Saturday, January 30, 2021

SHUGHULIKIENI CHANGAMOTO ZA WATUMISHI ILI KUWAONGEZEA ARI YA KUFANYA KAZI- DKT. NDUMBARO


Mary Mwakapenda-Dodoma

Tarehe 30 Januari, 2021

Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro amewataka Wanasheria na Maafisa Utumishi katika taasisi za umma nchini kuwathamini Watumishi wa Umma, kuwaheshimu na kuzifanyia kazi changamoto zinazowakabili lengo likiwa ni kupunguza malalamiko na kuwaongezea ari ya kufanya kazi na hatimaye kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Dkt. Ndumbaro ametoa maelekezo hayo Jijini Dodoma wakati akifunga kikao kazi cha siku mbili kwa Wanasheria na Maafisa Utumishi kutoka Halmashauri 31 nchini kilicholenga kutambua changamoto zinazojitokeza katika utekelezaji wa Sheria ya Utumishi Wa Umma Sura 298 ili kuzitafutia ufumbuzi utakaoboresha utoaji wa huduma kwa Watumishi wa Umma na wananchi.

Dkt. Ndumbaro amesema, Wanasheria na Maafisa Utumishi ni wadau wakubwa wanaoshughulika na masuala ya watumishi, hivyo ni muhimu sana kuwathamini, kuwaheshimu na kutambua changamoto wanazokabiliana nazo na kuzitatua kwani wakishindwa kufanya hivyo watasababisha malalamiko mengi yatakayoweza kushusha morali ya kufanya kazi kwa watumishi hao.

Dkt. Ndumbaro ameeleza kuwa, ili Maafisa hao waweze kushughulikia matatizo ya watumishi kwa ufasaha hawana budi kujiweka kwenye nafasi ya watumishi waliofikwa na matatizo kwani kwa kufanya hivyo watakuwa na moyo wa ya kuwasaidia kutatua na kupunguza malalamiko.

Aidha, Dkt. Ndumbaro amewasisitiza washiriki wa kikao kazi hicho kuzingatia uadilifu, uwajibikaji, utendaji kazi mzuri na uwepo wa sifa stahiki kwa Watumishi wa Umma kama ambavyo Mhe. Rais amekuwa akisisitiza mara kwa mara.

Amefafanua kuwa, Wanasheria na Maafisa Utumishi wanapaswa kuwa wasimamizi wa nidhamu kwa watumishi kwani kama uadilifu hauko kwenye taasisi basi wao ndio watakuwa watu wa kwanza kulaumiwa kwa kutokuwajibika ipasavyo.

Ametolea mfano wa suala la uadilifu katika zoezi la kuwabaini watumishi waliokuwa na vyeti vya kughushi na kusema kuwa kuna baadhi ya Maafisa Utumishi wameshiriki kuwasaidia watumishi waliokutwa na vyeti vya kughushi ili wabakie katika Utumishi wa Umma.

“Katika suala la vyeti vya kughushi kuna baadhi ya Maafisa Utumishi wameshiriki kuwasaidia watumishi waliokutwa na vyeti vya kughushi kwa kunyofoa vyeti kwenye mafaili yao ili wabaki kwenye utumishi wa umma. Sisi ndio tunaosimamia nidhamu, tuwe mfano wa kuigwa katika kuonyesha uadilifu kwa kufanya kazi zetu kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo.” Dkt. Ndumbaro amesisitiza.

Akizungumzia suala la uwajibikaji, Dkt. Ndumbaro amesema Watumishi walio katika ngazi za juu wanawajibika kwa Serikali iliyopo madarakani, kwa watumishi wenzao na kwa wananchi kwa kuwahudumia vizuri bila upendeleo wala chuki ili kujenga taswira nzuri katika jamii.

Pia, Dkt. Ndumbaro amewataka Maafisa Utumishi kuwakumbusha watumishi kufuatilia mara kwa mara taarifa za uwasilishaji wa michango katika Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ili wanapostaafu wasipate usumbufu.

“Suala la mafao ya watumishi, wengi wanajisahau au hawajui mpaka wakati wa kustaafu ndio wanagundua kuwa kuna baadhi ya michango haikuwasilishwa, hivyo ni vema kuwakumbusha watumishi kufuatilia michango yao kabla ya kustaafu ili kama kuna michango haijawasilishwa ifanyiwe kazi mapema.” Dkt. Ndumbaro ameongeza.

Kikao kazi hicho kiliandaliwa na Kitengo cha Huduma za Sheria cha Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ambapo mada zifuatazo ziliwasilishwa; Sheria ya Utumishi wa Umma Sura 298, Kanuni za Utumishi wa umma, Taratibu za Ushughulikiaji wa Masuala ya Kinidhamu, Ushughulikiaji wa Ajali kazini kwa ajali zilizotokea kabla ya Juni 2016 na Ushughulikiaji wa Mafao kwa Watumishi wa Umma.

