Friday, January 29, 2021

WATUMISHI WALIOUZIWA NYUMBA ZA WHC NA KUKIUKA MIKATABA KUVUNJIWA MIKATABA NA KUCHUNGUZWA NA TAKUKURU


Na. James K. Mwanamyoto-Morogoro

Tarehe 29 Januari, 2021

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi ameelekeza Watumishi wa Umma waliouziwa na kupangishwa nyumba za mradi wa Watumishi Housing zilizopo eneo la Mkundi Mkoani Morogoro, ambao wameshindwa kulipa deni na kodi huku wao wakizipangisha nyumba hizo na kunufaika na kodi toka kwa wapangaji wao, wavunjiwe mikataba mara moja na kuielekeza TAKUKURU kuwachunguza watumishi hao.

Mhe. Ndejembi ametoa maelekezo hayo kwa uongozi wa Watumishi Housing mara baada ya kufanya kikao na wapangaji na uongozi huo, ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa aliyemtaka Waziri mwenye dhamana ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kushughulikia changamoto zinazoukabili mradi wa Watumishi Housing eneo la Mkundi Mkoani Morogoro mara baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wapangaji wa nyumba hizo.

Mhe. Ndejembi amefafanua kuwa, kuvunjiwa mikataba kwa watumishi hao kunatokana na wao kukiuka masharti ya mikataba ya ununuzi wa nyumba walizouziwa na kupangishwa na Watumishi Housing.

Ameongeza kuwa, uamuzi wa kuvunja mikataba kwa watumishi waliokiuka masharti ya mikataba utatoa fursa kwa watumishi wengine kuzinunua na kupanga, ikiwa ni pamoja na kuiwezesha Watumishi Housing kupata nguvu ya kiuchumi ya kujenga nyumba nyingine za gharama nafuu kwa ajili ya kuwauzia Watumishi wa Umma nchini.

Aidha, Mhe. Ndejembi ameutaka uongozi wa Watumishi Housing kutafuta mafundi haraka iwezekanavyo ili waweze kuzikagua nyumba hizo za Mkundi na kufanya ukarabati wa milango, madirisha, dali na miundombinu iliyopo iwapo imeharibika, lengo likiwa ni kuwawekea mazingira mazuri ya kuishi watumishi waliozinunua na kupanga katika nyumba hizo.

Sanjali na hilo, Mhe. Ndejembi amesema, Watumishi Housing itajenga kisima cha maji chenye uwezo wa kuhifadhi maji yenye ujazo wa zaidi ya lita 10,000 ikiwa ni kwa ajili ya kuwahudumia watumishi walionunua na kupanga nyumba hizo za Mkundi na kusisitiza kuwa, kisima hicho kitakamilika ndani ya siku 14 na atahakikisha anafanya ufuatiliaji wa karibu ili ujenzi wa kisima hicho ukamilike kwa wakati.

Aidha, Mhe. Ndejembi ameahidi kuwa ifikapo mwezi Juni mwaka huu, maji ya MOROWASA yatapatikana kwani mamlaka hiyo inajenga tanki litakalowezesha kuwahudumia watumishi walionunua na kupanga nyumba hizo zilizojengwa na Watumishi Housing eneo hilo la Mkundi. 

Lengo kuu la miradi mbalimbali ya ujenzi wa nyumba za Watumishi Housing katika maeneo mbalimbali nchini ni kujenga nyumba za bei nafuu kwa ajili ya kuwauzia Watumishi wa Umma ili kuwawezesha kupata makazi bora yatakayowawezesha kuwa na nafasi nzuri ya kutoa huduma bora kwa wananchi.

  

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza na Watumishi (hawapo pichani) waliouziwa na kupangishwa nyumba za mradi wa Watumishi Housing zilizopo eneo la Mkundi Mkoani Morogoro, mara baada ya Naibu Waziri huyo kuutembelea mradi huo ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Mhe. Waziri Mkuu aliyemtaka kushughulikia changamoto zinazoukabili mradi huo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wanunuzi na wapangaji wa nyumba hizo.


Baadhi ya watumishi waliouziwa na kupangishwa nyumba za Watumishi Housing wakimsiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi mara baada ya Naibu Waziri huyo kuutembelea mradi wa nyumba hizo uliopo eneo la Mkundi Mkoani Morogoro ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Mhe. Waziri Mkuu aliyemtaka Waziri mwenye dhamana ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kushughulikia changamoto zinazoukabili mradi huo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wanunuzi na wapangaji wa nyumba hizo.

 


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akielekea kukagua miundombinu ya nyumba waliozouziwa na kupangishwa Watumishi wa Umma, nyumba zilizojengwa na Watumishi Housing eneo la Mkundi Mkoani Morogoro. 


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akitoa maelekezo ya kuboresha miundombinu ya nyumba walizouziwa na kupangishwa Watumishi wa Umma, nyumba zilizojengwa na Watumishi Housing eneo la Mkundi Mkoani Morogoro. 


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akiwahimiza Watumishi wa Umma waliouziwa na kupangishwa nyumba za mradi wa Watumishi Housing kuwasiliana nae pindi wanapokabiliana na changamoto zinazohusiana na nyumba hizo.


 

No comments:

Post a Comment