Tuesday, March 15, 2022

WAKULIMA 2409 WAWEZESHWA KUKOPA SHILINGI BILIONI 28.2 KUPITIA HATIMILIKI ZA ARDHI ZILIZOTOLEWA NA MKURABITA - Mhe. Jenista

Na. Veronika Mwafisi-Dodoma

Tarehe 15 Machi, 2022

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amesema wakulima 2,409 na Vyama vya Ushirika vitano wamewezeshwa kukopa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 28.2 kupitia hatimiliki za ardhi zilizotolewa na Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA).

Mhe. Jenista amesema hayo jijini Dodoma, wakati akizungumza na watumishi wa MKURABITA alipofanya ziara yake ya kikazi iliyolenga kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi hao.

Mhe. Jenista amesema kuwa, mikopo hiyo imewawezesha wakulima hao kuingia kwenye kilimo bora na cha kisasa ambacho kinaliwezesha taifa kuwa na akiba ya hifadhi ya chakula cha kutosha.

“Mikopo hiyo imewasaidia pia wakulima kuondokana na ukulima wa kawaida na kuingia kwenye kilimo cha biashara ambapo anakuwa ni mlipa kodi mzuri anayechangia ukuaji wa uchumi,” Mhe. Jenista amefafanua.

Mhe. Jenista ameongeza kuwa, wamiliki 206 waliorasimisha viwanja maeneo ya mjini wametumia hatimiliki kupata mikopo yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 3.

Akimkaribisha Mhe. Waziri kuzungumza na watumishi, Mratibu wa MKURABITA Dkt. Seraphia Mgembe amesema wakulima hao 2409 waliotumia Hatimiliki za ardhi kupata mikopo ya kiasi cha shilingi bilioni 28.2 wamethibitisha wenyewe kwa maandishi kupitia fomu walizojaza.

Aidha, Dkt. Mgembe amesema, wafanyabiashara waliopata mafunzo kupitia MKURABITA wameweza kukopa zaidi ya shilingi bilioni 9.38 kwa ajili ya kuongeza mitaji ya biashara zao.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akizungumza jijini Dodoma na watumishi wa MKURABITA wakati wa ziara yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa taasisi hiyo.  


Baadhi ya watumishi wa MKURABITA wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani) wakati ziara yake ya kikazi yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi hao. 


Mratibu wa Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA), Dkt. Seraphia Mgembe akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya MKURABITA jijini Dodoma kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama wakati wa ziara ya kikazi ya Waziri huyo iliyolenga kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa taasisi hiyo. 


Mkurugenzi wa Urasimishaji Ardhi wa MKURABITA, Bi. Jane Lyimo akitoa neno la shukrani kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama mara baada ya waziri huyo kuzungumza na watumishi wa ofisi hiyo jijini Dodoma wakati wa ziara yake ya kikazi yenye lengo la kujitambulisha na kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa taasisi hiyo.



Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akisalimiana na watumishi wa MKURABITA mara baada ya kuwasili katika Ofisi hiyo jijini Dodoma wakati wa ziara yake ya kikazi yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa taasisi hiyo.

 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa MKURABITA baada ya kuzungumza nao wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa taasisi hiyo. 





 















No comments:

Post a Comment