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Dkt. Laurean Ndumbaro akizungumza na Wanasheria na Maafisa Utumishi kutoka Halmashauri 31 nchini (hawapo pichani) wakati akifunga kikao kazi cha siku mbili Jijini Dodoma kilicholenga kutambua changamoto zinazojitokeza katika utekelezaji wa Sheria ya Utumishi Wa Umma Sura 298 ili kuzitafutia ufumbuzi na kuboresha utoaji wa huduma kwa Watumishi wa Umma. Kushoto kwake ni Mkurugenzi wa Usimamizi wa Rasilimaliwatu, ACP Ibrahim Mahumi na kulia kwake ni Mkurugenzi wa Huduma za Sheria, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Hilda Kabissa


Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Dkt. Laurean Ndumbaro akisisitiza jambo kwa Wanasheria na Maafisa Utumishi kutoka Halmashauri 31 nchini (hawapo pichani) wakati akifunga kikao kazi cha siku mbili Jijini Dodoma kilicholenga kutambua changamoto zinazojitokeza katika utekelezaji wa Sheria ya Utumishi Wa Umma Sura 298 ili kuzitafutia ufumbuzi na kuboresha utoaji wa huduma kwa Watumishi wa Umma. 


Baadhi ya washiriki wakimsikiliza Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Dkt. Laurean Ndumbaro wakati akifunga kikao kazi cha siku mbili kwa Wanasheria na Maafisa Utumishi kutoka Halmashauri 31 nchini Jijini Dodoma kilicholenga kutambua changamoto zinazojitokeza katika utekelezaji wa Sheria ya Utumishi Wa Umma Sura 298 ili kuzitafutia ufumbuzi na kuboresha utoaji wa huduma kwa Watumishi wa Umma.


Mmoja wa washiriki Bw. Baraka Kilagu kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, akichangia mada wakati wa kuhitimisha kikao kazi cha siku mbili cha Wanasheria na Maafisa Utumishi kutoka Halmashauri 31 nchini kilichofanyika Jijini Dodoma kwa lengo la kutambua changamoto zinazojitokeza katika utekelezaji wa Sheria ya Utumishi Wa Umma Sura 298 ili kuzitafutia ufumbuzi na kuboresha utoaji wa huduma kwa Watumishi wa Umma.

 

 

Friday, January 29, 2021

WATUMISHI WALIOUZIWA NYUMBA ZA WHC NA KUKIUKA MIKATABA KUVUNJIWA MIKATABA NA KUCHUNGUZWA NA TAKUKURU


Na. James K. Mwanamyoto-Morogoro

Tarehe 29 Januari, 2021

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi ameelekeza Watumishi wa Umma waliouziwa na kupangishwa nyumba za mradi wa Watumishi Housing zilizopo eneo la Mkundi Mkoani Morogoro, ambao wameshindwa kulipa deni na kodi huku wao wakizipangisha nyumba hizo na kunufaika na kodi toka kwa wapangaji wao, wavunjiwe mikataba mara moja na kuielekeza TAKUKURU kuwachunguza watumishi hao.

Mhe. Ndejembi ametoa maelekezo hayo kwa uongozi wa Watumishi Housing mara baada ya kufanya kikao na wapangaji na uongozi huo, ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa aliyemtaka Waziri mwenye dhamana ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kushughulikia changamoto zinazoukabili mradi wa Watumishi Housing eneo la Mkundi Mkoani Morogoro mara baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wapangaji wa nyumba hizo.

Mhe. Ndejembi amefafanua kuwa, kuvunjiwa mikataba kwa watumishi hao kunatokana na wao kukiuka masharti ya mikataba ya ununuzi wa nyumba walizouziwa na kupangishwa na Watumishi Housing.

Ameongeza kuwa, uamuzi wa kuvunja mikataba kwa watumishi waliokiuka masharti ya mikataba utatoa fursa kwa watumishi wengine kuzinunua na kupanga, ikiwa ni pamoja na kuiwezesha Watumishi Housing kupata nguvu ya kiuchumi ya kujenga nyumba nyingine za gharama nafuu kwa ajili ya kuwauzia Watumishi wa Umma nchini.

Aidha, Mhe. Ndejembi ameutaka uongozi wa Watumishi Housing kutafuta mafundi haraka iwezekanavyo ili waweze kuzikagua nyumba hizo za Mkundi na kufanya ukarabati wa milango, madirisha, dali na miundombinu iliyopo iwapo imeharibika, lengo likiwa ni kuwawekea mazingira mazuri ya kuishi watumishi waliozinunua na kupanga katika nyumba hizo.

Sanjali na hilo, Mhe. Ndejembi amesema, Watumishi Housing itajenga kisima cha maji chenye uwezo wa kuhifadhi maji yenye ujazo wa zaidi ya lita 10,000 ikiwa ni kwa ajili ya kuwahudumia watumishi walionunua na kupanga nyumba hizo za Mkundi na kusisitiza kuwa, kisima hicho kitakamilika ndani ya siku 14 na atahakikisha anafanya ufuatiliaji wa karibu ili ujenzi wa kisima hicho ukamilike kwa wakati.

