Na.
James K. Mwanamyoto-Mkinga
Tarehe
09 Januari, 2021
Wananchi wanaoishi katika kaya maskini Kijiji cha Bwiti, wilayani Mkinga wanaonufaika na ruzuku inayotolewa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii kupitia Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wamewezeshwa kuboresha makazi yao, kufanya shughuli za ufugaji, ujasiliamali, kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii, kujishughulisha na kilimo ikiwa ni pamoja na kumudu gharama za mahitaji ya shule kwa watoto wao.
Wananchi hao wametoa shuhuda
za mafanikio waliyoyapata kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius J. Ndejembi (Mb) wakati wa
ziara yake ya kikazi iliyolenga kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya
Maskini na kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma mkoani Tanga.
Mmoja wa wanufaika Bi.
Fatuma Mohamed Hamza amemueleza Mhe. Ndejembi kuwa, ruzuku aliyoipata kupitia
Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini imemuwezesha kununua bati 40 alizoziezeka
katika nyumba yake na hatimaye kuondokana na adha ya kunyeshewa na mvua
aliyokuwa akikabiliana nayo kwa kipindi kirefu.
Naye, mjane Bi. Mwajuma
Ayubu Bakari amesema, baada ya kupokea ruzuku yake kwa vipindi vitatu mfululizo
aliwekeza kidogo kidogo na hatimaye kuweza nununua mbuzi ambapo mpaka hivi sasa
amefanikiwa kuwa na mbuzi wapatao 14 na kuongeza kuwa, ruzuku pia inamuwezesha
kugharamia mahitaji ya watoto shuleni.
Mnufaika mwingine, Bi.
Mwajuma Said Kidevu amemthibitishia Mhe. Ndejembi kuwa, kabla ya kupokea ruzuku
alikuwa na mbuzi 6 lakini baada ya kuanza kupokea ruzuku ameweza kuongeza idadi
ya mbuzi anaowafuga hadi kufikia 12.
Akizungumzia mafanikio
aliyoyapata, Bi. Mwansaada Radoda Ramadhani amemueleza Mhe. Ndejembi kuwa, kupitia
ruzuku anayoipata ameweza kujenga nyumba bora yenye choo bora, anajishughulisha
na kilimo cha mazao ya chakula na ameweka umeme nyumbani kwake, hivyo
anaishukuru Serikali kwa kuanzisha Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini ambao kwa
kiasi kikubwa umeboresha maisha yake.
Kwa upande wake,
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,
Mhe. Deogratius J. Ndejembi (Mb) mara baada ya kupokea shuhuda hizo, amewataka
walengwa wote wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini nchini kutumia vema ruzuku
wanazozipata kujikwamua katika umaskini ili kutimiza lengo la Serikali kuwa na
Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini.
Mhe. Ndejembi
amesisitiza kuwa, matumizi mazuri ya ruzuku ni sehemu ya kuunga mkono azma ya
Mhe. Rais ya kuuendeleza Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini ili kuboresha maisha
ya wanyonge nchini.
Sanjali na hilo,
Mhe. Ndejembi amewataka waratibu wa TASAF nchini kuhakikisha wanatoa elimu ya
namna bora ya kutumia ruzuku wanazopatiwa walengwa wa TASA
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius J. Ndejembi
(Mb) akiwasisitiza wanufaika wa TASAF Kijiji cha Bwiti (hawapo pichani) kutumia
vizuri ruzuku wanayoipata ili kuboresha maisha yao wakati wa ziara yake ya
kikazi iliyolenga kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini mkoani
Tanga.
Baadhi ya wanufaika wa
Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini Kijiji cha Bwiti wakimsikiliza Naibu Waziri,
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius
J. Ndejembi (hayupo pichani) wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo
iliyolenga kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini mkoani Tanga.
Mmoja wa wanufaika wa TASAF Kijiji
cha Bwiti, Bi. Fatuma Mohamed Hamza akimueleza Mhe. Ndejembi mafanikio
aliyoyapata baada ya kunufaika na ruzuku ya Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini.
Kaimu Mtendaji Mkuu wa TASAF
Bw. Oscar Maduhu akifafanua malengo ya TASAF kwa wanufaika wa Mpango wa
Kunusuru Kaya Maskini Kijiji cha Bwiti wilayani Mkinga.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius J. Ndejembi
(kulia) akisikiliza ushuhuda wa mafanikio aliyoyapa Bi. Mwajuma Ayubu Bakari
baada ya kupokea ruzuku yake toka TASAF.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius J. Ndejembi
(kulia) akisikiliza kwa makini ushuhuda wa mafanikio aliyoyapata Bi. Mwajuma
Said Kidevu mara baada ya kuanza kupokea ruzuku toka TASAF.
Mnufaika wa Mpango wa
Kunusuru Kaya Maskini Kijiji cha Bwiti, Bi. Mwansaada Radoda Ramadhani akimueleza
Mhe. Ndejembi mafanikio aliyoyapata kupitia ruzuku anayoipata toka TASAF.
No comments:
Post a Comment