Tuesday, January 12, 2021

WAAJIRI WAHIMIZWA KUKITUMIA IPASAVYO CHUO CHA UTUMISHI

Na. James K. Mwanamyoto-Singida

Tarehe 12 Januari, 2021

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amewahimiza Waajiri katika Taasisi za Umma nchini kuwapeleka watumishi wao katika Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) kupatiwa mafunzo bora yatakayowajengea uwezo na kuwaongezea ufanisi kiutendaji ili waweze kutoa huduma bora kwa wananchi.

Mhe. Ndejembi ametoa wito huo wakati wa ziara yake ya kikazi katika Chuo cha Utumishi wa Umma Kampasi ya Singida yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma mkoani Singida.

Mhe. Ndejembi amefafanua kuwa, kuna tabia ya baadhi ya Watumishi wa Umma kulewa madaraka ambayo mara kadhaa imekemewa na Waziri mwenye dhamana ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt. (Mst) Mhe. George Mkuchika inatokana na watumishi hao kukosa maadili ya kiutumishi, hivyo Chuo cha Utumishi wa Umma ndicho pekee kina uwezo wa kutoa mafunzo yatakayojenga maadili bora kwa Watumishi wa Umma.

Ameongeza kuwa, lengo kuu la kuanzishwa kwa Chuo cha Utumishi wa Umma lilikuwa ni kuwajengea uwezo Watumishi wa Umma katika kutekeleza majukumu yao, hivyo ni wajibu wa waajiri wote kukitumia ipasavyo ili kuondokana na changamoto za kiutendaji na kimaadili zinazowakabili Watumishi wa Umma nchini.

Aidha, Mhe. Ndejembi amekanusha dhana iliyojengeka miongoni mwa baadhi ya watu wakidhani Chuo cha Utumishi wa Umma kipo kiushindani dhidi ya Vyuo Vikuu kama UDSM, UDOM, SAUT na Mzumbe na kuongeza kuwa, chuo hicho pia kina jukumu la kutoa mafunzo ya maadili na masuala kiutumishi kwa watumishi walioajiriwa na vyuo vikuu nchini ili vyuo hivyo viweze kuwaandaa wahitimu watakaotoa mchango katika maendeleo ya Taifa.

Kuhusiana na idadi ndogo ya Watumishi wa Umma wanaopatiwa mafunzo katika Chuo cha Utumishi wa Umma, Mhe. Ndejembi amehuzunishwa na idadi ndogo ya Watumishi wa Umma 86 tu wa mkoa wa Singida waliopata fursa ya mafunzo katika Kampasi ya Singida wakati chuo kina uwezo wa kutoa mafunzo kwa watumishi wote mkoani humo.

Mhe. Ndejembi amesema, waajiri wakishirikiana vema na Chuo cha Utumishi wa Umma katika kutoa mafunzo kwa watumishi watakuwa wametekeleza wajibu wa kujenga taifa lenye Watumishi wa Umma wenye tija katika maendeleo ya taifa.

Akizungumzia lengo la kuanzishwa kwa chuo, Mtendaji Mkuu na Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania, Dkt. Emmanuel Shindika amesema, Chuo kilianzishwa kwa lengo la kuboresha Utumishi wa Umma nchini licha ya kutoa mafunzo ya muda mrefu katika ngazi ya cheti, diploma na shahada.

Dkt. Shindika amefafanua kuwa, Chuo cha Utumishi wa Umma Kampasi ya Singida kama zilivyo kampasi nyingine kina majukumu makubwa matatu ambayo ni kutoa mafunzo ya muda mfupi na mrefu, kutoa shauri za kitaalam na kufanya tafiti zenye tija ambazo zinatumiwa kutatua changamoto mbalimbali zinazolikabili taifa.

Chuo cha Utumishi wa Umma Kampasi ya Singida kilianza kutoa huduma rasmi mwaka 2011 na kilisajiriwa na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) mwezi Novemba 2014, hivyo kimeweza kutoa mafunzo ya muda mrefu na mfupi katika ngazi  nne ambazo ni fani Utunzaji wa Kumbukumbu na Nyaraka, Uhazili na Utawala wa Umma na Rasilimaliwatu.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza na watumishi wa Chuo cha Utumishi wa Umma Kampasi ya Singida (hawapo pichani) wakati wa ziara yake ya kikazi katika chuo hicho yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa Kampasi hiyo.


Baadhi ya Watumishi wa Umma Kampasi ya Singida wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (hayupo pichani) wakati wa ziara yake ya kikazi katika chuo hicho yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi hao.


Mtendaji Mkuu na Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania, Dkt. Emmanuel Shindika akitoa taarifa ya utekelezaji ya Chuo cha Utumishi wa Umma Kampasi ya Singida kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (hayupo pichani) wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Kampasi ya Singida.



Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Chuo cha Utumishi wa Umma Kampasi ya Singida mara baada ya kufanya ziara ya kikazi katika chuo hicho yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa Kampasi hiyo.


 

No comments:

Post a Comment