Aidha, Mhe. Ndejembi ameahidi kuwa ifikapo mwezi Juni mwaka huu, maji ya MOROWASA yatapatikana kwani mamlaka hiyo inajenga tanki litakalowezesha kuwahudumia watumishi walionunua na kupanga nyumba hizo zilizojengwa na Watumishi Housing eneo hilo la Mkundi. 

Lengo kuu la miradi mbalimbali ya ujenzi wa nyumba za Watumishi Housing katika maeneo mbalimbali nchini ni kujenga nyumba za bei nafuu kwa ajili ya kuwauzia Watumishi wa Umma ili kuwawezesha kupata makazi bora yatakayowawezesha kuwa na nafasi nzuri ya kutoa huduma bora kwa wananchi.

  

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza na Watumishi (hawapo pichani) waliouziwa na kupangishwa nyumba za mradi wa Watumishi Housing zilizopo eneo la Mkundi Mkoani Morogoro, mara baada ya Naibu Waziri huyo kuutembelea mradi huo ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Mhe. Waziri Mkuu aliyemtaka kushughulikia changamoto zinazoukabili mradi huo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wanunuzi na wapangaji wa nyumba hizo.


Baadhi ya watumishi waliouziwa na kupangishwa nyumba za Watumishi Housing wakimsiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi mara baada ya Naibu Waziri huyo kuutembelea mradi wa nyumba hizo uliopo eneo la Mkundi Mkoani Morogoro ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Mhe. Waziri Mkuu aliyemtaka Waziri mwenye dhamana ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kushughulikia changamoto zinazoukabili mradi huo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wanunuzi na wapangaji wa nyumba hizo.

 


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akielekea kukagua miundombinu ya nyumba waliozouziwa na kupangishwa Watumishi wa Umma, nyumba zilizojengwa na Watumishi Housing eneo la Mkundi Mkoani Morogoro. 


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akitoa maelekezo ya kuboresha miundombinu ya nyumba walizouziwa na kupangishwa Watumishi wa Umma, nyumba zilizojengwa na Watumishi Housing eneo la Mkundi Mkoani Morogoro. 


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akiwahimiza Watumishi wa Umma waliouziwa na kupangishwa nyumba za mradi wa Watumishi Housing kuwasiliana nae pindi wanapokabiliana na changamoto zinazohusiana na nyumba hizo.


 

Thursday, January 28, 2021

MAAFISA UTUMISHI TEKELEZENI WAJIBU WENU BADALA YA KUMUACHIA MZIGO KATIBU MKUU - UTUMISHI

Na Mary Mwakapenda- Dodoma

Tarehe 28 Januari, 2021


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amewataka Maafisa Utumishi katika taasisi za umma nchini kuwajibika ipasavyo, kushughulikia na kutoa ufafanuzi wa masuala ya kiutumishi katika maeneo yao ya kazi kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu badala ya kukiuka au kuwashauri waajiri wao vibaya na kutaka Katibu Mkuu Utumishi kufanya kazi kwa niaba yao.

Mhe. Ndejembi ametoa maelekezo hayo leo Jijini Dodoma wakati akifungua kikao kazi cha siku mbili kwa Wanasheria na Maafisa Utumishi kutoka Halmashauri 31 nchini chenye lengo la kutambua changamoto zinazojitokeza katika utekelezaji wa Sheria ya Utumishi Wa Umma Sura 298 ili kuzitafutia ufumbuzi na kuboresha utoaji wa huduma kwa Watumishi wa Umma.

Mhe. Ndejembi amesema barua nyingi za kuomba ufafanuzi wa masuala mbalimbali ya kiutumishi zinazojibiwa na Ofisi yake zinaonesha Maafisa Utumishi hawawajibiki ipasavyo kwa kuwa Sheria, Kanuni, Taratibu na Nyaraka mbalimbali zipo lakini hawazitumii, badala yake Wakuu wa Taasisi wanapitisha au kuandika barua Utumishi ili Katibu Mkuu Utumishi azifanye kwa niaba yao.

Kumbukeni ‘upward delegation is insubordination’ huu ni ukiukaji mkubwa wa sheria na ni utovu wa nidhamu ambao hauvumiliki. Hatutasita kumchukulia hatua Kiongozi yeyote atakayemtaka Katibu Mkuu Utumishi kufanya majukumu yake.” Mhe. Ndejembi amesisitiza.

Mhe. Ndejembi amewataka Maafisa Utumishi hao kujitafakari kabla ya kuomba kupewa miongozo juu ya masuala ambayo yako ndani ya mamlaka yao kwa mujibu wa Sheria, la sivyo watakuwa wanatenda makosa ambayo yanaweza kumaanisha kutotii au kuonekana wanatekeleza majukumu yao chini ya viwango.


