Na. James K. Mwanamyoto-Dar es Salaam
Tarehe 19 Machi, 2022
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama ameielekeza Kampuni ya Serikali ya SUMA JKT Co. Limited (Eastern zone) kuhakikisha inakamilisha ujenzi wa jengo la ofisi za karakana ya ndege (HANGAR) tarehe 22, Mei 2022 ambalo ni muhimu kwa usalama wa safari za viongozi wakuu wa nchi.
Mhe. Jenista ametoa maelekezo hayo jijini Dar es Salaam, wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa ujenzi wa mradi wa karakana ya ndege ambao umegawanyika katika awamu mbili, awamu ya kwanza ikiwa ni ujenzi wa ofisi na ya pili ni karakana.
Mhe. Jenista amesema kuwa, hataki kuwa kiongozi aliyeshindwa kusimamia usalama wa safari za viongozi wakuu wa nchi ambao wanatumia usafiri wa anga kutekeleza majukumu yao ya kitaifa.
Amemtaka mkandarasi SUMA JKT na Mkandarasi Mshauri DIT-Institute pamoja na menejimenti ya Wakala wa Ndege za Serikali (TGFA) kila mmoja kwa nafasi yake kuona umuhimu wa kukamilisha ujenzi wa ofisi za karakana kwa wakati, kwasasabu ya kuimarisha usalama wa safari za viongozi wakuu wa kitaifa.
“Hakutakuwa na fursa kwa mkandarasi kuongezewa muda ili kukamilisha ujenzi, ongezeni nguvu kazi na ikiwezekana ombeni kibali cha kufanya kazi usiku na mchana, na ikiwa mtaona kuna ulazima wa kunishirikisha kwa hilo msisite kufanya hivyo,” Mhe. Jenista amefafanua.
Katika kuhakikisha maelekezo yake yanatekelezwa, Mhe. Jenista ameahidi kurejea tarehe 30 Aprili, 2022 kwa ajili ya ukaguzi na kujiridhisha ni kwa kiasi gani maelekezo yake yametekelezwa.
Mradi wa ujenzi wa karakana ya ndege, unajumuisha ujenzi wa jengo jipya la ofisi, tanki la maji na jengo la jenereta na kusimika miundombinu ya umeme, miundombinu ya kutambua viashiria vya moto na vizima moto.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akitoa maelekezo jijini Dar es Salaam kwa Kampuni ya SUMA JKT kuhakikisha inakamilisha ujenzi wa jengo la ofisi za karakana ya ndege akiwa kwenye ziara yake ya kikazi ya kukagua ujenzi wa jengo hilo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akikagua uimara wa moja ya dirisha katika jengo la ofisi za karakana ya ndege, wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua ujenzi wa jengo hilo.
Mwonekano wa jengo la ofisi za karakana ya ndege linalojengwa jijini Dar es Salaam na Kampuni ya SUMA JKT iliyopewa kandarasi hiyo.
No comments:
Post a Comment