Thursday, March 31, 2022

MALALAMIKO YA UKIUKWAJI WA MAADILI KWA VIONGOZI YASHUGHULIKIWE KIKAMILIFU KWA MANUFAA YA TAIFA-Mhe. Jenista

 Na. James K. Mwanamyoto-Dodoma

Tarehe 31 Machi, 2022

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama ameielekeza Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kushughulikia malalamiko na tuhuma zinazowasilishwa na wananchi kuhusu Viongozi wa Umma wanaokiuka maadili ili kuwa na viongozi waadilifu wanaotekeleza majukumu yao kwa maendeleo ya taifa.

Mhe. Jenista ameyasema hayo leo alipokutana na Menejimenti ya Sekretarieti hiyo kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji na kukagua ujenzi wa Ofisi za makao makuu ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma jijini Dodoma.

Mhe. Jenista amesema, kumekuwa na malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu mwenendo wa baadhi ya Viongozi wa Umma kwenye eneo la uadilifu, hivyo Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi ina jukumu kubwa la kuyapokea malalamiko hayo na kuyafanyia kazi ili viongozi wawe na maadili na miiko ya uongozi unaotakiwa.

“Mnapokea tuhuma zinazohusu ukiukwaji wa maadili ya viongozi, hivyo mna jukumu la kufanya uchunguzi ili kuthibitisha ukweli wa tuhuma hizo na kuzifanyia kazi kwa mujibu wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Na.13 ya Mwaka 1995,” Mhe. Jenista amesisitiza.

Aidha, Mhe. Jenista ameitaka Sekretarieti hiyo kutoa elimu ya uzingatiaji wa maadili kwa Viongozi wa Umma ili wasikiuke maadili na miiko ya uongozi kwa kutokuwa na uelewa.

“Katika kipindi hiki tujikite zaidi kutoa elimu ya uzingatiaji wa maadili ili viongozi wetu wa umma waelewe umuhimu wa kuzingatia maadili katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku, hii inatokana na baadhi ya viongozi kukiuka maadili kwa kutokuelewa na hatimaye kujihusisha na vitendo vya ukiukaji wa maadili.” Mhe. Jenista amehimiza.

Amesema azma ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan inamtaka kila Mtanzania ajifunze kutii sheria bila shuruti na kama ni kiongozi basi atii Sheria ya Maadili ya Viongozi bila kushurutishwa, hivyo suala ya utoaji wa elimu ya uzingatiaji wa maadili haliepukiki ili kuwa na uongozi unaozingatia utawala bora.

Kwa upande wake Kamishna wa Sekretarieti ya Maadili wa Viongozi wa Umma, Mhe. Jaji Sivangilwa Sikalalilwa Mwangesi amezitaja kazi za msingi za Sekretarieti hiyo kuwa ni pamoja na kupokea matamko yanayotakiwa kutolewa na Viongozi wa Umma kwa mujibu wa Katiba na Sheria, kupokea malalamiko na tuhuma za ukiukwaji wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, kuanzisha na kufanya uchunguzi dhidi ya tuhuma za ukiukwaji wa maadili na kufanya uhakiki wa Matamko na Rasilimali na Madeni yanayotolewa na Viongozi wa Umma kwa mujibu wa Sheria.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akizungumza na Menejimenti ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma alipokutana na Menejimenti hiyo kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji na kukagua ujenzi wa Ofisi za makao makuu ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma jijini Dodoma. Kulia kwake ni Kamishna wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Mhe. Jaji Sivangilwa Mwangesi na kushoto kwake ni Mkurugenzi Idara ya Ujenzi Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) Mhandisi Loishorwa Likimaitare.


Kamishna wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi, Mhe. Jaji Sivangilwa Mwangesi akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama kuzungumza na Menejimenti hiyo kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji na kukagua ujenzi wa Ofisi za makao makuu ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma jijini Dodoma. 