Ametolea mfano Sheria ya Utumishi wa Umma, Sura ya 298, Kanuni za Kudumu katika Utumishi wa Umma za Mwaka 2009 pamoja na Nyaraka mbalimbali zimeainisha bayana taratibu zinazopaswa kufuatwa katika kushughulikia masuala mbalimbali ambayo ni pamoja na utaratibu wa kuwasilisha mapendekezo ya upekuzi, likizo bila malipo, Ajira za Mikataba, Upandishwaji vyeo kwa utaratibu wa kawaida na mserereko, uhamisho na ubadilishaji kada watumishi.

“Badala ya Maafisa husika kuwashauri wakuu wa Taasisi zao kwa kuzingatia miongozo iliyopo wanawashauri vibaya viongozi wao kuandika barua utumishi kuomba maelekezo na ufafanuzi.” Mhe. Ndejembi ameongeza.

Mhe. Ndejembi amesema wakati mwingine waajiri wanawasilisha mapendekezo ya kukaimu nafasi za uongozi kwa Maafisa ambao hawana sifa, na kuongeza kuwa hali hii inatoa tafsiri mbili kuwa Wakuu wa Idara za Utawala na Utumishi wanawashauri vibaya Wakuu wa Taasisi ama kwa makusudi au kwa kutowajibika kusoma Miongozo husika.

Amesema baadhi wanawapandisha vyeo watumishi wakati hawana sifa zilizoainishwa katika Miundo ya Utumishi, hali inayowaathiri watumishi husika kwa sababu maombi ya kubadilisha mishahara ili ilingane na vyeo vipya yasipoidhinishwa na Ofisi yake, huwashusha ari na morali ya kazi na hivyo kuongeza malalamiko na manungĂșniko.

Akitoa maelezo ya awali kuhusu kikao kazi hicho, Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Francis Michael amesema masuala ya kusimamia utumishi ni magumu sana, hivyo ili kuifanya kazi iwe rahisi ni jukumu la Maafisa Utumishi kujua kwa usahihi Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozi ili kupunguza malalamiko na kutoiingizia Serikali hasara kutokana na maamuzi mengi ya kinidhamu yanayofanywa kimakosa.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza na Wanasheria na Maafisa Utumishi kutoka Halmashauri 31 nchini wakati akifungua kikao kazi cha siku mbili Jijini Dodoma leo chenye lengo la kutambua changamoto zinazojitokeza katika utekelezaji wa Sheria ya Utumishi Wa Umma Sura 298 ili kuzitafutia ufumbuzi na kuboresha utoaji wa huduma kwa Watumishi wa Umma. 


Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Francis Michael akitoa maelezo ya awali kuhusu kikao kazi cha siku mbili kwa Wanasheria na Maafisa Utumishi kutoka Halmashauri 31 nchini Jijini Dodoma leo chenye lengo la kutambua changamoto zinazojitokeza katika utekelezaji wa Sheria ya Utumishi Wa Umma Sura 298 ili kuzitafutia ufumbuzi na kuboresha utoaji wa huduma kwa Watumishi wa Umma. 


Mkurugenzi wa Huduma za Sheria, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Hilda Kabissa, akizungumza kwenye kikao kazi cha siku mbili kwa Wanasheria na Maafisa Utumishi kutoka Halmashauri 31 nchini Jijini Dodoma leo chenye lengo la kutambua changamoto zinazojitokeza katika utekelezaji wa Sheria ya Utumishi Wa Umma Sura 298 ili kuzitafutia ufumbuzi na kuboresha utoaji wa huduma kwa Watumishi wa Umma. 


Baadhi ya washiriki wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi wakati akifungua kikao kazi cha siku mbili kwa Wanasheria na Maafisa Utumishi kutoka Halmashauri 31 nchini Jijini Dodoma leo chenye lengo la kutambua changamoto zinazojitokeza katika utekelezaji wa Sheria ya Utumishi Wa Umma Sura 298 ili kuzitafutia ufumbuzi na kuboresha utoaji wa huduma kwa Watumishi wa Umma.


 

Monday, January 25, 2021

NI WAJIBU WA WANUFAIKA WA TASAF KUBORESHA MAISHA YAO


Na. James Mwanamyoto - Uyui

Tarehe 26 Januari, 2021 

Wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wanaopokea ruzuku inayotolewa na Serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) wamekumbushwa wajibu wa kuboresha maisha yao kwa kutumia vizuri fedha za ruzuku wanazopatiwa ili kuondokana na umaskini. 

Akiwa katika ziara ya kikazi kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika Kijiji cha Kinamagi Wilayani Uyui, Mkoa wa Tabora, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amewaasa wanufaika kutotumia kwa anasa ruzuku inayotolewa na TASAF na badala yake waitumie katika shughuli za maendeleo kama kilimo, ufugaji na ujasiriamali. 

