Na Mary Mwakapenda- Dodoma
Tarehe 28 Januari, 2021
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amewataka Maafisa Utumishi katika
taasisi za umma nchini kuwajibika ipasavyo, kushughulikia na kutoa ufafanuzi wa
masuala ya kiutumishi katika maeneo yao ya kazi kwa kuzingatia Sheria, Kanuni
na Taratibu badala ya kukiuka au kuwashauri waajiri wao vibaya na kutaka Katibu
Mkuu Utumishi kufanya kazi kwa niaba yao.
Mhe. Ndejembi ametoa maelekezo hayo leo Jijini Dodoma wakati akifungua
kikao kazi cha siku mbili kwa Wanasheria na Maafisa Utumishi kutoka Halmashauri 31
nchini chenye lengo la kutambua changamoto zinazojitokeza katika utekelezaji wa
Sheria ya Utumishi Wa Umma Sura 298 ili kuzitafutia ufumbuzi na
kuboresha utoaji wa huduma kwa Watumishi wa Umma.
Mhe. Ndejembi amesema barua nyingi za kuomba ufafanuzi wa masuala
mbalimbali ya kiutumishi zinazojibiwa na Ofisi yake zinaonesha Maafisa Utumishi
hawawajibiki ipasavyo kwa kuwa Sheria, Kanuni, Taratibu na Nyaraka mbalimbali
zipo lakini hawazitumii, badala yake Wakuu wa Taasisi wanapitisha au kuandika
barua Utumishi ili Katibu Mkuu Utumishi azifanye kwa niaba yao.
“Kumbukeni ‘upward delegation is insubordination’ huu ni ukiukaji mkubwa wa
sheria na ni utovu wa nidhamu ambao hauvumiliki. Hatutasita kumchukulia hatua
Kiongozi yeyote atakayemtaka Katibu Mkuu Utumishi kufanya majukumu yake.” Mhe.
Ndejembi amesisitiza.
Mhe. Ndejembi amewataka Maafisa Utumishi hao kujitafakari kabla ya
kuomba kupewa miongozo juu ya masuala ambayo yako ndani ya mamlaka yao kwa
mujibu wa Sheria, la sivyo watakuwa wanatenda makosa ambayo yanaweza kumaanisha
kutotii au kuonekana wanatekeleza majukumu yao chini ya
viwango.
Ametolea mfano Sheria ya Utumishi wa Umma, Sura ya 298, Kanuni za
Kudumu katika Utumishi wa Umma za Mwaka 2009 pamoja na Nyaraka mbalimbali
zimeainisha bayana taratibu zinazopaswa kufuatwa katika kushughulikia masuala
mbalimbali ambayo ni pamoja na utaratibu wa kuwasilisha mapendekezo ya upekuzi,
likizo bila malipo, Ajira za Mikataba, Upandishwaji vyeo kwa utaratibu wa
kawaida na mserereko, uhamisho na ubadilishaji kada watumishi.
“Badala ya Maafisa husika kuwashauri wakuu wa Taasisi zao kwa
kuzingatia miongozo iliyopo wanawashauri vibaya viongozi wao kuandika barua
utumishi kuomba maelekezo na ufafanuzi.” Mhe. Ndejembi ameongeza.
Mhe. Ndejembi amesema wakati mwingine waajiri wanawasilisha
mapendekezo ya kukaimu nafasi za uongozi kwa Maafisa ambao hawana sifa, na
kuongeza kuwa hali hii inatoa tafsiri mbili kuwa Wakuu wa Idara za Utawala na
Utumishi wanawashauri vibaya Wakuu wa Taasisi ama kwa makusudi au kwa
kutowajibika kusoma Miongozo husika.
Amesema baadhi wanawapandisha vyeo watumishi wakati hawana sifa
zilizoainishwa katika Miundo ya Utumishi, hali inayowaathiri watumishi husika
kwa sababu maombi ya kubadilisha mishahara ili ilingane na vyeo vipya
yasipoidhinishwa na Ofisi yake, huwashusha ari na morali ya kazi na hivyo kuongeza
malalamiko na manungĂșniko.
Akitoa maelezo ya awali kuhusu kikao kazi hicho, Naibu
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,
Dkt. Francis Michael amesema masuala ya kusimamia utumishi ni magumu sana,
hivyo ili kuifanya kazi iwe rahisi ni jukumu la Maafisa Utumishi kujua kwa
usahihi Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozi ili kupunguza malalamiko na kutoiingizia
Serikali hasara kutokana na maamuzi mengi ya kinidhamu yanayofanywa kimakosa.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza na Wanasheria na Maafisa Utumishi kutoka Halmashauri 31
nchini wakati akifungua kikao kazi cha siku mbili Jijini Dodoma leo chenye lengo
la kutambua changamoto zinazojitokeza katika utekelezaji wa Sheria ya Utumishi
Wa Umma Sura 298 ili kuzitafutia ufumbuzi na kuboresha utoaji wa
huduma kwa Watumishi wa Umma.
Naibu
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,
Dkt. Francis Michael akitoa maelezo ya awali kuhusu kikao kazi cha siku mbili kwa Wanasheria na Maafisa
Utumishi kutoka Halmashauri 31 nchini Jijini Dodoma leo chenye lengo la kutambua
changamoto zinazojitokeza katika utekelezaji wa Sheria ya Utumishi Wa Umma Sura
298 ili kuzitafutia ufumbuzi na kuboresha utoaji wa huduma kwa
Watumishi wa Umma.
Mkurugenzi
wa Huduma za Sheria, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala
Bora, Hilda Kabissa, akizungumza
kwenye kikao kazi cha
siku mbili kwa Wanasheria na Maafisa Utumishi kutoka Halmashauri 31 nchini
Jijini Dodoma leo chenye lengo la kutambua changamoto zinazojitokeza katika
utekelezaji wa Sheria ya Utumishi Wa Umma Sura 298 ili kuzitafutia ufumbuzi na kuboresha utoaji
wa huduma kwa Watumishi wa Umma.
Baadhi
ya washiriki wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya
Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi
wakati akifungua kikao kazi cha siku
mbili kwa Wanasheria na Maafisa Utumishi kutoka Halmashauri 31 nchini Jijini
Dodoma leo chenye lengo la kutambua changamoto zinazojitokeza katika utekelezaji
wa Sheria ya Utumishi Wa Umma Sura 298 ili kuzitafutia ufumbuzi na kuboresha utoaji
wa huduma kwa Watumishi wa Umma.
No comments:
Post a Comment