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akiwa katika kikao kazi na Menejimenti ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma alipokutana na Menejimenti hiyo kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji na kukagua ujenzi wa Ofisi za makao makuu ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma jijini Dodoma. 


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akiwasili eneo la Ujenzi wa Ofisi ya makao makuu ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma unaoendelea jijini Dodoma wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kukagua ujenzi huo. Kushoto kwake ni Kamishna wa Sekretarieti wa Maadili ya Viongozi, Mhe. Jaji Sivangilwa Mwangesi.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akimsikiliza Meneja wa Mkoa Dodoma, Mbunifu Majengo (TBA) Bw. Victor Balthazar alipokuwa akimuonesha mchoro wa jengo la ofisi ya Sekretarieti ya Maadili Makao Makuu wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kukagua Mradi wa Ujenzi wa Jengo hilo jijini Dodoma.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akimsikiliza Kamishna wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi, Mhe. Jaji Sivangilwa Mwangesi alipokuwa akimuonesha miundombinu wakati wa ziara yake ya kikazi yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji na kukagua ujenzi wa ofisi hizo.



Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akitoka kukagua jengo la la ofisi za makao makuu ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma linaloendelea kujengwa jijini Dodoma na Mkandarasi ambaye ni Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) wakati wa ziara yake ya kikazi yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji na kukagua ujenzi wa ofisi hizo.


Muonekano wa jengo la ofisi za makao makuu ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma linaloendelea kujengwa jijini Dodoma na Mkandarasi ambaye ni Wakala wa Majengo Tanzania (TBA)


Tuesday, March 29, 2022

MHE. NDEJEMBI AWATAKA WANANCHI KIJIJI CHA NANGE WILAYANI MISUNGWI KUITUNZA BARABARA INAYOJENGWA NA TASAF ILI IWANUFAISHE

 

Na. James K. Mwanamyoto-Mwanza

Tarehe 30 Machi, 2022

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amewataka wananchi wa Kijiji cha Nange wilayani Misungwi kuhakikisha wanaitunza barabara ya jamii yenye urefu wa kilometa 2.6 inayojengwa na TASAF kupitia mradi wa utoaji ajira za muda kwa walengwa, ulioibuliwa na wananchi wa eneo hilo kutokana na uhitaji wa barabara itakayowawezesha kusafiri ili kupata huduma muhimu za kijamii.

Mhe. Ndejembi ametoa wito huo kwa wananchi na walengwa wa TASAF wa Kijiji cha Nange, mara baada ya kutembelea mradi huo wa ujenzi wa barabara na kubaini uharibifu wa barabara unaosababishwa na wafugaji wa eneo hilo kupitisha ng’ombe kwenye barabara hiyo.

Mhe. Ndejembi amesema, pamoja na kuwa amefarijika kuwaona walengwa wa TASAF wakifanya kazi ya kujenga barabara hiyo na kupata kipato, lakini wanawajibika kuitunza ili jamii inufaike nayo badala ya kuiacha iendelee kuharibiwa na wafugaji wanaopitisha ng’ombe wao.

“Barabara hii inajengwa kwa fedha za Serikali kupitia TASAF, tukiendelea kuacha ng’ombe wapite na mvua ikinyesha tu itageuka kuwa tope na kuwapa changamoto ya kutokuwa na barabara itakayowawezesha kupata huduma za kijamii kama afya, elimu na usafiri,” Mhe. Ndejembi amesisitiza.

Katika kutatua changamoto hiyo ya ng’ombe kupita kwenye barabara hiyo, Mhe. Ndejembi ameutaka uongozi wa kijiji kushirikiana na wananchi kutengeneza maeneo ya kupita mifugo pembezoni mwa barabara ikiwa ni pamoja na kuhimiza uzingatiaji wa sheria ya matumizi ya barabara.

Ameongeza kuwa, wananchi wa eneo hilo wanahitaji barabara hiyo isiharibiwe na mifugo ili kuwawezesha akina mama wajawazito kufuata huduma ya afya ya uzazi kwa wakati, wanafunzi wanaotoka umbali mrefu kuwahi darasani na kushiriki masomo kikamilifu, ikiwa ni pamoja na kuwawezesha wakulima kusafirisha mazao yao baada ya mavuno.