Mhe. Ndejembe amefafanua kuwa, ni wajibu wa kila mnufaika kuhakikisha anajiinua kiuchumi kupitia fedha inayotolewa na TASAF, kwani Serikali kwa upande wake inaendelea kutekeleza wajibu wake na maelekezo ya Mheshimiwa Rais ya kuziwezesha kaya zote maskini nchini kupitia utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini.

Mhe. Ndejembi amewataka wanufaika wa TASAF kutosita kujikwamua katika umaskini kwa kuhofia kuondolewa kwenye Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini, na badala yake wajisikie fahari kuondokana na umaskini na hatimaye kuwa mfano bora wa kuigwa na wanufaika wengine ambao hawakutumia vema ruzuku inayotolewa na TASAF. 

Aidha, Mhe. Ndejembi amezitaka Serikali za Vijiji kuacha kudai tozo ndogo ndogo kama za ujenzi wa shule siku ambayo wanufaika wanapokea ruzuku, kwani tozo hizo zinawakwamisha wanufaika kutumia ruzuku wanayoipata kwa ajili ya shughuli zitakazowasaidia kujiondoa katika umaskini. 

Sanjali na hilo, Mhe. Ndejembi amewataka Watendaji wa Vijiji na Kata kutokata ruzuku za wanufaika kwa ajili ya kuchangia huduma za Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) kwani wanakwamisha jitihada za wanufaika kuboresha maisha yao, hivyo amewataka kuwaacha wanufaika wazalishe fedha ndipo wachangie huduma za mfuko huo. 

Mara baada ya kuzungumza na Wananchi na wanufaika wa TASAF katika Kijiji cha Kinamagi, Mhe. Ndejembi aliwatembea wanufaika ili kujionea maendeleo waliyoyapa na hatimaye kushuhudia maendeleo ya Bi. Enviolatha Gerald Kamage ambaye ametumia vizuri ruzuku kununua cherehani, kujenga nyumba, kununua sola na kuweka umeme wa REA.

Mhe. Ndejembi ameshuhudia pia, maendeleo ya mnufaika wa TASAF, Bi. Zena Hussein Maganga ambaye amefanikiwa kutumia vema ruzuku kwa kufuga mbuzi, kuku, kununua mbolea kwa ajili ya kilimo ikiwa ni pamoja na kununua sola inayowawezesha watoto wake kujisomea wakati wa usiku. 

Madhumuni ya utekelezaji wa Mpango wa Kuzinusuru Kaya Maskini nchini ni kuziwezesha kaya hizo kuboresha maisha kwa kuongeza kipato, fursa na uwezo wa kugharamia mahitaji ya msingi kama vile chakula, mavazi, malazi, huduma za afya na mahitaji ya wanafunzi shuleni.



Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza na wananchi na wanufaika wa TASAF (hawapo pichani) Kijiji cha Kinamagi Wilayani Uyui, Mkoa wa Tabora wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo iliyolenga kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini. 


Baadhi ya wananchi na wanufaika wa TASAF Kijiji cha Kinamagi Wilayani Uyui, Mkoa wa Tabora wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo iliyolenga kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini. 


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akiwahimiza wanufaika wa TASAF Kijiji cha Kinamagi Wilayani Uyui, Mkoa wa Tabora kutumia vizuri ruzuku wanayoipata ili kuboresha maisha yao na kuondokana na umaskini, wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo iliyolenga kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini.


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (kulia) akimsikiliza mnufaika wa TASAF, Bi. Zena Hussein wa Maganga wa Kijiji cha Kinamagi Wilayani Uyui, Mkoa wa Tabora akielezea mafanikio aliyoyapa kupitia TASAF, wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo iliyolenga kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini.


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akiwatazama mbuzi wa mnufaika wa TASAF Kijiji cha Kinamagi Wilayani Uyui, Mkoa wa Tabora, Bi. Zena Hussein Maganga alipomtembelea mnufaika huyo ili kujionea mafanikio aliyoyapata wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini.


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo pichani) kuhusu tathmini ya ziara yake ya kikazi yenye lengo la kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini, mara baada ya Naibu Waziri huyo kumaliza zoezi la kuwatembelea wanufaika wa TASAF katika Kijiji cha Kinamagi Wilayani Uyui, Mkoa wa Tabora.


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akiwa katika picha ya pamoja na viongozi na mnufaika wa TASAF, Bi. Enviolatha Gerald Kamage mbele ya nyumba ya mnufaika huyo ambaye ametumia ruzuku aliyoipata kujenga nyumba hiyo, kununua cherehani, sola na kuweka umeme wa REA. 


