Na Mwandishi wetu-Morogoro
Ofisi
ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora inaendesha mafunzo ya
siku tatu kwa Watumishi 100 waliopo katika Taasisi Rekebu zinazohusika na
uboreshaji wa mazingira ya biashara na Uwekezaji nchini, ili kuwaongezea ujuzi
na kuwajengea uwezo katika utekelezaji wa majukumu yao.
Mafunzo
hayo yamefunguliwa leo tarehe 28 Aprili, 2025 mjini Morogoro na
mwakilishi wa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma
ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Uendelezaji Maadili, Bi. Leila Mavika.
Bi. Mavika amesema
mafunzo hayo yanafanyika kufuatia eneo hilo kuwa na changamoto mbalimbali
zikiwemo kutumia muda mwingi na gharama kubwa za kifedha wakati wa kuanzisha
na kuendesha biashara, uwepo wa taratibu nyingi na zinazojirudia
zinazotakiwa kufuatwa na wawekezaji, pamoja na mapungufu katika baadhi ya
Sheria na Kanuni zinazotumiwa na Taasisi Rekebu.
Amesema pamoja na
mambo mengine, ilionekana masuala hayo yakifanyiwa kazi yatawezesha Nchi kuwa
na mazingira mazuri ya kufanyia biashara ambayo yatavutia wawekezaji wengi
zaidi.
Bi. Leila ameongeza kuwa,
Serikali imeanza utekelezaji wa Mpango wa Kuboresha Uwekezaji na Mazingira
ya Biashara (MKUMBI) awamu ya Kwanza kwa lengo la
kufanya mageuzi na kuboresha Mazingira ya Biashara nchini Tanzania ili
kuwapunguzia mzigo na vihatarishi wafanyabiashara kwa kuhusianisha mifumo ya
udhibiti wa biashara ili kuzuia uwepo wa taratibu nyingi zinazojirudia na
mwingiliano wa majukumu ndani ya Taasisi Rekebu na kuhakikisha kunakuwepo na
uwazi wa mifumo ya udhibiti wa uwekezaji na biashara kupitia majukwaa
mbalimbali ya TEHAMA ambayo hutoa taarifa za taratibu za udhibiti kwa Umma.
Amesema Ofisini hiyo
ni mojawapo ya Taasisi iliyopo katika Mpango huu kutokana na jukumu ililonalo
la kusimamia mafunzo katika Utumishi wa Umma kwa mujibu wa Hati idhini ya
uanzishwaji wa Wizara.
Amesema
katika mwaka wa fedha 2023/2024, Ofisi ya Rais-UTUMISHI ilifanya survey kwa
baadhi ya Taasisi Rekebu 31 ili kukusanya taarifa za upungufu wa ujuzi katika
Taasisi hizo na kuchukua hatua stahiki za kuondosha upungufu huo.
Mafunzo
yanayoanza leo yamejikita katika kushughulikia maeneo ya upungufu wa ujuzi
yaliobainishwa na survey hiyo ambayo ni Mafunzo mbalimbali
kama vile Kuimarisha Mazingira ya Uwekezaji; Ujuzi wa Majadiliano (Negotiation
Skills); Utunzaji na Matumizi Sahihi na Salama ya Nyaraka na Kumbukumbu; Uwezo
wa Kufikiri Kimkakati na Utoaji wa Maamuzi Sahihi; Utunzaji wa Muda; Namna ya
Kuwa Mtumishi wa Thamani katika Taasisi; Akili Hisia; Huduma kwa Mteja na
mengine mengi.
Bi. Mavika amewataka Watumishi wote
ambao wanahudumu katika Taasisi Rekebu kuzingatia Maadili ya Utumishi wa
Umma wakati wa utekelezaji wa majukumu yao ikiwemo kutumia lugha nzuri, bila
upendeleo na kuepuka RUSHWA ili kulinda taswira na heshima ya Utumishi wa Umma
na Taifa kwa ujumla.
“Ni Imani yangu kuwa uchaguzi wa Taasisi hizi haukuwa wa bahati mbaya bali ni wenye makusudi mahsusi yenye dhamira ya kuboresha utendaji kazi wenu kwa kuwaongezea ujuzi ili kuhakikisha Taasisi zenu zinatengeneza mazingira rafiki na wezeshi kwa Wawekezaji wanaokuja kupata huduma.” Amesisitiza Bi. Mavika.
Amesema uboreshaji wa mazingira ya ufanyaji Biashara na Uwekezaji katika nchi yetu ni jambo la muhimu kwa kuwa ni eneo linalowezesha Serikali kupata mapato na kuboresha huduma kwa Wananchi.
Mwaka 2018, Serikali kupitia Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji ilizindua Mpango wa Maboresho ya Mazingira ya Biashara, Mpango ambao uliwezesha nchi kufanya mapitio ya mfumo wa mazingira wezeshi ya biashara (BEE) kwa lengo la kuboresha mazingira ya biashara.
Kaimu Katibu Mkuu Bi. Leila Mavika akizungumza na Watumishi wa Umma kutoka Taasisi mbalimbali mara wakati akifungua mafunzo ya kuongeza ujuzi kuhusu uboreshaji wa mazingira ya biashara katika taasisi za umma yanayofanyika kwa muda wa siku tatu kuanzia leo Aprili, 2025 Mkoani Morogoro
Baadhi ya Watumishi wa Umma kutoka Taasisi mbalimbali wanaoshiriki mafunzo ya uboreshaji wa mazingira ya biashara katika Taasisi za umma rekebuyanayofanyika kwa muda wa siku tatu kuanzia leo tarehe 28 Aprili, 2025 Mkoani Morogoro