Antonia Mbwambo
Tarehe 8 Disemba, 2025.
Mkurugenzi wa Idara ya Uendelezaji Taasisi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Nolasco Kipanda ametoa rai kwa Watumishi wa Ofisi hiyo kuiishi Miongozo ya kiutendaji wanayoitoa kwa Watumishi wa Umma ili kuwa mfano bora wa kuigwa katika utekelezaji wa Miongozo hiyo hasa katika kuwahudumia wananchi.
Mkurugenzi Kipanda ameyasema hayo leo Desemba 8, 2025
alipokuwa akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu-UTUMISHI wakati akihitimisha Mafunzo ya Utoaji Huduma kwa Mteja
yaliyotolewa na Chuo cha Serikali za Mitaa-Hombolo kwa watumishi wa Ofisi hiyo
Mtumba Jijini Dodoma.
“Asili ya Ofisi yetu ni kutoa huduma, lakini pia sisi
ndio tunaotoa miongozo inayoendesha Utumishi wa Umma nchini, hivyo tunapaswa
kuiishi kikamilifu na kujenga taswira nzuri ya Ofisi na kuwa mfano kwa maslahi
ya taifa,” Bw. Kipanda amesisitiza.
Aidha, amewapongeza watoa mada ya Huduma kwa Mteja kutoka Chuo cha Serikali za Mitaa-Hombolo kwa mawasilisho
yao muhimu ya namna bora ya kuhudumia mteja kwa haraka na kwa wakati.
Kwa upande wake, Mhadhiri Msaidizi wa Chuo cha
Serikali za Mitaa Hombolo Bi. Scholastica Tibitha alisema kuwa Watumishi wa
Umma kwa dhamana waliyonayo wanatakiwa kutambua
saikolojia ya mteja na kuzingatia mambo
mbalimbali kabla ya kutoa majibu kwa mteja, mambo hayo ni pamoja na kusikiliza
kuliko kuongea, kuheshimu mteja bila kujali hali au mahali alipotoka, kutoa
majibu sahihi na yasiyo na ukakasi
kwa mteja
Bi. Tibitha alitumia fursa hiyo kuwakumbusha watumishi
hao kuwa kwa sasa wanahesabika katika kundi la watoa huduma lakini kesho
watakuwa waomba huduma, hivyo wanatakiwa kutoa huduma wakiwa na dhana hiyo
katika maisha yao ya utumishi wa umma.
Vile vile, Mhadhiri Msaidizi kutoka Chuo cha Serikali
za Mitaa Bi. Esther Mdegipala alisisitiza kuwa wateja wa ndani na wa nje
wanakuja kuomba huduma wakiwa na matarajio yao hivyo watumishi wa umma
wanatakiwa kuwa watulivu, wasikivu na kuelewa hoja aliyonayo mteja kisha kukidhi
matarajio
yake kwa mujibu wa taratibu na kanuni.
Pia, aliwaomba watumishi kutumia mifumo
ya TEHAMA katika utoaji wa huduma kwa kuwa mifumo hiyo inarahisisha kazi ya utoaji huduma kwa umma na
inapunguza mianya ya rushwa.
Akihitimisha mafunzo hayo, Kaimu Mkurugenzi Utawala na
Fedha Bw. Beyond Madege amesisitiza kuwa watumishi wa umma ni muhimu wakawa na taarifa
sahihi za mteja ili kutoa huduma bora itakayomridhisha mteja huyo kwa Ustawi wa
nchi.
Watumishi kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wakifuatilia mada iliyokuwa ikitolewa na mwezeshaji kutoka Chuo cha Serikali za Mitaa -Hombolo (hayupo pichani) yaliyofanyika katika eneo maalumu lililopo katika Ofisi hiyo Mtumba jijini Dodoma leo tarehe 8 Disemba, 2025
Mhadhiri Msaidizi kutoka Chuo cha Serikali za Mitaa
Hombolo Bi. Scholastica Tibitha akisisitiza jambo juu ya umuhimu wa kutoa
Huduma Bora kwa Mteja wakati akiendesha mafunzo kwa Watumishi wa Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ikiwa ni sehemu ya kuwajengea
uwezo wa kiutendaji yaliyofanyika leo tarehe 8 Disemba, 2025 katika Ofisi hiyo
iliyopo mtumba jijini Dodoma
Mhadhiri Msaidizi kutoka Chuo
cha Serikali za Mitaa Bi. Esther Mdegipala akitoa Mafunzo kwa Watumishi wa
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ikiwa ni sehemu
ya kuwajengea uwezo wa kiutendaji yaliyofanyika katika eneo maalumu la Ofisi
hiyo Mtumba jijini Dodoma leo tarehe 8 Disemba, 2025.
Mhadhiri Msaidizi kutoka Chuo cha Serikali za Mitaa
Hombolo Bi. Scholastica Tibitha akitoa mada iliyohusu Umuhimu wa kutoa Huduma
Bora kwa Mteja alipokuwa akiendesha
mafunzo kwa Watumishi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora ikiwa ni sehemu ya kuwajengea uwezo wa kiutendaji yaliyofanyika
leo tarehe 8 Disemba, 2025 katika Ofisi hiyo iliyopo mtumba jijini Dodoma
No comments:
Post a Comment