 

Wednesday, January 13, 2021

MAAFISA UGANI WATAKIWA KUTOA ELIMU YA KILIMO BORA CHA MAZAO YA BIASHARA KWA WANUFAIKA WA TASAF

Na. James K. Mwanamyoto-Singida

Tarehe 13 Januari, 2021

 Maafisa Ugani wametakiwa kutoa elimu ya kilimo bora cha mazao ya biashara  kwa kaya zote maskini nchini zinazonufaika na ruzuku inayotolewa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kupitia Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini  ili kaya hizo ziweze kupata mavuno bora yatakayoziwezesha kuboresha maisha yao na kuondokana umaskini.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi ametoa maelekezo hayo kwa Maafisa Ugani akiwa kijiji cha Mtinko Wilayani Singida katika ziara yake ya kikazi iliyolenga kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini mkoani Singida.

Mhe. Ndejembi amewahimiza Wakurugenzi Watendaji na Maafisa Ugani katika Halmashauri zote kutoa maelekezo kwa kaya maskini juu ya namna bora ya kulima mazao yanayostahimili ukame na kuendana na mazingira halisi ya maeneo husika ili kaya maskini ziweze kunufaika na kilimo.

“Maafisa Ugani katika ngazi ya kata na vijiji waanze kuzitembelea kaya maskini na kuzisaidia namna ya kulima kitaalamu ili ziweze kupata mavuno ya kutosha na kuongeza kuwa, Maafisa Ugani waache kwenda kwenye miradi ya nyama pekee ambayo inawanufaisha kwa kujipatia fedha”, Mhe. Ndejembi amesisitiza.

Sanjali na hilo, Mhe. Ndejembi amepokea shuhuda mbalimbali za mafanikio waliyoyapata wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika Kijiji cha Mtinko wilayani Singida.

Mmoja wa wanufaika, Bi. Leah Ibrahimu Shila amesema, ameitumia fedha ya ruzuku aliyoipokea kujiwekea akiba kidogo kidogo na hatimaye kupata mtaji wa shilingi 200,000/= uliomuwezesha kufungua mgahawa wa kuuza chakula.

Bi. Shila ameeleza kuwa, kabla ya kuwa mnufaika wa TASAF alikuwa akiishi maisha magumu yaliyomsababishia kula mlo mmoja kwa siku lakini hivi sasa anakula milo mitatu na anasomesha watoto wake katika shule za msingi na sekondari.

Naye, Bi. Zena Ramadhani Igwe amemueleza Mhe. Ndejembi kuwa, ametumia vizuri ruzuku aliyoipokea toka TASAF kwa kujenga nyumba bora ya bati kwani aliweza kuwekeza fedha kidogo kidogo ambazo zilimuwezesha kununua saruji na bati.

Ameongeza kuwa, fedha hizo zimemsaidia pia kuanza shughuli ya ufugaji wa kuku ambao wamefikia 30 na ameweza kujishughulisha na kilimo cha bustani, ikiwa ni pamoja na kumsomesha mtoto wake elimu ya sekondari.

Mhe. Ndenjembi ameridhishwa na mafanikio waliyoyapata wanufaika wa TASAF, Bi. Lea Ibrahimu Shila na Bi. Zena Ramadhani Igwe wa Kijiji cha Mtinko Wilayani Singida na kutoa wito kwa wanufaika wote wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini nchini, kuzitumia vema fedha za ruzuku katika shughuli mbalimbali za kiuchumi zitakazoboresha maisha yao na kuondokana na umaskini.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza na wananchi na wanufaika wa TASAF katika Kijiji cha Mtinko wilayani Singida wakati wa ziara yake ya kikazi wilayani humo yenye lengo la kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini mkoani Singida.


Baadhi ya wananchi na wanufaika wa TASAF katika Kijiji cha Mtinko Wilayani Singida wakisikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (Hayupo pichani) wakati wa ziara kikazi ya Naibu Waziri huyo wilayani humo yenye lengo la kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini mkoani Singida.


Mnufaika wa TASAF Kijiji cha Mtinko wilayani Singida, Bi. Leah Ibrahimu Shila akieleza mafanikio aliyoyapata kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (hayupo pichani) wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo yenye lengo la kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wilayani Singida.


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (kushoto) akila chakula kwenye mgahawa wa mnufaika wa TASAF kijiji cha Mtinko Wilayani Singida, Bi. Leah Ibrahimu Shila (wa kwanza kulia) wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo yenye lengo la kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini Wilayani Singida.


Mnufaika wa TASAF Kijiji cha Mtinko Wilayani Singida, Bi. Zena Ramadhani Igwe akieleza mafanikio aliyoyapata kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (hayupo pichani) wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo yenye lengo la kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini Wilayani Singida.


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akisisitiza jambo mbele ya nyumba ya mnufaika wa TASAF Kijiji cha Mtinko Wilayani Singida, wakati wa ziara yake ya kikazi wilayani humo yenye lengo la kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wilayani Singida.


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akipokea zawadi ya kuku kutoka kwa mmoja wa wanufaika wa TASAF Kijiji cha Mtinko Wilayani Singida, wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo yenye lengo la kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini Wilayani Singida.



