendaji kazi. Lengo ni kujenga na kumsaidia Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kupunguza kaya masikini katika taifa letu.

Pia Mhe. Kikwete amesema dhana ya ushirikishwaji wa walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini ni nzuri kwani imewasaidia kubuni miradi mbalimbali na imepunguza changamoto nyingi ikiwemo za miundo mbinu, afya na elimu.

Amesisitiza kuwajengea uwezo wa kifikra walengwa, fedha ziwafikie kwa wakati, usimamizi mzuri huku wakitambua kuwa msingi mkubwa wa Mpango huo walengwa wake ni wananchi na si vinginevyo. 

Kwa upande wake Naibu Waziri Mhe. Regina Qwaray ameipongeza TASAF kwa kazi nzuri wanayoifanya. “Mimi ni mgeni katika Ofisi hii, lakini napenda niwapongeze kwa kazi nzuri mnayoifanya, TASAF sio ngeni masikioni mwangu, hii inaonyesha ni kwa jinsi gani mnatekeleza majukumu yenu vizuri, naombeni ushirikiano ili tufanye kazi kwa pamoja na kuwa na matokeo chanya,” amesema Mhe. Qwaray.

Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa shughuli za Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF Bw. Shadrack Mziray amesema Mfuko huo ulianzishwa na Serikali mwaka 2000 kama mojawapo ya mikakati katika kupambana na umaskini kwa kutumia dhana ya ushirikishaji jamii na imetekelezwa kwa awamu tatu tangu kuanzishwa kwake.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete akizungumza na Watendaji na Menejimeti ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) wakati alipofanya ziara ya kikazi iliyolenga kuhimiza uwajibikaji katika ofisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam


Sehemu ya Watendaji na Menejimenti ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete (hayupo pichani) wakati Waziri huyo alipofanya ziara ya kikazi iliyolenga kuhimiza uwajibikaji katika ofisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Regina Qwaray akizungumza na Watendaji na Menejimeti ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kabla ya kumkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete (aliyekaa) kuzungumza na Watendaji hao walipokuwa kwenye ziara ya kikazi iliyolenga kuhimiza uwajibikaji katika ofisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam


Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), Bw. Shadrack Mziray akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa shughuli za TASAF kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete (hayupo pichani) wakati wa ziara ya kikazi ya Waziri huyo iliyolenga kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa ofisi hiyo jijini Dar es Salaam.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete (kushoto) akifuatilia taarifa ya utekelezaji wa shughuli za Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) iliyokuwa ikiwasilishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Bw. Shadrack Mziray (hayupo pichani) wakati wa ziara ya kikazi ya Waziri huyo iliyolenga kuhimiza uwajibikaji katika ofisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam. Kulia ni Naibu Waziri, Ofisi ya Rais-UTUMISHI na Utawala Bora, Mhe. Regina Qwaray.



Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete (katikati) akifurahia jambo na Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), Bw. Shadrack Mziray (wa kwanza kulia) wakati wa ziara ya kikazi ya Waziri huyo iliyolenga kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa ofisi hiyo jijini Dar es Salaam. Wa kwanza kushoto ni Naibu Waziri, Ofisi ya Rais-UTUMISHI na Utawala Bora, Mhe. Regina Qwaray.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili katika ofisi za Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) wakati alipofanya ziara ya kikazi katika ofisi hiyo iliyolenga kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa ofisi hiyo jijini Dar es Salaam.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete (kushoto) akisalimiana na Naibu Waziri wa Ofisi yake, Mhe. Regina Qwaray mara baada ya kuwasili katika ofisi za Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kwa lengo la kufanya ziara ya kikazi ili kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa ofisi hiyo jijini Dar es Salaam.


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Regina Qwaray (Wa kwanza kulia) akizungumza  jambo na Viongozi na Watendaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) mara baada ya Naibu Waziri huyo kuwasili katika ofisi hizo kwenye ziara ya kikazi iliyolenga kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa ofisi hiyo jijini Dar es Salaam. 



Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete (meza kuu kushoto) na Naibu Waziri wa Ofisi yake, Mhe. Regina Qwaray wakifuatilia taarifa ya utekelezaji wa shughuli za Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) iliyokuwa ikiwasilishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Bw. Shadrack Mziray (aliyesimama) wakati wa ziara ya kikazi ya Viongozi hao iliyolenga kuhimiza uwajibikaji katika ofisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam. Wengine ni Watendaji na Menejimenti ya TASAF.

Sehemu ya Watendaji na Menejimenti ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete (hayupo pichani) wakati Waziri huyo alipofanya ziara ya kikazi iliyolenga kuhimiza uwajibikaji katika ofisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete (waliokaa katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Menejimenti ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) jijini Dar es Salaam wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kuhimiza uwajibikaji wa Watumishi wa ofisi hiyo.

 




Monday, December 1, 2025

MAFUNZO

 Watumishi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wakifuatilia mada iliyokuwa ikitolewa na mwezeshaji ikiwa ni sehemu ya Mafunzo ya kuwajengea watumishi hao uwezo wa kiutendaji ambayo hufanyika kila jumatatu ya wiki katika eneo maalum la Ofisi hiyo lililopo Mtumba jijini Dodoma.












TAARIFA HII SIO SAHIHI