Aidha, amewaeleza walengwa wa TASAF wanaonufaika na ujenzi wa mradi huo wa barabara kuwa, ili waweze kuondokana na lindi la umaskini ni lazima miundombinu yao iwe mizuri, hivyo wanapaswa kuhakikisha barabara hiyo inatunzwa na kujengwa kwa viwango bora kulingana na thamani ya fedha.

Kwa upande wake, mlengwa wa TASAF Kijiji cha Nange, Bi. Flora Sospeter amesema, barabara hiyo imekuwa na faida kubwa kwa jamii yao kwani wanapougua inawawezesha kwenda zahanati ya kijiji kwa wakati ili kupata matibabu, tofauti na ilivyokuwa hapo awali wakati barabara ilikuwa mbaya.

Naye Mlengwa mwingine wa TASAF wa Kijiji cha Nange, Bw. Nkiyungu Nkiliga amesema kuwa, barabara hiyo ilikuwa ni mbaya sana, hivyo ulivyokuja mradi wa TASAF iliwalazimu kubuni mradi huo wa ujenzi wa barabara ili kusaidia wagonjwa kupata huduma za matibabu na kuweka miundombinu mizuri ya barabara itakayowawezesha kutoa mazao yao shambani.

Barabara hiyo inayogengwa na TASAF katika Kijiji cha Nange kilichopo katika Kata ya Igokelo Wilayani Misungwi inahudumia jumla ya vitongoji 6 vyenye wakazi 3,881, wanaume wakiwa ni 1,746 na wanawake 2,135. Takwimu hizo ni kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Nange Wilayani Misungwi, alipofanya ziara ya kikazi kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa barabara ya jamii yenye urefu wa Kilometa 2.6 inayojengwa na TASAF katika kijiji hicho kupitia mradi wa utoaji ajira za muda kwa walengwa wilayani humo.

 

Mwonekano wa barabara ya jamii yenye urefu wa Kilometa 2.6 inayojengwa na TASAF katika Kijiji cha Nange Wilayani Misungwi, kupitia mradi wa utoaji ajira za muda kwa walengwa katika wilaya hiyo.

 

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Deogratius Ndejembi akiwasisitiza wananchi wa Kijiji cha Nange Wilayani Misungwi kuitunza barabara ya jamii yenye urefu wa Kilometa 2.6 inayojengwa na TASAF, alipofanya ziara ya kikazi kukagua maendeleo ya ujenzi barabara hiyo wilayani humo.

 

 

Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF Bi. Sarah Mshiu akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Nange Wilayani Misungwi, wakati wa ziara ya kikazi ya Mhe. Deogratius Ndejembi ya  kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa barabara ya jamii yenye urefu wa Kilometa 2.6 inayojengwa na TASAF katika kijiji cha Nange kupitia mradi wa utoaji ajira za muda kwa walengwa katika kijiji hicho.


 

Mmoja wa walengwa wa TASAF wa Kijiji cha Nange akishiriki ujenzi wa mradi wa barabara ya jamii yenye urefu wa Kilometa 2.6 inayojengwa na TASAF katika kijiji hicho kupitia mradi wa utoaji ajira za muda kwa walengwa.


Mlengwa wa TASAF Kijiji cha Nange Bi. Flora Sospeter akieleza faida ya barabara ya jamii yenye urefu wa Kilometa 2.6 inayojengwa na TASAF katika kijiji hicho kupitia mradi wa utoaji ajira za muda kwa walengwa.

 

Mlengwa wa TASAF wa Kijiji cha Nange Bw. Nkiyungu Nkiliga akieleza sababu ya wananchi kuibua mradi wa ujenzi wa barabara ya jamii yenye urefu wa Kilometa 2.6 unaotekelezwa na TASAF katika kijiji hicho kupitia mradi wa utoaji ajira za muda kwa walengwa.