 

 

Tuesday, January 12, 2021

WAAJIRI WAHIMIZWA KUKITUMIA IPASAVYO CHUO CHA UTUMISHI

Na. James K. Mwanamyoto-Singida

Tarehe 12 Januari, 2021

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amewahimiza Waajiri katika Taasisi za Umma nchini kuwapeleka watumishi wao katika Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) kupatiwa mafunzo bora yatakayowajengea uwezo na kuwaongezea ufanisi kiutendaji ili waweze kutoa huduma bora kwa wananchi.

Mhe. Ndejembi ametoa wito huo wakati wa ziara yake ya kikazi katika Chuo cha Utumishi wa Umma Kampasi ya Singida yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma mkoani Singida.

Mhe. Ndejembi amefafanua kuwa, kuna tabia ya baadhi ya Watumishi wa Umma kulewa madaraka ambayo mara kadhaa imekemewa na Waziri mwenye dhamana ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt. (Mst) Mhe. George Mkuchika inatokana na watumishi hao kukosa maadili ya kiutumishi, hivyo Chuo cha Utumishi wa Umma ndicho pekee kina uwezo wa kutoa mafunzo yatakayojenga maadili bora kwa Watumishi wa Umma.

Ameongeza kuwa, lengo kuu la kuanzishwa kwa Chuo cha Utumishi wa Umma lilikuwa ni kuwajengea uwezo Watumishi wa Umma katika kutekeleza majukumu yao, hivyo ni wajibu wa waajiri wote kukitumia ipasavyo ili kuondokana na changamoto za kiutendaji na kimaadili zinazowakabili Watumishi wa Umma nchini.

Aidha, Mhe. Ndejembi amekanusha dhana iliyojengeka miongoni mwa baadhi ya watu wakidhani Chuo cha Utumishi wa Umma kipo kiushindani dhidi ya Vyuo Vikuu kama UDSM, UDOM, SAUT na Mzumbe na kuongeza kuwa, chuo hicho pia kina jukumu la kutoa mafunzo ya maadili na masuala kiutumishi kwa watumishi walioajiriwa na vyuo vikuu nchini ili vyuo hivyo viweze kuwaandaa wahitimu watakaotoa mchango katika maendeleo ya Taifa.

Kuhusiana na idadi ndogo ya Watumishi wa Umma wanaopatiwa mafunzo katika Chuo cha Utumishi wa Umma, Mhe. Ndejembi amehuzunishwa na idadi ndogo ya Watumishi wa Umma 86 tu wa mkoa wa Singida waliopata fursa ya mafunzo katika Kampasi ya Singida wakati chuo kina uwezo wa kutoa mafunzo kwa watumishi wote mkoani humo.

Mhe. Ndejembi amesema, waajiri wakishirikiana vema na Chuo cha Utumishi wa Umma katika kutoa mafunzo kwa watumishi watakuwa wametekeleza wajibu wa kujenga taifa lenye Watumishi wa Umma wenye tija katika maendeleo ya taifa.

Akizungumzia lengo la kuanzishwa kwa chuo, Mtendaji Mkuu na Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania, Dkt. Emmanuel Shindika amesema, Chuo kilianzishwa kwa lengo la kuboresha Utumishi wa Umma nchini licha ya kutoa mafunzo ya muda mrefu katika ngazi ya cheti, diploma na shahada.

Dkt. Shindika amefafanua kuwa, Chuo cha Utumishi wa Umma Kampasi ya Singida kama zilivyo kampasi nyingine kina majukumu makubwa matatu ambayo ni kutoa mafunzo ya muda mfupi na mrefu, kutoa shauri za kitaalam na kufanya tafiti zenye tija ambazo zinatumiwa kutatua changamoto mbalimbali zinazolikabili taifa.

Chuo cha Utumishi wa Umma Kampasi ya Singida kilianza kutoa huduma rasmi mwaka 2011 na kilisajiriwa na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) mwezi Novemba 2014, hivyo kimeweza kutoa mafunzo ya muda mrefu na mfupi katika ngazi  nne ambazo ni fani Utunzaji wa Kumbukumbu na Nyaraka, Uhazili na Utawala wa Umma na Rasilimaliwatu.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza na watumishi wa Chuo cha Utumishi wa Umma Kampasi ya Singida (hawapo pichani) wakati wa ziara yake ya kikazi katika chuo hicho yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa Kampasi hiyo.


Baadhi ya Watumishi wa Umma Kampasi ya Singida wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (hayupo pichani) wakati wa ziara yake ya kikazi katika chuo hicho yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi hao.


Mtendaji Mkuu na Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania, Dkt. Emmanuel Shindika akitoa taarifa ya utekelezaji ya Chuo cha Utumishi wa Umma Kampasi ya Singida kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (hayupo pichani) wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Kampasi ya Singida.



Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Chuo cha Utumishi wa Umma Kampasi ya Singida mara baada ya kufanya ziara ya kikazi katika chuo hicho yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa Kampasi hiyo.


