Mary Mwakapenda-Dodoma
Tarehe 30 Januari, 2021
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro amewataka Wanasheria na Maafisa Utumishi katika taasisi za umma nchini kuwathamini Watumishi wa Umma, kuwaheshimu na kuzifanyia kazi changamoto zinazowakabili lengo likiwa ni kupunguza malalamiko na kuwaongezea ari ya kufanya kazi na hatimaye kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Dkt. Ndumbaro ametoa maelekezo hayo Jijini Dodoma wakati akifunga kikao kazi cha siku
mbili kwa
Wanasheria na Maafisa Utumishi kutoka Halmashauri 31 nchini kilicholenga
kutambua changamoto zinazojitokeza katika utekelezaji wa Sheria ya Utumishi Wa
Umma Sura 298 ili kuzitafutia ufumbuzi utakaoboresha
utoaji wa huduma kwa Watumishi wa Umma na wananchi.
Dkt. Ndumbaro amesema, Wanasheria na Maafisa Utumishi ni wadau
wakubwa wanaoshughulika na masuala ya watumishi, hivyo ni muhimu sana kuwathamini,
kuwaheshimu na kutambua changamoto wanazokabiliana nazo na kuzitatua kwani wakishindwa
kufanya hivyo watasababisha malalamiko mengi yatakayoweza kushusha morali ya
kufanya kazi kwa watumishi hao.
Dkt. Ndumbaro ameeleza kuwa, ili Maafisa hao waweze kushughulikia
matatizo ya watumishi kwa ufasaha hawana budi kujiweka kwenye nafasi ya watumishi
waliofikwa na matatizo kwani kwa kufanya hivyo watakuwa na moyo
wa ya kuwasaidia kutatua na kupunguza malalamiko.
Aidha, Dkt. Ndumbaro amewasisitiza washiriki wa kikao kazi hicho
kuzingatia uadilifu, uwajibikaji, utendaji kazi mzuri na uwepo wa sifa stahiki kwa Watumishi wa Umma kama ambavyo
Mhe. Rais amekuwa akisisitiza mara kwa mara.
Amefafanua kuwa, Wanasheria na Maafisa Utumishi wanapaswa kuwa
wasimamizi wa nidhamu kwa watumishi kwani kama uadilifu hauko kwenye taasisi
basi wao ndio watakuwa watu wa kwanza kulaumiwa kwa kutokuwajibika ipasavyo.
Ametolea mfano wa suala la uadilifu katika zoezi la kuwabaini
watumishi waliokuwa na vyeti vya kughushi na kusema kuwa kuna baadhi ya Maafisa
Utumishi wameshiriki kuwasaidia watumishi waliokutwa na vyeti vya kughushi ili
wabakie katika Utumishi wa Umma.
“Katika suala la vyeti vya kughushi kuna baadhi ya Maafisa
Utumishi wameshiriki kuwasaidia watumishi waliokutwa na vyeti vya kughushi kwa
kunyofoa vyeti kwenye mafaili yao ili wabaki kwenye utumishi wa umma. Sisi ndio
tunaosimamia nidhamu, tuwe mfano wa kuigwa katika kuonyesha uadilifu kwa kufanya
kazi zetu kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo.” Dkt. Ndumbaro
amesisitiza.
Akizungumzia
suala la uwajibikaji, Dkt. Ndumbaro amesema Watumishi walio katika ngazi za juu
wanawajibika kwa Serikali iliyopo madarakani, kwa watumishi wenzao na kwa
wananchi kwa kuwahudumia vizuri bila upendeleo wala chuki ili kujenga taswira
nzuri katika jamii.
Pia, Dkt. Ndumbaro amewataka Maafisa Utumishi kuwakumbusha
watumishi kufuatilia mara kwa mara taarifa za uwasilishaji wa michango katika
Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ili wanapostaafu wasipate usumbufu.
“Suala la mafao ya watumishi, wengi wanajisahau au hawajui mpaka
wakati wa kustaafu ndio wanagundua kuwa kuna baadhi ya michango
haikuwasilishwa, hivyo ni vema kuwakumbusha watumishi kufuatilia michango yao
kabla ya kustaafu ili kama kuna michango haijawasilishwa ifanyiwe kazi mapema.”
Dkt. Ndumbaro ameongeza.
Kikao kazi hicho kiliandaliwa na Kitengo cha Huduma za Sheria cha
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ambapo mada
zifuatazo ziliwasilishwa; Sheria ya Utumishi wa Umma Sura 298, Kanuni za
Utumishi wa umma, Taratibu za Ushughulikiaji wa Masuala ya Kinidhamu,
Ushughulikiaji wa Ajali kazini kwa ajali zilizotokea kabla ya Juni 2016 na
Ushughulikiaji wa Mafao kwa Watumishi wa Umma.
No comments:
Post a Comment