 

Saturday, January 9, 2021

TASAF YABORESHA MAISHA YA WANANCHI KIJIJI CHA BWITI

 

Na. James K. Mwanamyoto-Mkinga

Tarehe 09 Januari, 2021

Wananchi wanaoishi katika kaya maskini Kijiji cha Bwiti, wilayani Mkinga wanaonufaika na ruzuku inayotolewa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii kupitia Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wamewezeshwa kuboresha makazi yao, kufanya shughuli za ufugaji, ujasiliamali, kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii, kujishughulisha na kilimo ikiwa ni pamoja na kumudu gharama za mahitaji ya shule kwa watoto wao.

Wananchi hao wametoa shuhuda za mafanikio waliyoyapata kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius J. Ndejembi (Mb) wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini na kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma mkoani Tanga.

Mmoja wa wanufaika Bi. Fatuma Mohamed Hamza amemueleza Mhe. Ndejembi kuwa, ruzuku aliyoipata kupitia Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini imemuwezesha kununua bati 40 alizoziezeka katika nyumba yake na hatimaye kuondokana na adha ya kunyeshewa na mvua aliyokuwa akikabiliana nayo kwa kipindi kirefu.

Naye, mjane Bi. Mwajuma Ayubu Bakari amesema, baada ya kupokea ruzuku yake kwa vipindi vitatu mfululizo aliwekeza kidogo kidogo na hatimaye kuweza nununua mbuzi ambapo mpaka hivi sasa amefanikiwa kuwa na mbuzi wapatao 14 na kuongeza kuwa, ruzuku pia inamuwezesha kugharamia mahitaji ya watoto shuleni.

Mnufaika mwingine, Bi. Mwajuma Said Kidevu amemthibitishia Mhe. Ndejembi kuwa, kabla ya kupokea ruzuku alikuwa na mbuzi 6 lakini baada ya kuanza kupokea ruzuku ameweza kuongeza idadi ya mbuzi anaowafuga hadi kufikia 12.

Akizungumzia mafanikio aliyoyapata, Bi. Mwansaada Radoda Ramadhani amemueleza Mhe. Ndejembi kuwa, kupitia ruzuku anayoipata ameweza kujenga nyumba bora yenye choo bora, anajishughulisha na kilimo cha mazao ya chakula na ameweka umeme nyumbani kwake, hivyo anaishukuru Serikali kwa kuanzisha Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini ambao kwa kiasi kikubwa umeboresha maisha yake.

Kwa upande wake, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius J. Ndejembi (Mb) mara baada ya kupokea shuhuda hizo, amewataka walengwa wote wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini nchini kutumia vema ruzuku wanazozipata kujikwamua katika umaskini ili kutimiza lengo la Serikali kuwa na Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini.

Mhe. Ndejembi amesisitiza kuwa, matumizi mazuri ya ruzuku ni sehemu ya kuunga mkono azma ya Mhe. Rais ya kuuendeleza Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini ili kuboresha maisha ya wanyonge nchini.

Sanjali na hilo, Mhe. Ndejembi amewataka waratibu wa TASAF nchini kuhakikisha wanatoa elimu ya namna bora ya kutumia ruzuku wanazopatiwa walengwa wa TASAF na kufanya ufuatiliaji wa karibu ili kuhakikisha ruzuku wanazopatiwa zinatumika kuboresha maisha yao na kuweza kuhitimu kwa lengo la kutoa fursa kwa kaya nyingine kunufaika na ruzuku inayotolewa na TASAF.


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius J. Ndejembi (Mb) akiwasisitiza wanufaika wa TASAF Kijiji cha Bwiti (hawapo pichani) kutumia vizuri ruzuku wanayoipata ili kuboresha maisha yao wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini mkoani Tanga. 


Baadhi ya wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini Kijiji cha Bwiti wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius J. Ndejembi (hayupo pichani) wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo iliyolenga kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini mkoani Tanga.


Mmoja wa wanufaika wa TASAF Kijiji cha Bwiti, Bi. Fatuma Mohamed Hamza akimueleza Mhe. Ndejembi mafanikio aliyoyapata baada ya kunufaika na ruzuku ya Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini.


Kaimu Mtendaji Mkuu wa TASAF Bw. Oscar Maduhu akifafanua malengo ya TASAF kwa wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini Kijiji cha Bwiti wilayani Mkinga.



Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius J. Ndejembi (kulia) akisikiliza ushuhuda wa mafanikio aliyoyapa Bi. Mwajuma Ayubu Bakari baada ya kupokea ruzuku yake toka TASAF.



Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius J. Ndejembi (kulia) akisikiliza kwa makini ushuhuda wa mafanikio aliyoyapata Bi. Mwajuma Said Kidevu mara baada ya kuanza kupokea ruzuku toka TASAF.


Mnufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini Kijiji cha Bwiti, Bi. Mwansaada Radoda Ramadhani akimueleza Mhe. Ndejembi mafanikio aliyoyapata kupitia ruzuku anayoipata toka TASAF.